MAPILI GWIJI ALlYETUMIA MAISHA YAKE YOTE KATIKA MUZIKI.
Machi, 2013.
MZEE KASSIM MAPILI
ni mwanamuziki mkongwe aliyeanza tasnia hiyo
kabla ya nchi yetu ya Tanganyika,
wakati huo haijapata Uhuru.
Mzee Mapili ni mwenye vipaji
vingi vya kutunga, kuimba nyimbo za muziki wa dansi na kupiga gita. Pamoja na
umri wake kumtupa, Mapili ni ‘mfua uji’ wakati wote wala haoneshi dalili za ‘kuchoka’ kama Wazee wengine wenye
umri kama wake.
Mwaka huu wa 2013,
Mapili ametimiza miaka 76 ya kuzaliwa kwake, bado ni mwenye nguvu, Afya njema na kumbukumbu nyingi zilizojaa kichwani mwake.
Mzee Mapili amekula chumvi
nyingi ingawaje ukikutana naye mitaani, unaweza kumdhania kuwa ni ‘Mzee kijana’ kwa jinsi anavyojichanganya katika maongezi
na watu wa rika na jinsia tofauti
Mzee Kassim Mapili ameeleza
kwamba amevuka mito,
mabonde na kuparamia milima iliyoshindikana katika kuyatafuta maisha. Na
amesisitaza kwamba hatokata tamaa kuendelea kutafuta mafanikio hadi ifikapo kipindi
atakapoishiwa nguvu.
.
Akisimulia historia ya maisha
yake, Mzee Mapili amesema kwamba alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu kilichopo
Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937.
Alipata elimu ya msingi sambamba
na ya Koraan, akiwa kijijini kwake Lipuyu mkoani Lindi. Anasema akiwa madrasa
alikuwa mahiri wa kughani kaswida katika Madrasa yake. Hata mapenzi yake ya kuimba
nyimbo aliyapata kupitia Madrasa hiyo.
Ni mwanamuziki mzoefu mwenye
uwezo mkubwa wa kuimba na kupiga gita. Anasema alianza kujifunza kupiga muziki wakati nchi
yetu ikiwa bado inatawaliwa na Ukoloni wa Waigereza.
Jina la Kassim Mapili likaanza
kusikika katika ulimwengu wa muziki mara tu alipojiunga katika bendi ya White
Jazz iliyokuwepo mjini Lindi mwaka 1958.
Sifa zake za kupiga muziki
zikazagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani. Hakuchuka muda mrefu katika
bendi hiyo, mwaka uliofuatia wa 1959 akahama na kujiunga na bendi ya Mtwara Jazz
wakati huo.
Bendi ya Holulu ya mjini
Mtwara, nayo ikaona ni bora inyakue ‘kifaa’ hicho. Mapili akashawishika na maslahi
aliyo ahidiwa, ndipo alipoamua kujiunga katika bendi yao mwaka 1962.
Kwa kuwa nchi yetu ya Tanganyika
wakati huo ilikuwa tayari
imekwisha pata Uhuru, Chama
TANU kiliazisha vikundi vya Vijana kukitangaza
chama hicho.
Hivyo mwaka 1963, Mzee Mapili akaoneka anafaa kusaidia kufanya
kazi hiyo, akachukuliwa kwenda katika bendi ya Jamhuri Jazz ambayo ilikuwa ya
vijana wa TANU (TANU Youth League) ya Lindi.
Baada ya kufanya kazi nzuri
hapo Lindi, akateuliwa kuwa muasisi wa bendi nyingine ya Vijana wa TANU (TANU
Youth League) huko Tunduru, mkoani Ruvuma mwaka 1964.
Katika kutafuta maslahi murua
wakati huo, alilazimika kwenda kujiunga
na bendi ya Luck Star mwaka 1965, iliyokuwa
na makazi yake Kilwa Masoko mkoani Lindi.
‘Kizuri hupendwa popote’
Kassim hakukaa sana
na Luck Star, mwaka huohuo alisakwa ‘kwa udi na uvumba’ na bendi ya Kilwa Jazz iliyokuwa
ikiongozwa na Ahmed Kipande, akajiunga nayo.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT ‘Kimbunga Stereo’ na JKT
‘Kimulimuli’. Kwa kuwa sifa za Mzee
Mapili zilikuwa zimezagaa kupitia wa muziki hapa nchini, Jeshi hilo lilimchukuwa
kwenda kuwa muasisi wa bendi ya JKT Mgulani, jijini Dar es Salaam mwaka 1965.
Ushindani wa bendi katika
Majeshi, ukaaza. Jeshi la Polisi nalo likamhitaji ajiunge nalo. Alikubali
kwenda kuasisi bendi yao
ya Polisi Jazz baada ya kupata ajira tarehe
15, Desemba 1965. Polisi Jazz ilikuwa ikipiga
muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.
Akiwa ‘Afande’ Mzee Kassim Mapili aliteuliwa
kuwa mwalimu wa bendi ya Wanawake
ikijulikana kama Woman Jazz Band Desemba
23,1965.
Bendi hiyo ilikuwa
ikimilikiwa na Umoja wa Vijana TANU (TANU Youth League) ambapo alisafiri na
bendi hiyo kwenda nchini Kenya,
kwenye sherehe za siku ya Kenyata.(Kenyata day) Kenyata alikuwa rais wa kwanza
wa nchi ya Kenya.
Mzee Kassim Mapili alipata
pigo kubwa Mei 1966, baada ya kuondokewa na baba yake mzazi Mzee Said Amri
Makolela, aliyeuawa wakati akipambana na
Nyati porini. Anamshukuru mungu kwani mama yake mzazi Bi. Ajena Mussa Mtikita,
bado yu hai.
Baada ya kuvunjika kwa bendi
ya Woman Jazz mwaka 1974, ndiyo ikwa
mwanzo wa kuanzishwa kwa bendi ya Vijana Jazz
baada ya kuwakusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti, Hassan Dalali, Manitu Mussa, Hamza Kalala
‘Komandoo’ Chakupele, Abdallah Kwesa ,
Agrey Ndumbaro na wengine wengi.
Kassim Mapili alistaafu toka
jeshi la Polisi Mei 05, 1981 akiwa na
cheo cha Sajenti. Mara baada ya kustaafu mwishoni mwa mwaka 1981, alijiunga na
bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz.
Kwa kipindi kirefu Mzee
Mapili amekuwa akiitwa kuhudhuria semina
nyingi. Mwaka 1982, alishiriki katika semina
ya wanamuziki iliyofanyika mjini Bagamoyo. Katika semina hiyo ilipelekea
kuundwa kwa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), naye akachaguliwa
kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho.
Kila panapofanyika jambo la
manufaa katika muziki hapa nchini, Mzee Mapili amekuwa akishirikishwa
kikamilifu. Amekuwa akitoa michango ya mawazo yenye busara katika tasnia ya muziki kwa nyakati tofauti.
Busara zake zilipelekea mwaka
1986 kuchaguliwa kuwa mmoja wa washiriki katika uundwaji wa kundi la wanamuziki
57, lililoitwa Tanzania All Stars.
Mwaka huohuo alishiriki
katika tamasha la utoaji wa zawadi kwa
Wasanii wakongwe, akiwemo Mzee Morris Nyunyusa, Mzee Makongoro, Mzee Mwinamira,
Mbaraka Mwinshehe na wengine.
Kassim Mapili alikuwa muasisi
katika shindano la nyimbo kumi bora za wanamuziki wa dansi (Top Ten Show) mwaka
1988, akiwa kama Mwenyekiti wa CHAMUDATA.
Mzee Mapili akiwa kama Baba, aliwakumbuka watoto wa mitaani wanaosumbuka
katika kutafuta maisha. Alianzisha bendi ya watoto wa umri wa miaka 16, ambao baadaye walifanya onesho kamambe, sambamba na siku ambayo watoto wa Afrika
Kusini waliteswa huko Soweto.
Mapili mwaka 1993, alikuwa
mstari wa mbele wa uanzishwaji wa bendi ya Wazee ya Shikamoo Jazz. Bendi hiyo
bado ipo ikiongozwa na Mzee Salumu Zahoro.
Hekima na busara za Mzee huyu, zilipelekea mwaka 1974, kuteuliwa kuwa mlezi
wa bendi ya Super Matimila.
‘Aliyena nacho huongezewa’
usemi huu ulijiri kwa Mzee Kassimu Mapili, ambaye Nyota yake aliendelea kung’ara, aliteuliwa
kuwa mkufunzi wa bendi ya Gold All Stars mwaka 1977.
Mzee Mapili hakuwa mchoyo wa
kugawa ujuzi alionao, kwani alishiriki kikamilifu katika uundwaji upya wa bendi
ya Super Volcano, akiwa na binti ya Mbaraka Mwinshehe, Taji.
Kama nilivyotangulia kukujuza kwamba Mzee Mapili anaonekana si mtu wa kuchoka
kiafya, siri yake alilidokeza hivi. “Nakula chakula vizuri, ninafanya mazoezi ya viungo kila siku, Sigara,
Pombe na starehe zisizokuwa za lazima, kwangu ni mwiko…”
Mzee Mapili anafafanua siri ya mafanikio ya afya yake kuwa imara hadi
leo.
Pamoja na umri wake kuwa mkubwa,
anasema bado hajafikia wakati wa kuwa tegemezi
kwa watoto wake. Anamiliki bendi ya Orchestra Mapili Jazz ambayo bado
haijafahamika kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya washabiki wake.
“Bendi yangu huwa
inawasisimua mno wapenzi wa muziki wa zamani kwa kuwapigia nyimbo za zamani kwa
maombi yao maalum…”
anasema Mapili.
Kassim alienda mbali zaidi akijigamba
kwamba wakati akipiga gita, huimba kufanya
‘shoo’ mwenyewe akiwakumbusha wazee
wenzake mitindo yao
ya zamani ya Twist, Bumping, Charanga,
Chacha na Pachanga.
“Nikianza kucheza Twist, juu…
juu… chinii… chinii… juu… chiniii, watu
ukumbini huzizima na kunizunguka wakinipongeza wangine wakisema “Wazee dawa…” Mapili anatamka kwa kijiamini huku akionesha
jinsi ya kucheza mtindo huo.
“Ninauheshimu sana muziki kwani ndiyo
ulionilea hadi sasa. “Nimekulia na kuzeeka nikiwa katika muziki, sijawahi
kufanya kazi nyigine tofauti na muziki katika maisha yangu yote. Hata
nilipopata ajira katika Jeshi la Polisi, nilikuwa akifanya kazi ya muziki…”
Anasema Mapili.
Kassim Mapili ni baba wa
familiya ya mke na watoto watatu, aliowataja kwa majina ya Kuruthum, Said na
Hassan. Kati yao
hakuna hata mmoja aliyefuata nyao zake za muziki.
Mapili amekuwa mstari wa
mbele katika shughuli takriban zote za kifamiliya za wasanii na wanamuziki
wenzake hapa nchini. Huwa habagui kwamba ni Mtanzania ama vinginevyo. Mfano
halisi wiki iliyopita kabla ya kifo cha mwanamuziki
Kabeya Budu wa bendi ya Le Capitale, Mapili alikuwa mstari wa mbele kwenda kumjulia hali akiwa hospitalini. Pia alishiriki kikamilifu
katika mazishi ya mwanamuziki huyo Kabeya Badu, aliyefariki tarehe 06
Machi, 2013 katika hospitali ya
Muhimbili kwa maradhi ya figo. Badu alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC).
Mzee Kassim Mapili amemalizia
kwa kuwasihi wanamuziki hususani vijana, kujifunza kupiga ala za muziki, ili wafikie
malengo yao ya
kuwa wanamuziki watakao kubalika kimataifa. Aidha amewataka kuzingatia heshima
na upendo miongoni mwao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment