Ahmed Kipande (kushoto) akiwa na wanamuziki wenzake wa Kilwa Jazz.
Wanamuziki wa Kilwa Jazz wakiwa pembeni mwa gari lao liliohaibika njiani.
Kwa wale wale wapenda miziki
ya zamani nikiaanza na sehemu ya ndogo ya mashairi ya wimbo huu, ninauhakika
watang’amua ninani nitamzugumzia katika kipindi cha leo cha ‘Enzi hizo’ sikiliza wimbo huu…
“Napenda nipate
lau nafasii, nipate kusema nawe kidogo aah mamaa aah rohoni
inaumiaa, hakika lakufanya bado sijaliona, nimeona leo bora nikuimbee,
huenda punde roho yako ikadundaa ikaja siku ukaja nipoza moyo ooh mama rohoni
naumia…” huyo ni marehemu Ahmedi Kipande akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.
Jumamosi ijayo ya tarehe 27, 2013 Ahmedi Kipande atatimiza miaka 26
tangu aiage dunia Aprili 27, 1987.
Wasifu wa mwanamuziki
huyu umeelezwa kwamba alikuwa
mwanamuziki nguli aliyeshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na
kupigani Uhuru wa Tanganyika
kupitia tasnia ya muziki akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.
Kilwa Jazz ilishiriki
kikamilifu siku Tanganyika
inapata Uhuru Decemba 09, 1961 kwa kuimba wimbo wa kusifia nchi yetu kupata
Uhuru toka wa Wakoloni.
Chini ya uongozi wa Ahmed
Kipande Kilwa Jazz mwaka 1964, ilishiriki kutoa burudani wakati mikakati ya
kuandaa Mapinduzi ya Zanzibar
kwenye maeneo ya makao makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam.
Ahmed Kipande na bendi yake
waliteuliwa na serikali ya Tanganyika
kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa nchi za Malawi
na Uganda.
Ni miaka 26 imetimia tangu
Ahmed Kipande alifariki dunia Aprili 27,
1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kuharusi kwa kipindi kirefu, lakini
ataendelea kukumbukwa kwa mazuri aliyofanya katika taifa hili.
Historia ya mwanamuziki huyu
iliyotolewa na mwanawe wa mwisho Kipande Ahmed, ameeleza kwamba jina kamili
la baba yake alikuwa ikiitwa Ahmed
Mohammed Kipande, aliyezaliwa mwaka 1937
huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi.
Miaka michache baada ya kifo
cha mama yake Ahmed Kipande alifuatana na Baba yake kuja Dar
es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Wavulana ya Uhuru
maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam
ambapo alisoma hadi darasa la nne.
Katikati ya miaka ya 1950
Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo violin, katika bendi ya
Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidasi. Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao
hivi sasa unaitwa mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki wa miaka hiyo
walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz
walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Ahmed Kipande aliyekuwa
akitoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi, akishirikiana na mwanamuziki mwenzake
aliyetajwa kwa jina moja la Shamte nao wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka
Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958.
Kilwa Jazz ikaanza kujizolea
umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbali mbali zikiwemo za siasa, mapenzi na
za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.
Alitunga na kuimba nyimbo za
‘TANU yajenga nchi’, nchi yetu’ ‘enyi
Vijana tujenga yetu, Doli na ‘It can be done, play your party’
Zingine zilikuwa za Nipate
lau nafasi’ Rose waniuwa uwa’, ‘Nacheka cheka Kilwa leo’ na Maneno hayafai’
Wimbo wa Nacheka cheka
ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kukopi wimbo wa John Bokelo na Tabu Ley wakiwa
na bendi ya African Jazz wa ‘Mokolo
Nakokufa’ halikadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo, Rose waua na Maneno
hayafai nazo walikopi na kupesti toka wimbo wa Course au Povouir na Est ce Que za T.P.OK. Jazz.
Mwaka 1973 Kilwa jazz
ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco
Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz iliyefanya onyesho kwenye Uwanja wa taifa
jijini Dar es Salaam.
Luambo Makiadi baada ya
kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake
mkubwa wa ‘kokopi nyimbo hizo.
Kipande Ahmed alisema mwaka
1961 siku Tanganyika inapewa
Uhuru toka kwa Wakoloni, bendi yake ya Kilwa Jazz ilikuwa Uwanja wa Taifa
ikiporomosha muziki ambapo ilitoka na wimbo wa
kumshukuru mungu kwa Tanganyika
kupata Uhuru.
Mtoto huyo wa marehemu Ahmed,
aliimba mistari sehemu fupi ya wimbo huo.
“Ewe
mola tunakuomba uibariki Tanganyika
yetu na jirani zetu, Uhuru tumepata
lakini Nyoyo zinasikitika, wenzetu
wanateseka Wakoloni wamewashika…”
Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa
na makao makuu yake katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako siku moja
ilipiga muziki nje ya Ofisi yao
na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana.
Lakini ilikuwa ni mipango
kamambe ikipangwa na wazee toka Zanzibar maeneo
hayo siku chache kabla ya mapinduzi ya Zanzibar.
Wazee hao walikuwa wakipanga mikakati ya
mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964, huko Zanzibar.
Bendi ya Kilwa Jazz baadaye
haikueleweka miongoni mwa jamii. Wengine wakafika mbali zaidi wakizusha maneno
kwamba ni bendi ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika
shughuli nyingi za kitaifa.
Kilwa jazz pia ilialikwa
kutoa burudani katika sherehe ya ndoa ya mmoja wa mawaziri wa serikali ya Tanganyika
wakati huo, Oscar Kambona.
Katika hafla hiyo Ahmed
Kipande alionesha kipaji chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa
papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao,
Oscar Kambona na mkewe.
Wakati Ahmedi Kipande akiimba
wimbo huo, Bwana harusi Kambona aliinuka
toka kwenye kiti cha maharusi na kwenda
kumkumbatika kisha akamtunza kwa pesa.
Bendi hiyo ya Kilwa jazz
ilikuwa chini ya udhamini mkubwa wa Mzee
Nangwanda Lawi Sijaona, ambaye anaelezewa kuwa alitoa mchango mkubwa mno
wa hali na mali.
Kilwa jazz ilikuwa na
wanamziki wenye vipaji tofauti. Walikuwepo ambao walikuwa wakipiga ala za
muziki zaidi ya moja pamoja na kuimba.
Ahemed Kipande alikuwa kiongozi, mtunzi wa nyimbo, alikuwa akiimba
pia alikuwa hodari wa kupuliza ‘mdomo wa
bata’ Saxophone. Duncan Njilima, Zuberi Makata, na Hassan Shabani ‘Kichwa’ wote
walikuwa na uwezo wa kupiga gita la solo. Kwa taarifa yako msomaji wa gazeti
hili kwamba Hassan ‘Kichwa’ alikuwa kaka
mkubwa wa Ahmedi Kipande.
Kwa upande wa saxophone
walikuwepo akina Kisi Rajabu, Juma
Town na Abbas. Waimbaji
alikuwa yeye Ahmedi Kipande, Juma Mrisho’ Ngulimba wa ngulimba’ na Kassimu
Mapili. Gita la kati lilikuwa likiungurumishwa na Abdull Ngatwa wakati Drum
zilikuwa zikicharangwa na Said na Abdallah Kanjo.
Upigaji wao wa muziki ulikuwa
ukiwakuna vilivyo viongozi wengi wa siasa na serikali, ilifikia kiongozi mkubwa
wa nchi wakati huo, Mzee Rashid Mfaume
Kawawa alitoa ofa ya suti kwa wanamuziki wote wa Kilwa jazz.
Ahemed Kipande katika maisha
yake alifanikiwa kupata watoto sita, lakini wawili kati yao, walikwisha tangulia mbele za haki.
Mzee Kassimu Mapili
aliyejiunga na bendi hiyo mwaka 1965,
amelieleza gazeti hili kwamba Kilwa jazz wakati wa enzi zake haikuwa na
mpinzani katika muziki licha ya kuwepo bendi kubwa za Dar Jazz na Western Jazz.
Kilwa jazz miaka hiyo alitoka na vibao vingi vya Mapenzi
yananivunja mgongo, Nipate lau nafasi, Nacheka cheka Kilwa leo, Rose waniuwa,
Maneno hayafai na nyinginezo nyingi.
Nyimbo hizo baadhi yake hadi
sasa zinapigwa na baadhi ya bendi za
muziki wa dansi, kwenye vituo vya Redio mbalimbali na wengine wameziweka kama miito ya simu zao.
Mtoto wa mwisho wa Ahmed
Kipande, Kipande Ahemd alisema kwamba
pamoja na juhudi kubwa za baba yake za kufanikisha mambo mengi ya maendeleo
toka Tanganyika hadi kuwa Tanzania,
alipokuwa akiumwa nyumbani kwake hauonekana mtu yeyote wa kwenda kutoa msaada
wala kumjulia hali.
Kipande akafika mbali zaidi
kwa kusema kwamba licha ya mchango mkubwa wa baba yake Mzee Ahmed Kipande kwa
taifa, bado hajamkumbukwa japo kwa kumpa tuzo ya heshima kama
walivyofanyiwa wanamuziki wengine.
Ni miaka 26 tangu Ahmedi
Mohammed Kipande afariki dunia Aprili
27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu.
Alizikwa kwenye makaburi ya Tandika
Maguruwe, mkoani Dar es Salaam Aprili
28,1987.
Mugu ailaze roho ya marehemu
Ahmedi Kipande pahala pema peponi, Amen.
Mwisho.