KING KIKI ALIAPA KUFIA KATIKA
MUZIKI
King Kiki ni mwanamuziki mwenye
historia ndefu yenye mvuto wa kipekee. Hajawahi kufanya kazi nyingine tofauti
na muziki katika kipindi chote cha maisha yake.
Amejijengea umaarufu kwa wapenzi wa
muziki wa dansi kila kona hapa nchini kwa kutoa burudani katika sherehe
mbalimbali zikiwemo za Kitaifa.
Kiki aliingia hapa nchini kwa mara
ya kwanza mnamo miaka ya 1970, alipofuatana na bendi ya Orchestra Fouvette toka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Bendi hiyo iliyofanya maonesho yake
ya muziki humu nchini ikiwa ya uongozi wa Fred Ndala Kasheba.
Jamhuri ilifanikiwa kufanya
mahojiano maalumu na nguli huyo nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ali, jijini Dar
es Salaam hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo King Kiki
alieleza kwa undani historia ya maisha yake, ikiwamo ya muziki, mafanikio
na njia alizopitia hadi kufikia hapo alipo.
Akiwa na tabasamu tele usoni mwake,
alianza kuelezea Wasifu wake akitamka majina yake kuwa anaitwa Kikumbi Mwanza
Mpango.
Kiki alisema kwamba alizaliwa
Januari 01, 1947 katika mji wa Lubumbashi uliopo katika mkoa Katanga huko
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Mimi ni mtoto wa tano kwa kuzaliwa
toka kwa wazazi wangu mzee Katambo Wabando Paulino na mama yangu Mwanza Jumban
Elia Maria…” alisema Kiki.
Mwaka 1953 alipelekwa kwenda kuanza masomo ya awali akiwa na umri wa
miaka sita, baadaye aliendelea na elimu ya msingi katika shule ya Officialle Laique de Kolwezi, ambako
alimaliza darasa la Saba mwaka 1959.
Kiki alitamka kuwa wakati akiwa darasa la nne, baba yake
aliyekuwa mfanyakazi katika kampuni ya madini inayotambulika kwa majina ya
Gecamiou Athenee Royale kwa sasa, alipata uhamisho na kuhamia katika mji wa
Likwasi huko DRC.
Wakati huo kampuni hiyo ilikuwa ikijulikana kama
Union Miniere Du Hut Katanga,
King Kiki tangu zamani alikuwa mpenda kuimba ambapo
mwalimu wake akaliona hilo, akamjumuisha katika vikundi vya ngoma na muziki
shuleni hapo.
Akawa anachukuwa utaalamu wa kucheza
mitaani na kuupeleka shuleni ambapo aliwaunganisha wanafunzi wenzake watatu na
kuanzisha kikundi cha muziki wa dansi wakiwa darasa la tano.
Walimu wake waliupenda muziki wao ambapo walikuwa
wakiimba na kucheza, hivyo kila sherehe za shule waliitwa kutoa burudani.
Sifa za umahiri wa kundi hilo zikavuma ikizingatiwa
kwamba walikuwa vijana wadogo wanaofanya mambo makubwa.
“Haikuishia hapo hata katika sherehe za watu wa karibu na
shule yetu, wanafunzi waliokuwa na sherehe majumbani mwao walikuwa wanatualika
tunakwenda kuimba na kucheza bure…” alisema King Kiki.
Alifafanua kuwa
mbali na kupenda muziki, pia alikuwa mahiri katika masomo.
Kiki alijigamba
kwamba hakuwahi kuwa mtu wa tatu kila anapofanya mtihani na akifeli sana
alishika nafasi ya pili.
Alieleza kwamba akiwa na umri wa
miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952, kundi la muziki kutoka nchini
Afrika Kusini likiwa limeambatana na mwanamuziki mahiri Miriam Makeba ‘Mama
Afrika’, lilifanya ziara nchini mwao.
Kiki aliendelea
kusimulia kwamba wakati huo alikuwa na kaka yake aliyemtaja kwa majina ya
Koroumba Joseph.
“Kwa bahati nzuri kaka yangu alikuwa akinipenda sana,
hivyo muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kwenye dansi, hasa mwishoni mwa
wiki, hata kwenye onesho la Miram Makeba alinipeleka...” alisema King Kiki.
Licha ya miaka mingi kupita hajamsahau kiongozi wa kundi
hilo aliyekuwa anaitwa Dambuza Mulele. Wanamuziki wengine wa kundi hilo
walikuwa akina Sekena Kolaye, Tigizi Kwankwa, Dolira Jebe na mwenyewe nguli
Miriamu Makeba.
Kiki aliongeza kusema majina hayo hakuwahi kuyaandika
wala kuyasoma mahali popote zaidi ya siku hiyo, yalipotambulishwa hadi leo
anayakumbuka kikamilifu.
Miriam Makeba aliyekuwa akiongoza safu ya uimbaji kwa
pamoja na wanamuziki wa kundi hilo, waliimba na kucheza kama vile hawana mifupa
kwenye miguu na mwili kwa ujumla.
Kiongozi wao Dambuza Mulele, alikuwa na sauti nzito hivyo
alikuwa ‘akichombeza’ maneno walipokuwa wakiimba kama afanyavyo Koffi Olomide
katika baadhi ya nyimbo zake.
Kiki alisema kwamba mwimbaji Miriam Makeba alipokuwa
anaimba, alikuwa anaona kama jina hilo halikumstahili kuitwa.
Akawaza kama angelipewa fulsa ya kumtafutia jina
linaloendana na hadhi yake.
Kwa bahati nzuri wakati akiwaza hivyo, akasikia kiongozi
wa bendi hiyo akipaza sauti akisema anapenda kumwita mwanamama huyo ‘Chocolate
girl’.
“Kwa kweli nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki,
nimeona shoo nyingi za Kimataifa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile
nilichokiona siku hiyo kwa Miriam Makeba...” alisisitiza King Kiki.
Akiwa bado masomoni mwaka 1958,
alijiunga na kikundi cha watoto wenzake cha Bantu Negro, waliweza kubadili
muziki huo kwenda kwenye muziki wa rhumba.
Bendi ya Bantu Negro ilikuwa
ikifanya maonesho ambayo watazamaji walikuwa wanaketi wakiwatazama na
kusikiliza jinsi vijana hao wanavyo poromosha muziki wakitumia ala.
Akiwa shuleni hapo, alikuwa
akipendekezwa kufanya fani mbalimbali zikiwemo za maigizo, ngoma kuimba na
kucheza.
Kikumbi alijiunga na masomo ya
sekondari kidato cha kwanza katika shule ya Attene Iwayala, mwaka 1960
alikosoma hadi kidato cha tatu.
Alikuwa akikumbana na kizingiti
kikubwa toka kwa wazazi wake ambao hawakupenda kabisa awe mwanamuziki,
walimtaka aendelee na masomo shuleni.
Kikumbi anakiri kuwa muziki ulikuwa
umemuingia ndani ya damu, akawa akipigwa na wazazi wake ili aende shule lakini
hakubadili msimamo wake.
“Kaka yangu alikuwa akinifunga
kamba kwenye baiskeli huku akinikimbiza umbali wa Kilometa takribani 20, kama
adhabu ya kutokwenda shule lakini yote hayo haikusaidia…” alitamka Kiki huku
akitabasamu.
Alisema ukali wa kaka na wazazi wake
alilazimika kutoroka nyumbani na kwenda kujihifadhi kwa marafiki zake.
Usemi usemao kwamba “Uchungu wa mwana
ajuwae mzazi” ulijidhihirisha pale wazazi wa Kiki kuaona kwamba kijana wao
mwenye akili sana darasani ameshindikana.
Baba yake alimuweka chini akamuuliza
iwapo atakuwa tayari kufanya kazi nyingine yeyote tofauti na muziki.
Pasipo woga mbele ya baba huyo, Kiki
alimjibu kwamba muziki umemteka sana na kwamba atakufa nao.
Kwa majibu hayo baba yake akawa hana
jinsi, ila ilimbariki na kumtakia mafanikio mema.
“Baba aliposema hivyo, niliruka ruka
kwa furaha, nikajihisi kama nilikuwa naelea katika dunia ya wapenda muziki…”
anasema Kiki.
Kwa kuwa Kiki muziki ulikuwa
umemtawala sana, mwaka 1962 ilimlazimu kuacha shule akiwa Sekondari kidato cha
tatu, akaanza kuimba rasmi mwaka huo.
Katika mazungumzo hayo, Mwanza
Mpango aliwataja wanamuziki wakongwe waliomfanya kubadili mfumo wa muziki akiwa
katika bendi ya Norvella Jazz.
Aliwataja akina Tchamala Kabasele
Joseph ‘Grand Kale’, Tabu Ley na Fanco Luambo Makiadi.
Walilazimika kutafuta vyombo vingine
vizuri vya muziki, hivyo wakapita katika vikundi mbalimbali hadi wakafika mkoa
wa Kasai (Mbudji Mai).
Huko walikutana na vikundi
mbalimbali kutoka mkoa wa Kinshasa vya African Jazz, Conga Success, Negro
Success, Eco Bantu, African Fiesta vita na vingine mbalimbali, vilivyomfanya
kupata uzoefu zaidi katika muziki wa rhumba mwaka 1965.
Mwaka 1968 Kiki alirudi mkoa wa
Katanga ambako alikutana na wanamuziki wa bendi ya Videt Jazz, iliyokuwa
ikitoka nchini Zimbabwe.
Mwanza Mpango alisimulia Kaka yake aliyekuwa na bendi
yake, iliyomzidishia hamasa katika muziki.
Aliwakumbuka
baadhi ya wanamuziki
waliokuwa wakifanya kazi na kaka yake ambao ni Zapta Mfana, Kumaro Kadima,
Andre Kaka na Joseph Kolomba.
“Naweza kusema hao walinipa ujuzi mkubwa kwani
nilijifunza kupiga vyombo pamoja nao, hapo ndipo nilipopenda kucheza, sikuwa
mnene kama nilivyo sasa ungeniona ungefurahi…” alisema Kikii akiyatikisa maungo
yake yaliyojaa minofu.
Alieleza kuwa ipo picha ya video iliyorekodiwa wimbo wa
‘Kasongo rudia’ wanaonekana yeye, Chinyama Chiyaza, Mtombo Lufungula, Mbuya
Makonga, Kanku Kelly wakicheza kwa kupishana huku na kule wakati huo bado
vijana.
Kuna wakati
Kikumbi alikuwa akipata mialiko ya huku na kule kiasi cha kutambuliwa na
Wakurugenzi wa makampuni ambao walimuahidi kumpatia vyombo vya muziki.
Kwa ujasiri wa aina yake alikuwa
akikataa. Hakuwa tayari kufanya kazi chini ya kampuni ya mtu, akijielekeza
katika kutafuta njia ya kujikwamua mwenyewe kwa kutumia jasho lake.
“Nikiwa napiga muziki kwa
kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baadhi ya pesa nilizokuwa nikizipata nilipelekea
kwa baba yangu kumuonesha kuwa muziki unalipa…” Kiki alitamka.
Hata hivyo wazazi wake pamoja na
kuzipokea pesa hizo, bado walikuwa wakimshauri kwamba anayo nafasi ya kurudi
shule kuendelea na masomo.
Kauli hizo za wazee wake akaona bora
awe mbali na nyumbani. Mwaka 1964 akaenda mkoa wa Kasai ambako alijiunga na
bendi ya Norvella Jazz alikopiga muziki hadi mwaka 1967.
Baadaye bendi hiyo kasambaratika
naye mwaka 1968 akarudi mkoa wa Katanga.
Alikuwa mwanamuziki Fred Ndala Kasheba
aliyemkaribisha King Kiki kujiunga katika bendi ya Orchestra Fouvette.
Alipojiunga na bendi hiyo Kiki
alianza kuimba nyimbo mbili zilizotamba sana, nazo ni ‘Jacqueline’ na ‘Kamarade
ya Nzela’ ambazo ndiyo zilizompa nafasi ya kufuatana na bendi ya Fouvette kuja
nchini Tanzania.
Ikiwa hapa nchini bendi hiyo iliweza
kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi katika maonesho yao
kadhaa.
Bendi hiyo baada ya kufanya maonesho
hayo, ilirejea kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako waliamua kubadili
jina ikaitwa Safari Nkoi.
Mwaka 1977 Kikumbi Mwanza Mpango
akiwa kwao DRC, alifuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, aliyekuwa mmoja kati
ya viongozi wa bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa tayari ipo katika jiji la Dar
es Salaam.
Kiki hukukurupuka kukubali bali
alianza kumhoji Mzee Paul iwapo Wanamuziki waliopo Maquis du Zaire wanakidhi
viwango.
Majibu ya Mzee Paul yalionesha
wasiwasi, ndipo yeye akapendekeza wachukuliwe wanamuziki wengine toka huko DRC.
Kiki aliwapendekeza wanamuziki wa
kuondoka naye kuja nchini Tanzania akiwemo Kanku Nkashama Kelly, Mutombo Sozy
na Ilunga Banza ‘Mchafu’.
Wakiwa safarini kuja nchini,
walipitia mji wa Kamina ambako walimpata mwanadada Ngalula Tshiandanda,
aliyekuwa mnenguaji katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo.
Bendi ya Maquis du Zaire wakati huo
ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki Chinyama Chiaza ‘Chichi’.
Iliingia nchini mwanzoni mwa miaka
ya 1970 kwa mbwembwe nyingi ikipiga muziki kwa mtindo wa ‘Chakula chakula
Kapombe’
Baada ya kutua Maquis, Kiki alianza
kuonesha cheche zake baada ya kubuni mtindo wa Kamanyola ambao baadaye ukawa
gumzo katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.
Alieleza maana halisi ya Kamanyola
akisema Kamanyola ni mji huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
“Nilitunga mtindo huo baada ya
kujiunga na bendi hiyo mwaka 1977, niliongeza maneno ya ‘bila jasho’. Kwa maana
mchezaji wa muziki huo atacheza taratibu kwa raha zake huku akijidai…” Kiki
alifafanua.
Mwaka huo huo wa 1977, sherehe za
sikukuu ya Wakulima kitaifa zilifanyika mkoani Mbeya. Bendi ya Maquis du Zaire
ilialikwa kwenda kutoa burudani. Baada ya kurejea Dar es Salaam, walitunga
wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’.
Kwenye wimbo huo, sauti ya King Kiki
inasikika akianza kwa kughani.
Umahiri wa kutunga na kuimba Kiki
aliedelea kuachia vibao vya ‘Nimepigwa Ngwala’, Kiongo na ‘Kyembe’.
Baadhi ya nyimbo nyingine
alizoshiriki kutunga na kuimba ni pamoja na Kasongo, Kibwe Mutondo, Sofia,
Mokili, Yoka Mateya Babote, Dora mtoto wa Dodoma, Sababu ya Nini, Usinifiche
siri na Noele Krismas.
Bendi ya Maquis du Zaire kabla ya
kusambaratika ilikuwa ikiporomosha muziki maridadi katika ukumbi wa White
House, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Safu ya waimbaji wenzake wakati huo
walikuwa ni akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule
Lolembo ‘Parashi’, Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo
wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Kiniki Kieto, na Masiya Radi ‘Dikuba
Kuba’. Safu hiyo ilikamilishwa kwa waimbaji Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.
Waswahili wanasema “Chema Chajiuza”
Usemi huo ulijidhihirisha baada ya miaka miwili, akatafutwa na mfanyabiashara
maarufu katika jiji hilo la Dar es Salaam, Hugo Kisima.
Kisima alikuwa mmiliki wa ukumbi wa
Safari Resort na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS), iliyokuwa na makao yake
katika huko Kimara, jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao waliafikina kuondoka
katika bendi ya Maquis du Zaire, akajiunga na OSS, baada ya ‘kumegewa’ kitita
cha fedha.
Baada ya kuingia OSS, alishirikiana
vyema na waimbaji wa bendi hiyo akina Skassy Kasambula, Monga Stani Liki,
Dingituka Molay, Mobali Jumbe, Kalala Mbwebwe, Tshibanda Sony na Kabeya Badu.
Aidha Kiki alitambulisha mtindo mpya
wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’.
Kiki pamoja na tungo zake nyingi
kuna kumbukumbu zisizosahaulika katika enzi za mtindo wa Masantula, alipotunga
na kuimba nyimbo za Mimi msafiri, Mama Kabibi na Kitoto kaanza tambaa.
Wimbo wa Mimi msafiri alikuwa
akijibashiria kuwa bendi hiyo ndiyo ingelikuwa ya kuzeeka nayo. Lakini mambo
hayakuwa hivyo kwa kuwa aliamua kujikwamua badala ya kuajiriwa.
Alianzisha bendi yake ya King Kiki
Double O, iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa shika Breki’.
Kiki katika bendi hiyo aliachia
vibao baadhi yake ni pamoja na Njigina, Salamule, Mtoto wa Elia, Sababu ya Nini
na Malalamiko. Bendi hiyo haikudumu kwa kipindi kirefu, ikisambaratika kwa
sababu ya uchakavu wa vyombo.
Baada ya kusambaratika bendi hiyo,
Kiki aliitumia talanta yake katika muziki akawa msanii mgeni au mwalikwa katika
bendi mbalimbali.
Moja kati ya bendi ambazo alikuwa
akishiriki maonesho yao bila kuajiriwa, ilikuwa ni ya Orchestra Sambulumaa
‘Wana Zuke Muselebende’.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na
mfanyabiashara Emmanuel Mpangala pamoja na mwanamuziki Chimbwiza Mbambu Nguza
‘Vicking’, aliyekuwa ameiacha bendi ya Maquis du Zaire.
Kiki alifanya shughuli hiyo kwa
takribani miaka minne, akaondoka kwenda kuungana na Fred Ndala Kasheba. Kwa
umoja wao wakaunda bendi ya Zaita Musica mwaka 1994 iliyokuja kuwa maarufu
hususani baada ya kuachia wimbo wa ‘Kesi ya Kanga’. Hapo ndipo mtindo wa
‘Kitambaa Cheupe’ ulipozaliwa.
Mwaka 2003 akiwa na Ndala Kasheba
walianzisha bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’. Lakini kwa mapenzi ya mungu mwenzangu
Kasheba akafariki dunia mwaka mmoja baadaye, yaani 2004…”
Bendi hiyo bado inauendeleza mtindo
wa Kitambaa cheupe hadi.
Alisema mtindo huo umeiletea bendi
yake wateja wengi wanaopenda muziki wa kistaarabu wakicheza na vitambaa vyeupe
mikononi.
Alifafanua kitendo cha kuweka
Kitambaa Cheupe ni kama ishara ya upendo na amani.
Kikumbi alishirikana vyema na mtunzi
na mwimbaji mahiri Baziano Bwetti, ambaye pia walikuwa wote katika bendi ya
Orchestra Fouvette.
Baada ya kuishi kwa muda mrefu humu
nchini, aliamua kuomba Uraia wa Tanzania. Kiki alizifuata taratibu zote za
Idara ya Uhamiaji, hadi mwaka 1997, alipokubaliwa kuwa raia halali wa Tanzania.
Kiki na bendi yake hiyo miaka ya
2000, walifanikiwa kwenda katika jiji la London nchini Uingereza, ambako waliporomosha
muziki maridadi kwa Wantanzania waishio huko.
Baada ya kurejea nchini, akatunga
wimbo uliopewa jina la ‘Safari ya London’.
Katika wimbo huo uwalielezea jinsi
safari yao ilivyofana wakiwataja baadhi ya watu waliofanikisha ziara hiyo
wakiwemo baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Ukisikiliza mirindimo ya wimbo huo,
hataitofautisha sana na ile ya wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’.
Baada ya kukongwa na nyoyo za baadhi
ya mashabiki na wapenzi wake walimpachaki majina ya ‘Bwana Mukubwa’.
King Kiki anayo imani kwamba bendi
ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyoundwa mwaka 2003, ndiyo bora kwa muziki wa
dansi kwa sasa.
Alipoulizwa nini
kilichomshawishi zaidi kuwa mwanamuziki.
Kiki alieleza kuwa alishawishika kuingia
kwenye muziki akiwa na miaka sita, baada ya kumshuhudia mwanamama Miriam
Makeba, toka Afrika ya Kusini alipofanya maonesho nchini mwake.
Kikumbi akiwa na tabasamu alitamka
siri ya kung’aa kwake licha ya umri wake wa miaka 69 sasa alizema
“…inawezekana kung’aa kwangu katika
muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa
Januari Mosi, saa 11 alfajiri.”
Kikumbi ‘alijifagilia’ bendi yake ya
La Capitale iliyoundwa mwaka 2003, kuwa ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa
sasa, na huenda ikawa ndiyo atakayozeekea nayo.
Aidha Kiki aliweza kusimulia siri ya
mafanikio ya kung’ara kwake akisema
“…inawezekana kung’aa kwangu katika
muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa
Januari Mosi, saa 11 alfajiri…”
Akiainisha baadhi ya mafanikio
aliyokwisha yapata katika muziki kuwa ni pamoja na kuweza kusafiri kwenda
kufanya maonesho katika mataifa mbalimblai makubwa duniani likiwemo la
Marekani. Kiki alitamka kuwa alipokuwa huko Marekani, aliweza kukidhi kiu ya Waafrika
waishio huko alipoporomosha ‘bonge la shoo’ akiwashirikisha wanamuziki wa kundi
la Soukuos Stars Lokassa ya Mbongo na Ngouma Lokito.
Aidha alisema ameweza kumudu maisha
yake na familiya kwa ujumla pia kumiliki bendi mbili nyingine ipo katika jiji la
Mwanza.
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ni
baba wa familiya ya mke na watoto kadhaa. Kati yao ni binti mmoja pekee
aliyefuata nyayo za baba yake katika uimbaji.
Nguli huyo alionesha kujali ukweni
kwake mkoani Mbeya, alipotunga na kuimba wimbo wa Barua. Katika wimbo huo
anaagiza kufikishiwa salamu afikapo Igulusi, Uyole, Makambako na kwingineko.
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’
bado anaendeleza talanta yake ya muziki katika jiji la Dar es Salaam na
kwingine anako alikwa.
Mwisho.