Monday, November 5, 2012

TSHIMANGA KALALA ASSOSA. ‘Mtoto mzuri’


 Mwimbaji mashuhuri Thsimanga Kalala Assosa akiimba katika moja ya maonyesho alipokuwa Maquidu Zaire.
 
Novemba 05,2012.

Tshimanga  Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za Negro Success, Les Kamalee,  Lipua Lipua na Fuka Fuka.

Assosa ni mwenye  kipaji cha kutunga na kuimba  nyimbo za muziki dansi pia ni  kiongozi wa Bendi ya Bana Maquis iliyopo jijini Dar es  Salaam.

Kwa hali isiyokuwa ya kawaida, Tshimanga Assosa amekuwa akikataa Ofa lukuki za kwenda ‘kula maisha’ Ulaya na Marekani na kuamua kuishi katika Jijini la Dar es Salaam hapa Tanzania.

Akiwa katika bendi hizo alishirikiana wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na  Kiamuangana Mateta  Wazola Mbongo ‘ Verckies’

Historia ya maisha yake inaanzia siku aliyoiona dunia baada ya kuzaliwa katika mji wa Kamina uliopo Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Aprili 04, 1949.
Alipata elimu ya Sekondari katika Shule iliyojulikana kama Charles Ruangwa hapo Kamina.

 Akielezea  historia hiyo Tshimanga Assosa anasema alianza kuimba akiwa bado mdogo na kwamba aliyejipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina ambako maPadri walimsaidia kumfundisha muziki.

Pamoja na juhudi zake hizo, Baba yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye  ajitumbukize katika muziki na kumtaka afuate masomo yake shuleni.

Baada kumaliza kidato cha nne, Baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Assosa Muziki ulikuwa ndani ya damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa  akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo hapo Kamina ya Super Gabby.

Anasema mazoezi ya hiyo yalimtia hamasa kubwa ya kupenda muziki. Anaeleza kwamba siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa  kuimba katika bendi hiyo. Assosa alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla Baba yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko.

 Waswahili wanasema ‘Sikio la  kufa halisikii dawa’ Baba yake mwisho wake alikubali ombi la mwanaye  baada ya kubaini kuwa hashikiki wala habadiliki kitabia, akamruhusu afanye muziki aupendao.

 Mwaka 1969  Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana na mwanamuziki Bavon Marie Marie  na akampeleka kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo aliyejulikana kama Didi Kalombo.
Assosa aliitumia vyema nafasi hiyo ya kujaribiwa sauti. Mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika  bendi hiyo.

Assosa anazikumbuka changamoto alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti  na wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo)
Anasema sauti yake ndiyo iliyomuokoa na kupewa heshima  kama wanamuziki wengine.

Tshimanga Kalala Assosa anafafanua kwamba kufa kwa Kiongozi ‘Star’ yeyote katika bendi, mara nyingi husababisha bendi aliyoiacha kuteteleka hatimaye kufa. Akitolea mifano  ya Bendi za T.P.OK. Jazz na Empire Bakuba ziliondoka katika sura muziki baada ya vifo vya Franco Lwambo Lwanzo Makiadi  na Pepe Kalle Yampanya.

Anasema ndivyo ilivyoitokea kwa Negro Success baada ya kufariki  kiongozi wao Bavon Marie Marie kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye ikafa.


Mwaka 1974 Assosa alikutana na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa Bendi ya Lipua Lipua, aliyejulikana kwa jina Kiamuangana Mateta Wazo la Mbongo‘Verckies’
Alipofika huko alitakiwa kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka.

Anasema hajui ujasiri uliupata wapi siku hiyo pale alipomtamkia  mmiliki huyo kwamba  hayuko tayari kuimba sauti ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.

Aliungana na wanamuziki wengine wakali akina Chizunga Ricks (Solo), Mutembu  Chibau, Basikita na Kayembe waliokuwa wamemtangulia katika bendi hiyo.

Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya Mombasa, Nikibwe na  Amba.

 Mwaka 1975  bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na wanamuziki. Aliamua kuondoka  na kwenda kujiunga na Bendi ya Les Kamalee.
Akiwa na Les  Kamalee walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na zingine nyingi.

 Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa sifa na kujiamini kupita kiasi. Walilipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao vya  muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo.
Mbwembwe zikazidi na kusababisha kusahau wajibu wao katika kazi. Bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975.

Mwenye bahati habahatishi, Assosa alikaribishwa katika Bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma. Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tannzania.

 
Fuka Fuka ilipoingia Dar es Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga Funga ambazo anazielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa  jiji la Dar es Salaam wakati huo.

 Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga muziki kwa miezi sita  na Chama cha mateksi Dereva cha  Tanzania Transport, Tax and Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park.

Baada ya kumaliza mkataba Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi nchi Kenya na Kampala huko Uganda.

Wakiwa Kampala kwa bahati mbaya  nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani, ikipigana na Tanzania mwaka 1979.
Vita hivyo viliiwaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri  kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia, wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ili hali  kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha yake.

Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita.

Akiwa  Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa muziki wa Tanzania, akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule.

‘Mungu hamtupi mja wake’ Baada ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Assosa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986. Akiwa hapo alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani.

Mwaka huo huo aliamua kuanzisha bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na maadili mema.Bendi  hiyo ilijengewa mizengwe na  kusababisha kasambaratika baada ya muda mfupi.

Assosa alichukuliwa na  bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987.

Alipigia bendi ya Maquis hadi ilipo sambaratika ikipiga kayika ukumbu wa Lang’ata, Kinondoni miaka ya 1990. Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia utanashati wake.

‘Chema chajiuza kibaya chajitembeza’ Mwanamuziki huyu alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi.

Baada ya kumaliza mkataba aliungana na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya Bana Maquis.
Anawataja akina Kasongo Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’,  Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’. Hadi sasa bado yuko na bendi hiyo ya Bana Maquis.
Mwanamuziki Tshimanga anasema amekuwa alikataa mialiko lukuki ya kwenda kuishi na kufanya kazi ya muziki Ulaya na Marekani. Anakiri kuipenda Tanzania kwa vile anaona maisha yake yanamyookea vyema.

Anasema uhakika anao kwamba yeye yuko vizuri kimaisha kuliko ya hao waliopo huko Ulaya na kwengineko. Anabeza kwa kusema kwamba baadhi yao tayari wameanza kurejea Kongo baada ya kushindwa kumudu maisha.


‘Mtoto mzuri’ Assosa ni Baba wa familia ya mke na watoto kadhaa. Hakukosa kusifia muziki wa kizazi kipya kwa kusema kwamba wanafanya vizuri.

Lakini akatoa angalizo kwamba muziki wao wa kutumia CD ni wa muda mfupi  hauwezi kudumu kwa kipindi kirefu,vilevile makosa kubwa kwa vijana hao kutojifunza kupiga Ala za muziki.

Mwisho.