Wednesday, January 23, 2013

TABORA JAZZ ILIVYOTIKISA MJI WA TABORA






TABORA JAZZ   ‘Wana Segere Matata’ ni bendi pekee ya muziki wa dansi  inayojulikana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kauli hiyo nzito ilitolewa na mkongwe wa muziki wa dansi toka Jamhuri  na Kidemokrasia ya Congo, Tabu Ley  Rochereau.

Akiwa ziarani hapa Tanzania, Tabu Ley aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari katika hoteli Kilimanjaro. Moja kati ya  maswali aliyoulizwa ni kutaka kufahamu ni bendi gani hapa Tanzania wanayoijua huko kwao DRC. Tabu Ley pasipo kupepesa macho, alikiri kwa kujibu kwamba  ni Tabora Jazz pekee ndiyo inayojulikana huko.

Tabora Jazz ni bendi kongwe iliyoanzishwa mwaka 1954, ambao katika historia ya Tanzania ndiyo mwaka ambao chama cha TANU kilianzishwa.

Bendi hiyo ilikuwa  ikiongozwa na waanzilishi akina  Hamis Ali Songo na Mlekwa Selemani, ikiwa na makazi yake mjini Tabora ikipiga na kutoa burudani murua za muziki wa dansi katika kumbi za  Lumumba kwenye kona ya mitaa ya Usagara na Rufita ambako ndiko yalikuwa makao makuu yake. Pia walikuwa wakipiga katika Baa za Bizeta, Maua na nje ya mji wakialikwa.

Miaka ya nyuma Tabora Jazz ilikuwa na upinzani mkubwa na bendi ya Western Jazz ya jijini Dar es Salaam. Upinzani huo ulijiri baada ya Bendi ya Western Jazz kukwapua kwa nyakati tofauti nguli wawili toka Tabora Jazz., kwa ambao walihamisha ‘melody’ yao kuipeleka huko.

Wanamuziki hao walikuwa  akina Wema Abdallah na Rashidi Hanzuruni ambao walikuwa mahiri kwa kulicharaza gitaa la solo,ambao walihamisha ‘melody’ kuzipeleka Western Jazz.


Nyimbo nyingi za bendi hiyo zilipigwa mno katika  kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kusikika  sehemu kubwa Afrika ya Mashariki na Kati.

Huko nchini Rwanda kulikuwepo redio Rwanda iliyokuwa na kipindi cha muziki nyakati za jioni kikiendeshwa na mtangazaji Kabendera Shinani, ambaye alikuwa akizipiga nyimbo za Tabora Jazz kila mara. Redio hiyo ilikuwa ikisikika hapa nchini maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera (Ziwa Magharibi) wakati huo.

‘Wana Segere matata’ waliwika sana miongoni mwa bendi kubwa hapa nchini zikiwemo Morogoro Jazz, Cuban Marimba, Western Jazz, NUTA Jazz, Dar. Jazz, Kilwa Jazz, Urafiki Jazz, Jamhuri Jazz na nyingine nyingi.

Mji wa Tabora wakati huo ulikuwa na ushindani mkubwa katika muziki kati ya Tabora Jazz na bendi zingine zilizokuwepo wakati huo za Kiko Kids iliyokuwa ikiongozwa na Salimu Zahoro na Nyanyembe Jazz iliyoibuka na kibao chake cha ‘Rangi ya Chungwa’ wimbo ambao hadi sasa bado unarindima kwenye vituo vingi vya redio na kumbi nyingi  za burudani hapa nchini.
Pia mji wa Tabora enzi hizo kulikuwa na umkumbi mkubwa wa Disco uliokuwa ukijulikana kwa jina la ‘Mwana Isungu’ uliokuwa ikiteka kundi kubwa la  vijana wa mji huo kwa kuporomosha muziki maridhawa, zikiwemo nyimbo za Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz.

Kama nilivyokudokeza hapo awali kwamba bendi hiyo ilianzaishwa kabla ya  Tanganyika kupata Uhuru, hivyo iliendeleza mfumo wa kikoloni. Mfano mmoja ni kwamba katika miaka ya 1960 ilikuwa ni marufuku kwa mpenzi au shabiki kuingia ukumbini kucheza muziki pasipo ‘kunyonga’ Tai shingoni, licha ya pesa zake. Hii ilikuwa ni moja ya njia ya kuzingatia utanashati na nidhamu  kwa ujumla.

Bendi hiyo ilipiga katika mitindo ya  Segere matata, Segua Segua, na Mambo Milekana, ikiwazingua wapenzi wa muziki mjini humo.
Miaka hiyo Tabora Jazz alitoka na nyimbo zao ngingi zikiwemo za Usijifanye mwewe, Mariam mpenzi, Zabibu No.2, Anna, Regina, Mambo Mileka, Tucheza Segere, Dada Mwantumu, Serafina,Tamaa yako, Alhamdulilah, Nashukuru sana, na Dada Asha.

Zingine ni pamoja na Zabibu, Halima, Dada Helena, Lucie, Farida na Dada Mwantumu.
Kufuatia ushindani mkubwa uliokuwepo mjini humo  kati yake na Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, Tabora Jazz ilifumua vibao ingine vikali  vya Chakula kwa Jirani, Mapenzi hayana mganga, Mambo Mileka, Ujana una mwisho. Salima, Dada Remmy, Tucheze Segere na  Rukia wajidanganya.

‘Segere matata’ wakati huo ilikuwa na mashabiki waliokubuhu. Kwa wakazi wa Tabora mjini hawawezi kumsahau shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mzee Segua’ ambaye alikuwa hakosi onyesho lolote la bendi hiyo akicheza ‘Segua Segua, mtindo aliokuwa aikiumudu hadi kufikia kupachikwa jina la ‘Mzee Segua’

Alikuwa ni Mzee mwenye vituko ukumbini, akiwa na mfanyakazi katika Ofisi moja ya serikali mjini humo  kama dereva. ‘Mzee Segua kwa mapenzi yaliyopitiliza mbele ya tabora Jazz, alidiriki kukakataa uhamisho kwenda Wilaya ya Urambo, akitoa sharti ili aende huko basi Bendi hiyo nayo ihamishiwe Urambo. Yaelezwa kwamba baadaye alifukuzwa kazi.


Kikosi kamili cha wanamuziki waliokuwa wakiunda kikosi kamili cha bendi hiyo kilikuwa cha akina  Athumani Tembo kwa upande wa gitaa la Soloakisaidiana na  Shem Ibrahim Karenga aliyekuwa akipiga gitaa la solo, akitunga na kuimba.  Salumu Luzira  alikuwa akiliungurumisha gitaa zito besi na  ugeweza kulilingalinisha na alivyokuwa akipiga Suleiman Mwanyiro ama Lofombo wa  Empire Bakuba.

Wengine katika safu hiyo walikuwa  Kassim Kaluwona, aliyekuwa akilicharaza gitaa la rhythm akisaidiana na  Issa Ramadhani ‘Baba Isaya’  Waimbaji walikuwa ni akina Ramadhani Hamis Nguligwa, Ismail Mwangoko, na Msafiri  Haruob, ambaye baadaye alijiunga na Mwenge Jazz ya Jijini Dar es Salaam.

Kuna msemo wa waswahili usemao kwamba ‘ Vizuri huigwa na Vitamu huonjwa’  Msemo huo ulijidhihirisha wazi kwa Bendi kubwa toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Soukos Stars, ambayo iliiba nyimbo za Dada Asha wa Tabora Jazz na Vigeregere wa Western Jazz.


Kwa umahiri mkubwa wa bendi hiyo ya  Soukous Stars ilitoka na mseto wa nyimbo nyingi zikiwemo za Dada Asha na Vigeregere  katika album moja ya ‘ Nairobi by Night’

Shem Karenga alijaribu kufuatilia  haki miliki yake pasipo mafanikio kwa kuwa nchi yetu ilikuwa bado haijatunga sheria ya haki miliki.

Tabora Jazz iliposambaratika mwaka 1980, sanjari na Bendi za Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, nazo zilienda mrama na baadaye kuondoka katika taswira ya muziki hapa nchini.
Kutoweka kwa Bendi hizo kuliwaacha wapenzi wa muziki wa dansi wa mji huo ambao waliupachika jina la ‘Mboka’ wakijawa na simanzi tele, licha ya kuanzishwa kwa bendi nyingine ya Tabora Jazz ‘Sensema Malunde’ ambayo imeibuka miaka ya karibuni ikiwapa burudani.


Picha zinafyatia....

Thursday, January 3, 2013

MWIMBAJI MASHUHURI TSHIMANGA ASSOSA





Novemba 05,2012.

Tshimanga  Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za Negro Success, Les Kamalee,  Lipua Lipua na Fuka Fuka.

Assosa ni mwenye  kipaji cha kutunga na kuimba  nyimbo za muziki dansi pia ni  kiongozi wa Bendi ya Bana Maquis iliyopo jijini Dar es  Salaam.

Kwa hali isiyokuwa ya kawaida, Tshimanga Assosa amekuwa akikataa ofa lukuki za kwenda ‘kula maisha’ Ulaya na Marekani na kuamua kuishi katika Jijini la Dar es Salaam hapa Tanzania.

Akiwa katika bendi hizo alishirikiana wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na  Kiamuangana Mateta  Wazola Mbongo ‘ Verckies’

Historia ya maisha yake inaanzia siku aliyoiona dunia baada ya kuzaliwa katika mji wa Kamina uliopo Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Aprili 04, 1949.
Alipata elimu ya Sekondari katika Shule iliyojulikana kama Charles Ruangwa hapo Kamina.

 Akielezea  historia hiyo Tshimanga Assosa anasema alianza kuimba akiwa bado mdogo na kwamba aliyejipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina ambako maPadri walimsaidia kumfundisha muziki.

Pamoja na juhudi zake hizo, Baba yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye  ajitumbukize katika muziki na kumtaka afuate masomo yake shuleni.

Baada kumaliza kidato cha nne, Baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Assosa Muziki ulikuwa ndani ya damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa  akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo hapo Kamina ya Super Gabby.

Anasema mazoezi ya hiyo yalimtia hamasa kubwa ya kupenda muziki. Anaeleza kwamba siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa  kuimba katika bendi hiyo. Assosa alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla Baba yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko.

 Waswahili wanasema ‘Sikio la  kufa halisikii dawa’ Baba yake mwisho wake alikubali ombi la mwanaye  baada ya kubaini kuwa hashikiki wala habadiliki kitabia, akamruhusu afanye muziki aupendao.

 Mwaka 1969  Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana na mwanamuziki Bavon Marie Marie  na akampeleka kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo aliyejulikana kama Didi Kalombo.
Assosa aliitumia vyema nafasi hiyo ya kujaribiwa sauti. Mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika  bendi hiyo.

Assosa anazikumbuka changamoto alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti  na wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo)
Anasema sauti yake ndiyo iliyomuokoa na kupewa heshima  kama wanamuziki wengine.

Tshimanga Kalala Assosa anafafanua kwamba kufa kwa Kiongozi ‘Star’ yeyote katika bendi, mara nyingi husababisha bendi aliyoiacha kuteteleka hatimaye kufa. Akitolea mifano  ya Bendi za T.P.OK. Jazz na Empire Bakuba ziliondoka katika sura muziki baada ya vifo vya Franco Lwambo Lwanzo Makiadi  na Pepe Kalle Yampanya.

Anasema ndivyo ilivyoitokea kwa Negro Success baada ya kufariki  kiongozi wao Bavon Marie Marie kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye ikafa.


Mwaka 1974 Assosa alikutana na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa Bendi ya Lipua Lipua, aliyejulikana kwa jina Kiamuangana Mateta Wazo la Mbongo‘Verckies’
Alipofika huko alitakiwa kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka.

Anasema hajui ujasiri uliupata wapi siku hiyo pale alipomtamkia  mmiliki huyo kwamba  hayuko tayari kuimba sauti ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.

Aliungana na wanamuziki wengine wakali akina Chizunga Ricks (Solo), Mutembu  Chibau, Basikita na Kayembe waliokuwa wamemtangulia katika bendi hiyo.

Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya Mombasa, Nikibwe na  Amba.

 Mwaka 1975  bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na wanamuziki. Aliamua kuondoka  na kwenda kujiunga na Bendi ya Les Kamalee.
Akiwa na Les  Kamalee walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na zingine nyingi.

 Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa sifa na kujiamini kupita kiasi. Walilipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao vya  muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo.
Mbwembwe zikazidi na kusababisha kusahau wajibu wao katika kazi. Bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975.

Mwenye bahati habahatishi, Assosa alikaribishwa katika Bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma. Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tannzania.


Fuka Fuka ilipoingia Dar es Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga Funga ambazo anazielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa  jiji la Dar es Salaam wakati huo.

 Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga muziki kwa miezi sita  na Chama cha mateksi Dereva cha  Tanzania Transport, Tax and Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park.

Baada ya kumaliza mkataba Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi nchi Kenya na Kampala huko Uganda.

Wakiwa Kampala kwa bahati mbaya  nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani, ikipigana na Tanzania mwaka 1979.
Vita hivyo viliiwaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri  kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia, wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ili hali  kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha yake.

Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita.

Akiwa  Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa muziki wa Tanzania, akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule.

‘Mungu hamtupi mja wake’ Baada ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Assosa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986. Akiwa hapo alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani.

Mwaka huo huo aliamua kuanzisha bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na maadili mema.Bendi  hiyo ilijengewa mizengwe na  kusababisha kasambaratika baada ya muda mfupi.

Assosa alichukuliwa na  bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987.

Alipigia bendi ya Maquis hadi ilipo sambaratika ikipiga kayika ukumbu wa Lang’ata, Kinondoni miaka ya 1990. Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia utanashati wake.

‘Chema chajiuza kibaya chajitembeza’ Mwanamuziki huyu alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi.

Baada ya kumaliza mkataba aliungana na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya Bana Maquis.
Anawataja akina Kasongo Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’,  Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’. Hadi sasa bado yuko na bendi hiyo ya Bana Maquis.
Mwanamuziki Tshimanga anasema amekuwa alikataa mialiko lukuki ya kwenda kuishi na kufanya kazi ya muziki Ulaya na Marekani. Anakiri kuipenda Tanzania kwa vile anaona maisha yake yanamyookea vyema.

Anasema uhakika anao kwamba yeye yuko vizuri kimaisha kuliko ya hao waliopo huko Ulaya na kwengineko. Anabeza kwa kusema kwamba baadhi yao tayari wameanza kurejea Kongo baada ya kushindwa kumudu maisha.


‘Mtoto mzuri’ Assosa ni Baba wa familia ya mke na watoto kadhaa. Hakukosa kusifia muziki wa kizazi kipya kwa kusema kwamba wanafanya vizuri.

Lakini akatoa angalizo kwamba muziki wao wa kutumia CD ni wa muda mfupi  hauwezi kudumu kwa kipindi kirefu,vilevile makosa kubwa kwa vijana hao kutojifunza kupiga Ala za muziki.

Mwisho.


Posted by KIYUNGI at 6:01 AM
Email ThisBlogThis!Share to TwitterShare to Facebook
No comments:

Post a Comment

Newer Post Older Post Home
Subscribe to: Post Comments (Atom)
Followers
About Me

KIYUNGI

View my complete profile
Blog Archive

    ►  2013 (1)

    ▼  2012 (7)
        ▼  November (1)
            Mwa<!--[if gte mso 9]> Normal 0 false ...

MKONGWE SHEM KARENGA

MTAMMBUE MKONGWE SHEM  IBRAHIM  KARENGA.

 Shem Ibrahim Karenga akiwa katika picha na mpigaji wa gita la rythm , wa Soukous Stars, Lokassa ya Mbongo(kushoto) walipokutana jijini Dar es Salaam. 


Na Moshy Kiyungi.

SHEM IBRAHIM KARENGA ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wenye uwezo wa kucharaza gita huku akiimba kwa wakati mmoja. Shem alitamba sana miaka ya 1970  akiwa na bendi ya Tabora Jazz wana Segere Matata.

Alizaliwa mwaka 1950 eneo la Bangwe mkoani Kigoma na kupata elimu yake katika shule ya msingi Kihezya kati ya mwaka 1957 na 1964.

Alianza kujifunza muziki akiwa mwanafunzi katika shule ya wamissionari na huko ndiko fani hiyo ilianza kuchipua hatimaye mwaka huo huo wa 1964  akajiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz iliyokuwa na maskani yake mjini Kigoma.
Alipoingia Lake Tanganyika Jazz alijifunza Ala za muziki za drums, Kinanda na gita la rhythm, Solo. Besi gita pamoja akiimba.

Alidumu  katika bendi hiyo kwa kipindi cha miaka minane na mwaka 1972 Shem Kalenga aliitwa katika bendi ya Tabora Jazz ambako aliingia kwa kishindo na nyimbo zake alizozitunga akiwa na Lake Jazz na kuanza kuzipiga katika bendi yake mpya.

Nyimbo hizo zilikuwa Dada Asha na Remmy ambazo zilimpa umaarufu na kujulikana kwa haraka na kuwa simulizi katika kila pembe za mji  huo wa Tabora.

Shem alipata ushindani mkubwa baada ya kuwakuta wakali wengine wa kupiga gita akina Kassimu Kaluwona, Athuman Tembo pamoja na Salumu Luzila na  Issa Ramadhan ‘Baba Isaya’ lakini alijitutumua  na kuwa mmoja kati ya wapiga solo gita  bora la katika bendi hiyo.

Mwaka wa 1983 Shem Kalenga aliicha bendi hiyo kwa sababu zake mwenyewe na kuachana na mambo ya muziki kwa muda.Lakini baada ya kuondoka yeye bendi hiyo haikudumu tena na ikapotea katika ramani ya muziki.

Aliondoka Tabora  mwaka 1990  baada ya kuitwa na mfanyabiashara wa jijini Dar  es Salaam Baraka Msilwa ambaye alimuomba ajiunge katika bendi yake ya M.K. Beat iliyokuwa ikipiga katika mtindo wa ‘Tunkunyema’ Bendi hiyo ilikuwa ndugu na ile ya M.K. Group.

Ndani ya M.K.Beat Shem Kalenga  aliwakuta vijana machachari akina Maliki Star, Bwani  Fanfan, Sisco Lunanga na Fungo Shomari. Kwa mshikamano waliokuwa nao  waliweza kuiinua Bendi hiyo vilivyo na kuwa tishio kwa bendi zingine za jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ilisambaratika mwaka 1995 na mwaka uliofuatia alianzisha bendi yake ya Tabora Jazz Star ambayo ina wanamuziki sita na huburudisha katika kumbi mbalimbali za jijini Dar  es Salaam hadi sasa. 

Anasema miaka ya hivi karibuni biashara huria ziliporuhusiwa, Studio nyingi binafsi zilifunguliwa lakini hazina manufaa kwao kufuatia kiwango cha pesa zinazotozwa na Studio hizo  kuwa kubwa mno kiasi cha wao kushindwa kumudu kulipia.

Kalenga anatoa wito kwa Serikali aidha kwa  wafadhili kuwaona kwa jicho la huruma wanamuziki hao wazamani kuwawezasha  kwa vile bado wanao uwezo mkubwa wa kupiga muziki na kutoa elimu kwa jamii pamoja burudani kwa wapenzi kama zamani.

Anajutia umaskini na ufinyu wa fikra uliowakumba wanamuziki wa dansi wa zamani umewafanya kushindwa kujitutumua na kwamba wanchosubiri ni kudra za mwenye mungu, serikali, wafadhili au yeyote atakayeguswa  kutaka kuwakwamua  wakongwe hao kwa kuwapatia vyombo vya muziki.

Shem Kalenga anakumbuka miaka ya nyuma jinsi Serikali ilivyokuwa ikiwasaidia kurekodi nyimbo zao bure katika Studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambapo  gharama yao ilikuwa ni nauli ya kwenda Dar na kurejea  Tabora.

Anaendelea kuifagilia Studio RTD  enzi hizo ilivyokuwa ikichuja nyimbo zao  tofauti na sasa ambapo  Studio nyingi zinarekodi pasipo kuzichuja matokeo yake baadhi ya nyimbo zinazosikika katika vituo vya redio hazina maadili mema kwa jamii.
Mzee mzima Kalenga ambaye sifa zake zimezagaa kila kona Afrika ya Mashariki na Kati anawaasa vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kupiga Ala za muziki badala ya kutembea na CD mkononi. 

PICHA ZAIDI.
MTUNZI NA MWIMBAJI WA SOUKOUS STARS, MAYAULA MAYONI, AKIMPONGEZA SHEM KARENGA{kushoto} KWA UHODARI WA KULIKUNG'UTA SOLO,JIJINI DAR ES SALAAM.


KANKU KELLY, ALIYEFUKUZWA SHULE KWA SABABU YA KUPENDA MUZIKI




NKASHAMA KANKU KELLY ni mpigaji mashuhuri trampeti mwenye historia ya ndefu katika muziki.
Ni mwanamuziki aliyewahi kushikana mikono na viongozi wakubwa wanaoheshimika  duniani kote, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Nelson Mandela.
Kanku ambaye alifukuzwa shule kwa ajili ya muziki, jina lake halisi ni Nkashama Luis Polycarp, alizaliwa Januari 20, 1958, katika mji wa Kananga Mkoa wa Kasai, Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kanku ambaye aliingia nchini Tanzania akiwa kinda ‘Under Twenty’ alikuwa kivutio kikubwa kwenye safu ya wapulizaji wa trumpet katika bendi iliyokuwa tishio miaka ya 1970 hadi 1990 ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa White House,Ubungo jijini Dar es Salaam.

Baba yake mzee Chasuma Leonard alikuwa Daktari wa binadamu na mama yake Chibwabwa Kayipu, alikuwa mfanyabiashara katika mji huo wa Kananga.

Kelly alipata elimu ya msingi katika shule ya Kamilabi ambayo miongoni mwa masomo yaliyokuwa yakifundishwa somo la muziki lilikuwemo. Baadaye aliendelea na masomo ya juu  katika shule ya Sekondari ya Lyceede Kelekele, ambako aliishia kidato cha tano kwa kufukuzwa shule baada ya kufumwa na mwalimu akiandika  wimbo wa Nyboma Mwandido darasani mwaka 1973.

Akiwa shule ya msingi walifundishwa somo la muziki na yeye alikuwa akifanya vizuri sana na kuwa mmoja kati ya wanafunzi bora wa somo hilo.

Akifafanaua juu ya kufukuzwa shule, Kelly anasema “Nilikuwa anapenda muziki kupita kiasi, nikiwa darasani mwalimu alinikuta nikiandika wimbo wa ‘Amba’ uliotungwa na Nyboma Mwandido ndipo nikafukuzwa shule”

Kanku anasema baada ya kufukuzwa shule mwaka 1974, alihitajika kujiunga na jeshi la nchi hiyo katika kitengo cha muziki wa Brass band, lakini akakataa akiwa na dhamira kubwa kuwa mwanamuziki masuhuri.
Anajuza kuwa jamaa zake aliokuwa nao darasani asilimia tisini  walipelekwa jeshini kupiga muziki wa Brass band.

Katika kujitafutia maisha mwaka 1975  Nkashama Kelly aliamua kwenda mji wa Katanga uliopo jimbo la Shaba, huko alijiunga katika bendi ya Safari Nkoi iliyokuwa na wanamuziki mahiri akina Ndala Kasheba na Baziano Bwetii.

Nyota yake  ilianza kutoa nuru njema, kwani mwezi Febrauri 1977 baadhi ya wanamuziki Kongo walifuatwa na Chibangu Katai ‘mzee Pual’ kuja Tanzania kujiunga na bendi ya Maquis du Zaire.

Anamtaja Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Mutombo Sozzy (drums), Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’(besi gita)  Ngalula Chandanda (stage shoo) pamoja na yeye Kanku ndiyo kwa pamoja  walichukuliwa kuja Tanzania waka huo.

 Alipofika Maquis du Zaire jijini Dar es Salaam, aliungana na wapulizaji wa trumpet wengine akina Mwema Mudjanga ‘mzee Chekecha’, Mino wa Mwamba ‘mzee Tito, Mpoyo Kalenga, Kaumba Kalemba  na Ngenda Kalonga.
Safu hiyo ilikuwa burudani tosha katika ukumbi wa White House wakati huo kwa jinsi walivyokuwa wakimudu kulimiliki jukwaa kwa uchezaji wao.
Kanku Kelly anatamka kwamba mwaka 1978 ilikuwa kama ‘bahati ya mtende kuotea Jangwani’ anasema hatakuja kuisahau siku ile  aliyopelekwa kukutana na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam.

Anakumbuka alishikana mikono na rais wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Nyerere na  alimuuliza “unatoka Kongo ya Lumumba”? Akiwa na hofu isiyokuwa na sababu, Kelly alijibu ‘ndiyo’

Maisha ni kutafuta. Ndivyo alivyosema Kanku kwamba mwanzoni wa mwaka 1981 alichomoka na kwenda kujiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS). Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima.
Katika kipindi  cha mwaka mmoja wa 1981 aliondoka Orchestra Safari Sound(OSS) kwenda kujiunga katika bendi ya mzee Makassy ambako huko nako hakudumu kipindi kirefu na alirudi tena OSS.

Mwaka 1982 Kanku alichupa hadi Nairobi nchini Kenya, na akajiunga na bendi ya Orchestra Virunga iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki mkongwe Samba Mapangala, ambako alidumu na bendi hiyo kwa takriban miaka miwili.

Akiwa huko Kenya mwaka 1984 Nkashama Kanku Kelly akiwa na wanamuziki wenzake, waliamua  kuanzisha bendi yao ya Orchestra Vundumuna ikiwa na wanamuziki nguli akina Sammy Kasule (kuimba), Nsilu wa Bansilu ‘Manicho’(gita), Tabu Ngongo(sax), na  Tabu Fratal (gita/drums).
Wengine walikuwa akina Munamba Jean(keyboard)na Botanga Mofrank Bijing, ambaye alikuwa kiongozi wa bendi na mpiga keyboard.
Anamtaja Mofank kuwa ndiye aliyekuwa chanzo cha bendi hiyo kupata mikataba wa kupiga muziki nchini Japan kwa  kupitia nafasi yake ya kuoa mwanamke wa nchi hiyo.

Kanku Kelly ni Baba wa familiya. Alifunga ndoa ya kiserikali mwaka 1987 na  Bi. Mwajuma Kibwana ambaye ni mtanzania, katika jiji la Nairobi huko Kenya.

Katika maisha yao ya ndoa wamefanikiwa kupata mabinti wawili Agnes Chichi Kelly (26), anayesoma katika Chuo Kikuu nchini Malaysia na mdogo wake Lucy Kelly (20) ambaye anamuelezea kwamba amefuata nyayo zake  katika muziki.

Baada ya kuachiwa huru mzee Nelson   Mandela  toka gerezani, mwaka 1990 alifanya ziara ya kuizunguka dunia. Katika ziara yake hiyo alifika nchini Japan ambako bendi yao ya Vundumuna ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za mapokezi ya shujaa huyo kwenye uwanja uliokuwa umefurika kumpokea.

Anasema mzee Mandela alivutiwa na wanamuziki wa Vundumuna ambao ni weusi. Mandela alipanda kwenye jukwaa lao kuja kuwashika mikono huku akiwauliza wanatoka nchi gani.

 Alipomfika yeye, akamuuliza swali lilelile kama aliloulizwa na Mwalimu Nyerere kuwa natoka Zaire ya Lumumba? “ Sitoshau maishani mwangu  siku hiyo” anasema Kanku.

Vundumuna ilifanya safari zaidi ya mara kumi kati ya miaka ya 1987 na 1991 kisha wakatengenezewa vikwazo vya hati yakufanya kazi hapo Japan (working permit), na walirudi nyumbani na ndiyo ikawa mwisho wa bendi hiyo.

Kanku Kelly akiwa bado kijana kwa wakati huo alikuwa ni mwenye ujasiri usiyetaka kushindwa kitu. Mei 15, 1992 aliingiwa na ujasiri wa kusimama kama yeye na  kuazisha bendi yake ya  The Kilimanjaro Connection.

Alifanikiwa kuwapata wanamziki mahiri na makini akina Asia Darwesh ‘super mama’ aliyekuwa mbonyezaji wa kinanda, Mafumu Bilari ‘Bombenga’ kwenye  Saxophone,  Andy Swebe kwa upande wa gita zito la besi, Burahan Muba, aliyekuwa mpiga gita la solo na Shomari Abdalah akizicharaza drums.

The Kilimanajaro Connection Band imekuwa ikipata mikataba ya kupiga muziki katika nchi mbalimbali za Singapore, Malaysia, Thailand na Oman.
 Ni usimamizi makini wa Kanku Kelly umeifikisha bendi hiyo kupata mafanikio makubwa pia bendi hiyo imekubalika sana nchini Malaysia.

Mwanamuziki huyo Kanku Kelly Nkashama ameviomba vyombo vya habari hususani vya utangazaji kuzicheza na kuzipiga nyimbo zao za zamani katika redio na Luninga ambazo kwake yeye anaziona kama ni ‘Lulu’ inayotoweka.

Anasema si vyema kubeza vya zamani ambavyo ndivyo vilivyotufikisha hapa tulipo.  Anawaasa vijana wanaopenda muziki kujifunza kutumia ala katika nyimbo zao. Kanku akafika mbali zaidi kwa kusema kwamba hakuna mafanikio bila kuvuja jasho.

Kanku Kelly ni raia halali wa Tanzania aliyefanikiwa kupata uraia  mapema Aprili 27, 2011. Matarajio yake ya baadaye ni kuwa ProdAuza mkubwa aiyekamilika kwa vyombo vya kufanyia kazi hiyo.
Ametoa shukrani nyingi za dhati  kwa watanzania wote waliomlea toka alipokuja hapa nchini, akiwa bado kinda wa miaka 19 hadi leo ana zaidi ya nusu karne.
PICHA ZAIDI.

Tuesday, January 1, 2013

MJUE MKONGWE ABUBAKAR KASONGO MPINDA 'CLAYTON'

Abubakar Kasongo Mpinda akiimba kwenye moja ya
maonyesho na bendi ya  Maquis du Zaire enzi hizo
ABOUBAKAR KASONGO MPINDA ‘Clayton’ ni mwanamuziki mkongwe katika tasnia ya muziki aliyezaliwa wakati vita kuu vya pili vya dunia vikikaribia kumalizika.

Kasongo Mpinda ‘Clayton’anatoka katika ukoo wa ki Chifu. Baba wa Babu yake alikuwa Chifu akiitwa Chifu Kasongo huko Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kasongo ni mtoto wa kwanza kati ya wanane aliyezaliwa Februari 02, 1945, katika  mji wa Lubumbashi jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baba yake mzazi mzee Boniface Mpinda Kasongo, alikuwa mfanyabiashara maarufu katika mji wa Lubumbashi, wakati mama yake Kanku wa Mokendi alikuwa muumuni na  mwimbaji mashuhuri katika  Kanisa la kikatoliki mjini humo.

Mpinda anamuelezea mama yake kwamba ndiye chanzo cha yeye kupenda kuimba kwa kuwa kila mara alikuwa akifuatana na mama yake kwenda Kanisani  kuimba.

Kasongo Mpinda ‘Clayton’ hakuweza kuendelea na masomo ya  Sekondari baada ya wazazi wake wote  kufariki dunia akiwa kidato cha kwanza.

‘Clayton’ ni mtunzi na mwimbaji mwenye sauti nyororo isiyochusha masikioni, anaeleza kwamba kamwe hawezi kuisahau siku aliyoshikana mikono na rais Alli Hassan Mwinyi.

Anasema hakuwa na ndoto hata siku moja ya kuja kushikana mikono na rais katika maisha yake yote, lakini siku hiyo ikatokea.

 Bendi ya M.K.Group ilishinda kupitia wimbo wake wa ‘Uwajibikaji’ katika shindano la Top Ten Show mwaka 1988.

Uwajibikaji ilikuwa ni kauri mbiu ya rais wa awamu ya pili, Alhaj Alli Hassan Mwinyi kwa wantanzania akiwataka kuwajibika katika kazi ipasavyo.

Kasongo alianza safari yake katika muziki kwa  kujiendeleza kidogo kidogo katika bendi mbalimbali zikiwemo za Ode Jazz na Lupe Jazz mjini Lubumbashi.

Mwaka 1965 alikwenda Kinshasa na akajiunga na mkongwe wa muziki wakati huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Dokta Nico Kasanda wa Mikalaia aliyekuwa akimiliki bendi ya L'Africa Fiesta Sukisa.

Mwaka 1968 aliachana na Dokta Nico akaamua kuvuka mpaka akaingia mji wa Lusaka nchini Zambia. Mwaka uliofuatia wa 1969 na kuanzisha bendi yake ya The Wings Brother’s.

The Wings Brother’s ilijumuisha vijana toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokuwa wamechipukia katika  muziki wakati huo.
Anawataja kuwa ni akina Kibambe Ramadhani, Lomani, Jozee, Lushiku wa Lushiku na Kayembe Trumbloo.

Chini ya uongozi  wake bendi, hiyo ilisafiri kwenda kupiga muziki katika nchi za Botswana, Zambia hatimaye wakatua hapa nchini Tanzania mwaka 1979.

Walipofika hapa nchini wanamuziki wa bendi hiyo  waligawanyika. Wengine wakajiunga na Orchestra Safari Soud (OSS) na baadhi wakajiunga na Maquis du Ziare akiwemo yeye.

Baada ya ujio wa vijana hao kukawa na ushidani mkali kati ya bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa ikipiga muziki wake kwenye ukumbi wa Kimara resort na Maquis du Zaire iliyokuwa imejikita ukumbi wa White House Ubungo.

Pamoja na umri wake kuwa mkubwa, Kasongo bado ana kumbukumbu akizitaja nyimbo alizotunga na kuimba akiwa Maquis du Zaire za Angelo, Mwana Malole, Nasononeka, Baharia, Siri ya Mkoko na zingine kibao.

Kasongo alifunga ndoa ya kiisilamu na Bi. Habiba….. mwaka 1984, jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kupata watoto kadhaa kati yao wawili ndiyo waliofuata nyao za Baba yao. Kabla ya kufunga ndoa alilazimika kuingia dini ya kiislamu,  hivyo alisilimishwa na kupewa jina la Abubakar Kasongo Mpinda.

Anawataja wanaye hao kuwa ni Idd Kasongo ‘Clayton’ na Kiloman Kasongo. Idd ‘Clayton’ yupo katika kikosi cha Twanga Pepeta Academy akifanya vizuri katika muziki wa dansi wakati Kiloman anapiga muziki wa kizazi kipya.

Abubakar Kasongo ‘Clayton’ akisaidiana na Mbombo wa Mbomboka walikuwa waanzilishi wa bendi ya M.K. Group iliyokuwa ikiporomosha muziki wake katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ya M.K.Group ndiyo iliyozaa bendi za M.K. Beat na M.K .Sound zikimilikiwa kwa pamoja wafanayabiashara wawili  Mayalu na Kilomoni.

Abubakar   Kasongo Mpinda aliwakusanya wanamuziki mahiri ili kuunda kikosi cha mashambulizi dhidi ya bendi zingine hapa nchini.

Safu hiyo ilikuwa ni ya waimbaji mahiri akiwemo Kalala Mbwembwe, Paul Vitangi, Issa Nundu, Green Simutowe (nyimbo za kizungu), Rahma Shaari  na yeye Kasongo Mpinda. Upande wa gita alikuwepo Monga Stanie na Kasongo Ilunga (solo), Omari Makuka (rhythm) na Andy Swebe (besi). Saxophone ilikuwepo Mafumu Billari ‘Bombenga’ na trumpet zilipulizwa na Abdallah Tuba na Kayembe Ndalabuu.

Kinanda kilikuwa kikipapaswa na Asia Darwesh ‘Mama lao’ na upande wa tumba alikuwepo Sidy Morris ‘Super Konga’

Wakiwa na M.K. Group walitoka na nyimbo za Kibera, Nishike mkono, Kitendawili,  Nipe ukweli, Habiba, Waniumbua, Mwintunpe na nyingine nyingi zilizokuwa zikikonga nyoyo za wapenzi wa ‘ngoma za maghorofani’

Ili kuongeza nguvu katika bendi hiyo,  waliamua kuwachukuwa wapiga magita wengine wakali Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’, Kawelee Mutimwana na baadaye Miraji Shakashi ambaye wakati huo alikuwa bado akijifunza ‘Lena’.

Bendi hiyo ilijizolea sifa kubwa ambapo kila mwisho wa wiki wapenzi na washabiki wa bendi hiyo walisikika wakihimizana kwamba  leo twende ‘ngoma za maghorofani’ Ndiyo sababu ya bendi hiyo kupachikwa jina la ‘Ngoma za maghorofani’

Kasongo anaeleza jinsi alivyo ibua kipaji cha mpiga solo Miraji Shakashia ‘Shakazulu’ambaye kwa sasa anatamba katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’

Ansema kuna kipindi mpiga gita Joseph Mulenga alikuwa akiumwa kila mara na Kawelee Mutimwana alikuwa katimkia Ulaya wakiiacha M.K. Group bila ya  mpiga wa gita la Solo.

Bahati nzuri mkataba wao na Hoteli ya New Afrika ukamalizika na kupata mkataba mwingine mjini Morogoro wa kupiga muziki katika Hoteli za Morogoro na Luna.

Msemo wa ‘ukishikwapo shikamana’ ulijidhihirisha baada ya kufika Morogoro ambapo Kasongo alimlazimisha Miraji  Shakashia kupiga gita la solo nyimbo zote.

Abubakar Kasongo anamsifia Shakashia kwa kipaji alichojaaliwa na mwenyezi mungu, kwa kuweza kuokoa jahazi lililokuwa likienda mrama. Alizipiga nyimbo zote pasipo kugundua dosari yeyote.

‘Clayton’ alidumu na M.K. Group kwa takribani miaka minane na baadaye akajiunga na bendi ya Zaita Muzika ya Ndala Kasheba ambapo walisafiri na bendi hiyo kwenda London nchini Uingereza kwa mwaliko wa watanzania waishio nchini humo.

Kasongo ansema yeye ni mithiri ya ‘Panga kukuu lenye, makali yaleyale’  pale anapotababaisha kwamba baadaye alikuwa akisaidia kupiga muziki katika bendi ya Bakulutu kabla ya kujiunga katika bendi ya Bana Maquis  ambayo inayoongozwa na Tshimanga Kalala Asssosa hadi sasa.

Abubakar  Kasongo hivi sasa afya yake si njema sana anasumbuliwa na maradhi ya kisukari na  gazi iliyotanda maungoni mwake, kiasi kwamba humfanya wakati mwingine asifike kupiga muziki pindi  anapozidiwa.

Mkewe Bi. Habiba Kasongo anasema mumewe  siku zingine hataka kujilazimisha kwenda kupiga muziki hata kama hali yake si nzuri. Lakini kama mke anayejua majukumu yake, humkataza akihofia kuzidiwa akiwa mbali naye.  

Kasongo Mpinda ‘Clyaton’ ameusifia muziki wa kizazi kipya kwa kusema kwamba ‘Hakuna muziki mbaya ili mradi  unapendwa na jamii’ Akawasisitiza wakaze Buti.
 Abubakar Kaosngo Mpinada akiimba. Kushoto ni Abdalah Tuba na Kayembe Ndalabuu (Trumapet)
 Kaongo Mpinda (katikati), akiwa na mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa
 Mpina akiimba Nyuma Ilunga Kalinji ' Vata'