Sunday, November 20, 2016

KING KIKI ALIAPA KUFIA KATIKA MUZIKI



KING KIKI ALIAPA KUFIA KATIKA  MUZIKI


King Kiki ni mwanamuziki mwenye historia ndefu yenye mvuto wa kipekee. Hajawahi kufanya kazi nyingine tofauti na muziki katika kipindi chote cha maisha yake.
Amejijengea umaarufu kwa wapenzi wa muziki wa dansi kila kona hapa nchini kwa kutoa burudani katika sherehe mbalimbali zikiwemo za Kitaifa.
Kiki aliingia hapa nchini kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 1970, alipofuatana na bendi ya Orchestra Fouvette toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Bendi hiyo iliyofanya maonesho yake ya muziki humu nchini ikiwa ya uongozi wa Fred Ndala Kasheba.
Jamhuri ilifanikiwa kufanya mahojiano maalumu na nguli huyo nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ali, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo King Kiki  alieleza kwa undani historia ya maisha yake, ikiwamo ya muziki, mafanikio na njia alizopitia hadi kufikia hapo alipo.
Akiwa na tabasamu tele usoni mwake, alianza kuelezea Wasifu wake akitamka majina yake kuwa anaitwa Kikumbi Mwanza Mpango.
Kiki alisema kwamba alizaliwa Januari 01, 1947 katika mji wa Lubumbashi uliopo katika mkoa Katanga huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Mimi ni mtoto wa tano kwa kuzaliwa toka kwa wazazi wangu mzee Katambo Wabando Paulino na mama yangu Mwanza Jumban Elia Maria…” alisema Kiki.

Mwaka 1953 alipelekwa kwenda kuanza masomo ya awali akiwa na umri wa miaka sita, baadaye aliendelea na elimu ya msingi katika shule ya Officialle Laique de Kolwezi, ambako alimaliza darasa la Saba mwaka 1959.
Kiki alitamka kuwa wakati akiwa darasa la nne, baba yake aliyekuwa mfanyakazi katika kampuni ya madini inayotambulika kwa majina ya Gecamiou Athenee Royale kwa sasa, alipata uhamisho na kuhamia katika mji wa Likwasi huko DRC.
Wakati huo kampuni hiyo  ilikuwa ikijulikana kama Union Miniere Du Hut Katanga,

King Kiki tangu zamani alikuwa mpenda kuimba ambapo mwalimu wake akaliona hilo, akamjumuisha katika vikundi vya ngoma na muziki shuleni hapo.
Akawa anachukuwa utaalamu wa kucheza mitaani na kuupeleka shuleni ambapo aliwaunganisha wanafunzi wenzake watatu na kuanzisha kikundi cha muziki wa dansi wakiwa darasa la tano.

Walimu wake waliupenda muziki wao ambapo walikuwa wakiimba na kucheza, hivyo kila sherehe za shule waliitwa kutoa burudani.
Sifa za umahiri wa kundi hilo zikavuma ikizingatiwa kwamba walikuwa vijana wadogo wanaofanya mambo makubwa.
“Haikuishia hapo hata katika sherehe za watu wa karibu na shule yetu, wanafunzi waliokuwa na sherehe majumbani mwao walikuwa wanatualika tunakwenda kuimba na kucheza bure…” alisema King Kiki.
Alifafanua kuwa mbali na kupenda muziki, pia alikuwa mahiri katika masomo.
Kiki alijigamba kwamba hakuwahi kuwa mtu wa tatu kila anapofanya mtihani na akifeli sana alishika nafasi ya pili.
Alieleza kwamba akiwa na umri wa miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952, kundi la muziki kutoka nchini Afrika Kusini likiwa limeambatana na mwanamuziki mahiri Miriam Makeba ‘Mama Afrika’, lilifanya ziara nchini mwao.
Kiki aliendelea kusimulia kwamba wakati huo alikuwa na kaka yake aliyemtaja kwa majina ya Koroumba Joseph.
“Kwa bahati nzuri kaka yangu alikuwa akinipenda sana, hivyo muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kwenye dansi, hasa mwishoni mwa wiki, hata kwenye onesho la Miram Makeba alinipeleka...” alisema King Kiki.
Licha ya miaka mingi kupita hajamsahau kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa anaitwa Dambuza Mulele. Wanamuziki wengine wa kundi hilo walikuwa akina Sekena Kolaye, Tigizi Kwankwa, Dolira Jebe na mwenyewe nguli Miriamu Makeba.
Kiki aliongeza kusema majina hayo hakuwahi kuyaandika wala kuyasoma mahali popote zaidi ya siku hiyo, yalipotambulishwa hadi leo anayakumbuka kikamilifu.
Miriam Makeba aliyekuwa akiongoza safu ya uimbaji kwa pamoja na wanamuziki wa kundi hilo, waliimba na kucheza kama vile hawana mifupa kwenye miguu na mwili kwa ujumla.
Kiongozi wao Dambuza Mulele, alikuwa na sauti nzito hivyo alikuwa ‘akichombeza’ maneno walipokuwa wakiimba kama afanyavyo Koffi Olomide katika baadhi ya nyimbo zake.
Kiki alisema kwamba mwimbaji Miriam Makeba alipokuwa anaimba, alikuwa anaona kama jina hilo halikumstahili kuitwa.
Akawaza kama angelipewa fulsa ya kumtafutia jina linaloendana na hadhi yake.
Kwa bahati nzuri wakati akiwaza hivyo, akasikia kiongozi wa bendi hiyo akipaza sauti akisema anapenda kumwita mwanamama huyo ‘Chocolate girl’.
“Kwa kweli nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki, nimeona shoo nyingi za Kimataifa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile nilichokiona siku hiyo kwa Miriam Makeba...” alisisitiza King Kiki.
Akiwa bado masomoni mwaka 1958, alijiunga na kikundi cha watoto wenzake cha Bantu Negro, waliweza kubadili muziki huo kwenda kwenye muziki wa rhumba.
Bendi ya Bantu Negro ilikuwa ikifanya maonesho ambayo watazamaji walikuwa wanaketi wakiwatazama na kusikiliza jinsi vijana hao wanavyo poromosha muziki wakitumia ala.
Akiwa shuleni hapo, alikuwa akipendekezwa kufanya fani mbalimbali zikiwemo za maigizo, ngoma kuimba na kucheza.
Kikumbi alijiunga na masomo ya sekondari kidato cha kwanza katika shule ya Attene Iwayala, mwaka 1960 alikosoma hadi kidato cha tatu.
Alikuwa akikumbana na kizingiti kikubwa toka kwa wazazi wake ambao hawakupenda kabisa awe mwanamuziki, walimtaka aendelee na masomo shuleni.
Kikumbi anakiri kuwa muziki ulikuwa umemuingia ndani ya damu, akawa akipigwa na wazazi wake ili aende shule lakini hakubadili msimamo wake.
 “Kaka yangu alikuwa akinifunga kamba kwenye baiskeli huku akinikimbiza umbali wa Kilometa takribani 20, kama adhabu ya kutokwenda shule lakini yote hayo haikusaidia…” alitamka Kiki huku akitabasamu.
Alisema ukali wa kaka na wazazi wake alilazimika kutoroka nyumbani na kwenda kujihifadhi kwa marafiki zake.
Usemi usemao kwamba “Uchungu wa mwana ajuwae mzazi” ulijidhihirisha pale wazazi wa Kiki kuaona kwamba kijana wao mwenye akili sana darasani ameshindikana.
Baba yake alimuweka chini akamuuliza iwapo atakuwa tayari kufanya kazi nyingine yeyote tofauti na muziki.
Pasipo woga mbele ya baba huyo, Kiki alimjibu kwamba muziki umemteka sana na kwamba atakufa nao.
Kwa majibu hayo baba yake akawa hana jinsi, ila ilimbariki na kumtakia mafanikio mema.
 “Baba aliposema hivyo, niliruka ruka kwa furaha, nikajihisi kama nilikuwa naelea katika dunia ya wapenda muziki…” anasema Kiki.

Kwa kuwa Kiki muziki ulikuwa umemtawala sana, mwaka 1962 ilimlazimu kuacha shule akiwa Sekondari kidato cha tatu, akaanza kuimba rasmi mwaka huo.
Katika mazungumzo hayo, Mwanza Mpango aliwataja wanamuziki wakongwe waliomfanya kubadili mfumo wa muziki akiwa katika bendi ya Norvella Jazz.
Aliwataja akina Tchamala Kabasele Joseph ‘Grand Kale’, Tabu Ley na Fanco Luambo Makiadi.
Walilazimika kutafuta vyombo vingine vizuri vya muziki, hivyo wakapita katika vikundi mbalimbali hadi wakafika mkoa wa Kasai (Mbudji Mai).
Huko walikutana na vikundi mbalimbali kutoka mkoa wa Kinshasa vya African Jazz, Conga Success, Negro Success, Eco Bantu, African Fiesta vita na vingine mbalimbali, vilivyomfanya kupata uzoefu zaidi katika muziki wa rhumba mwaka 1965.
Mwaka 1968 Kiki alirudi mkoa wa Katanga ambako alikutana na wanamuziki wa bendi ya Videt Jazz, iliyokuwa ikitoka nchini Zimbabwe.
Mwanza Mpango alisimulia Kaka yake aliyekuwa na bendi yake, iliyomzidishia hamasa katika muziki.

Aliwakumbuka baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakifanya kazi na kaka yake ambao ni Zapta Mfana, Kumaro Kadima, Andre Kaka na Joseph Kolomba.
“Naweza kusema hao walinipa ujuzi mkubwa kwani nilijifunza kupiga vyombo pamoja nao, hapo ndipo nilipopenda kucheza, sikuwa mnene kama nilivyo sasa ungeniona ungefurahi…” alisema Kikii akiyatikisa maungo yake yaliyojaa minofu.
Alieleza kuwa ipo picha ya video iliyorekodiwa wimbo wa ‘Kasongo rudia’ wanaonekana yeye, Chinyama Chiyaza, Mtombo Lufungula, Mbuya Makonga, Kanku Kelly wakicheza kwa kupishana huku na kule wakati huo bado vijana.

Kuna wakati Kikumbi alikuwa akipata mialiko ya huku na kule kiasi cha kutambuliwa na Wakurugenzi wa makampuni ambao walimuahidi kumpatia vyombo vya muziki.
Kwa ujasiri wa aina yake alikuwa akikataa. Hakuwa tayari kufanya kazi chini ya kampuni ya mtu, akijielekeza katika kutafuta njia ya kujikwamua mwenyewe kwa kutumia jasho lake.
 “Nikiwa napiga muziki kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baadhi ya pesa nilizokuwa nikizipata nilipelekea kwa baba yangu kumuonesha kuwa muziki unalipa…” Kiki alitamka.
Hata hivyo wazazi wake pamoja na kuzipokea pesa hizo, bado walikuwa wakimshauri kwamba anayo nafasi ya kurudi shule kuendelea na masomo.
Kauli hizo za wazee wake akaona bora awe mbali na nyumbani. Mwaka 1964 akaenda mkoa wa Kasai ambako alijiunga na bendi ya Norvella Jazz alikopiga muziki hadi mwaka 1967.
Baadaye bendi hiyo kasambaratika naye mwaka 1968 akarudi mkoa wa Katanga.
Alikuwa mwanamuziki Fred Ndala Kasheba aliyemkaribisha King Kiki kujiunga katika bendi ya Orchestra Fouvette.
Alipojiunga na bendi hiyo Kiki alianza kuimba nyimbo mbili zilizotamba sana, nazo ni ‘Jacqueline’ na ‘Kamarade ya Nzela’ ambazo ndiyo zilizompa nafasi ya kufuatana na bendi ya Fouvette kuja nchini Tanzania.

Ikiwa hapa nchini bendi hiyo iliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi katika maonesho yao kadhaa.
Bendi hiyo baada ya kufanya maonesho hayo, ilirejea kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako waliamua kubadili jina ikaitwa Safari Nkoi.
Mwaka 1977 Kikumbi Mwanza Mpango akiwa kwao DRC, alifuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, aliyekuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa tayari ipo katika jiji la Dar es Salaam.
Kiki hukukurupuka kukubali bali alianza kumhoji Mzee Paul iwapo Wanamuziki waliopo Maquis du Zaire wanakidhi viwango.
Majibu ya Mzee Paul yalionesha wasiwasi, ndipo yeye akapendekeza wachukuliwe wanamuziki wengine toka huko DRC.
Kiki aliwapendekeza wanamuziki wa kuondoka naye kuja nchini Tanzania akiwemo Kanku Nkashama Kelly, Mutombo Sozy na Ilunga Banza ‘Mchafu’.
Wakiwa safarini kuja nchini, walipitia mji wa Kamina ambako walimpata mwanadada Ngalula Tshiandanda, aliyekuwa mnenguaji katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo.
Bendi ya Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki Chinyama Chiaza ‘Chichi’.
Iliingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1970 kwa mbwembwe nyingi ikipiga muziki kwa mtindo wa ‘Chakula chakula Kapombe’
Baada ya kutua Maquis, Kiki alianza kuonesha cheche zake baada ya kubuni mtindo wa Kamanyola ambao baadaye ukawa gumzo katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.
Alieleza maana halisi ya Kamanyola akisema Kamanyola ni mji huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
“Nilitunga mtindo huo baada ya kujiunga na bendi hiyo mwaka 1977, niliongeza maneno ya ‘bila jasho’. Kwa maana mchezaji wa muziki huo atacheza taratibu kwa raha zake huku akijidai…” Kiki alifafanua.
Mwaka huo huo wa 1977, sherehe za sikukuu ya Wakulima kitaifa zilifanyika mkoani Mbeya. Bendi ya Maquis du Zaire ilialikwa kwenda kutoa burudani. Baada ya kurejea Dar es Salaam, walitunga wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’.
Kwenye wimbo huo, sauti ya King Kiki inasikika akianza kwa kughani.
Umahiri wa kutunga na kuimba Kiki aliedelea kuachia vibao vya ‘Nimepigwa Ngwala’, Kiongo na ‘Kyembe’.
Baadhi ya nyimbo nyingine alizoshiriki kutunga na kuimba ni pamoja na Kasongo, Kibwe Mutondo, Sofia, Mokili, Yoka Mateya Babote, Dora mtoto wa Dodoma, Sababu ya Nini, Usinifiche siri na Noele Krismas.
Bendi ya Maquis du Zaire kabla ya kusambaratika ilikuwa ikiporomosha muziki maridadi katika ukumbi wa White House, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Safu ya waimbaji wenzake wakati huo walikuwa ni akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’,  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Kiniki Kieto, na Masiya Radi ‘Dikuba Kuba’. Safu hiyo ilikamilishwa kwa waimbaji Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.
Waswahili wanasema “Chema Chajiuza” Usemi huo ulijidhihirisha baada ya miaka miwili, akatafutwa na mfanyabiashara maarufu katika jiji hilo la Dar es Salaam, Hugo Kisima.
Kisima alikuwa mmiliki wa ukumbi wa Safari Resort na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS), iliyokuwa na makao yake katika huko Kimara, jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao waliafikina kuondoka katika bendi ya Maquis du Zaire, akajiunga na OSS, baada ya ‘kumegewa’ kitita cha fedha.
Baada ya kuingia OSS, alishirikiana vyema na waimbaji wa bendi hiyo akina Skassy Kasambula, Monga Stani Liki, Dingituka Molay, Mobali Jumbe, Kalala Mbwebwe, Tshibanda Sony na Kabeya Badu.
Aidha Kiki alitambulisha mtindo mpya wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’.
Kiki pamoja na tungo zake nyingi kuna kumbukumbu zisizosahaulika katika enzi za mtindo wa Masantula, alipotunga na kuimba nyimbo za Mimi msafiri, Mama Kabibi na Kitoto kaanza tambaa.
Wimbo wa Mimi msafiri alikuwa akijibashiria kuwa bendi hiyo ndiyo ingelikuwa ya kuzeeka nayo. Lakini mambo hayakuwa hivyo kwa kuwa aliamua kujikwamua badala ya kuajiriwa.
Alianzisha bendi yake ya King Kiki Double O, iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa shika Breki’.
Kiki katika bendi hiyo aliachia vibao baadhi yake ni pamoja na Njigina, Salamule, Mtoto wa Elia, Sababu ya Nini na Malalamiko. Bendi hiyo haikudumu kwa kipindi kirefu, ikisambaratika kwa sababu ya uchakavu wa vyombo.
Baada ya kusambaratika bendi hiyo, Kiki aliitumia talanta yake katika muziki akawa msanii mgeni au mwalikwa katika bendi mbalimbali.
Moja kati ya bendi ambazo alikuwa akishiriki maonesho yao bila kuajiriwa, ilikuwa ni ya Orchestra Sambulumaa ‘Wana Zuke Muselebende’.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na mfanyabiashara Emmanuel Mpangala pamoja na mwanamuziki Chimbwiza Mbambu Nguza ‘Vicking’, aliyekuwa ameiacha bendi ya Maquis du Zaire.
Kiki alifanya shughuli hiyo kwa takribani miaka minne, akaondoka kwenda kuungana na Fred Ndala Kasheba. Kwa umoja wao wakaunda bendi ya Zaita Musica mwaka 1994 iliyokuja kuwa maarufu hususani baada ya kuachia wimbo wa ‘Kesi ya Kanga’. Hapo ndipo mtindo wa ‘Kitambaa Cheupe’ ulipozaliwa.  
Mwaka 2003 akiwa na Ndala Kasheba walianzisha bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’. Lakini kwa mapenzi ya mungu mwenzangu Kasheba akafariki dunia mwaka mmoja baadaye, yaani 2004…”
Bendi hiyo bado inauendeleza mtindo wa Kitambaa cheupe hadi.
Alisema mtindo huo umeiletea bendi yake wateja wengi wanaopenda muziki wa kistaarabu wakicheza na vitambaa vyeupe mikononi.
Alifafanua kitendo cha kuweka Kitambaa Cheupe ni kama ishara ya upendo na amani.
Kikumbi alishirikana vyema na mtunzi na mwimbaji mahiri Baziano Bwetti, ambaye pia walikuwa wote katika bendi ya Orchestra Fouvette.
Baada ya kuishi kwa muda mrefu humu nchini, aliamua kuomba Uraia wa Tanzania. Kiki alizifuata taratibu zote za Idara ya Uhamiaji, hadi mwaka 1997, alipokubaliwa kuwa raia halali wa Tanzania.
Kiki na bendi yake hiyo miaka ya 2000, walifanikiwa kwenda katika jiji la London nchini Uingereza, ambako waliporomosha muziki maridadi kwa Wantanzania waishio huko.
Baada ya kurejea nchini, akatunga wimbo uliopewa jina la ‘Safari ya London’.
Katika wimbo huo uwalielezea jinsi safari yao ilivyofana wakiwataja baadhi ya watu waliofanikisha ziara hiyo wakiwemo baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Ukisikiliza mirindimo ya wimbo huo, hataitofautisha sana na ile ya wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’.
Baada ya kukongwa na nyoyo za baadhi ya mashabiki na wapenzi wake walimpachaki majina ya ‘Bwana Mukubwa’.
King Kiki anayo imani kwamba bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyoundwa mwaka 2003, ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa sasa.
Alipoulizwa nini  kilichomshawishi zaidi kuwa mwanamuziki.
Kiki alieleza kuwa alishawishika kuingia kwenye muziki akiwa na miaka sita, baada ya kumshuhudia mwanamama Miriam Makeba, toka Afrika ya Kusini alipofanya maonesho nchini mwake.
Kikumbi akiwa na tabasamu alitamka siri ya kung’aa kwake licha ya umri wake wa miaka 69 sasa alizema
“…inawezekana kung’aa kwangu katika muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa Januari Mosi, saa 11 alfajiri.”

Kikumbi ‘alijifagilia’ bendi yake ya La Capitale iliyoundwa mwaka 2003, kuwa ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa sasa, na huenda ikawa ndiyo atakayozeekea nayo.
Aidha Kiki aliweza kusimulia siri ya mafanikio ya kung’ara kwake akisema
“…inawezekana kung’aa kwangu katika muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa Januari Mosi, saa 11 alfajiri…” 
Akiainisha baadhi ya mafanikio aliyokwisha yapata  katika muziki kuwa ni pamoja na kuweza kusafiri kwenda kufanya maonesho katika mataifa mbalimblai makubwa duniani  likiwemo la Marekani. Kiki alitamka kuwa alipokuwa huko Marekani, aliweza kukidhi kiu ya Waafrika waishio huko alipoporomosha ‘bonge la shoo’ akiwashirikisha wanamuziki wa kundi la Soukuos Stars Lokassa ya Mbongo na Ngouma Lokito.
Aidha alisema ameweza kumudu maisha yake na familiya kwa ujumla pia kumiliki bendi mbili nyingine ipo katika jiji la Mwanza.
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ni baba wa familiya ya mke na watoto kadhaa. Kati yao ni binti mmoja pekee aliyefuata nyayo za baba yake katika uimbaji.
Nguli huyo alionesha kujali ukweni kwake mkoani Mbeya, alipotunga na kuimba wimbo wa Barua. Katika wimbo huo anaagiza kufikishiwa salamu afikapo Igulusi, Uyole, Makambako na kwingineko.
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ bado anaendeleza talanta yake ya muziki katika jiji la Dar es Salaam na kwingine anako alikwa.
   
Mwisho.

Tuesday, September 6, 2016

KWAHERI BANZA STONE



BURIANI RAMADHANI MASANJA  “BANZA STONE” KAULI HII NINAITOA KWA DHATI KWA ALIYEKUWA MWANAMUZIKI HUYO MAHIRI, ALIYEFARIKI DUNIA HIVI KARIBUNI.

KABLA YA KIFO CHAKE BAADHI YA WATU WALIKUWA WAKIMZUSHIA KIFO MARA KWA MARA, NDOTO ZAO ZILITIMIA IJUMAA YA JULAI 17, 2015 BAADA YA BANZA STONE KUIAGA DUNIA AKIWA NYUMBANI KWAO SINZA JIJINI DAR ES SALAAM. 

SIKU ILIYOFUATIA YA JUMAMOSI JULAI 18, 2015, TARATIBU ZOTE ZA DINI YA KIISLAMU ZILIFANYIKA. RAMADHANI MASANJA ‘BANZA STONE’ AKAZIKWA KATIKA MAKABURI YA SINZA JIJINI DAR ES SALAAM.
MARADHI YALIPELEKEA KULAZWA KATIKA HOSPITALI YA MWANANYAMALA NA KUGUNDULIKA KUWA NA UGONJWA WA SARATANI YA UBONGO.

ALIWAHI KUWALALAMIKIA MARA KADHAA BAADHI YA WATU WALIOKUWA ‘WAKIMCHULIA’ KIFO. 

AKISEMA ANAJISIKIA VIBAYA SANA NA SI JAMBO JEMA KUZUSHIWA KIFO.

BANZA AKIZUNGUMZA KWA TABU ALITAMKA KWAMBA ANATAMANI APONE ILI ARUDI JUKWAANI, HIVYO MAOMBI YAO YALIKUWA NI MUHIMU KULIKO KITU CHOCHOTE NA NI MSAADA TOSHA KWAKE.

“KIKUBWA NAWAOMBA WATANZANIA WANIOMBEE KWANI HALI NILIYONAYO SIYO YA KAWAIDA, NASIKIA MAUMIVU MAKALI SANA YA KICHWA NA SHINGO HADI NASHINDWA KULA…” BANZA ALIKUWA AKITAMKA KWA TABU AKIWA KWENYE KOCHI.

ALIELEZA KUWA HATA KUONGEA KWAKE NI SHIDA NA MUDA MWINGI ALIKUWA AKIWEKA KITAMBAA CHA MAJI YA BARIDI KWENYE PAJI LA USO ILI KUPUNGUZA MAKALI YA MAUMIVU.

WASIFU WA BANZA UNAELEZA KUWA ALIZALIWA KATIKA HOSPITALI YA OCEAN ROAD, JIJINI DAR ES SALAAM, OKTOBA 20, 1972.

NI MTOTO WA TISA KATI YA 11 KATIKA FAMILIA YAO, AYELIPATA ELIMU YA MSINGI KATIKA SHULE YA MNAZI MMOJA JIJINI DAR ES SALAAM NA ALIFANIKIWA KUMALIZA MWAKA 1987.

BANZA BAADA YA KUMALIZA SHULE, ALIANZA TARATIBU ZA KUJIHUSISHA NA MASUALA YA MUZIKI AKIWA ANGALI MDOGO.

ALIJIUNGA KATIKA MUZIKI WA HIP HOP ULIOKUWA UKISIKIKA KATIKA REDIO.

“MARA TU BAADA YA KUMALIZA ELIMU YANGU YA MSINGI, NILIANZA KUJIHUSISHA NA MUZIKI WA HIP HOP, ENZI HIZO TULIKUWA TUKISIKIA KATIKA REDIO, PIA UKIENDA DANSI UNAKUTANA NA NYIMBO ZA WASANII KADHAA WA HIP HOP. 

WAKATI HUO NILIKUWA NA WENZANGU KAMA KINA K ONE NA SCOZ MAN…” ANASEMA BANZA.

ALIWATAJA BAADHI YA WASANII WENZAKE ALIOKUWA AKIWAKUMBUKA KWA WAKATI HUO WALIKUWA AKINA K ONE NA SCOZ MAN.

ALIELEZA KUWA WAKATI HUO ILIKUWA VIGUMU SANA KUPATA NAFASI YA KUTUMBUIZA ENEO LOLOTE LILE KWANI MUZIKI HUO HAKUKUBALIKA. 

ALIKUMBUKA MWISHONI MWA MWAKA 1989, WALIKUWA WAKIENDA COCO BEACH KUONESHA VIPAJI VYAO VYA KUIMBA MUZIKI WA HIP HOP. 

VIJANA WENGI WALIONESHA KUUKUBALI MUZIKI HUO.

BANZA ALISEMA KUWA ILIKUWA NGUMU SANA KUELEWEKA MBELE YA JAMII KUTOKANA NA MUZIKI HUO WA HIP HOP KUONEKANA KAMA UHUNI.

“TULIKUWA NA KAZI KUBWA YA ZIADA KUFANYA VILE INAVYOTAKIWA, LAKINI BAHATI HAIKUWA YETU WAZAZI WALILETA KIPINGAMIZI. 

HATA HIVYO TULIONEKANA KAMA VIJANA WA KIHUNI….” ANASIKITIKA MASANJA.

JAPO ALIPENDA SANA MUZIKI, WAZAZI WAKE WALIWEKA PINGAMIZI BAADA YA KUONEKANA MUZIKI HUO WA HIP HOP KUWA NI WA KIHUNI.

MWAKA 1990 AKAAMUA KUANZA MCHAKATO MPYA WA ‘KUNENGUA’ MUZIKI WA DANSI, AMBAPO ALIKUWA AKICHEZA KWENYE HARUSI NA KUFANIKIWA KUPATA FEDHA KIDOGO.

MWAKA 1995 BANZA ALIJIUNGA KATIKA BENDI ILIYOCHINI YA KAMPUNI YA AFRICAN STARS ENTERTAINMENT TANZANIA (ASET) YA TWANGA PEPETA KABLA YA KUCHEPUKIA KATIKA BENDI YA EXTRA BONGO ILIYOKUWA IKIONGOZWA NA ALLI CHOKI.

BANZA ALIONESHA KUPEVUKA KIFIKRA MWAKA 2000, ALIPOMUA KWENDA KUPATA MAFUNZO YA MUZIKI SEHEMU TOFAUTI IKIWEMO KITUO CHA UTAMADUNI CHA WATU WA KOREA.

AIDHA ALIPOKUWA KATIKA BENDI YA TOT, WANAMUZIKI WAKE WALIPELEKWA KUAPATA MAFUNZO HAYO KATIKA CHUO CHA SANAA BAGAMOYO AKIWEMO YEYE.

BAADA YA KUHITIMU ALIANZA KUIMBA KATIKA BENDI MBALIMBALI ZIKIWAMO ZA THE HEART STRINGS, BENDI ZA TWIGA  NA ACHIGO, AKIWA MPIGA NGOMA PAMOJA NA  AFRI-SWEZ NA ZINGINE NDOGO NDOGO.

KATIKA BENDI HIZO ZOTE HIZO ALIKUWA AKIDUMU KWA MIEZI KADHAA, KABLA YA KUHAMIA KATIKA BENDI NYINGINE HADI ALIPOINGIA KATIKA BENDI YA THE AFRICAN STARS, “WANA TWANGA PEPETA” AKAWA NA AHUWENI YA MAISHA.

SOKO LA BANZA LILIKUWA KUBWA HIVYO BAADA YA KUIPAISHA TWANGA PEPETA KWA KIASI KIKUBWA, ALICHUKULIWA KWENDA KUJIUNGA KATIKA KUNDI LA TANZANIA ONE THEATRE (TOT) “WANA ACHIMENENGULE”

AKIWA HAPO ALIJULIKANA ZAIDI KWA JINA LA ‘MWALIMU WA WALIMU’ JAPO NAKO HAKUKAA SANA.

RAMADHANI MASANJA ‘BANZA STONE’ ALIAMUA KUANZISHA BENDI YAKE ILIYOKUWA IKIITWA BAMBINO SOUND. 

KWA BAHATI MBAYA BENDI HIYO ILIDUMU KWA MIEZI KADHAA KABLA YA KUSAMBARATIKA KUTOKANA NA UONGOZI MBOVU.

ALIWAHI KUELEZEA KWAMBA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 23 TANGU AANZE MUZIKI WA DANSI RASMI, HAIKUWA RAHISI KWAKE KUPATA MAFANIKIO MAZURI LICHA YA KUZUNGUKA SANA KUTAFUTA MAISHA.

BANZA STONE ALIPITIA ZAIDI YA BENDI TISA IKIWEMO RUFITA BAND.

MWAKA JANA 2014, MSANII WA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA, HAMISI RAMADHANI ‘H-BABA’ ALIMSHIRIKISHA BANZA KUREKODI WIMBO WAKE MPYA WA ‘SINA RAHA’

BANZA STONE HATUNAE TENA HAPA DUNIANI, LAKINI AMETUACHIA UKUMBUSHO WA NYIMBO NYINGI ZAILIZOWAHI KUTAMBA. BAADHI YAKE ZIKIWEMO ZA MTAJI WA MASKINI, KUMEKUCHA, ELIMU YA MJINGA, ANGURUMAPO SIMBA MCHEZA NANI NA FALSAFA YA MAISHA.

RAMADHANI MASANJA ALIKUWA ‘MSANII WA UKWELI’ KWANI ALITHUBUTU KUIMBA VIBAO KADHAA VYA TAARABU UKIWAMO ‘KUZALIWA MJINI’ NA ULE WA ‘PLAY BOY’

BANZA ALIYEANZA MUZIKI MIAKA 25 ILIYOPITA, MAPEMA  ALIELEZA JINSI ALIVYOHANGAIKA ILI KUFIKIA KUWA MWANAMUZIKI MKUBWA HADI KUJULIKANA. ALISEMA ALIFANYA SUBIRA ILI KUTIMIZA DOTO ZAKE ZILIZOKUJA  HATUA KWA HATUA.

MWAKA 1990 WALIAMUA KUANZA MCHAKATO  MWINGINE WA KUWA WANENGUAJI WA MUZIKI WA DANSI. ALISEMA KUWA  WALICHEZA SANA KWENYE MAHARUSI NA WALIFANIKIWA KUPATA FEDHA KIASI.

BANZA ALIFAFANUA KUWA WALIKUWA WAKIFANYA MAONESHO KWA MUDA MREFU KIDOGO NA WAKATI HUO WALIKUWA WAKICHEZA KWA KUFUATISHA NYIMBO ZA WANAMUZIKI KUTOKA NJE, KAMA WA MICHAEL JACKSON NA WENGINEO.

“MWAKA 1995 NILIINGIA TWANGA PEPETA, WAKATI HUO BENDI HIYO ILIKUWA BADO CHANGA SANA, TULIANZA KWA KUTOA ALBAMU YA KISA CHA MPEMBA” NA KUENDELEA KUKUA ZAIDI KIMUZIKI MPAKA KUFIKIA KATIKA HATUA YA BENDI BORA YA MUZIKI WA DANSI NCHINI WAKATI HUO ILIKUWA NI MWISHONI MWA MIAKA YA 1990…” ANASEMA BANZA ALIYEVUMA NA WIMBO WA KUMEKUCHA, ULIOKUWA WA KWANZA KUTUNGA NA KUREKODI STUDIO MWAKA HUOHUO.

ANASEMA HAPO NDIPO SAFARI YA MUZIKI ILIPOANZA, ALIAMUA KUENDELEA NA SHULE YA MUZIKI BAADAE MWAKA 2000, ILI KUONGEZA UJUZI NA MAARIFA KATIKA KAZI YAKE. 

BAADAE ALIICHA BENDI YA TWANGA NA KUTIMKIA KATIKA BENDI TANZANIA ONE THEATER (TOT PLUS) AMBAKO NYOTA YAKE ILIZIDI KUNG’ARA.

AKIWA TOT PLUS, ALISHIRIKIANA NA WAKALI WENGINE WAKIWEPO ABDUL MISAMBANO, PAPII KOCHA NA WENGINE WENGI WALIOSABABISHA KUWEPO UPINZANI MKUBWA WA KIMUZIKI DHIDI YA TWANGA PEPETA.

WAKATI HUO NDIPO BANZA ALIPOTOA ‘RAP’ MPYA WA ‘ULIONA WAPI TINGATINGA LIKAENDA KWENYE STAREHE’ KIKIA NI KIJEMBE  KWA RAFIKI YAKE WA KARIBU ALLY CHOKI AMBAYE WAKATI HUO ALIKUWA TWANGA PEPETA.

CHOKI KUNA KATIKA UZINDUZI WA MOJA YA ALBAMU, ALIINGIA KATIKA UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE AKIWA JUU YA KIJIKO AU TINGATINGA.

MBALI YA RAP HIYO AKIWA TOT, BANZA  PIA ALITUNGA VIBAO KAMA ELIMU YA MJINGA NI MAJUNGU, MTAJI WA MASKINI NGUVU ZAKE MWENYEWE,  ANGURUMAPO NA SIMBA SEHEMU YA PILI.

BANZA ALITUA TOT PLUS 1999 CHINI YA UKURUGENZI WA KAPTENI JOHN KOMBA (SASA MAREHEMU), AMBAYE ALIMCHUKUA MWIMBAJI HUYO ILI KULIIMARISHA KUNDI HILO LIWEZE KUPAMBANA NA TWANGA PEPETA.

MWAKA HUOHUO  BANZA ALIREJEA KATIKA BENDI YA TWANGA PEPETA AMBAKO ALIKUTANA NA ALLI CHOKI PAMOJA LUIZA MBUTU CHINI YA UONGOZI WA MKURUGENZI ASHA BARAKA, ILIPOEDELEA KUPATA UMAARUFU MKUBWA ZAIDI. 

WIMBO KAMA ANGURUMAPO SIMBA, KISA CHA MPEMBA, MTAJI WA MASKINI, ELIMU YA MJINGA, MTU NA PESA ZAKE NA NYINGINE NYINGI ZILIZOVUMA NA KUIPA UMAARUFU BENDI HIYO NI KIELELEZO HALISI CHA  UWEZO ALIOKUWA NAO MAREHEMU BANZA STONE, KIASI CHA KUJIPATIA UMAARUFU AMBAO SASA KIFO CHAKE KIMELETA SIMANZI KWENYE TASNIA HIYO.


BANZA STONE HUKO ALIJULIKANA ZAIDI KWA JINA LA ‘MWALIMU WA WALIMU’ JAPO HAKUKAA KWA MUDA MREFU KATIKA BENDI HIYO. 

BAADAYE MWANAMUZIKI HUYO ALIONDOKA TOT PLUS NA KWENDA KUANZISHA KUNDI LAKE LA BAMBINO SOUND AMBAKO ALITOKA NA KIBAO CHA ‘MIMI NISEME NA WEWE USEME NANI ATAMSIKILIZA MWENZIE? 

 “BENDI YANGU ILIKUWA INAITWA BAMBINO SOUND, AMBAYO ILIDUMU KWA MIEZI KADHAA TU, LAKINI ILIVUNJIKA KUTOKANA NA  KUTOKUWA NA UONGOZI MZURI, HAIKUWA NA MTU MAKINI HILO NDILO LILIANGUSHA BENDI HII, HATIMAYE NIKARUDI TENA AFRICAN STARS BAND. 

BAADAYE NILIENDA EXTRA BONGO…” ALISEMA BANZA KATIKA MAHOJIANO WAKATI WA UHAI WAKE. BENDI HIYO HAIKUDUMU KWA KIPINDI KIREFU, IKAFA.

BANZA STONE ALIKUWA MWIMBAJI, MTUNZI NA RAPA WA MUZIKI HUO NCHINI, PIA ALIANIKA IDADI YA BENDI ALIZOPITIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 23 TANGU AANZE MUZIKI WA DANSI RASMI.

AMEWEKA WAZI KWAMBA ALIPITA KUPIGA MUZIKI KATIKA BENDI ZAIDI YA BENDI TISA, KATIKA HARAKATI ZAKE ZA ZA MUZIKI.

ALIWAHI KUTUNGA NA KUIMBA NYIMBO AKIWA KATIKA BENDI YA TWANGA CHIPOLOPOLO NA RUFITA JAZZ KABLA YA KUJIUNGA NA EXTRA BONGO, INAYOONGOZWA NA ALLY CHOKI.

MWAKA 2003 BANZA ALIKUWA MIONGONI MWA WANAMUZIKI WATATU NGULI NCHINI, WENGINE WAKIWA ALLY CHOKY NA MUUMINI MWINJUMA WALIOIBUKA NA ZING ZONG YAO ILIYOANDALIWA NA MOHAMED MPAKANJIA (SASA MAREHEMU).

MWAKA MMOJA BAADAYE BANZA ALIREJEA TENA TWANGA PEPETA NA KUIBUKA NA KITU KIKALI KILICHOJULIKANA KAMA ‘MTU PESA’ HUKU AKIACHIA TENA KIBAO CHA ‘HUJAFA HUJASIFIWA’, AMBACHO ALISEMA ALITUNGA BAADA YA MARA KADHAA KUZUSHIWA KIFO.

NGULI HUYO ALISEMA KUWA ALIKWISHA REKODI VIBAO KADHAA ALIVYOIMBA KWA MTINDO WA HIP HOP. KATI YA HIZO UPO WIMBO ALIOUTENGENEZA AKIWA NA CHID BENZ MIAKA MIWILI ILIYOPITA AMBAO HAKUFANIKIWA KUUTOA.

“NINA WIMBO AMBAO HAUJATOKA, LAKINI NIMESHAACHIA WIMBO MMOJA MSHENGA, NILIOREKODI NA MAN DOJO NA DOMO KAYA AMBAO HAUKUFANIKIWA KUFANYA VIZURI KATIKA CHATI ZA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA…” ALITAMKA MASANJA BANZA STONE.

WIMBO MWINGINE ALIOREKODI NI SEMA UNACHOTAKA ALIOIMBA AKISHIRIKIANA NA GODZILLA. HUO ALIPANGA KUUPELEKA REDIONI MWAKA HUU.

MAREHEMU BANZA  ATAKUMBUKWA KWA MENGI KUTOKANA NA UMAHIRI WAKE WA KUIMBA NA KUTUNGA NYIMBO AMBAZO ‘ZILIWABAMBA’ MASHABIKI WA MUZIKI HUO NA KUJIKUTA AKIWA KIPENZI CHA WATU WENGI WA MUZIKI WA DANSI.

MSANII MWENZAKE  ALIYEFANYA NAYE KWA UKARIBU, ALLY CHOKI  ALISEMA KUWA BANZA STONE ALIKUWA NA KIPAJI CHA KIPEKEE NA ALIKUWA CHACHU KUBWA YA KUKUA KWA MUZIKI WA DANSI TANGU ALIPOJITUMBUKIZA KWENYE TASNIA HIYO 1991 AKIANZIA KAMA MNENGUAJI KWENYE KUNDI LA SINZA STARS.

ALISEMA KUWA KUNA KIPINDI ALIWAHI KUWA MPINZANI MKUBWA WA BANZA STONE KWENYE USHINDANI WA MUZIKI, ALIKUWA AKIVUTIWA NA UIMBAJI WA BANZA. 

ALILAZIMIKA KUFANYA MAZOEZI YA ZIADA ILI AWEZE KUHIMILI USHINDANI KUTOKA KWA MKALI HUYO AMBAYE NYOTA YAKE IMEZIMIKA GHAFLA.

“MWAKA 1995 NILIINGIA TWANGA PEPETA, WAKATI HUO BENDI HII ILIKUWA BADO CHANGA SANA, TULIANZA KWA KUTOA ALBAMU YA KISA CHA MPEMBA NA KUENDELEA KUKUA ZAIDI KIMUZIKI, MPAKA KUFIKIA KATIKA HATUA YA BENDI BORA YA MUZIKI WA DANSI NCHINI WAKATI HUO ILIKUWA NI MWISHONI MWA MIAKA YA 1990,” ANASEMA BANZA ALIYEVUMA NA WIMBO WA KUMEKUCHA, ULIOKUWA WA KWANZA KUTUNGA NA KUREKODI STUDIO MWAKA HUOHUO.

LICHA YA KUWA MWANAMUZIKI BORA WA MUZIKI WA DANSI BANZA STONE ANASEMA, “…NASHINDWA KUKUA ZAIDI KATIKA MUZIKI KUTOKANA NA MARADHI YANAYONISUMBUA, MUDA MWINGI NINAKUWA KITANDANI, HIVYO NASHINDWA KUENDELEA VIZURI KATIKA KAZI ZANGU, KIPINDI CHA HIVI KARIBUNI NILIPUMZIKA MUZIKI KWA MIEZI KADHAA LAKINI MUNGU MKUBWA KWANI HIVI SASA NINAENDELEA VIZURI…”

BANZA BAADA YA KUPATA AHUWENI ALIREJEA TENA KATIKA BENDI YAKE ALIYOKUWA AKIITUMIKIA YA EXTRA BONGO NA ALITARAJIA  MAMBO MAKUBWA ZAIDI. 

“NATARAJIA KUFANYA KAZI AMBAYO MASHABIKI WATAFURAHIA, TUMESHAZINDUA ALBAMU YA ‘MTENDA AKITENDEWA’ NA ‘KINACHOSUBIRIWA’ HIVI SASA NI KAZI MPYA, TAYARI NINA VIBAO KADHAA AMBAVYO VITATOKA MAPEMA MWAKA HUU...” ALISEMA BANZA STONE.

AKIWA NA EXTRA BONGO, BANZA ALIKUWA AKITAMBA NA KIBAO CHAKE KINACHOJULIKANA KWA JINA LA ‘FALSAFA YA MAISHA’. PIA ALIKUWA AKIIMBA NYIMBO ALIZOWAHI KUTAMBA NAZO KATIKA BENDI MBALIMBALI.

MWAKA JANA 2014,  MSANII WA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA HAMISI RAMADHANI ‘H-BABA’ ALIAMUA KUMSHIRIKISHA BANZA KUREKODI WIMBO WAKE MPYA WA SINA RAHA.

KIBAO HICHO KIMO KWENYE ALBAMU MPYA YA MSANII HUYO INAYOJULIKANA KWA JINA LA ‘SHIKA HAPA, ACHA HAPA’.

RAMADHANI MASANJA  ALIWAHI KUTAMBA NA NYIMBO KADHAA ZIKIWEMO ZA MTAJI WA MASKINI, KUMEKUCHA, ELIMU YA MJINGA NA ANGURUMAPO SIMBA MCHEZA NANI.

PIA ALIWAHI KUIMBA VIBAO KADHAA VYA TAARABU UKIWAMO KUZALIWA MJINI NA ULE WA PLAY BOY.
HAPANA SHAKA KWAMBA BANZA STONE AMEACHA ALAMA KATIKA MUZIKI WA DANSI, NYIMBO ZAKE ZITAENDELEA KUISHI NA KUWA KUMBUKUMBU NA ELIMU KWA JAMII.

KABLA YA KULAZWA HOSPITALINI BANZA TAYARI ALIKUWA AMEKWISHA KATA TAMA YA KUISHI. 

ALIWAHI KUTAMKA KWAMBA AMEKATA TAMAA YA KUISHI KWA VILE AMEOTA NDOTO KUWA MWISHO WAKE WA KUISHI DUNIANI UMEKARIBIA.

ALISEMA ALIOTA NDOTO  ANAKUFA NA AMEONESHWA JINSI KIFO CHAKE KWAMBA ATAUGUA GHAFLA NA KUFARIKI DUNIA.

NYOTA HUYO ALISEMA KUFUATIA ‘MAONO’ HAYO, AMEANZA KUTUNGA NYIMBO AMBAZO ZITAZUNGUMZIA HISTORIA YA MAISHA YAKE.

“NI KWELI NAONA MWISHO WANGU UMEKARIBIA, NIMEONESHWA NDOTONI, INAWEZEKANA NI MPANGO WA MUNGU ILI NITENGENEZE MAISHA, NIMESHAANZA KUANDAA ALBAMU ITAKAYOHUSU HISTORIA YA MAISHA YANGU…” ALISEMA BANZA STONE.



BANZA ALISEMA KWAMBA  NDANI YA MOYO WAKE ANA SIRI NZITO AMBAYO ANGELITOA KWENYE MOJA YA NYIMBO ZAKE.


ALIZIDI KUSEMA KWA MASIKITIKO KUWA BAADA YA NDOTO HIYO AMEKOSA RAHA YA KUISHI TENA NA HAJUI YUPO KATIKA ULIMWENGU UPI, KWANI ANAFIKIRIA MAISHA YA ULIMWENGU MWINGINE ATAKAOELEKEA.

“YAANI MAWAZO YANGU HAYAPO HAPA, SIJUI NIKO DUNIA GANI, NIMEKATA TAMAA, NINAUONA MWISHO WA MAISHA YANGU UPO KARIBU LAKINI SIOGOPI, NATAMANI KUFA KWA SABABU NI LAZIMA NITAKUFA HATA NIKIISHI MIAKA MINGAPI…” ALISEMA BANZA.


MWAKA JANA 2014, NYOTA HUYO ALIUGUA KWA MUDA NA KULAZWA KWENYE HOSPITALI YA MWANANYAMALA, JIJINI DAR ES SALAAM NA HABARI ZA MARA KWA MARA ZILIKUWA ZIKIZUSHA KUWA AMEFARIKI DUNIA.

LAKINI SIKU YAKE ILIPOWADIA, JULAI 17, 2015 RAMADHANI MASANJA AKAAGA DUNIA.

MUNGU UIWEKE ROHO YAKE PAHALA PEMA PEPONI, AMINA.

SHUKURANI ZA PEKEE ZIWAFIKIA WENYE  MITANDAO WALIONIWEZESHA KUKUSANYA HABARI HIZI.

MWISHO.