Thursday, March 14, 2013

KASSIM MAPILI NA MAISHA YAKE KATIKA MUZIKI



MAPILI  GWIJI  ALlYETUMIA MAISHA YAKE YOTE  KATIKA MUZIKI.

Machi, 2013.

MZEE KASSIM  MAPILI  ni mwanamuziki mkongwe aliyeanza tasnia hiyo kabla ya nchi yetu ya Tanganyika, wakati huo haijapata Uhuru.
Mzee Mapili ni mwenye vipaji vingi vya kutunga, kuimba nyimbo za muziki wa dansi na kupiga gita. Pamoja na umri wake kumtupa, Mapili ni ‘mfua uji’ wakati wote  wala  haoneshi  dalili za ‘kuchoka’ kama Wazee wengine wenye umri kama wake.

Mwaka huu wa 2013, Mapili  ametimiza miaka 76 ya  kuzaliwa kwake, bado ni  mwenye nguvu, Afya njema  na kumbukumbu nyingi zilizojaa kichwani mwake.

Mzee Mapili amekula chumvi nyingi ingawaje ukikutana naye mitaani,  unaweza kumdhania kuwa  ni ‘Mzee kijana’  kwa jinsi anavyojichanganya katika maongezi na watu wa rika na jinsia tofauti

Mzee Kassim Mapili ameeleza kwamba amevuka mito, mabonde na kuparamia milima iliyoshindikana katika kuyatafuta maisha. Na amesisitaza kwamba hatokata tamaa kuendelea  kutafuta mafanikio hadi ifikapo kipindi atakapoishiwa nguvu.

.
Akisimulia historia ya maisha yake, Mzee Mapili amesema kwamba alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu kilichopo Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937.

Alipata elimu ya msingi sambamba na ya Koraan, akiwa kijijini kwake Lipuyu mkoani Lindi. Anasema akiwa madrasa alikuwa mahiri wa kughani  kaswida katika  Madrasa yake. Hata mapenzi yake ya kuimba nyimbo  aliyapata kupitia Madrasa hiyo.

Ni mwanamuziki mzoefu mwenye uwezo mkubwa wa kuimba na kupiga gita. Anasema  alianza kujifunza kupiga muziki wakati nchi yetu ikiwa bado inatawaliwa na Ukoloni wa Waigereza.

Jina la Kassim Mapili likaanza kusikika katika ulimwengu wa muziki mara tu alipojiunga katika bendi ya White Jazz iliyokuwepo mjini Lindi mwaka 1958.

Sifa zake za kupiga muziki zikazagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani. Hakuchuka muda mrefu katika bendi hiyo,  mwaka uliofuatia wa 1959  akahama na kujiunga na bendi ya Mtwara Jazz wakati huo.
Bendi ya Holulu ya mjini Mtwara, nayo ikaona ni bora inyakue ‘kifaa’ hicho. Mapili akashawishika na maslahi aliyo ahidiwa, ndipo alipoamua kujiunga katika bendi yao mwaka 1962.

Kwa kuwa nchi yetu ya Tanganyika wakati huo  ilikuwa tayari
imekwisha pata Uhuru, Chama TANU kiliazisha vikundi vya  Vijana kukitangaza chama hicho.
Hivyo mwaka 1963,  Mzee Mapili akaoneka anafaa kusaidia kufanya kazi hiyo, akachukuliwa kwenda katika bendi ya Jamhuri Jazz ambayo ilikuwa ya vijana wa TANU (TANU Youth League) ya Lindi.

Baada ya kufanya kazi nzuri hapo Lindi, akateuliwa kuwa muasisi wa bendi nyingine ya Vijana wa TANU (TANU Youth League) huko Tunduru,  mkoani Ruvuma mwaka 1964.

Katika kutafuta maslahi murua wakati huo, alilazimika  kwenda kujiunga na bendi ya Luck Star mwaka 1965,  iliyokuwa na makazi yake Kilwa Masoko mkoani Lindi.

‘Kizuri hupendwa popote’ Kassim hakukaa sana na Luck Star, mwaka huohuo alisakwa ‘kwa udi na uvumba’ na bendi ya Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande, akajiunga nayo.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT ‘Kimbunga Stereo’ na JKT ‘Kimulimuli’. Kwa kuwa sifa za  Mzee Mapili zilikuwa zimezagaa kupitia wa muziki hapa nchini,  Jeshi hilo lilimchukuwa kwenda kuwa muasisi wa bendi ya JKT Mgulani, jijini Dar es Salaam mwaka 1965.

Ushindani wa bendi katika Majeshi, ukaaza. Jeshi la Polisi nalo likamhitaji ajiunge nalo. Alikubali kwenda kuasisi bendi yao ya Polisi Jazz  baada ya kupata ajira tarehe 15, Desemba 1965. Polisi Jazz  ilikuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.

 Akiwa ‘Afande’ Mzee Kassim Mapili aliteuliwa kuwa mwalimu wa bendi ya  Wanawake ikijulikana kama Woman Jazz Band Desemba 23,1965.
Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Umoja wa Vijana TANU (TANU Youth League) ambapo alisafiri na bendi hiyo kwenda nchini Kenya, kwenye sherehe za siku ya Kenyata.(Kenyata day) Kenyata alikuwa rais wa kwanza wa nchi ya Kenya.

Mzee Kassim Mapili alipata pigo kubwa Mei 1966, baada ya kuondokewa na baba yake mzazi Mzee Said Amri Makolela, aliyeuawa wakati akipambana  na Nyati porini. Anamshukuru mungu kwani mama yake mzazi Bi. Ajena Mussa Mtikita, bado yu hai.

Baada ya kuvunjika kwa bendi ya Woman Jazz  mwaka 1974, ndiyo ikwa mwanzo wa kuanzishwa kwa bendi ya Vijana Jazz  baada ya kuwakusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti,  Hassan Dalali, Manitu Mussa, Hamza Kalala ‘Komandoo’ Chakupele,  Abdallah Kwesa , Agrey Ndumbaro na wengine wengi.
Kassim Mapili alistaafu toka jeshi la Polisi  Mei 05, 1981 akiwa na cheo cha Sajenti. Mara baada ya kustaafu mwishoni mwa mwaka 1981, alijiunga na bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz.

Kwa kipindi kirefu Mzee Mapili amekuwa  akiitwa kuhudhuria semina nyingi. Mwaka 1982,  alishiriki katika semina ya wanamuziki iliyofanyika mjini Bagamoyo. Katika semina hiyo ilipelekea kuundwa kwa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), naye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho.

Kila panapofanyika jambo la manufaa katika muziki hapa nchini, Mzee Mapili amekuwa akishirikishwa kikamilifu. Amekuwa akitoa michango ya mawazo yenye busara katika tasnia ya muziki  kwa nyakati tofauti.
Busara zake zilipelekea mwaka 1986 kuchaguliwa kuwa mmoja wa washiriki katika uundwaji wa kundi la wanamuziki 57, lililoitwa Tanzania All Stars.

Mwaka huohuo alishiriki katika tamasha la utoaji  wa zawadi kwa Wasanii wakongwe, akiwemo Mzee Morris Nyunyusa, Mzee Makongoro, Mzee Mwinamira, Mbaraka Mwinshehe na wengine.

Kassim Mapili alikuwa muasisi katika shindano la nyimbo kumi bora za wanamuziki wa dansi (Top Ten Show) mwaka 1988, akiwa kama Mwenyekiti wa CHAMUDATA.

Mzee Mapili akiwa kama Baba, aliwakumbuka watoto wa mitaani wanaosumbuka katika kutafuta maisha. Alianzisha bendi ya watoto  wa umri wa miaka 16,  ambao baadaye walifanya onesho kamambe,  sambamba na siku ambayo watoto wa Afrika Kusini waliteswa huko Soweto.

Mapili mwaka 1993, alikuwa mstari wa mbele wa uanzishwaji wa bendi ya Wazee ya Shikamoo Jazz. Bendi hiyo bado ipo ikiongozwa na Mzee Salumu Zahoro.
Hekima na busara za Mzee  huyu,  zilipelekea mwaka 1974, kuteuliwa kuwa mlezi wa bendi ya Super Matimila.

‘Aliyena nacho huongezewa’ usemi huu ulijiri kwa Mzee Kassimu Mapili,  ambaye Nyota yake aliendelea kung’ara, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa bendi ya Gold All Stars mwaka 1977.

Mzee Mapili hakuwa mchoyo wa kugawa ujuzi alionao, kwani alishiriki kikamilifu katika uundwaji upya wa bendi ya Super Volcano, akiwa na binti ya Mbaraka Mwinshehe, Taji.

Kama nilivyotangulia kukujuza kwamba  Mzee Mapili anaonekana si mtu wa kuchoka kiafya, siri yake alilidokeza hivi. “Nakula chakula vizuri,  ninafanya mazoezi ya viungo kila siku, Sigara, Pombe na starehe zisizokuwa za lazima, kwangu  ni  mwiko…”  Mzee Mapili anafafanua siri ya mafanikio ya afya yake kuwa imara hadi leo.

Pamoja na umri wake kuwa mkubwa, anasema bado  hajafikia wakati wa kuwa tegemezi kwa watoto wake. Anamiliki bendi ya Orchestra Mapili Jazz ambayo bado haijafahamika kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya washabiki wake.
“Bendi yangu huwa inawasisimua mno wapenzi wa muziki wa zamani kwa kuwapigia nyimbo za zamani kwa maombi yao maalum…”  anasema Mapili.
Kassim alienda mbali zaidi akijigamba kwamba wakati akipiga gita, huimba  kufanya ‘shoo’ mwenyewe  akiwakumbusha wazee wenzake mitindo yao ya  zamani ya Twist, Bumping, Charanga, Chacha na Pachanga.

“Nikianza kucheza Twist, juu… juu… chinii… chinii… juu… chiniii,  watu ukumbini huzizima na kunizunguka wakinipongeza wangine wakisema  “Wazee dawa…”  Mapili anatamka kwa kijiamini huku akionesha jinsi ya kucheza mtindo huo.

“Ninauheshimu sana muziki kwani ndiyo ulionilea hadi sasa. “Nimekulia na kuzeeka nikiwa katika muziki, sijawahi kufanya kazi nyigine tofauti na muziki katika maisha yangu yote. Hata nilipopata ajira katika Jeshi la Polisi, nilikuwa akifanya kazi ya muziki…” Anasema Mapili.


Kassim Mapili ni baba wa familiya ya mke na watoto watatu, aliowataja kwa majina ya Kuruthum, Said na Hassan. Kati yao hakuna hata mmoja aliyefuata nyao zake za muziki.

Mapili amekuwa mstari wa mbele katika shughuli takriban zote za kifamiliya za wasanii na wanamuziki wenzake hapa nchini. Huwa habagui kwamba ni Mtanzania ama vinginevyo. Mfano halisi wiki iliyopita  kabla ya kifo cha mwanamuziki Kabeya Budu wa bendi ya Le Capitale, Mapili alikuwa mstari wa mbele kwenda  kumjulia hali  akiwa hospitalini. Pia alishiriki kikamilifu katika mazishi ya mwanamuziki huyo Kabeya Badu, aliyefariki tarehe 06 Machi,  2013 katika hospitali ya Muhimbili kwa maradhi ya figo. Badu alikuwa raia wa  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC).

Mzee Kassim Mapili amemalizia kwa kuwasihi wanamuziki hususani vijana, kujifunza kupiga ala za muziki, ili wafikie malengo yao ya kuwa wanamuziki watakao kubalika kimataifa. Aidha amewataka kuzingatia heshima na upendo miongoni mwao.


Mwisho.



MIRIAM MAKEBA ‘Mama Afrika’




MIRIAM MAKEBA ‘Mama Afrika’

Novemba 05, 2012.

Laiti kama angelikuwa hai Miriam Makeba ‘ Mama Afrika’  Ijumaa iliyopita Novemba 09, 2012, tungelisherehekea miaka 80 ya kuzaliwa kwake. Lakini kwa masikitiko makubwa siku hiyo ndugu na wapenzi wa muziki wake duniani walikuwa katika maombolezo ya miaka minne tangu kifo chake.

Mwanamuziki Makeba alizaliwa Machi 04, 1932 huko Afrika ya Kusini na alifariki Novemba 09, 2008 akiwa na umri wa miaka 76.

Wazazi wake walikuwa Sangoma, Baba yake alikuwa mganga wa kienyeji toka Kabila la Xhosa.
Mama huyu Miriam  katika maisha yake amekumbana na matatizo mengi likiwemo lile la kukaa jela miezi Sita akiwa bado mchanga wa miezi sita akiambatana na mama yake mzazi aliyekuwa akitumikia kifungo.


Miriam ataendelea kukumbukwa kwa sauti  yenye mvuto wa aina yake ambayo yaelezwa kwamba haijawahi kusikika toka kwa mwanamuziki mwingine wa kike huko Afrika ya  Kusini.

Yaelezwa kwamba baada ya kutoweka kwa miongo mitatu akiwa nje ya nchi yake, Miriam Makeba siku aliyotua nchini humo alipokelewa na kufanyiwa sherehe kamambe iliyofananishwa mithiri ya sherehe ya malkia aliyerudi katika kiti chake.

Makeba alikuwa mwanzilishi wa nyimbo za kiafrika na alisaidia kuleta mageuzi  ya muziki wa kiafrika hadi akaitwa ‘Mama Afrika’ miaka ya 1960.

Kipaji chake kilianza kuonekana mwaka 1953  baada ya kuimba wimbo wake wa kwanza wa 'Laktshona Liange’. Wimbo huo  ulibeba  ujumbe mzito akiwa katika kundi  la akina Kaka la Manhattan Brothers.

Makeba aliachana na kundi hilo na akaanzisha kundi la wanawake lilijulikana kama Skylarks. Lakini mwaka mwaka 1958 alirejea tena katika kundi la Manhattan baada ya wao kukubali kazi ya mwanamke katika muziki.

Mwaka 1959 alianza ziara ya miezi 18 akizunguka nchini Afrika Kusini akishirikiana na bendi ya Aifherbert’s Musical Extravaganza African Jazz.

Miriam alitengeneza video yake ya kwanza inayoitwa Come back Africa ambayo ilimletea  mafanikio makubwa ya kupata mialiko mingi ya kwenda kuimba nchi za Ulaya na Marekani.

Akiwa Marekani Makeba aliifurahisha jamii ya Wamerekani weusi kwa wimbo wake wa ‘Pata Pata’ uliokuwa ndiyo Nembo yake.

Wimbo huo uliandikwa na Dorothy Masuka na kurekodiwa nchini Afrika ya Kusini mwaka 1956, kabla ya kuanza kuwa rekodi kali huko Marekani mwaka 1967.

Mwishoni mwa mwaka 1959, Makeba alifanya maonyesho kwa wiki nne mfululizo katika kijiji cha Vanguard huko New York, nchini Marekani.  

Umaarufu wake uliongezeka maradufu baada ya kufanywa kuwa mgeni maalumu wakati wa  tamasha la mwanamuziki Harry Belafonte katika ukumbi wa Carnegie, nchini Marekani.

Mwaka 1960 alifayatua album mbili kali ambazo zilimletea tuzo ya heshima ya Grammy.  

Makeba aliingia mkataba wa kushirikiana na mwanamuziki Harry Belafonte, ambapo mwaka 1972 walitoa Album iliyokuwa na jina la Belafonte & Miriam Makeba.

Miriam kwa mara nyingine tena mwaka 1997 alifanywa mgeni rasmi kwenye onyesho la Harry Belafonte Tribute kwenye bustani ya Madison Square.

Nyimbo zake alizotunga za kutangaza kupinga vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, zilimletea mafanikio makubwa mwaka 1960.

Baada ya miaka 30 Makeba alilazimishwa kuwa raia wa Ulimwengu baada ya kutunukiwa zawadi ya Amani ya  Dag Hammarskjöld mwaka 1968.

‘Ndoa ndoana’ usemi ulijionyesha wazi kwa Makeba baada ya kuolewa na mwanaharakati mweusi Stokely Carmichael. Matamsha mengi yalifutwa pia mkataba wake wa kurekodi RCA ukafutwa. Matokeo yake ilikuwa matatizo makubwa yakamkumba  msanii huyu.

Rais wa Guinea wakati huo, Sekou Toure  alimwalika nchini mwake, naye akakubali na  akafanywa kuwa mmoja wa wanamsafara wa Guinea kwenda Umoja wa Mataifa.

Miaka ya 1964 na 1975 Mama Afrika Makeba alihutubia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu ubaguzi wa rangi huko New York nchini Marekani.

Mwaka 1988 Makeba aliandaika wasifu wake ulioitwa Miriam: My Story, kwa lugha ya Kiingereza. Baadaye wasifu huo ulitafsiriwa na kuchapishwa katika lugha za Kijerumani, Kifaransa, Kitaliani Kiispaniola na Kijapani.

Kufuatika kuachiwa huru kwa  Nelson Mandela ‘mzee Madiba’ toka gerezani, Makeba alirudi nchini mwake Afrika ya Kusini mwezi Desemba 1990.

Alifanya onyesho lake la kwanza chini humo mwezi Aprili 1991 baada ya kutoweka kwa  miaka 30 akiwa nje ya nchi yake.

Alitunukiwa tuzo ya ushindi kwa wimbo wa  Sarafina mwaka 1992. Kwenye wimbo huo Makeba alicheza kama mama wa Sarafina.

Baada ya miaka miwili alirudiana na mume wake wa kwanza mpulizaji wa Trumpeti Hugh Masekela.

 Mwaka 1995 Makeba aliunda taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) ya  kutunisha mfuko wa kusaidia na kulinda haki za wanawake wa Afrika ya Kusini.

Mwaka huohuo alifanya tamasha kubwa kwenye ukumbi wa huko Vatican's Nevi wakati wa sikukuu ya Krismasi.


Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.

 Mwisho.

Sunday, March 10, 2013

SAMBA MAPANGALA ‘ANAYE VUNJA MIFUPA MAREKANI’



SAMBA MAPANGALA ANAYE VUNJA MIFUPA MAREKANI


SAMBA MAPANGALA ni mtunzi na mwimbaji maarufu wa kimataifa aliyejizolea sifa tele   Afrika ya Mashariki na Kati hususani katika nyimbo zake za ‘Vunja Mifupa’ na ‘Dunia tunapita’

Ni mwanamuziki mwenye kipaji cha aina yake, anaye kula ‘Kuku’ katika jiji la Washington DC nchini Marekani. Alimfanyia kampeni rais Barack Obama wa Marekani mwaka 2008.

Alizaliwa huko  Matadi  katika  mkoa uliojulikana  kama Bas-Congo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Miaka ya 1970 alipiga muziki na bendi nyingi katika jiji la Kinshasa wakati akiwa katika masomo ya Sekondari.

Kipaji cha Mapangala kigundulika kupitia  tungo zake ambazo kila wimbo una ujumbe mzito masikioni mwa msikilizaji. Mfano wa karibu ni wimbo wa ‘ Dunia tunapita’ Wimbo huu unaelezea juu ya jamaa ambaye hawezi kufanya chochote kile bila kupita kwa waganga.

Kunyooka kwa Safari ya Samba Mapangala  katika masuala ya muziki kulianza kuonekana  mapema miaka ya 1970 alipoondoka Matadi kwenda katika Jiji la Kinshasha kwa ajili ya masomo ya Sekondari.

Sifa kubwa aliyonayo  Mapangala ni ya kuweza  kutunga, kuimba nyimbo kwa lugha za Lingala na Kiswahili  pia uwezo mkubwa alionao wa kumiliki Jukwaa.

‘Kizuri chajiuza kibaya chajitembeza’ Usemi huu ulijidhihirisha kwa Mapangala baada ya kuonyesha umahiri mkubwa kupitia sauti yake nyororo kulipelekea kupata kazi ya kupiga muziki kwenye bendi za Bariza, Super Tukina, Bella Bella na Saka Saka katika jiji la Kinsahasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


Juhudi zake katika muziki zilimfikisha kusafiri na wanamuziki wenzake kwenda  Mashariki mwa Kongo mwaka 1975. Mwaka iliofuatia wa 1976 walivuka mpaka kwenda Kampala nchini Uganda hako wakaunda bendi ya Le Kinois.

 Akiwa mwimbaji Kiongozi Samba Mapangala  na bendi yake ya Les Kinois ilihamisha makazi toka Kampala na kwenda jiji la Nairobi nchini  Kenya mwaka 1977.

Licha ya kuwa na ushindani mkali toka bendi zingine kubwa katika jiji katika hilo la Nairobi, bado Les Kinois walifanikiwa kuliteka jiji hilo kwa kasi kubwa.

Wakati huo jiji la Nairobi kulikuwa na bendi za Super Mazembe, Orchestra  Les Mangelepa, Les Wanyika, Orchestra Moja One , Baba Gaston  na nyingine nyingi.

Ili kuonyesha ukomavu katika muziki, Samba aliamua kujitegemea mwenyewe kwa kuunda bendi yake na kuipa jina la Orchestra Virunga mwaka 1981 bendi ambayo kwa kipindi kifupi  ikakubalika na wapenzi wa muziki na kuwa moja kati ya bendi maarufu Afrika Mashariki.

Samba Mapangala hupiga muziki wake ukiwa na mchanganyiko wa staili za rumba na Soukous kutoka Kongo. Ili kuwaridhisha wapenzi wa muziki wa Nairobi na vitongoji vyake  walipiga muziki kwa staili za watu wa Kenya.

Rekodi ya kwanza ya Virunga  iliyoitwa ‘It's Disco Time with’  ilitoka mwaka 1982.

Mapangala na bendi yake ya  Virunga walisafiri kwenda  nchini Uingereza  mwezi Aprili  1991 na huko walifanya maonyesho makubwa takribani 23.

Baada ya kufurahia mafanikio ya safari yao, walifanya safari nyingine ya mwisho mwaka 1997 wakipitia nchi za Afrika hadi Marekani ya Kaskazini.

Album za Samba Mapangala  zilizopo ni pamoja na Virunga Volcano  ya mwaka 1990, Evasion ya  1983, Feet on Fireya ya 1991, na  Karibu Kenya iliyofyatuliwa mwaka 1995 zilizorekodiwa katika jiji la  Paris  nchini Ufaransa  akiwashirikishwa wanamuziki toka bendi  ya  Les Quarters Etoiles na  wanamuziki wengine nguli waliokuwa hapo Paris.

Album ya  Vunja Mifupa  iliyotoka mwaka 1997  ilichukua soko kubwa la mauzo hususani Afrika ya Mashariki ikizingatiwa  Ujumbe unatolewa kwa lugha ya Kiswahili.
Virunga Roots Volume 1,  ulijumisha nyimbo zilizo katika kumbukumbu  Virunga  na kutolewa mwaka 2005.

Samba kwa kawaida ni mpole na mcheshi, mwaka   2000,  alialikwa kwenye  Sherehe ya siku ya Jamhuri ya watu wa Kenya katika jiji la London,  ambapo muziki waliopiga ‘uliwachengua’ watu  wote waliofika katika sherehe hiyo.

Mzee wa ‘Vunja Mifupa’ Samba Mapangala  alikuja Tanzania mwezi Mei 2004 kwa ziara ya wiki mbili  na kufanya  maonyesho kadhaa.

Nguli huyu hupenda kushirikina na wanamuziki wengine ili kubadilishana ujuzi na uzoefu. Aliwahi kupiga muziki akiwa na safu ya wanamuziki nyota toka nchi za Kenya na Tanzania.

Album yake mpya ya Song and Dance iliyorekodiwa mwaka 2006 katika Studio za Virunga reocords, wakimshirikisha mwanamuziki  
Bopol na wangine wakali  toka bendi yake ya Orchestra Virunga. Abum hiyo iliyokuwa  na nyimbo nyingi ilizinduliwa rasmi walipokuwa kwenye ziara nchi za Ulaya mwezi March 2006.

Mwezi Juni 4 2006 Samba alikuwa nchini Kenya  kawa ajili  shughuli maalumu ya  Ecofest,

Wakati wa Kampeni ya Urais wa Marekani mwaka 2008, Samba Mapangala alionyesha ni jinsi gani wananchi wa Kenya wanavyomshabikia mgombea wa kiti hicho Barack Obama. Alifyatua wimbo maalumu wa kumtakia heri Obama ulioitwa '
Obama Ubarikiwe'

SambaMapangala na bendi yake ya Orchestra Virunga walirejea Afrika ya Mashariki mapema mwaka 2009, na kutoa burudani katika jiji la Nairobi na  Zanzibar ambako alialikwa katika tamasha la Sauti za Busara .

Mwishioni mwa mwaka 2009 Samba aliuongezea nguvu mfuko wa World Wildlife Fund  kwa kutunga na kutoa  bure  wimbo  wa ‘ Mlima wa Magorila’ uliokuwa ukitoa wito kusaidia kuwalinda magorila waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyamapori ya Virunga ya nchini Kenya ambako wanyama hao adimu hupatikana.
Mangwana anakumbukwa na wapenzi wa muziki wa dansi katika nchi za Afrika ya mashariki na Kati pale wasikiapo nyimbo za Hadija, Marina Nyama Choma,  Alimasi, Dunia haina mwisho na  Dunia tunapita. Nyingine ni  Jaffar, Mapenzi hayana macho, Muniache, Virunga, Vijana, Ufunguo, Vunja mifupa, Siri na Vidonge  uliopigwa kwa staili ya mduwara. Nyimbo zote  zimeimbwa kwa lugha ya Kiswahili.
Samba Mapangala na familia yake wanaishi katika jiji la Washington DC nchini  Marekani.

Mwisho.


MAQUIS ILIVYOWATESA WATANZANIA.

March , 2013

MAQUIS du ZAIRE ni bendi ambayo ‘iliwatesa’ Watanzania kwa kuwaporomoshea burudani za  muziki wa dansi maridhawa katika kumbi mbalimbali hapa nchini.

Kwa wale waliokuwa vijana kati ya miaka ya 1970 na 1990, katu hawawezi kuisahau bendi hiyo ambayo iliingia hapa nchini kwa kishindo kikubwa ikitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire) wakati huo.


Mwaka 1981, niliwahi kufanya mahojiano maalumu na mmoja wa viongozi wa bendi hiyo Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye alinipa wasifu wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.

Kwa kuwa wasifu huo uandikwa na kuchapishwa katika gazeti la serikali la Nchi Yetu la kila mwezi, ambalo lilikuwa likuzwa kwa senti 30, likitolewa na mwajiri wangu wakati huo, Idara ya habari (MAELEZO).

Hivyo basi  si vibaya nikirejea kuwapasha wale ambao hawafahamu na kwa waliosahau, nichukue muda wenu kwa kuwapa wasifu wa bendi hiyo tangia ilivyoanzishwa hadi kutoweka kwake  katika taswira ya muziki.

Historia ya bendi hiyo inaanzia mwaka 1960 kwa waliokuwa vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire), walioungana na kuunda bendi yao wakaiita Super Theo.

Bendi hiyo ilitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki  wa Kamina  na vitongoji vinavyouzunguka mji huo, baadaye wakaibadilisha jina kuwa  Super Gabby.

Katika kile kilichoelezwa na uongozi wa Super Gabby kuwa ni kuleta mageuzi katika muziki, bendi hiyo mwaka 1972, ilibadili jina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.

Maquis du Zaire iliingia hapa Tanzania mwaka huohuo wa 1972, kwa mwaliko wa mfanyabishara maarufu Mzee Batengas. Walianza kutumbuiza kwa mkataba katika ukumbi wa Mikumi Tours uliokuwa maeneo la Tazara  Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Baada ya  kumaliza mkataba wao waliachana na Mzee Batengas,  wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa  kipindi kifupi. Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima aliyekuwa akimiliki wa  ukumbi wa Safari Resort  maeneo ya Kimara.

Mnamo mwaka 1977 Maquis du Zaire waliamua kuongeza nguvu kwa  kuimarisha kikosi chao. Hivyo uongozi huo ulimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ kwenda Congo kutafuta wanamuziki wapya.

‘Mzee Paul’  alibahatika kuwachukuwa akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Kanku Kelly, Ilunga  Banza ‘Mchafu’, Mutombo Sozy na  mnenguaji Ngalula  Tshiandanda. Wakati huo walikuwa wakicheza katika mtindo wa ‘Chakula Kapombe’ ambao kwa watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na mashabiki.


Kufika kwa wanamuziki hao kulileta mabadiliko makubwa sana katika muziki husuani tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ambaye yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.

Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, mtindo uliowapagaisha  wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es  Salaam. Mpulizaji wa Tarumbeta  Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake akitoavibwagizo vya  “cheza Kamanyolaa.. ,cheza ukijidai’ cheza  Kamanyola bila jasho…”

Mwaka huo wa 1977 mwishoni  Maquis  walimaliza mkataba na wakaondoka kwa Hugo Kisima. Bahati nyingine ikawaangukia tena kwani  walisaini  mkataba mwingine na  Mzee Makao aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah,  maeneo ya Ubungo.

Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya Sanifu na Ogelea piga mbizi baadaye ukumbi huo ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba  wakati huohuo Maquis pia ilikuwa ikipiga  kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge. Ukumbi wa  Mpakani  baadaye ulibadilishwa jina kuwa   Silent Inn.  Kisha kuishia kuwa Kanisa.

Mwishoni mwaka 1978 waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka Congo ambao ni akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na  Khatibu Iteyi Iteyi.


Maquis du Zaire ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.

Chini  ya uongozi huo miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana. Mojawapo ni lile la kuanzisha Orchestra Maquis Company (OMACO). Kampuni hiyo ilikuwa ikimiliki shamba la matunda, wakilima kwa kutumia matreka yao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko  Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

OMACO pia  ilimiliki mradi mwingine wa viwanja  tisa na nyumba kadhaa maeneo ya Sinza na pia waliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.

Vijana wa wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu kila siku za Jumamosi, kuwashuhudia vijana wa Maquis du Zaire waliokuwa watanashati na nidhamu ya hali ya juu wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.

Enzi hizo ilikuwa ukiingia katika ukumbi huo wa White House, mbele yako macho lazima yakutane na mbao zilizo nakshiwa kwa maandishi ya majina ya wanamuziki wote na kukomelewa juu ya mwembe uliokuwa katikati ya ukumbi huo.

Maquis du Zaire ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha muziki kwa muda  na kusikika kipaza sauti kikiuliza “Wapenzi mumekuja na miswakii?  Wapenzi walikuwa wakijibu “ndiyooooo…” Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo. Watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima  hadi alfajiri, muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi.


Bendi hiyo ikiwa hapa nchini ilikuwa ikipiga na kucheza katika  mitindo  mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya Chakula kapombe, Kamanyola, Bishe Bishe, Zembwela, Chekecha na Ogelea Piga mbizi.

Mwema Mudjanga ‘ Mzee Chekecha’ ndiye aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo. Alikuwa kivutio kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya  kupuliza tarumbeta, aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia  vibwagizo vya “Chekeee….  Chekechaaa”  “Tusangalaa”, “Aima imaa”,  ‘Bishe bishee”, “Saa… Sanifuu”,  “cheza Kamanyolaa”  “cheza kwa maringo”, “ Cheza  ukijidai” na mengine mengi.

Maquis du Zaire wakati huo  ilikuwa imesheheni wanamuziki zaidi ya 40 wenye vipaji vilivyopishana. Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.

Nina uhakika kwamba msomaji wangu unashauku ya  kujua au kukumbushwa kikosi kamili kilichokuwa kinatengeneza Maquis du Zaire wakati huo. Nikianza na safu ya waimbaji walikuwepo akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na  Kyanga Songa.
Wengine walikuwa  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Tshimanga Kalala Assosa, Kabeya Badu, Masiya Radi ‘Dibakuba kuba’,  Issa Nundu na waimbaji wa kike  Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.

Wapiga gita  la solo alikuwepo  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo, wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha   ‘Field Marshal’.
Wengine katika gitaa hilo  walikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.

Gitaa la rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Bila kuwashau akina Mbambu Kazadi, Mondo Mondonde na  Nawayi Kabwila.

Gitaa  zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kulicharaza gita hilo  akiwa kajitwisha kwenye upara uliozungushiwa simbi kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.

Kama nilivyokujuza hapo awali kwamba bendi hiyo ilikuwa imejaza mseto wa vipaji mbalimbali. Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga/‘Super Sax’,  Khatibu Iteyi Iteyi, Kalamzoo,  Alex Kanyimbo,  Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna ‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na  Majengo Selemani.

Wapuliza tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku Kelly,  Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’, Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’, Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde,  Kaumba Kalemba,  Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan Machege na Ngenda Kalonga.

Madoido na mbwembwe hizo, ziliwavutia  wapenzi wengi na kupenda kuhamishia viti vyao wakisogea  sehemu iliyokuwa karibu, ili kushuhudia vijana hao wakifanya maajabu ya kuchezea vyombo hivyo.



Pamoja na uimbaji  Mbuya Makonga ‘Adios’  alikuwa mbonyezaji  wa kinada  huku Mutombo Sozzy  akizicharaza drums akisaidiana na  Matei Joseph.  Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu Wabandoki Motto.



Walikuwepo na wanenguaji  mahiri  ambao walikuwa wakitoa burudani za pekee akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashid, Anna Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima,  Zuwena na  Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.



Ikiwa White House bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Mwana yoka ya Babote, Ngalula, Nasononeka, Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane wimbo ambao ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.



Zingine zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma, Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo idadi.

Kuna msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo”  msemo huo uliisibu bendi ya  Maquis du Zaire baada ya kiungia katika maelewano ‘hafifu’ na mmili wa ukumbi  wa White House hadi kulazimika kuondoka wakiacha ukumbi huo ukibadilishwa kuwa gereji hadi leo.



Baadaye bendi hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Maquis Original wakipiga muziki katika kumbi za Wapiwapi’s pale maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke, kabla ya kuhamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata pale  Kinondoni.



Maquis Original ilileta wanamuziki  wengine toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo muda mfupi kabla ya mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kuondoka kwenda Stockholm nchini Sweden.



Wanamuziki hao walikuwa Kivugutu Motona Chatcho (Solo), na waimbaji Freditto Butamu na Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.



Walitikisa ukumbi wa Lang’ata  kwa nyimbo zao kali za Mangolibo, Mayanga, Makumbele, zikisindikizwa na wimbo wa Ngalula ambapo wakati wa chorus katika wimbo huo, Tshimanga Assosa alikuwa akimpandisha mori mpiga gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ akimwita “vumbiii… Vimbiiii… Vumbiii…” Nyimbo za Maquis Original zilikuwa  zikipigwa na kutamba kwa staili za ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.



Maquis Original ikiwa Lang’ata, kuna shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’  ambaye  alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis. Alikuwa akiachwa uwanja akionehsa uhodari wake wa kucheza mtindo wa  ‘Sendema’  huku akiwa kajitwisha chupa yenye Bia juu ya kichwa chake.



Ni miaka takriban 23 toka  jina la Maquis litoweke masikioni mwa wadau na wapenzi wa muziki wa dansi baada ya kusambaratika katika  miaka ya 1990, ikiwaachia simanzi na majonzi wapenzi wake yasiyokwisha hadi leo.
Lakini Tshimanaga Kalala Assosa ‘mtoto mzuri’ baadaye alitumia weledi wake katika muziki kwa kuienzi  jina la Maquis kwa kuanzaisha bendi ya ‘Bana Maquis’  ambayo hupiga na kukumbushia nyimbo zilizopigwa na Maquis  du Zaire na Maquis Original.



Ikumbukwe kwamba idadi kubwa miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa humu, wameshatangulia mbele za haki.



Wengine ni wale wanaumwa maradhi mbalimbali akina Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mboka na Mutombo Lufungula ‘Audax’



 Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotangulia mbele za haki na awape tahfifu wanaoumwa, Amen.





 Nguza Vicking akilicharaza gita la solo na nyuma yake ni Kasongo Mpnda 'Clayton' mwimbaji wa bendi hiyo.
 Wapiga magita Dekula Kahanga 'Vumbi' na Ilunga Banza 'Mchafu' (kushoto) wakionesha manjonjo ya kupiga gita sakafuni.
 Waimbaji wa Maquis du Zaire Kasongo Mpinda (katikati) na mapacha Kasalo Kyanga na Kyanga Songa (kulia)
 Mpiga tumba Sidy Morris 'Super Konga' akionyesha mbwembwe za kupiga tumba hizo kwa mikono na mguu.
 Mpulizaji wa Tarumbeta wa Maquis du Zaire, Nkashama Kanku Kelly akifanya vitu vyake.
Kiongozi wa Maquis du Ziare, Chinyama Chiyaza akicheza katika  mtindo wa 'Chakula kapombe' unavyochezwa.
Wanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire wakiwa katika picha ya pamoja. Toka kushoto ni Suleiman Mbwana' Cox', Mbuya Makonga 'Adios', Mujos wa Bayeke, Steven Kaingila Mauffi na dekula Kahanga 'Vumbi'. Wengine ni Issa Nundu, Mukumbule Lolembo 'Parashi' na Roy Mukuna 'Mukuna wa Mukuna.