Sunday, June 29, 2014

UNAMKUMBUKA SALUMU ABDALLAH WA CUBAN MARIMBA ?




UNAMKUMBUKA SALUMU ABDALLAH WA CUBAN MARIMBA ?

Morogoro, moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya 1950, 1960 na ya 1970. Watu wengi walitoka Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro.

Kati ya hizo bendi mbili shindani Morogoro Jazz na Cuban Marimba Band. Bendi ya Cuban Marimba ilikuwa ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah aliyezaliwa Mei 5, 1928, mkoani humo.

Baba yake alikuwa mwarabu na mama yake mwenyeji wa Morogoro. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule huko Dar es Salaam, maana wakati ule ililazimika kwenda Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo.  Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara.

Katika kipindi hicho Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika.

Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki.

Alitoroka hadi Mombasa ili apande Meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia Mombasa, nchini Kenya.

Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote.
Hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana.  La Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah –Band Master.

Katika kuiona Dar es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es Salaam Jazz band.

Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Nzige, Daulinge.

Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band ambalo lilianza kuwa maarufu kiasi cha kwamba mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hii.

Bendi ya Cuban Marimba ikiwa na nguli hiyo iliwahi kurekodi vibao vingi vikiwamo vya Ngoma iko huku, Naumiya, Ubaya, Nalia Nalia, Wanipendeza, Cuba Chacha na Ndiyo hali ya Dunia. Zingine ni Kazi Tanzania,Shemeji, Tanzania Twist, Sipati majibu, Salaam kwa jumla na Wanawake Tanzania. Salumu Abdalaah hakuishia hapo alitoka na vibao vingine vya Kachacha, Tulime Mashamba, Wabeberu, Kimanzi, Si kosa lako Unavunja Utu, Mpenzi Wee na Maisha matamu

Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba 1965.

Cuban Marimba Band iliendelea kupiga muziki mjini humo ikiongozwa na Juma Kilaza hadi naye alipofariki dunia.

Mwisho.

Nashukuru kupata msaada mkubwa kupitia Blog ya ‘Kijiwe cha Kitime’