Monday, November 5, 2012

TSHIMANGA KALALA ASSOSA. ‘Mtoto mzuri’


 Mwimbaji mashuhuri Thsimanga Kalala Assosa akiimba katika moja ya maonyesho alipokuwa Maquidu Zaire.
 
Novemba 05,2012.

Tshimanga  Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za Negro Success, Les Kamalee,  Lipua Lipua na Fuka Fuka.

Assosa ni mwenye  kipaji cha kutunga na kuimba  nyimbo za muziki dansi pia ni  kiongozi wa Bendi ya Bana Maquis iliyopo jijini Dar es  Salaam.

Kwa hali isiyokuwa ya kawaida, Tshimanga Assosa amekuwa akikataa Ofa lukuki za kwenda ‘kula maisha’ Ulaya na Marekani na kuamua kuishi katika Jijini la Dar es Salaam hapa Tanzania.

Akiwa katika bendi hizo alishirikiana wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na  Kiamuangana Mateta  Wazola Mbongo ‘ Verckies’

Historia ya maisha yake inaanzia siku aliyoiona dunia baada ya kuzaliwa katika mji wa Kamina uliopo Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Aprili 04, 1949.
Alipata elimu ya Sekondari katika Shule iliyojulikana kama Charles Ruangwa hapo Kamina.

 Akielezea  historia hiyo Tshimanga Assosa anasema alianza kuimba akiwa bado mdogo na kwamba aliyejipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina ambako maPadri walimsaidia kumfundisha muziki.

Pamoja na juhudi zake hizo, Baba yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye  ajitumbukize katika muziki na kumtaka afuate masomo yake shuleni.

Baada kumaliza kidato cha nne, Baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Assosa Muziki ulikuwa ndani ya damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa  akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo hapo Kamina ya Super Gabby.

Anasema mazoezi ya hiyo yalimtia hamasa kubwa ya kupenda muziki. Anaeleza kwamba siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa  kuimba katika bendi hiyo. Assosa alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla Baba yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko.

 Waswahili wanasema ‘Sikio la  kufa halisikii dawa’ Baba yake mwisho wake alikubali ombi la mwanaye  baada ya kubaini kuwa hashikiki wala habadiliki kitabia, akamruhusu afanye muziki aupendao.

 Mwaka 1969  Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana na mwanamuziki Bavon Marie Marie  na akampeleka kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo aliyejulikana kama Didi Kalombo.
Assosa aliitumia vyema nafasi hiyo ya kujaribiwa sauti. Mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika  bendi hiyo.

Assosa anazikumbuka changamoto alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti  na wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo)
Anasema sauti yake ndiyo iliyomuokoa na kupewa heshima  kama wanamuziki wengine.

Tshimanga Kalala Assosa anafafanua kwamba kufa kwa Kiongozi ‘Star’ yeyote katika bendi, mara nyingi husababisha bendi aliyoiacha kuteteleka hatimaye kufa. Akitolea mifano  ya Bendi za T.P.OK. Jazz na Empire Bakuba ziliondoka katika sura muziki baada ya vifo vya Franco Lwambo Lwanzo Makiadi  na Pepe Kalle Yampanya.

Anasema ndivyo ilivyoitokea kwa Negro Success baada ya kufariki  kiongozi wao Bavon Marie Marie kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye ikafa.


Mwaka 1974 Assosa alikutana na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa Bendi ya Lipua Lipua, aliyejulikana kwa jina Kiamuangana Mateta Wazo la Mbongo‘Verckies’
Alipofika huko alitakiwa kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka.

Anasema hajui ujasiri uliupata wapi siku hiyo pale alipomtamkia  mmiliki huyo kwamba  hayuko tayari kuimba sauti ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.

Aliungana na wanamuziki wengine wakali akina Chizunga Ricks (Solo), Mutembu  Chibau, Basikita na Kayembe waliokuwa wamemtangulia katika bendi hiyo.

Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya Mombasa, Nikibwe na  Amba.

 Mwaka 1975  bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na wanamuziki. Aliamua kuondoka  na kwenda kujiunga na Bendi ya Les Kamalee.
Akiwa na Les  Kamalee walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na zingine nyingi.

 Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa sifa na kujiamini kupita kiasi. Walilipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao vya  muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo.
Mbwembwe zikazidi na kusababisha kusahau wajibu wao katika kazi. Bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975.

Mwenye bahati habahatishi, Assosa alikaribishwa katika Bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma. Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tannzania.

 
Fuka Fuka ilipoingia Dar es Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga Funga ambazo anazielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa  jiji la Dar es Salaam wakati huo.

 Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga muziki kwa miezi sita  na Chama cha mateksi Dereva cha  Tanzania Transport, Tax and Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park.

Baada ya kumaliza mkataba Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi nchi Kenya na Kampala huko Uganda.

Wakiwa Kampala kwa bahati mbaya  nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani, ikipigana na Tanzania mwaka 1979.
Vita hivyo viliiwaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri  kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia, wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ili hali  kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha yake.

Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita.

Akiwa  Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa muziki wa Tanzania, akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule.

‘Mungu hamtupi mja wake’ Baada ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Assosa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986. Akiwa hapo alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani.

Mwaka huo huo aliamua kuanzisha bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na maadili mema.Bendi  hiyo ilijengewa mizengwe na  kusababisha kasambaratika baada ya muda mfupi.

Assosa alichukuliwa na  bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987.

Alipigia bendi ya Maquis hadi ilipo sambaratika ikipiga kayika ukumbu wa Lang’ata, Kinondoni miaka ya 1990. Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia utanashati wake.

‘Chema chajiuza kibaya chajitembeza’ Mwanamuziki huyu alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi.

Baada ya kumaliza mkataba aliungana na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya Bana Maquis.
Anawataja akina Kasongo Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’,  Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’. Hadi sasa bado yuko na bendi hiyo ya Bana Maquis.
Mwanamuziki Tshimanga anasema amekuwa alikataa mialiko lukuki ya kwenda kuishi na kufanya kazi ya muziki Ulaya na Marekani. Anakiri kuipenda Tanzania kwa vile anaona maisha yake yanamyookea vyema.

Anasema uhakika anao kwamba yeye yuko vizuri kimaisha kuliko ya hao waliopo huko Ulaya na kwengineko. Anabeza kwa kusema kwamba baadhi yao tayari wameanza kurejea Kongo baada ya kushindwa kumudu maisha.


‘Mtoto mzuri’ Assosa ni Baba wa familia ya mke na watoto kadhaa. Hakukosa kusifia muziki wa kizazi kipya kwa kusema kwamba wanafanya vizuri.

Lakini akatoa angalizo kwamba muziki wao wa kutumia CD ni wa muda mfupi  hauwezi kudumu kwa kipindi kirefu,vilevile makosa kubwa kwa vijana hao kutojifunza kupiga Ala za muziki.

Mwisho.

Wednesday, October 31, 2012

TUMSAIDIE MZEE MUHIDINI MAALIM GURUMO Oktoba 2012.



TUMSAIDIE MZEE MUHIDINI  MAALIM  GURUMO
Oktoba 2012.
Kuna wimbo ilioimbwa na bendi ya Mlimani Park ukiitwa ‘Nani kaiona siku’ Wimbo huo mwimbaji Hassan Rehani Bichuka ameuimba kwa uchungu akikemea baadhi ya watu ambao mtu akiwa anaumwa yu Hospitali au nyumbani, ndugu, jamaa na marafiki hawajali kutoa msaada wowote kwa mgonjwa au familia.
Katika wimbo huo Bichuka anasema kwamba pindi mtu huyo anapoaga dunia, siku ya msiba haohao hujitokeza vifua mbele kuchangia vifaa mbalimbali ya vyakula vikiwemo  mchele,unga, maharage,  mafuta, nyama  hata maji ya kunywa huku wakitamba katika magari yao ya  kifahari, na Kamera za Video mazikoni.
Yawezekena baadhi yetu macho yalishindwa kusoma magazeti, masikio yalishindwa kusikiliza redio na kuona Televisheni zetu zilizotujuza  kwamba gwiji la muziki wa dansi hapa chini Muhidini Maalimu  Gurumo anateseka kwa maradhi yanayomsibu muda mrefu sasa na hali yake si nzuri kiafya.
Mwaka huu wa 2012 tulishuhudia vifo vya  aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Haroun Mahundi, Msanii wa tasnia ya filamu Steven Charles Kanumba na aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la wananchi Tanzania(CDF), Jenerali Ernest Mwita Kyaro.Mungu aziweke pema roho zao pahala pema peponi, Amina.
Kifo cha ghafla cha msanii wa filamu Tanzania marehemu Steven Charles Kanumba (28) ambaye  hakuugua japo mafua bali  yadaiwa kwamba aliuliwa na aliyekuwa ‘hawara’ yake ambaye ni  msanii mwenzake maarufu kwa jina la Elizabeth Michael  ‘Lulu’ ambaye hivi sasa yupo kizuizini akisubiri kujibu mashitaka ya mauaji.
Kanumba alikuwa msanii maarufu katika tasnia ya filamu aliyejizolea sifa lukuki alizostahili katika kutunga na kucheza filamu nyingi ndani na nje ya nchi yetu.
Msiba huo ulichukua nafasi kubwa na kuleta taharuki kwa waombolezaji wakati wa mizishi ya msanii huyo.
Kanumba akazikwa kwa heshima zote zilizoandaliwa. Wakati wa maombolezo alisisika Kiongozi  mmoja wa dini akisema  Kwa umati ule wa watu ni mfano tosha kwa mazuri aliyoyafanya Kanumba hapa duniani! Tulitarajia kusikia kauli toka kwa Kiongozi huyo japo ya kugusia au kukemea tabia ya vijana kutofanya uzinzi hapa duniani.
Kama hiyo haitoshi baadhi ya watu waliulinganisha msiba wa Kanumba kama ulivyokuwa wa rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ama wa aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Edward Moringe Sokoine!
Mmoja wa waombolezaji alifika mbali zaidi  alisikika redioni akipendekeza  kwamba eneo hilo la Sinza alipokuwa akiishi Kanumba mtaa huo upewe jina la Kanumba The Great!
Ikumbukwe  huko nyuma Tanzania tumepoteza wasanii wengi wakubwa amabo hadi leo  hawajakubukwa wala kupewa hadhi inayo stahiki.Walikuwepo akina mzee Jongo, mzee Morris Nyunyusa, mzee Issa Matona, Juma Mrisho, Ahmed Kipande, mzee Mayagilo, Salumu Abdallah, Mbaraka Mwinshehe Mwaluka, Patrick Balisdya, Marijani Rajabu, mzee Kipara na wengine wengi. Je, wote hao tutawaenzi kwa lipi?
Mzee Gurumo alizaliwa mwaka 1940, katika  Kijiji cha Masaki Wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani  ni  mwanamuziki mkongwe mwenye historia  ndefu katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki   na hata nchi  zilizo chini ya Jangwa la Sahara. Hivi sasa  ana umri wa zaidi ya miaka 70  ameshatoa mchango mkubwa katika nchi hii kupitia tungo za nyimbo zake zilizojaa ujumbe mzito.
Amefikia hatua ya kuwatamani wanamuziki wa kizazi kipya na taarabu kuwa wana mafanikio makubwa kimaisha kwa vile soko la sasa limewapokea vyema na kujisikia wivu kuwaona vijana wakiendesha maisha mazuri wakiwa na magari ya kifahari wakati yeye akitembea kwa miguu na hata kwenda Hospitali kutibiwa hutumia usafiri wa daladala licha ya muda mrefu alioutumia katika muziki.
Mke wa mzee Gurumo  Pili Said Kitwana alitoa manung’uniko yake kwa kusema kwamba yeye binafsi huwa anaumia roho wanapokuwa kwenye daladala  akimpeleka mumewe  hospitali, abiria  wengine huwashangaa. Lakini anasisitiza kwa kusema wana haki ya kuwashangaa  kufuatia jina kubwa la mume wake Gurumo ambaye kwa hali ya kawaida hakustahili kutumia usafiri wa daladala.
Mama huyo ambaye aliolewa na mzee Gurumo mwaka 1967 na kupata watoto wanne akina Mariamu, Mwalimu, Omar na Mwazani. Anamtaja  Binti yao wa kwanza Mariamu kwamba amefuata nyayo za Baba yake za usanii japo anaimba nyimbo za kizazi kipya.
Mama Pili akasema laiti  kama angelikuwa na uwezo, angemtaka mumewe apumzike na masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kupata mafanikio ya maana.
Kifo cha Kanumba tulishuhudia jinsi nguvu ya serikali ikiongozwa na rais wetu Dkt. Jakaya  Mrisho Kikwete, akifuatia na Waziri mkuu Mizengo Pinda jinsi  walivyoshiriki ipasavyo katika msiba huo ambako walitoa mkono wa pole kwa niaba ya serikari kwa kuubeba msiba huo hadi siku ya mwisho wa mazishi. Mazishi hayo yakaongozwa na makamu wa rais Dkt. Mohammed Ghalib Billar  kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mzee Gurumo mwimbaji mwenye sauti isiyoigika anakiri fani yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na watu wengi  wakiwemo viongozi  mbalimbali hapa nchini  akiwemo rais Jakaya Kikwete anamuelezea kuwa ni mmoja kati ya  marafiki zake.
Mzee Gurumo alisema kitendo cha rais Kikwete kuacha kazi zake akafuatana na mkewe mama Salma kuja kumjulia hali pia kumsaidia katika matibabu wakati alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kulimfariji  sana.
Anasema baada ya kutembelewa na rais Kikwete hapo Muhimbili, huduma zilizofuatia toka kwa  madaktari na manesi zilikuwa ‘Baabu’ kubwa. Hivi sasa amepewa Daktari maalumu wa kuiangalia Afya yake kila aendapo Hospitalini humo.
Mzee Gurumo mwenye uso wenye bashasha licha ya kudhoofu ki- afya, hakukosa kutoa shukurani za dhati kwa mmiliki wa Kampuni ASET mama Asha Baraka  kwa kuandaa onyesho maalumu kwa ajili ya kumchangia pesa.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’ ‘Sikinde’ na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park na Orchestra Safari Sound (OSS). Mwenyewe anasema mitindo hiyo ilitokana  na ngoma za asili ya kabila lake la Kizaramo ambazo mama yake mzazi  alikuwa gwiji wa kuimba na kucheza enzi zake.
Gurumo alianza muziki akiwa na miaka 12 lakini muziki  wa dansi alianza rasmi mwaka 1961 baada ya  kumaliza elimu ya Quraan katika madrasa ambako alikuwa hodari wa kughani na kuimbaji kwa ustadi mkubwa Kaswida.

Bendi yake ya kwanza ilikuwa Kilimanjaro Chacha iliyokuwa ya ikiongozwa na Mkurugenzi  wa bendi anamtaja kwa jina la  Samwel Machango  aidha  anasema alipofika alipokelewa na Salumu Monde ambaye alikuwa mpigaji wa gita la rhythm. Anakiri kwamba wote wawili walimpa ujasiri wa jinsi ya kulitawala Jukwaa na vilevile kwa juhudi zake binafsi alijifunza kupiga Saxaphone. Bendi hiyo iliyokuwa na makao makuu katika ukumbi wa Amana jijini Dar-es-Salaam.
Mzee Gurumo anakumbuka anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba katika bendi yake ya kwanza ukiwamo wa ‘Nilipoingia Bar watu walinionea kijicho’ Anasema  hawezi kuisahau siku ambayo kwa mara ya kwanza alianza kupata pesa aliyoitolea jasho lake ilikuwa ni shilingi  Tano  baada ya onyesho hilo.

Mwaka 1962 Kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz  Ahmed Kipande alimrubuni kwa kumpa Shilingi mia mbili ili ajiunge na bendi yake. Anasema Shilingi mia mbili miaka hiyo ilikuwa na thamani kubwa sana naye alipokea na kukubali kujiunga na Kilwa Jazz.

Mzee Gurumo anatabanaisha kwamba uongozi  wa  Ahmed Kipande, Duncan Njilima na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ hawakumtendea haki iliyostahili na  baada ya  mwaka kupita  akaamua kutafuta bendi nyingine. Alifanikiwa kupata bendi ambayo ilikuwa ndogo kuliko Kilwa jazz  ikiitwa Rufiji jazz mwaka 1963.

Mawaka 1964  Gurumo aliitwa na uongozi wa NUTA Jazz ili akubali kuwa muanzilishi wa bendi hiyo na aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama , Mnenge Ramadhani na Wilfred  Boniface.
Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine zilikuwa Kilimo ni Kazi yetu na Mwenmgele.

Mzee Gurumo pamoja na uzee alionao bado kumbukumbu kichawani zijemjaa. Anakumbuka mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri  John Simon alijiunga na bendi yao ya NUTA  Jazz na anamtaja mpiga Solo Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa NUTA Jazz.

NUTA jazz alikuwa ikimilikiwa   Chama cha Wafanyakzi  ambacho baadaye kikawa JUWATA, OTTU, TFTU hadi TUCTA.
Wakati wakiwa na TUCTA mishahara yao ilikuwa duni kiasi cha kushindwa kijikimu kimaisha, hivyo kwa pamoja wanamuziki hao wakajipanga kwa kununua vyombo vyao vya muziki kidogo kidogo hadi wakatimiza adhma yao ya kujitegemea. Ndipo bendi ya Msondo Ngoma Bendi ilopanzisha  ikilibakiza jina la Msondo kwa kuienzi staili iliyowapa  umaarufu.

Mwaka 1978 Gurumo alihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde ngoma ya Ukae’ na akawa Kiongozi wa bendi hiyo baada ya muda mfupi alitunga nyimbo zikiwemo Baba na Mama na Weekend.
Akiwa na bendi hiyo maisha yake yalianza kubadilika na kuwa mazuri kufuatia malipo na maslahi ya kuridhisha aliyokuwa akilipwa na uongozi wa Mlimani Park.
Anajigamba kwamba maslahi hayo ndiyo uliofikisha kujenga nyumba yake na kunua eneo la shamba maeneo ya Masaki Wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani  na kuwapeleka watoto wake katika Shule nzuri.

Anasisitiza kwa kusema kwamba hatoweza kuwasahau wanamuziki alioshirikiana nao kwa karibu akiwemo aliyekuwa Kiongozi msaidizi  Comas  Tobias Chidumule  ambaye hivi sasa ameokoka na anaimba nyimbo za Injiri, Joseph Bartholomew Mlenga ‘King Spoiler’ na Abdallah Gama
Pamoja na kipato alichokuwa akikipata Mlimani Park Orchestra, ,mwaka 1985 mfanyabiashara maaraufu jijini Dar- es -Salaam  Bwana Hugo Kisima akamshawishi kujiunga katika bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) ambayo ilikuwa ikiongozwa na Supreme  Ndala Kasheba aliyekuwa akipiga katika staili ya ‘Dukuduku’ Gurumo aliingia na staili ya Ndekule.

Alijiunga na OSS akifuatana  na wanamuziki wawili toka  Mlimani Park akina Abel Bartazar na Kassim Rashid ‘Kizunga’wakatoka na nyimbo za ‘Chatu mkali’ na ‘Bwana Kinyogoli’
Bendi ya OTTU ilikuwa bado inamuhitaji kurudi ndipo mwaka 1990 uongozi ulifaulu kumrudisha katika bendi hiyo ambayo tayari  ilikuwa ilikuwa  imebadili jina kuwa  JUWATA.

Enzi za ujana wake ‘Bitozi’ wakati huo, Gurumo alipitia mambo mengi ya ujana ya kuvuta sigara na  alikuwa mywaji wa pombe kupindukia ‘Cha Pombe’ Tabia hiyo ilikifikia kukorofishana na mama yake mzazi aliyetishia hata kumutolea  ‘Radhi’ kama angeendekeza ulevi.
Mkewe Pili Siad Kitwana naye alikwaruzana kila mara juu ya hiyo ya ulevi uliokithiri  na aliwahi kutishia kuomba talaka. Hatimaye mwaka 1982 akaamua kumshinda ‘Shetani’ akaachana na ulevi kwa shinikizo la mama yake na mkewe.
Mzee huyu mwenye historia ndefu ya muziki na maisha yake kwa ujumla, amekuwa kiongozi katika bendi hiyo akisaidiana na Said Mabela, anasema furaha aliyonayo ni kuona pale pamoja na umri wake kuwa mkubwa akiwa na msondo ngoma amekwisha tunga  na kuimba nyimbo nyingi na kuzirekodi katika Studio zikiwemo za ‘Mama nipeleke kwa Baba’ Mwanangu acha Wizi, Wosi wa Baba na nyingine nyingi.
Muhidini Maalimu Gurumo amesema kwamba hana muda mrefu kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya na umri wake kutupa mkono.
Anasema atakapostaafu atajikita katika kuwasaidia vijanaili atimize ndoto zake ni kujenga Chuo cha muziki katika shamba lake  lililopo Masaki wilayani Kisarawe iwapo atapata wafadhili wa kumsapoti adhma yake.
Kama walivyowahi kutamka wanamuziki wengine wa zamani, mzee Gurumo naye amewasisitiza Vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kutumia Ala za muziki ili kuweka kumbukumbu ya kazi zao ziwe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Mzee huyo anasema mazoezi ni muhimu kwa kila binadamu. Yeye hulazimika kujikongoja kwenda kuimba katika bendi yake ya Msondo Ngoma ambapo anasema kuna muda huimba akiwa amekaa kwenye Kiti. Mzee huyu ni muwazi kwa kusema anapo imba na bendi yake pamoja na mazoezi pia huambulia posho inayomuwezesha kujikimu kimaisha.
Gwiji huyu ametunga nyimbo zaidi ya 54 ambazo anasema zinapendwa na watu japo yeye anasema kwamba hazina faida yeyote kwa kuwa hapati hata senti tano ya nyimbo zake hizo. Hivyo anawaomba wadau na  wasamaria wema kumsaidia ili aweze kuzirekodi upya nyimbo hizo ili ziuzwe na yeye aweze kunufaika.
Mzee Gurumo anamalizia kwa kusema kama tuliweza kujitoa katika msiba wa Kanumba na wengineo hivyo anaomba serikali, mawaziri, wabunge na wadau  wote  wamuangalie kwa jicho la  huruma, wamsaidie kufuatia  hali yake kudhoofu na hana msaada mwingine.

 

Add comment



Friday, October 26, 2012

Waliokuwa wanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari (TSJ) wakiwa katika Picha ya pamoja na Waziri wa Habari na Utamaduini Dk.William Shija(watatu kushoto). Wakati wa mahafari Chuoni hapo mwaka 1991 Jijini Dar es Salaam.Wengine toka kusoto ni mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Profesa Geofrey Mmari, Mbunge wa Bumbuli Charles Kagonji, Mkuu wa Chuo Samwilu Mwaffisi na Mmoja wa walimu wa chuo hicho Wallace Mauggo.

MTAMMBUE SHEM IBRAHIM KALENGA.


MTAMMBUE  SHEM  IBRAHIM  KALENGA.


Shem Ibrahim Kalenga (kushoto)akipongezwa na mwanauziki wa Soukous Stars Mayaulla Mayoni

Shem Ibrahim Kalenga ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wenye uwezo wa kucharaza gita huku akiimba kwa wakati mmoja. Shem alitamba sana miaka ya 1970  akiwa na bendi ya Tabora Jazz wana Segere Matata.

Alizaliwa mwaka 1950 eneo la Bangwe mkoani Kigoma na kupata elimu yake katika shule ya msingi Kihezya kati ya mwaka 1957 na 1964.

Alianza kujifunza muziki akiwa mwanafunzi katika shule ya wamissionari na huko ndiko fani hiyo ilianza kuchipua hatimaye mwaka huo huo wa 1964  akajiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz iliyokuwa na maskani yake mjini Kigoma.
Alipoingia Lake Tanganyika Jazz alijifunza Ala za muziki za drums, Kinanda na gita la rhythm, Solo. Besi gita pamoja akiimba.

Alidumu  katika bendi hiyo kwa kipindi cha miaka minane na mwaka 1972 Shem Kalenga aliitwa katika bendi ya Tabora Jazz ambako aliingia kwa kishindo na nyimbo zake alizozitunga akiwa na Lake Jazz na kuanza kuzipiga katika bendi yake mpya.

Nyimbo hizo zilikuwa Dada Asha na Remmy ambazo zilimpa umaarufu na kujulikana kwa haraka na kuwa simulizi katika kila pembe za mji  huo wa Tabora.

Shem alipata ushindani mkubwa baada ya kuwakuta wakali wengine wa kupiga gita akina Kassimu Kaluwona, Athuman Tembo pamoja na Salumu Luzila na  Issa Ramadhan ‘Baba Isaya’ lakini alijitutumua  na kuwa mmoja kati ya wapiga solo gita  bora la katika bendi hiyo.

Mwaka wa 1983 Shem Kalenga aliicha bendi hiyo kwa sababu zake mwenyewe na kuachana na mambo ya muziki kwa muda.Lakini baada ya kuondoka yeye bendi hiyo haikudumu tena na ikapotea katika ramani ya muziki.

Aliondoka Tabora  mwaka 1990 baada ya kuitwa na mfanyabiashara wa jijini Dar  es Salaam Baraka Msilwa ambaye alimuomba ajiunge katika bendi yake ya M.K. Beat iliyokuwa ikipiga katika mtindo wa ‘Tunkunyema’ Bendi hiyo ilikuwa ndugu na ile ya M.K. Group.

Ndani ya M.K.Beat Shem Kalenga  aliwakuta vijana machachari akina Maliki Star, Bwani  Fanfan, Sisco Lunanga na Fungo Shomari. Kwa mshikamano waliokuwa nao  waliweza kuiinua Bendi hiyo vilivyo na kuwa tishio kwa bendi zingine za jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ilisambaratika mwaka 1995 na mwaka uliofuatia alianzisha bendi yake ya Tabora Jazz Star ambayo ina wanamuziki sita na huburudisha katika kumbi mbalimbali za jijini Dar  es Salaam hadi sasa. 

Anasema miaka ya hivi karibuni biashara huria ziliporuhusiwa, Studio nyingi binafsi zilifunguliwa lakini hazina manufaa kwao kufuatia kiwango cha pesa zinazotozwa na Studio hizo  kuwa kubwa mno kiasi cha wao kushindwa kumudu kulipia.

Kalenga anatoa wito kwa Serikali aidha kwa  wafadhili kuwaona kwa jicho la huruma wanamuziki hao wazamani kuwawezasha  kwa vile bado wanao uwezo mkubwa wa kupiga muziki na kutoa elimu kwa jamii pamoja burudani kwa wapenzi kama zamani.

Anajutia umaskini na ufinyu wa fikra uliowakumba wanamuziki wa dansi wa zamani umewafanya kushindwa kujitutumua na kwamba wanchosubiri ni kudra za mwenye mungu, serikali, wafadhili au yeyote atakayeguswa  kutaka kuwakwamua  wakongwe hao kwa kuwapatia vyombo vya muziki.

Shem Kalenga anakumbuka miaka ya nyuma jinsi Serikali ilivyokuwa ikiwasaidia kurekodi nyimbo zao bure katika Studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambapo  gharama yao ilikuwa ni nauli ya kwenda Dar na kurejea  Tabora.

Anaendelea kuifagilia Studio RTD  enzi hizo ilivyokuwa ikichuja nyimbo zao  tofauti na sasa ambapo  Studio nyingi zinarekodi pasipo kuzichuja matokeo yake baadhi ya nyimbo zinazosikika katika vituo vya redio hazina maadili mema kwa jamii.


Mzee mzima Kalenga ambaye sifa zake zimezagaa kila kona Afrika ya Mashariki na Kati anawaasa vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kupiga Ala za muziki badala ya kutembea na CD mkononi.

Mwisho.

Wednesday, October 17, 2012

Mwanamuziki raia wa Sweden mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Dekula Kahanga 'Vumbi' akiwa amepozi na mwandishi wa habari mwandamizi mzee Moshy Kiyungi Mikocheni kwa Warioba jijini Dar es Salaam September 2012.