UNAMKUMBUKA ‘KING MAKUSA’ JUMA UBAO?
JUMA UBAO ‘KING MAKUSA’ halitakuwa jina geni hususani kwa wale waliokuwa vijana na wapenzi wa muziki wa
dansi kati ya miaka ya 1970 na 1990 hapa nchini.
Ubao ni mwanamuziki mwenye vipaji vya pekee, ambavyo sitakosea
nikitamka kwamba wanamuziki wengine hawakujaaliwa kuvipata. Kubwa zaidi ni lile
la kuwa na uwezo wa kitumia kila aina za ala za muziki.
Juma Ubao aliwahi kuonesha
maajabu wakati akirekodi nyimbo katika kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam
(RTD) wakati huo, ambapo alirekodi (single
track) ndani ya dakika 8, akishiriki katika sehemu sita tofauti Studioni.
Nguli huyu alikuwa mastari wa
mbele katika uhamasishaji wa wananchi kwenda kujiunga katika vijiji vya Ujamaa,
ukimbizaji wa mbio za Mwenge, na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kupitia
tasnia ya muziki.
Akieleza Wasifu wake anasema
jina lake halisi
ni Juma Salim Laizer, aliyezaliwa mkoani Dodoma
mwaka 1950.
“Kabila langu na Mmasai, ni
mzaliwa wa Dodoma
lakini asili yangu ni kijiji cha Mabebu kilichopo Longido, mkoani Arusha…”
anasema Ubao.
Akisimulia asili yake ya
Arusha anasema babu wa babu zake walikuwa watu wa kuhamahama kama
ilivyokwaida ya kabila lao la Masai. Walihamia Kondoa mkoani Dodoma,
ambako ndiko mababu hao wakasilishwa kuingia
dini ya Kiislamu, baadaye wakafanya makazi yao Dodoma mjini.
Anawataja wazazi wake kuwa
ni Mama Sheila Sindano na Mzee Salim Laizer, aliyeishia elimu ya msingi
ya darasa la tano. Alikuwa mhasibu katika Shirika la Reli la Afrika ya
Mashariki (EAR) akifanyika kazi katika mji wa Iringa.
Mzee Laizer alishatangulia
mbele za haki.
Jina la Ubao si halisi, bali
alipachikwa na wapenzi na mashabiki wa muziki wake baada ya kuridhishwa na upigaji wa ala nyingi
kwa wakati mmoja, wakimlinganisha na ubao ambao hutumiwa katika kufanya kazi nyingi.
Juma Ubao alipata elimu yake katika
shule ya msingi ya Wamissionari ya Konsolata
mjini Iringa hadi alipomaliza darasa la nane mwaka 1965.
Alikuwa ni miongoni mwa
wanafunzi wa shule hiyo waliofaulu
mtihani wa darasa la nane, akachaguliwa kwenda kujiunga katika shule ya Sekondari ya Tosamaganga ya mkoani humo hadi alipomaliza kidato cha nne mwaka 1969.
Miaka hiyo hapa nchini wasomi
hawakuwa wengi, elimu ilikuwa mithiri ya
‘lulu’. Hivyo elimu yake ya kidato cha
nne ilimpatia kazi nzuri mwaka 1970
kwenye kitengo cha Colito Barracks iliyopo Lugalo jeshini, akijifunza muziki
katika bendi ya blass.
Munkari wa muziki ukaanzia
hapo kwani mwaka 1972, alijiunga na bendi ya Polisi Jazz. Ubao baadaye
akijiunga katika bendi ya King Afrika iliyokuwa na wanamuziki mchanganyiko toka
nchi za Zambia
na Frolie, Monga Stanii na Tomaa‘Kabotolo’Congo.
Bendi hiyo ilikuwa ikiporomosha
muziki wake katika ukumbi wa Mikumi Tours,
uliokuwa ukimilikiwa na mfanyabiashara
maarufu Mzee Fadhili Batengas, maeneo ya Tazara, Buguruni.
Mwaka 1973 kulipoanzishwa vijiji
vya Ujamaa hapa nchini, Juma Ubao
alishiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika vijijini
hivyo. “tulinusurika kuliwa na Simba tukiwa porini huko Mkongo wilaya ya Rufiji, wakati wa oparasheni ya vijiji vya ujamaa…”
anatamka Juma Ubao.
Safari yake katika muziki
iliendelea kwa kujiunga katika bendi ya STC Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na
Shirika la Umma la (State Trade Corporation) mwaka 1975.
Baadaye Shirika hilo la STC ikabadilishwa kuwa
Bodi ya Biashara ya ndani(Board of Internal Trade.) halikadhalika bendi nayo
ikawa Biashara Jazz. Juma Ubao alipigia bendi hiyo hadi mwaka 1982 bendi ilipotoweka
katika taswira ya muziki.
Ikumbukwe kwamba miaka ya
1970 baadhi ya mashirika ya umma yalianzisha vitengo vya michezo na burudani. Shirika
la usafiri Dar es Salaam lilikuwa na bendi ya UDA Jazz waliokuwa wakipiga
katika mtindo wao wa ‘Bayankata’,
Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilikuwa na bendi ya Urafiki Jazz ‘wakitamba na
mtindo wa ‘Chakachuwa’ Shirika la Bima la Taifa (NIC), nalo lilikuwa na bendi
ya Orchestra Bima Lee, wakitamba katika mtindo wao wa ‘Magneti tingisha’
Akielezea kisa cha kuitwa ‘King
Makusa’ Ubao anasema
“mwaka 1976 tulikwenda Studio
za Redio Tanzania (RTD), kurekodi nyimbo zetu. Niliwaacha midomo wazi
watayarishaji na watangazaji wa wakati huo akina Khalid Ponela, John Luanda, Charles
Hirali, Frank Kirumbi, Gilbert Boma na fundi mitambo wao James Mhillu na Crispin Lugongo, wakinishuhudia nikipiga sehemu sita katika
wimbo mmoja ndani ya dakika nane…”
Juma Ubao ambaye ni mcheshi
na mwenye masihara mengi, anasimulia
zaidi jinsi alivyofanya ‘vimbwanga’ siku hiyo akisema
“nilitayarisha wimbo, nilipiga
solo, niliimba, nilipapasa kinanda, nilipuliza saxophone, na kutwanga tumba
katika ‘single track’ ndani ya dakika nane…”
Kwa Watangazaji hao, ilikuwa
ni kitu kipya ambacho hakikuwahi
kufanywa na mwanamuziki mwingine yeyote.
Ndipo hapo walipompachika
jina la King Mkusanya, likiwa na maana ya Mfalme(King) wa kukusanya. Lakini
wakashauriana na kufupisha kuwa ‘King Makusa’ jina linalovuma hadi leo.
Ubao anasema enzi zake wakati
akipiga muziki ukumbini, alikuwa apiga gita, na kinanda, kila ala kwa wakati wake.
“Wakati ninaimba gita
huliweka mbavuni, saxophone huliweka mgongoni na Kinanda pembeni huku watu
wakinishangaa…” anajisifia Juma Ubao.
Nguli huyo mwaka 1987 aliwahi
kuteuliwa kuwa miongoni mwa wanamuziki 57 waliounda kundi la Tanzania All
Stars, waliotoka na wimbo wa ‘Fagio la Chuma’ ukiwa ni kauli mbiu ya rais wa awamu
ya pili Alli Hassan Mwinyi, juu ya
uwajibikaji.
Juma Ubao mwaka 1989, alikuwa
muasisi wa bendi ya Six Manyara akiwa na wanamuziki wakongwe akina Suleiman
Mwanyiro, Hassan Bichuka, Kassim Rashid ‘Kizunga’ Kasola Rajabu na Manicho
Athumani. Wakiwa katika bendi hiyo walifumua vibao vya Batuli na Salama zikiwa
ni tungo za Juma Ubao. Zingine ni Maselina, Fatuma Samahani sana na Tabu.
Bendi hiyo ya Six Manyara iliundwa
kwa madhumuni ya kutangaza fahari za Utalii wa nchi yetu zikiwemo mbuga za
wanyama, mlima Kilimanjaro na vivutio vingine vilivyopo hapa nchini.
Bendi hiyo ilisafiri kwenda
kutangaza utalii katika nchi za Uganda
na Kenya
mwaka 1991.
Wakiwa huko Kenya walifanikiwa kurekodi nyimbo
nne katika kampuni ya PolyGram nchini humo
kwenye Long Play.
Waliporejea toka Kenya,
wanamziki wake wengine walirudi katika bendi zao za zamani ila yeye ‘akakomaa’
na bendi hiyo hadi sasa.
Juma aliamua kupumzika mambo
ya muziki kwa muda. Akuamua kuutumia
muda huo kwenda kusoma masomo ya jioni
akiwa na lengo la kuendeleza elimu yake. Alisoma masomo ya Uhasibu na Biashara
na kupata cheti.
Cheti chake kilimpa nafasi ya
kupata ajira katika shirika la ndege la Tanzania
(ATC), kama
mhasibu katika klabu ya Jet.
Baadaye alihamishiwa kwenda Uwanja
wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambako alipewa kitengo cha kusimamia vyakula
vya kwenye ndege.
Katika kitengo hicho, Ubao
alilipunguzia kwa kiasi kikubwa gharama za malipo zilizokuwa zikilipwa na
Shirika la ATC. Yeye aliweza kusimamia ipasavyo vyakula vyote kuandaliwa toka Klabu
ya Jet, badala ya kuvinunua katika hoteli ya Kilimanjaro.
Shirika hilo la ATC baadaye likaanza kuyumba kiuchumi uliopelekea
kupunguza baadhi ya wafanyakazi wake
mwaka 2002, miongoni mwao akiwa Juma Ubao.
Mwaka 2000 Six Manyara ilirekondi
nyimbo za Somo somo, Leo leo zilizopigwa katika mahadhi ya mduwara. Wimbo wa
‘Zongolo jangu’ uliimbwa kwa lugha ya
Kizaramo ikiwa na maana ya Jogoo langu. Wimbo wa Sakina ulipigwa katika mtindo
wa rage na nyingine ni Msichana, Tuluka
chibite ulirekodiwa kwa lugha ya Kigogo ukiwa na maana ya Inuka tuondoke. Wimbo
mwingine uliotia fora wakati huo ni Bide, alitunga na kuimba kwa lugha ya Kipogoro.
Demokrasia katika tasnia ya
muziki ilifanya kazi yake pale mwaka
2008, ilipomchagua Juma Ubao kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi
Tanzania (CHAMUDATA) Alichukuwa nafasi hiyo baada ya Kassim Mapili aliyekuwa
mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, kumaliza muda wake.
Juma Ubao umekwisha pewa
nafasi nyingi za uongozi katika tasnia ya muziki. Mwaka 2009, aliteuliwa kuwa
mjumbe wa bodi ya Baraza la Sanaa Tanzania
(BASATA)
Juma Ubao ni baba wa familiya
ya mke na watoto watano. Anamtaja mkewe Ashanti Mwinjuma kwamba katika kipindi
chote katika muziki, ndiye aliyekuwa akimfariji na kumpa moyo kila alipokuwa akikwama.
Watoto wake anawataja kwa
majina ya Athumani, ambaye amefuata nyayo zake, yupo nchini Austria, akifanya mambo ya muziki. Laizer, Ibrahimu, Aboubakar na Salma.
Nguli huyu hakuchelea kuiomba
serikali kuwatambua wanamuziki wa zamani
ambao anasema walitoa mchango mkubwa kupitia tasnia ya muziki wakati wa
kutafuta Uhuru, pia walishiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini
mwa Afrika na kuhamasisha maendeleo ya taifa letu.
“Kuthaminiwa kwa wanamuziki
hawa si kwa kuwapa pesa pekee, la hasha, bali ni kuwepo kwa utaratibu japo wa kuweka majina
yao kwa baadhi ya mitaa, shule ama hospitali katika halmashauri za Manispaa
zetu ili yawe kama vielelezo kwa vizazi
vijavyo….” anasisitiza Ubao.
Juma Ubao akatolea mifano ya
maeneo ya Makumbusho ambako mitaa mingi imepewa majina ya nchi za Afrika. Mzee Ubao hakuacha kamka mifano mingine
akisema “ ukienda Muhimbili Wodi zote
zimepewa majina maarufu ya Mwaisela, Sewa Haji, pia kuna shule za sekondari ya Shaaban Robert, Benjamin Mkapa, mitaa ya
Samora, Bibi Titi, Fundikira,
Makamba, barabara ya Kawawa barabara ya Ali Hassan Miwnyi na sasa hivi ipo
ya Mwai Kibaki. Hizi ni kumbukumbu kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo…”
Aidha akaviomba vyombo vya utangazaji hususani vya Redio, kutenga
muda japo kidogo wa kupiga nyimbo zao za zamani.
Kama gwiji huyo wa
muziki hakusita kukemea vijana wa muziki wa kizazi kipya kufanya upuuzi wa kutotaka
kujifunza kupiga ala za muziki. Kwa kufanya hivyo ni kama
wanacheza ‘maigizo au makida makida’
Juma Ubao huku akikomelea
msumari mwingine kwa wanamuziki wa kizazi kipya, akiwaasa wasibweteke na sifa wanazopambwa na mashabiki wao
kwani sifa na mafanikio waliyonayo, anasema si endelevu.
Juma Salim Laizer ‘Ubao’ mwaka huu ametimiza miaka 63 ya
kuzaliwa kwake. Huruma imemjaa kwa kuona jinsi vijana hao walivyopoteza
muelekeo katika muzuki. ‘ Wazee dawa’
Juma Ubao ameamua kutumia ujuzi wake
alionao kuwafundisha muziki. “nipo
tayari kutumia weledi wangu kuwafundisha kupiga ala za muziki na kuimba kwa wale
vijana watakaopenda…” anamalizia nguli huyo.
JUMA UBAO AKIIMBA NA KULIUNGURUMISHA GITA LA SOLO.
No comments:
Post a Comment