Friday, December 2, 2016

TUIKUMBUKE TABORA JAZZ




 TUIKUMBUKE TABORA JAZZ

Bendi ya Tabora Jazz ilikuwa na makazi yake mjini Tabora ikipiga muziki wake katika ukumbi wa  nyumbani wa Lumumba.

Nyimbo nyingi za bendi hiyo zilipigwa mno kwenye kumbi za starehe pamoja na kituo cha Radio Tanzania Dar es Salaam(RTD) na vituo vingine vya Radio vya Afrika ya mashariki.

Tabora Jazz ilitamba kwa mitindo yake ya za Segere Matata, Segua Segua na  Mambo Mileka.

Mji wa Tabora unaelezwa kwamba ulianza kupata burudani za muziki wa dansi  hata kabla ya chama cha TANU hakichaanzishwa.

Kwa mujibu wa Hassan Athuman ambaye aliyekuwa mwanamuziki wa enzi hizo akipiga gita la solo katika bendi za Tabora Jazz, Kiko Kids, Nyanyembe Jazz  na Milambo Jazz ‘Sona Sona’ kwa nyakati tofauti.

Alisimulia kuwa  mnamo mwaka 1953 ilianzishwa bendi ya muziki wa dansi iliyopewa jina la Staff Jazz ikiongozwa na Hamisi Wampa.

Vyombo vya muziki vya bendi hiyo vilinunuliwa na mfadhili mmoja wa kabila la Kimmanda’ toka nchini Malawi, aliyenunua vyombo hivyo wakati huo akiwa mfanyakazi wa Bomani. 

Staff Jazz ilikuwa na mdhamini akiitwa  mwalimu Hasanari. Waanzilishi wake walikuwa akina Hamisi Ali Songo ‘ngoma kubwa’ , Hamisi Ngege alikuwa  mpiga ngoma ndogo, Dani Kafumu na Nzige   wapulizaji tarumbeta, Akbaru Hasanari Dremsi ‘ngoma kubwa’ Joseph Kayombo ‘bambo’ mwimbaji, Moshi ‘marakasi’,  Saidi ngoma ndogo’ Haji Sungura ‘mlangoni’, Swedi Mandanda 1953/56/58 Hamisi Issa ‘’trarumbeta’ na ryhtm. Hii ilikuwa kati ya miaka ya 1953 hadi 1958.

Wanamuziki wengine walikuwa akina Abdi Fundi upande wa ‘sax’ Athuman Tembo kuimba na ‘solo’ Zakaria Tenda wema(mwimbaji) Sylvester Chifunda ‘mwimbaji’ Juma Athumani ‘drums’ aka Juma Lumango na Mlekwa Suleimani mmoja wa viongozi. Rajabu Risasi upande wa gita la besi.

Staff Jazz ilikuwa ikipiga muziki kwenye ukumbi wa baa ya Rufita ambayo baadaye ukabadilishwa na kuwa Lumumba uliyokuwa katika kona ya barabara za  Rufita na Kapembe, katikati ya mji wa Tabora.
Bendi hiyo kwa sababu ambazo hazikuainishwa, mwaka 1954 ilisambaratika.

Busara na hekima za Hamis Alli Songo zilimfanya aifufue bendi hiyo mwaka 1956 kwa jina lingine la Tabora Jazz.

Yaelezwa kuwa Mlekwa Selemani aliyekuwa shabiki mkubwa wa bendi ya Kiko Kids, akajiunga na Tabora Jazz na kuwa mmoja wa viongozi wa bendi hiyo.

Mwaka 1958 bendi hiyo ilichukuliwa kwenda Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuhamashisha nguvu ya chama cha TANU wakiongozana na viongozi wake  Rashid  Mfaume  Kawawa, Mzee Herman Pacha, mama Mosi Tambwe na mumuwe Abdallah Selemani.

Bendi iliporudi Rashidi Hazuruni mwaka 1959 aliondoka kwenda Dar es Salaam akajiunga na Quban Branch iliyokuwa ikiongozwa na Mzee Mwaipungu.

Kati ya mwaka 1960 na 1961 bendi ilikuwa na wapigaji gita la solo wawili akina Abdi Fundi na Matata. Mwaka uliofuatia Athumani Tembo akaongezeka katika ukung’utaji wa gita hilo.

‘Maisha ni kuhangaika’ usemi huu ulijionesha wakati Rashidi Hazuruni aliporejea tena kupiga muziki na Tabora Jazz mwaka 1963.

Tabora Jazz ilisheheni wanamuziki wengi wakiwemo akina Hamisi Wampa aliyekuwa Kiongozi, Hamisi Alli Songo na Akbaru Hasanari Dremsi walikuwa wadunda ngoma kubwa, Mambosasa alikuwa akipiga ukulele (gita la kizamani). Mambosasa ndiye aliyekuwa baba yake mzazi na Athumani Mambosasa, aliyewahi kuwa mlinda mlango wa Klabu  ya Simba.

Said na Hamis Ngege walikuwa wakipiga  ngoma ndogo, Dani Kafundu na  Nzige walikuwa wapulizaji wa tarumbeta wakati Joseph Kayombo ‘Bambo’ alikuwa mwimbaji.

Kwa upande wa marakasi alikuwemo Moshi, Haji Sungura aliyekuwa mlinzi ‘mlangoni’, Swedi Mandanda alikuwa mcharazaji wa gita la solo, Hamisi Issa alikuwa akipiga gita la kati ‘rhythm’ na Tarumbeta. 

Wanamziki wengine walikuwa Athumani Tembo kwenye solo, upande wa gita la  rhythm walikuwa Hamis Issa na Fundi Hassan Athumani.

Besi liliungurumishwa na Kassim Mponda aliyeondoka katika bendi hiyo mwaka 1965 mwishoni, akifuatana wanamuziki wengine akina Rashidi Hazuruni na Omari Kayanda wakaenda kujiunga na Western Jazz.

Mwaka 1966 Tabora Jazz ikapata mpiga solo mwingine aliyejulikana kwa jina la Stan kuziba pengo la Rashidi Hanzuruni.

Upande wa safu ya waimbaji walikuwa Atrhumani Tembo, Omari Kayanda , Sylvester Chifunda na Joseph Kayombo ‘Bambo’

Mpigaji bongos (ngoma ndogo) alikuwa Juma Athumani ‘kisegeju’ Abdi Fundi alikuwa akipuliza saxophone ’mdomo wa bata’

Kati ya mwaka 1964 na 1965, Tabora Jazz walirekodi nyimbo baadhi yake zikiwa za Ndugu sikilizeni, Tuambie, Dunia haina mwisho, Mwanawanyeje na nyinginezo.

Mwaka 1967 Kassimu Kaluwona  alikwenda Kigoma na kuweza kuwaleta Wema Abdallah, Hamis Kitambi, Issa Ramadhani ‘ ‘Baba Watoto’ Mabrushi
 Ramadhani Mgoligwa na  Hamisi Mkongo.

Mwaka 1968 Salumu Luzira akaijunga na  Tabora Jazz akitokea Nzega.
Mwaka 1971 Wema Abdallah akaondoka Tabora Jazz akaenda Western Jazz, nafasi yake ikachukuliwa na mpiga solo mwingine aliyejulikana ka jina la Kalii, alikitokea Kigoma Jazz.
Kwa kipindi kifupi Said Mabera na Hassan Rehan Bichuka nao walijiunga na Tabora Jazz wakitokea Rumonge Jazz.
Shem Karenga aliletwa na Kassim Kaluwona toka Kigoma, kuja Tabora kujiunga na bendi hiyo Aprili 1972.
Shem baada ya kutua, alishiriki vilivyo katika utengenezaji wa wimbo wa Dada Asha ambao baadaye
Wimbo wa Dada Asha uliibwa na bendi ya Sokous Stars ya akina Lokassa ya Mbongo ya nchini Kongo na kuichakachua  ukiwemo wimbo wa Vigeregere uliopigwa na Western Jazz. Pia mwanamuziki Lita Bembo na vijana wake wa  Stukas nao walikwapua na kuupiga wimbo huo.
Kwa mujibu wa Hassan Athumani amsema kuwa wimbo wa Dada Asha, mtunzi wake alikuwa askari jeshi aliyeomba atengenezewe wimbo huo.

Tabu Ley aliiona album yenye wimbo huo wa Dada Asha akiwa Nairobi na aliinunua akaenda kuiuza nchini Kongo, Poland na Ubelgiji.

Bendi hiyo baadaye akajipanga upya kwa kupata damu changa ili kuendeleza muziki wake.
Iliongeza watunzi na waimbaji wengi akiwemo Msafiri Horoub,  Madaraka Morris, Ismail Wangoko na wengine wengi.

Kwa umoja wao wakafyatua nyimbo nyingi zilizoweza kuridhisha nyoyo za wapenzi na mashabiki wa Tabora Jazz. Nyimbo hizo ni Ashura, Helena, Mapenzi ulimi, Visa uache, Lucie umeniacha, Zabibun na Niambie leo Kaka. Ziningine zilikuwa za Usijifanye Mwewe, Mariam mpenzi, Zabibu No.2, Sofia mpenzi,  Tatu, Serafina, Tamaa yako na  Asha No. 1. Zote hizo  zilikuwa zikitamba mno wakati huo. Zingine ni pamoja na Alhamdulilah, Nashukuru sana, na Dada Asha.
Nyingine ni pamoja na Dada Mwantumu, Ujana una mwisho, mwisho wake ni uzee. Zingine zilikuwa za Salima, Mapenzi Ulimi, Dada Remmy na Rukia wajidanganya.

Wanamuziki wengi wanatajwa katika bendi hii ya Tabora Jazz, baadhi yao wapo hai kama vile Shem Karenga, Ramadhani Mwanangwa (rhythm) Salumu Luzira na wengine wengi.

Baadhi ya wanamuziki wanaotajwa katika makala hii wamekwishafariki.

Walio haihaajishughulishi tena na maswala ya muziki kufuatia umri kuwatupa mkono.

Bendi ya Tabora Jazz haipo tena katika ulimwengu wa muziki.

Mwisho.