Monday, September 7, 2015

MUTOMBO LUFUNGULA NGUZO YA MAQUIS ILIYOTOWEKA



MUTOMBO LUFUNGULA NGUZO YA MAQUIS ILIYOTOWEKA
Kwa wale waliokuwa vijana wapenda muziki wa dansi kati ya miaka ya 1970 hadi 1990, jina la mwanamuziki Mutombo Lufungula ‘Audax’ haliwezi kuwa geni.
Alikuwa mtunzi na mwimbaji katika bendi za Maquis du Zaire na Maquis Original. Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi na wanahisa  wa bendi hiyo pamoja na Kampuni ya Orchestra Maquis Company (OMACO).
Mutombo aliitumikia bendi hiyo kwa nguvu zake zote tangu akiwa kijana, hadi mauti yake yaliomfika akiwa na miaka takribani 70.
Kabla ya kifo chake aliugua kwa kipindi kirefu, hatimae akafariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi ya Aprili 23, 2015 akiwa nyumbani kwake Kimara Michungwani Jijini Dar es Salaam.
Lufungula alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Kiharusi tangu mwaka 2005, yaliyopelekea kupooza upande mmoja wa mwili.
Kipindi chote alikuwa akiuguzwa na wanawe ikizingatiwa kwamba mkewe, alikwisha tangulia mbele za haki miaka kadhaa kabla ya yeye kupatwa na maradhi hayo.
Adhi ugonjwa huo ulimfanya ashindwe kuendelea na shughuli zake za muziki, akajikuta akiishi katika hali ngumu akiwategemea baadhi ya marafiki, jamaa na mabinti zake.
Audax alisikika akifanya mahojiano na mtangazaji wa TBC  ‘manju wa muziki’ Masoud Masoud, akaelezea hali yake ilivyo mbaya kimaisha.
Hakuwa na msaada wowote toka kwa watu aliokuwa akiwatarajia. Alisema ni wachache sana waliojaribu kwenda japo kumjulia hali nyumbani kwake.
Baada ya kifo maadalizi ya mazishi yakafanywa na ilipotimu Aprili 26, 2015, Sala ya kuaga mwili wa Mutomba ilifanywa katika hospitali ya Mwananyamala kabla ya kuwekwa katika nyumba yake ya milele, katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mutombo ‘Audax’ ataendelea kukumbukwa na wakazi wengi wa Magomeni Mapipa, mtaa wa Mikumi, ambako aliishi kwa kipindi kirefu kabla ya kuweka makazi yake huko Kimara Michungwani.
Wasifu wake umeelezwa kwamba alizaliwa mwaka 1945 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyejiunga na bendi ya Maquis du Zaire katika mji wa Kamina Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bendi hiyo iliingia hapa nchini mwaka 1972, ikiwa na jina la  Maquis Du Zaire. Kundi hilo awali likuwa na wanamuziki tisa waanzikishi
Kundi hilo lilianza likiwa na jina la Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken Success na baadaye Super Gabby.
Bendi hiyo iliingia hapa nchini Tanzania mwaka 1972 likiwa na jina jipya la Orchestra Maquis Du Zaire.

Walipoingia nchini walipiga katika kumbi nyingi hususani Mikumi na White House pale Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Walianza kwa mbewembwe nyingi wakitumia mtindo wa ‘Chakula chakula kapombe’ ukaja mtindo wa ‘Zembwela’ ukafutiwa na ‘Kamanyola bila Jasho’
Mzee Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ alikuwa kivutio kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya  kupuliza tarumbeta. Aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia  vibwagizo vya “Chekechaa Chekeeee….  Chekechaaa”  “Tusangalaa”, “Aima imaa”, ‘Bishe bishee”, “Saa… Sanifuu”,  “cheza Kamanyolaa”  “cheza kwa maringo”, “ Cheza  ukijidai” na mengine mengi.
Wanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘Kiki’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Nkashama Kanku Kelly, Chinyama Chiaza, Mukuna Roy na yeye Mutombo Lufungula, walikuwa kivutio kikubwa katika jukwaa wakionesha uchezaji wa mtindo wa Kamanyola.
Mutombo alikuwa mfano wa kuingwa na wanamuziki wengine wa bendi hiyo kwa jinsi alivyokuwa akijitoa kwa uwezo wake wote kutekeleza  majukumu yake ipasavyo. Hakuwahi kukosa onesho lolote ukumbini, ila kwa sababu ya msingi.
Kwa ushirikiano mkubwa wa  wanahisa chini ya uongozi wa Chinyama Chaiza bendi hiyo baadae ilifungua Kampuni iliyoitwa Orchestra Maquis Company (OMACO ).
Kampuni hiyo iliweza kuingia mkataba na Kampuni ya Scania pia ilikuwa na mashamba maeneo ya Mbezi wakilima mazao na kuyapeleka sokoni Kariakoo.
Wanahisa hao walikuwa akina Chinyama Chiaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mbuya Makonga ‘Adios’ pamoja na yeye Mutombo Lufungula ‘Audax’

Kifo cha Lufungula kiligeuza historia ya wanamuziki waanzilishi wa bendi hiyo. Katika orodha ya hapo juu, ni mwanamuziki Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Vicking’, ambaye anatumikia  kifungo cha maisha jela ndiye aliye hai.

Mutombo Lufungula kwa nyakati tofauti alikuwa akishirikiana vyema na waimbaji wenzake akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Mbuya Makongo ‘Adios’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Mbombo wa Mbomboka, Kiniki Kieto, Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari,  Tshimanga Kalala Asossa na Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’.
Audax na bendi yao waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi wakitumia mitindo mingi iliyokuwa ikibadilika kila mara kufuatia ubunifu wa wanamuziki hao.
Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Chinyama Chiaza ‘Chichi’ akisaidiana na Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Vicking’.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Mutombo alikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo. Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na ‘Mpenzi Luta’, ‘Mimi’na nyingine nyingi alizotunga na kushiriki kuimba akiwa katika bendi ya Orchestra Maqis du Zaire
Kila jema hukumbwa na matatizo, Maquis du Zaire baadae ilikutana na matatizo yaliyosababisha bendi hiyo kusambaratika. Audax na wanamuziki wengine wakauda bendi nyingine kwa jina la Maquis Original.
Lufungula aliungana na baadhi ya wanamuziki akina Tshimanga Kalala Asossa, Dekula Kahanga ‘Vumbi’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Mukuna Roy, Ilunga Banza ‘Mchafu’, Mujos wa Bayeke, Kaumba Kalemba, Mulenga Kalondji ‘Vata’ na wengine wengi wakaunda bendi hiyo.
Akiwa na Maquis Original Audax kwa kutumia talanta yake, aliweza kuachia kibao kilichoshika chati cha ‘Kisembengo’ wakati huo bendi hiyo ikiwa na jina la Maquis Original iliyokuwa na mako makuu yake katika ukumbi wa Lang’ata maeneo ya Kindondoni jijini Dar es Salaam.
Maquis Original iliongeza wanamuziki wengine toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akina Kivugutu ‘Motto na Chacho’ aliyekuwa akipiga gitaa la solo, Bobo Sukari na Freditto ‘Butamu’ waliokuwa watunzi na waimbaji.
Mutombo alishirikiana vyema na safu ya wanamuziki wa bendi hiyo akiwemo waimbaji wakipiga katika mtindo wao mpya wa ‘Sendema’ na ‘Washa washa’ .

Mungu iweke roho yake pahala pema peponi, amina.



MZEE WA FARASI ALLY CHOKI.




 MZEE WA FARASI ALLY CHOKI.
Ally Choki ni mwanamuziki anayetamba miongoni mwa wanamuziki wa muziki wa dansi hapa nchini.
Ana talanta vingi zilizojengeka kichwani mwake zikiwemo za kutunga, kuimba pamoja na uongozi.
Historia yake katika muziki Choki iliieleza kwamba alianza muziki rasmi mwaka 1988 nilipojiunga na bendi ya Lola Africa.
Baadae akajiunga na bendi ya Mwenge Jazz iliyokuwa chini ya Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ).
Hakudumu kwa kipindi  kirefu baada ya miezi sita alihamia katika bendi ya Bantu Group iliyokuwa ikiongozwa na ‘Komandoo’ Hamza Kalala.
“Mwaka 1990 nikiwa Bantu na Hamza Kalala akiwa kiongozi tulitoa albamu ya Baba Jane. Mwaka 1991 nilitoka Bantu, nikajiunga na Legho Stars chini ya Tshimanga Kalala Asosa...” alisema Ally Choki
Safari ya kusaka mafanikio ilikuwa ikisababisha kwenda huku na kule. Alijikuta yuko katika bendi ya Legho Stars. Hata hivyo huko nako hakudumu sana akaamua kurudi katika bendi ya Bantu group.
Choki alikuwa mithiri ya 'Kunguru' kwani  huko Bantu group nako hakukaa sana, akaenda kujiunga na  bendi ya Bendi ya MK Beat ‘Tukunyema’, iliyokuwa ikiongozwa na Shem Ibrahim Karenga.
Mwaka 1992 alihamia katika bendi ya Washirika Stars ‘Watunjatanjata’ ambako walitoa albamu iliyopewa jina la Gubu la Wifi. 
Huko aliwakuta mwimbaji mwingine mahiri akiwemo Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, mpapasaji Kinanda Abdul Salvado ‘Father Kidevu’ na wengine wengi.

Katika harakati za kusaka maisha Choki aliamua kuvuka mpaka wa nchi nakuingia  katika jiji la Nairobi, nchini Kenya mwaka 1994.
Akiwa katika jiji hilo aliungana na wanamuziki wengine akiwemo Muumini Mwinjuma, ambako huko wakaanzisha bendi yao ikiitwa 'Extra Kimwa' mwaka 1998.
Choki ilipotimu mwaka  mwaka 1999, aliamua kurejea nchini  baada ya kupata taarifa kuwa mama yake mzazi kuwa alikuwa mgonjwa.
Akiwa hapa nchini aliamua kujiunga katika bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’  chini ya uongozi wa mkurugenzi Asha Baraka. 
 Alikubali kujiunga na bendi  hiyo baada ya kupokea ushauri kwa mwanamuziki mwenzake Robert Hegga ‘Caterpillar’ ambaye walikuwa wote Nairobi.
Mwaka 2000 walitoa albamu iitwayo 'Jirani', iliyokuwa na nyimbo nyingi lakini hiyo ulikuwa ni utunzi wake yeye Choki.

Kama kuna kitu ambacho hawezi kukisahau wakati akiwa Twanga, ni pale wanamuziki wengi waliihama bendi hiyo na kwenda kujiunga na bendi nyingine ya Chuchu Sound. Baadhi yao wakatimkia katika bendi ya Mchinga Sound, akiwemo Adolf Mbinga aliyekuwa gitaa la mpiga solo.
Busara zake akazitumia kwa kumfuata mpiga solo mwingine Miraji Shakashia ‘Shaka Zulu’.
Shakashia naye hakudumu kwa kipindi kirefu akatimka ndipo nafasi yake ilishikwa na Kassim Rashid ‘Kizunga’ aliyekuja kupiga gitaa la rhythm.
Baadaye alipewa cheo kuwa kiongozi wa bendi na ndipo walipotengeneza albamu ya Fainali uzeeni. Albamu hiyo ilifuatiwa na ile ya ‘Ukubwa Jiwe’ hatimae ‘Chuki Binafsi’.
Ally Choki alikuwa na kila sababu  za kujivunia akiwa hapo Twanga, kwa kuwa alikuwa akiongoza kwa kutunga nyimbo nyingi zilizovuma.
Baada ya kujipima uwezo wake, akanzisha bendi yake ya Extra Bongo mwaka 2003. Bendi hiyo ilikusanya wanamuziki wengi mahiri hapa nchini na kuweza kuwa tishio kwa bendi zingine hususan katika jiji la Dar es Salaam.
Lakini kama wasemavyo waswahili “Penye riziki hapakosi fitina” ndivyo ilivyotokea kwa Ally Choki ambapo fitina ikatengenezwa  na wanamuziki wake wakanunuliwa akabaki ‘mweupe’ pasipo na mwanamuziki.
Kutokana na hali hiyo, alilazimika kuiacha bendi yake na kwenda kujiunga katika bendi ya Mchinga.
Huko nako hakudumu kwa kipindi kirefu, akarejea tena Twanga Pepeta. Baadae tena akajiunga na kundi zima la Tanzania One Theater, lililokuwa likiongozwa na Kapteni mstaafu John Komba.
Akiwa ni mmoja wa viongozi wa TOT, Choki alifanikiwa kuipandisha chati bendi hiyo baada ya kuwaleta wanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Alidumu na bendi hiyo ya TOT hadi mkataba wake  ulipokwisha, akaamua kuifufua tea bendi yake ya Extra Bongo mwaka 2009.
Ally Choki akizungumzia kisa cha sababu za kushuka kwa kiwango cha muziki wa dansi, Choki alikanusha kauli hiy.
Alisema kwamba muziki wa dansi haujashuka kiwango isipokuwa vyombo vya habari vimeupa kisogo kwa kuangalia zaidi muziki wa Bongo Fleva licha ya wao kuntoa nyimbo nzuri na hata video nzuri.

“Uongozi wa bendi za muziki ni mgumu ukilinganisha na mwanamuziki wa Bongo Fleva ambapo kiongozi hana wanamuziki wengi. Hata hivyo naamini ni wakati na kuna muda utafika muziki huu utakuwa juu…” alisema Ally Choki.
Choki akithamini mchango mkubwa wa wanamuziki waliomtangulia, alimuelezea marehemu Muhidin Maalim Gurumo kuwa alikuwa mwalimu na mtu anayesikiliza ushauri.
Alisema kwamba yeye binafsi nilifanya naye kazi nyingi zikiwapo zili waizotoa albamu yenye nyimbo zake tatu na za Gurumo tatu.
“Album hiyo ilifanya vizuri sana na tulipata fedha nyingi mpaka kila ninapokutana naye akawa anasema nakushukuru sana kijana….” Alisema Ally Choki.
Akielezea siri ya mafanikio yake , Choki alieleza kuwa yanatokana na yeye kufanya juhudi, kutokunywa pombe aliyoanchana nayo mwaka 1994.
Aidha amesema kwamba havuti sigara, amefanikiwa kujenga nyumba,kununua gari aidha ni baba wa familiya ya mke na watoto sita.

Ikumbukwe kabla ya kuondoka The African Star, Choki alikwaruzana na mkurugenzi wa ASET Asha Baraka. Katika  purukushani hizo alifika mbali kwa kutoa kiapo kibaya dhidi ya Mkurugenzi wake Asha Baraka.

Choki akasema kitendo cha ASET kumpeleka mahakamani kumdai gari ambalo walimpa mwenyewe kilimkera sana. Pia ASET kukataa kurudisha pesa za Miraji Shakashia vilevile ASET kutothamini michango ya wasanii walioizalishia ASET pesa nyingi.

Msomaji wa makala haya hauwezi kaumini kwamba Choki hivi karibuni amerejea tena kwa kishindo kwenye bendi yake ya zamani ya African Star Entertainment (Twanga Pepeta)
Alitanganzwa mbele ya waandishi wa habari na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka aliyekuwa amefuatana na Katibu wa bendi, Luiza Mbutu.
Mwisho.






ABETI MASEKINI ‘ALIYEWATOA’ TSHALA MUANA NA MBILIA BEL



ABETI MASEKINI ‘ALIYEWATOA’ TSHALA MUANA NA MBILIA BEL

Jina la Abeti Masekini lilikuwa maarufu masikioni mwa wapenda muziki nchi za Afrika ya Mashariki na Kati mnamo miaka ya 1960. Alikuwa mwanamuziki aliyefanya juhudi za ziada ili 'kuwatoa' baadhi ya wanamziki wanaotamba hivi sasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Elisabeth Finant ndiyo majina yake kamili aliyezaliwa Novemba 09, 1954 katika mji wa Kisangani, Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mama huyo alitokea katia familia yenye ukwasi mkubwa yenye watoto wanane. Baba yake mzazi mzee Jean Fionant, alikuwa Chotara wa mchanganyioko wa Ukongomani na Ubelgiji.
Mwaka 1961 Masekini alipatwa na pigo baada ya Baba yake kauawa kikatili mjini Mbujimayi kutokana matatizo ya Kisiasa.
Mzee Finant alikua mwanachama wa cha MLC, kilichokuwa kikiongozwa na hayati Emery Patrice Lumumba.
Lumumba alikuwa Waziri Mkuu wa zamani nchini DRC Kongo ambae pia anaelezwa kuwa ndie Shujaa wa Uhuru wa nchi hiyo.

Kufuatia hali hiyo ikampelekea mama yake Abeti Masekini kuchukua uamuzi wa kuhamia katika jiji la Kinshasa, ili apate kujihifadhi akiwa na wanawe.

Walipofika Kinshasa, mama yake alimchukua Abeti Msekini akarejesha darasani kwenye shule iliyokuwa ikijulikana kwa Jina la ‘Lycee Ycee Sacre Ceur, Kwa sasa inaitwa  ‘Bosongani’.

Baada ya kumaliza shule ya sekondari, Masekini akaajiriwa kama Katibu kwenye Ofisi ya Waziri wa Utamaduni.

Aliwashangaza baadhi ya ndugu zake na Familia kuona  Abeti  Masekini alipoamua kujiuzuru kwenye kazi aliokua nayo. Akaelekeza mawazo yake kwenye  fani ya muziki, ndipo wakati akajipachika jina la ‘Betty’.
Mwaka 1971 chini ya usimamizi wa mwanamuziki  ‘Gerard Madiata’, palitokea mashindano ya kumtafuta mwanamuziki chipukizi. ‘Betty’akaamua kushiriki kwenye mashindano hayo, ambayo kwa bahati mbaya hajafaulu.
Changamoto ya kupenda muziki ndipo ilipoongezeka huku akiwa mdogo akichipukia mwenye umri wa miak 17 wakati huo.
Ili apate kuruhusiwa kudumbwiza katika unenguaji kwa jina lake  mwenyewe, ilibidi ajiongezee miaka mitatu zaidi,  akawa anasema yeye ni mkubwa wa miaka 20.
Abeti akisaidiwa na kaka yake ‘Jean Abumba’ ambae alikuwa mpiga gitaa mashuhuri, akawa kila siku anafanya onesho kwenye vilabu vidogodogo Jijini Kinshansa.

Abeti Masekini alikutana na Gerard Akueson, aliyekuwa raia wa nchi ya  Togo katika jiji la Kinshasa mwaka 1971. Hapo ndipo fani yake ya muziki ilipoanza rasmi.
Gerard Akueson ndiye akawa meneja wake mkuu tangia mwaka 1972. Abeti na Akueson wakaanzisha mahusiano ya kimapenzi na ilipotimu mwaka1989, wakakufunga ndoa jijini Paris nchini Ufaransa.

Walibahatika kupata watoto wanne, wa kike 3 na mvulana mmoja.

Mumewa huyo alimshauri waongozane kwa kuhamia kwenye nchi za Afrika ya Magharibi, ambako walitumaini kupata mafaanikio zaidi.

Wikiwa hukowalijikuta akiwa na Mashabiki wengi sana kwenye nchi za Benin, Conte D’ivoire, Togo, Niger, Nigeria, Guinea na Ghana.

Baada ya miaka kadhaa akiwa kwenye nchi hizo, Abeti Masikini aliaamua kurudi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aliporejea mapokezi hayakuwa mazuri kwa kuwa watu wengi walikua hawamfahamu kabisa.

Kilicho mponza zaidi ni kwa kipindi chote hicho, alikua hajaweka hata na album japo moja sokoni.
Licha ya kutofahamika kwake, aliamua kufanya onesho kubwa katikati ya jiji la Kinshasa kwenye ukumbi wa CINE Palldium ambako aliambulia watu 12 pekee ndio walio jitokeza kumuangalia.
Tukio hilo halikumdhoofisha moyo Abeti, aliendelea kufanya kazi kwa bidii ili malengo yake yakamilike.

Baada ya kufanya mazoezi makubwa ya kuboresha sauti yake, mwaka 1973 alitoka na album yake ya kwanza ‘Pierre Cardin’ ikiwa na nyimbo kadhaa zikiwemo Mutoto wangu, Bibile, Aziza, Miwela na Safariet Papy yaka.

Album hiyo haikupokelewa vilivyo na wakazi wa jiji la Kinsahasa. Machoni mwao walimchukulia Abeti kama mgeni.

Walimlaumu kwa tabia yake ya kupenda kuimba baadhi ya nyimbo zake kwa lugha ya Kiswahili.
Nguli huyo Abeti Masekini akapatwa na wazo la kuunda kundi lake akalipa jina la ‘Les Redoutables’.

Kundi hilo lilikuwa na wanenguaji wake machachari walio julikana kama ‘Les Tigresses’, ambalo lilifanya watu wengi waanze kuvutiwa naye.

Maonesho yake katika jiji la Kinshasa yakawa gumzo mitaani. Kazi lizokuwa akizifanya meneja wake, zikazaa matunda mema.

Alifanikiwa kupata mkataba uliompeleka kwenda kufanya onesho katika ukumbimaarufu wa Olympia uliopo katika jiji la Paris, ncini Ufaransa.

Mwaka1973 akiwa njiani kuelekea Paris kwenye onesho hilo, alitua katika jiji la Dalkar nchini Senegal. Huko alifanya onesho ambalo pia rais wa nchi hiyo wakati huo Leopald Seadar Senghor alihudhuria.

Pesa zilizopatikana katika onesho hilo alizotoa kama msaada wake kwa watu walioathiriwa kwa ukame wa ardhi.

Alipotuwa katika jiji la Paris Februari 02, 1973 aliporomosha onesho kabambe lilowavutia hasa mashabiki wakizungu kwenye ukumbi wa Olympia.

Abeti Maseki alifanikiwa kufanya onesho jingine Juni 06, 1974  kwenye ukumbi wa Carnegie, uliopo katika jiji ma New York nchini Marekani.

Umaarufu wake ulizidi kuja juu zaidi hususani pale alipopewa fursa ya kutumbuiza kwa pamoja katika jukwaa moja na nguli wa muziki duniani.

Jukwaa hilo lilipambwa na wanamuziki akina James Brown, Miriam Makeba, Tabu Ley na Franco Luambo Makiadi, kabla ya pambano la masumbwi la kihistoria kati ya Mohammed Alli ‘Clay’ na George Foreman jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Albam yake ya pili alifyatua mwaka 1975 ikiwa na jina la ‘La Voix Du Zaire’.

Nyimbo zilizokuwa zimesheheni katika albam hiyo ni Likayabo,Yamba yamba, Kiliki, Bamba, Nalikupenda na Ngoyaye.

Mwaka huo huo Abeti alipokea mualiko kutoka kwa  ‘Bruno Coquatrix’  ambae ndie aliyekuwa mmiliki wa ukumbi wa Olympia ya jijini Paris.

Akaenda kwa mara nyingine tena kufanya maonesho kwa Siku mbili mfululizo.

Ndipo hapo akapachikwa jina bandia la ‘Tiger mwenye kucha za dhahabu’
Mwaka uliofuatia wa 1976, ulikuwa mbaya ki maslahi kwa Abeti Masekini.

Alimpata mpinzani wa uhakika katika muziki aliyejulikana kwa majina ya Mpongo Love, aliyekuja juu kuliko yeye.

Mpongo akaongoza Hit Parade kwenye radio ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( Zaire) wakati huo.

Wimbo wake ‘Pas Possible’ ulimafanya kuwa ni mwenye kupendwa mno na mashabiki.

Pamoja na yote mwaka 1977 wanamuziki hao Abeti na Mpongo, walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi.

Walifanya onesho kubwa la pamoja kwenye ukumbi wa ‘Cine Palldium’ katika jiji la Kinshasa na kuacha simulizi kubwa.

Kila mmoja wao kaimba kiaina yake, wakaweka  misingi mizuri ya kupendana kwa wanamuziki wa kike wa kizazi kijacho.

Historia ya Abeti Masekini itaendelea kukumbukwa daima kwa kuwa yeye ni darasa tosha,
Wanamuziki wengi maarufu wamepitia kwenye bendi yae wakiwamo  akina Mbilia Bel, aliyenengua toka 1976  hadi1981, Lokua Kanza aliyekuwa mpiga gitaa mwaka 1980- hadi 1981, Abby Surya aliyekuwa mnenguaji mwaka 1984 hadi 1986 na  Malage De Lugendo aliyekuwa mwimbaji.
Wengine walikuwa wanenguaji Joëlle Esso, Tshala Muana mwaka 1978 hadi 1979, Yondo Sister mwaka 1986 na Lambio Lambio ‘Komba Bellow’ kwan upande wa kinanda.
Abeti Masekini ni mmoja kati ya wanamuziki wa kike barani Afrika waliofanikiwa kujiwekea jina Kimataifa.
Alidhihirisha uwezo wa kipaji chake na kufahamika nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,  ambayo muziki umetawalia na  Wanaume.
Abeti pia alikuwa mstari wa mbele kupigania haki ya Wanawake.
Kwa miujiza ya mungu, Abeti alifariki dunia Septemba 09, 1994 akiwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa.Tarehe hiyo inafanana na ile aliyozaliwa ya Novemba 09, 1954.

Ni mwaka wa 21 tangu atutoke mwana muziki huyo, mungu ailaze pahala pema peponi, Amina.

Mwisho.