Saturday, April 16, 2016

JEAN ‘JOHNNY’ BOKELO ISENGE



 JEAN ‘JOHNNY’ BOKELO ISENGE

Jean Bokelo alizaliwa mwaka 1939 nchini Kongo, nje kidogo ya jiji la Kinshasa. 

Familia yake ilikuwa ni ya wanamuziki. Johnny alikuwa mdogo wa Paul Ebengo’Dewayon’ Isenge.

Mwanamuziki mwingine aliyekuwa mkubwa sana nchini Kongo toka mwanzoni mwa miaka ya 50. 

Huyu Dewayon alikuwa na bendi inaitwa Watam, hapa ndipo Johnny alipoanzia muziki akipiga na mtoto mwingine aliyekuja kutikisa ulimwengu wa muziki Franco Luambo Luanzo, wakati huo Franco akiwa na miaka 12 tu.

Johnny Bokelo aliendelea kupiga katika bendi alizoanzisha kaka yake kama vile Conga Jazz na Orchèstre Cobantu, lakini mwaka 1958 John akaanzisha bendi yake, Orchestre Conga Succès, akiwa na mdogo wake Mpia Mongongo maarufu kwa jina la Porthos Bokelo, ambaye alikuwa mpiga gitaa la rhythm mahiri sana. 

Kaka yao Dewayon, akaja kujiunga na kundi hilo1960 lakini miaka miwiwli baadae1962 Johny na kaka yake wakatengana. 

Bokelo alifanikiwa kulijenga kundi lake kuwa na nguvu na likawa kwa namna fulani linafanana sana na OK Jazz.
Hata tungo nyingine zilikuwa ni za kujibu tungo za OK Jazz au kuzungumzia mada ambayo imeanzishwa na OK Jazz. 

Kuna wakati Bokelo alianzisha kuimba nyimbo alizozipa jina la Mwambe no 1 na 2 mpaka 5 ambapo alikuwa akiongea na kushangaa jamii inaelekea wapi. 

Upigaji wa Bokelo Dewayon na Franco ulishabihiana, pengine ni kutokana na wote kuanzia Watam.

Mwaka 1968 Johnny Bokelo akabadili jina la kundi lake la “Conga success” na kulita “Conga 68” akaanzisha Label yake akaanza kutoa santuri, hii ilimuongezea kipato japo wanamuziki wake walitishia kuachana nae kwani walisema hawakuwa wanapata fedha zozote kutokana na mradi huo.

Santuri nyingi wakati huu alikuwa akiziachia kwanza kutoka Ufaransa ili kupata mapato zaidi. 

Kati ya 1972 mpaka 1974 Bokelo Isengo alikuwa anatumia muda mwingi zaidi akiwa studio, kwenye mwaka 1970, viwanda vya kutengeneza santuri vya Kinshasa vikawa vimechoka hivyo bokelo akaanza kupeleka master zake ili kutengeneza santuri. 

Mwaka 1980 Bokelo aliachana sana na shughuli za muziki.

Bokelo alifariki 15 January 1995 baada ya kuugua kwa muda mrefu
 Mwisho.
Mungu alilaze roho yake pahala pema peponi, amina. 

BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI NA CHOC STARS



BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI NA CHOC STARS

“Nzawisaa, Nzawisaaa maama Nzawisaaa..Yeloo!!!..” 

Haya ni baadhi ya maneno alikuwa akiyatamka kama vibwagizo katika nyimbo za mwanamuziki maarufu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bozi Boziana.

Jina lake halizi anaitwa Mbenzu Ngamboni Boskill, ni mtu mzima aliyetimiza umri wa miaka 63, baada ya kuzaliwa   mwaka 1952 huko Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Kongo.

Amepigia bendi nyingi kubwa na ndogo nchini mwake zikiwa ni pamoja na Bamboula de Papa Noel, Minzoto Sangela, Zaiko Langa Langa, Isifi Lokole, Yoka Lokole, Langa Langa Stars na Choc Stars

‘Mzee Benzi’ kama anavyojulikana na wengi baadae aiunda bendi yake Orchestra Anti-Choc, anayeiongoza hadi sasa.

Licha ya utunzi na uimbaji, pia ni mkung’utaji mzuri wa gitaa kulishambulia jukwaa akishirikiana na akina dada wawili Betty na Scolla Miell.

Mzee Benzi alianzia muziki wa Afro-Pop katika  bendi ya Air Marine lakini aliyaona mafanikio ya kazi zake ilipotimu mwaka 1974, alipojiunga na bendi ya Zaiko Langa Langa

Zaiko LangaLanga ilikuwa na waimbaji  mashuhuri wakati huo  wakiongozwa na mkongwe  Papa Wemba na mwezake Evoloko Jocker.

Lakini haikuzidi mwaka, Papa Wemba na Evoloko waliondoka  bendi hiyo baadae hata Bozi Boziana aliwafuata  kwenda kuanzisha bendi mpya ikaitwa Isifi Lokole

“ Fahari wawili hawakai zizi moja” usemi huo ulijidhirisha baada ya wanamuziki hao kushindwa kukubaliana katika maswala mbalimbali ya msingi yaliyopelekea wanamuziki wake akina Papa Wemba, Boziana, Mavuela Somo na wengine kuondoka bendi ya Isifi Lokole. Walienda kuunda bendi yao mpya iliyopewa jina la Yoka Lokole.

Bendi ya Yoka Lokole ilipata  mafanikio makubwa mwaka 1976, japokuwa ilipotimu mwinshoni mwa mwaka huo, Papa Wemba aliicha bendi hiyo na akaenda kuanzisha bendi ya Viva la Musica

Bozi Boziana naye mwaka 1977 naye aliicha bendi hiyo ya Yoka Lokole, licha ya bendi hiyo kuwa maarufu kwa kipindi kifupi.

Kwa miezi michache  Boziana alishirikiana na mwanamuziki Efonge Gina, ambaye naye alikuwa katika bendi ya Zaiko Langa Langa. 

Walirekodi nyimbo kadhaa kama vile Selemani iliyotungwa na Bozi Boziana na  Libanko Ya Ngai utunzi wake Gina.

 Kiamuangana mwaka 1981, aliibadilisha  bendi ya Soukous super group  na kuita  Langa Langa Stars ikiwa imesheheni vipaji vya wanamuziki kaiwemo Evoloko Jocker, Dindo Yogo na  wnengine wengi.  

Bozi Biziana aliakwa kujiunga vijana hao naye akaubali na kuicha  Zaiko Langa kwa mara ya pili.

Langa Langa Stars ilidumu kwa miaka michache iliyofuatia kabla na Boziana naye akaondoka kwenda kujiunga na bendi kubwa nchini humo  Choc Stars aliyokuwa chini Ben Nyamabo ambako alipiga hadi mwezi Novemba 1985.

Akiwa na bendi hiyo ya Choc Stars Boziana alirekodi baadhi ya nyimbo ambazo zilikuja kuwa maarufu za Sandu Kotti, Alena, Mbuta-Mutu na Retrouvailles a Paris.


Anti –Choc ilikuwa na wanamuziki wengi wenye vipaji lukuki wakiwemo akina Fifi Mofude, Djo Nolo, Koffi Alibaba, Wally Ngonda, Rigo Star, Ngouma Lokito, Deesse Mukangi, Marthe Lamugenia, Ngimbi Yespe na Maoussi Solange

Mpiga gita wa kwanza katika bendi hiyo alikuwa Matou Samuel ambaye  kwa sasa anaimba muziki wa Injili  na nafasi yake ilishikwa na Dodoly ambaye kabla ya kujiunga humo alitokea katika bendi ya mwanamuziki Lita Bembo ya Orchestre Stukas.

Dodoly alipachikwa jina bandia la ‘The sewing machine’ kwa umahiri wake wa kutumia vidole vyake kucharaza nyuzi  kwa kasi kubwa.

Tokea miaka ya 1980  Boziana aliendelea katika bendi yake ya Anti-Choc ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo  akishirikiana na wanamuziki wengine mahiri.

Boziana aliwahi kushinda zawadi ya Kora All-African kwa album yake kuwa bora toka nchi za Afrika ya Kati.

Kwa wapenzi wa muziki hapa nchini watamkumbuka Bozi jinsi alivyoteka wapenzi katika maonesho kadhaa aliyoyafanya hapa nchini kwa ushirikiano walioonshea kati ya Bozi Boziana, Deesse Mukangi na Joly Detta walivyokuwa wakilishambulia jukwaa kwka staili ya ‘Nzawisa’ katika nyimbo za Tembe na Tembe, Palpitation na zingine nyingi zilifanya watu kuviacha viti vyao kwenda kuwatuza.

Bozi Boziana ana sauti nzuri, yakupendeza akimba huku akipokezana na timu yake ya wanadada wawili, Joly pamoja na Deesse.

Sifa nyingine za mwanamuziki huyu mzee Benzi ni kwamba muziki wake hauna mwingiliano kati ya sauti ,gitaa na synthesizer katika nyimbo zake zote.

Mfano katika wimbo wa ‘Ngoyartong020’ tune tatu za mwanzo Boziboziana amemshirkisha Jolly Detta na Deesse,  na sehemu ya pili ya wimbo huo aliongeza nguvu kwa kumuongeza waimbaji na wanenguaji  Scola Miel maarufu kwa jina ‘Nzawissa’ na Betty. 

Bozi alifyatua vibao vingi vilivyompa sifa nyingi ukiwemo wa La reine de Sabah, Lelo Makambo Lobi Makambo Evelyne na Fleur de Lys ambazo alimshirikisha mwimbaji wa kike Joly Delta.

Boziana aliachia wimbo mwingine akimshirikisha Deesse na Ba Bokilo.

Bozi Boziana na bendi yake bado anaendeleza muziki akiwa na bendi yake na watanzania watakumbuka kwa mara ya mwisho alikuja hapa nchini kwa mwaliko wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Asha Baraka.

Mwisho.



MTUNZI NA MWIMBAJI KASONGO WA KANEMA



MTUNZI NA MWIMBAJI KASONGO WA KANEMA
“Kakolele mama Kakolele Kako mama Kako mama…Viva Krismasi… Viva Krismasi, Viva mamaa…, Noele Mamaa…Noele mamaa.. ” 

Haya ni maneno yanayosikika katika wimbo wa Viva Krismasi ambao bado siku chache yataanza kusikika tena katika vituo vya redio humu nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla kukaribisha sherehe za Krismasi na Mwaka mpya wa 2016.

Matamshi ya maneno hayo hutamkwa mwimbaji Kasongo wa Kanema wakati alipokuwa katika bendi ya Baba Nationale iliyokuwa ikiogozwa na Baba Gaston Ilunga wa Ilunga. 

Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu yake katika jiji la Nairobi nchini Kenya.

Katika makala haya yatamzungumzia mwanamuziki huyo Kasongo wa Kanema, aliyekuwa na vipaji  vya utunzi na mwimbaji wa muziki wa dansi.

Ni mwenye asili toka Jakhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyeanza muziki  akiwa na umri mdogo wa miaka 10 huko nchini mwake.

Kasongo wakati akijifunza kuimba, alikuwa akitamani kufikia viwango vya nguli wa muziki za Franco Luambo Makidi na Tabu Ley. Hivyo alichukua muda mwingi kusikiliza nyimbo zao pia kuziimba.

Familiya yake haikumtupa, ilimpa moyo baada ya kumuona kuwa ana juhudi za kuupenda muziki. 



Akiwa na  wenzake waliokuwa na mawazo kama yake, walifikia kuunda bedi ya Super Mazembe.
Wanzake hao walikuwa akina Atia Joe, Lovi Longomba, Bukalos Kayembe Rapok, Songole, Lobe Mapako, Talos, Longwa Didos nan Fataki Lokasa Losi Losi ‘Masumbuko ya duniya’,  hawa wote walikwisha tangulia mbele za haki. Kati yao walio hai yeye Kasongo wa Kanema na anayeishi katika jiji la Nairobi na  Dodo Dorris, ambaye anakula maisha huko Afrika ya Kusini.

Wanamuziki wengine walikuwa wakiunda kikosi cha Super Mazembe ni pamoja na Kasongo Songo  au maarufu kama Kasongo Jnr. 


Huyo alikuwa akipapasa kinada  na kuimbaj. Aidha alikuwepo Maranata, gitaa zito la besi liliungurumishwa na Kashindi , kwenye gitaa la solo alikuwa Alpha Nyuki na Ale Maindu. 

Mcharanga drums alikuwa Lei Mkonkole na Longwa Disco alikuwa mwimbaji.

Kasongo  anaishi katika jiji la Nairobi ni baba wa familiya ya mke  aitwaye Achieng, na wamebarikiwa kupata watoto watano.

 
Mwisho.


BELLA BELLA ILIYOTIKISA VIGOGO WA MUZIKI DRC



BELLA BELLA ILIYOTIKISA VIGOGO WA MUZIKI DRC.

Miaka ya nyuma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulikuwa na ushindani mkubwa katika muziki. 

Walikuwapo wanamuziki wakubwa kama Franco Luambo Makaidi, Tabu Ley, Mpongo Love, Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’, na wengine wengi waliokuwa wakitamba katika muziki wa dansi.

Katika makala haya yanawaeelezea ndugu wawili Maxime Soki Vangu na Emile Dianzenza ambao kwa pamoja walaimua kuunda bendi yao ya Orchestra Bella Bella ililojulikana pia kwa majina ya Frères Soki & l’Orchestre Bella Bella iliyoanzishwa mwaka 1969.

Bendi hiyo ilileta chamgamoto kubwa kwa vigogo hao katika muziki, wakajikuta wakikwaa vikwazo vya kunyang’ayana wapenzi wa dansi toka kwa vijana hao.

Orchestra Bella Bella iliwajumuisha wanamuziki wengine akina Nyboma Mandido, Pepe Kalle, Shaba Kahamba na wengine wengi, waliofanya bendi hiyo kama jukwaa la kuanzia umaarufu.

Waliongozwa na ndugu hao Maxime Soki Vangu na Emile Dianzenza, wakiwa na wapiga magitaa Johnny Rodgers na Jean Bosco, Kahamba Uzalu maarufu kama Shaba Kahamba.

Wakati huo Emile Soki alikuwa na miaka 16 tu hivyo kuwa kipenzi cha vijana wenzie wakati huo.

Bendi hiyo ilirekodi vibao vilivyotikisa Afrika ya Mashariki na kati na kama vile “Baboti Bapekisi”, “Sylvie”, “Alexandrine”, “Mwasi ya moto”, “Luta”, “Lina”, Mandendeli”, “Mbuta”, “Bipale ya pembeni” na “Sofele”.

Kama wasemavyo waswahili kuwa “ngoma ikipigwa sana hupasuka” haya yalijiri baada ya ugomvi kutokea mwaka 1972, kati ya wanamuziki, uliopelekea bendi ipate mabadiliko makubwa.

Ile semi isemayo “hasira za mkizi…” zikajionesha kwa Emile, ailiyekuwa nguzo katika bendi ya Bella Bella, kuliacha kundi hilo na kwenda kuanzisha kundi la Bella Mambo.

Mtunzi na mwimbaji  Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’ akajiunga na kundi hilo kwa miaka michache ili aweze kupata fedha za kununulia vyombo vyake mwenyewe.

Kujiunga kwa Pepe Kalle kukafanya Bella Bella iendelee kushikilia chati kwa kwa kufyatua vibao vya “Mbuta”, “Kamale”, “Kimbundi”, “Lipua Lipua” na “Sola”.
 
Kama wasemavyo waswahili kuwa “ Ngoma ya watoto haikeshi”, mwaka 1973 Emile Dianzenza aliicha bendi aliyoianzisha ya Bella Mambo na kurudi tena Orchesta Bella Bella kwa kaka yake Soki Vangu.

Alipotua kundini, wakatengeneza nembo ya kurekodia yenye majina ya “Allez-y frères Soki”

Kwa kupitia nembo hiyo waliachia vibao viwili vilivyoandikwa  “Dizzy Mandjeku”, ambavyo ndivyo vilivyowaingizia fedha nyingi kuliko kazi nyingine yoyote walizowahi kuzifanya kabla ya hapo. 

Baada ya vibao hivyo, vilifuatia vingine vyaMwana yoka toil”, “Menga”, “De base”, “Tikela ngai mobali”, “Pambindoni”, “Nganga”, “Houleux-houleux” na “Zamba”.
 
Ukwasi ulipowakolea walifikia kuanza kukodi vikundi vingine wakitaka kufanya maonesho kwa niaba yao.

Mwaka 1977, wakati wakiwa kwenye maonesho huko Ulaya, Emile akaanza kupatwa na maradhi yaliyosababisha kuchanganyikiwa.

Maradhi hayo hayakumpa nafasi tena ya kucheza muziki, akalazimika kuacha bendi.
Maxime alijitahidi kufufua upya bendi yao baada ya kupwaya kwa kiasi kikubwa, lakini wale wanamuziki alioanza nao wengi walikuwa wamekwisha ondoka.

Licha ya wanamuziki nguli akina Kanda Bongoman na Diblo Dibala kujiunga, hata nao walishindwa kuirudisha bendi katika uhai wa enzi zake.

Maji yalipozidi unga, Maxime Soki Vangu hatimaye aliiacha bendi yake ya Bella Bella na kuhamia nchini Ujerumani.

Maxime Soki Vangu aliyezaliwa Agosti 08, 1947, aliishi nchini humo hadi mauti yalipomfioka Mei 18, 1990 akiwa mjini Cologne.

Nduguye Emile Soki Dianzenza aliyezaliwa Kinshasa, Dec. 14, 1954, alifariki dunia Mei 04, 1990 akiwa na umri mdogo wa miaka 36. 

Orcherstra Bella Bella haipo tena kwenye taswira ya muziki, lakini nyimbo zake bado zinarindima.

Mungu azilaze roho zao pahala pema peponi, amina.

Mwisho.