MUHIDINI
MAALIM GURUMO
‘JEMBE’ LINAUMWA’
December 30, 2012.
MUHIDINI MAALIM
GURUMO ni
mwanamuziki aliyetumikia nchi hii kwa ufanisi mkubwa toka miaka ya 1960, lakini
hadi leo yupo katika dimbwi la ufukara uliokithiri.
Katika kipindi chote hicho Mzee Gurumo ametunga nyimbo
nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kulinda
uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani pamoja na kuwaasa wazazi kutumiza
wajibu wao kwa kulea watoto na
vijana kutimiza wajibu wao.
Licha ya sifa zilizoainishwa hapo juu, mzee Gurumo
hakuwahi kukumbukwa kwa lolote pamoja na mchango wake mkubwa kwa taifa hili
tangia uhuru wa nchi hii mwaka 1961.
Hatimaye kwa mara ya kwanza Mzee Gurumo amekumbukwa kwa kutunukiwa
nishani ya heshima ya Muungano na rais Jakaya Kikwete, siku ya maadhimisho ya
miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye uwanja wa uhuru
Desemba 09, 2012 Jijini Dar es Salaam.
Gurumo alivishwa nishani hiyo na rais Jakaya Kikwete
ambaye aliwatunuku pia wanamuziki wengine watatu, msanii wa maigizo na
mwanariadha mkongwe katika viwanja vya Ikulu, jiji Dar es Salaam.
Wasanii wengine waliotunukiwa siku hiyo ni pamoja na
kiongozi wa zamani wa Dar. International, Marijani Rajabu, mwimbaji mkongwe wa
taarabu, Fatuma Baraka ‘Bi. Kidude’, msanii wa maigizo ya filamu Fundi Said
‘Mzee Kipara’ na mwanariadha mkongwe,
John Steven Akwari.
Baada ya kuvishwa nishani hiyo, Mzee Gurumo alionyesha
furaha yake na kumshukuru rais Kikwete na wananchi kwa ujumla kwa kutambua kazi
yake ambayo alisema iwe changamoto kwa vijana kutambua kuwa muziki si kwa
ajili mapenzi pekee, bali kila kitu kinachoihusu jamii.
Mwandishi wa habari
hii alifika nyumbani kwa Mzee Gurumo huko Makuburi, Ubungo ambapo alielezea historia
yake na akasema haijui tarehe kamili aliyozaliwa, japo anafahamu kuwa alizaliwa
katika Kijiji cha Masaki, Wilaya ya
Kisarawe mkoa wa Pwani mwaka 1940.
Ni mwanamuziki
mkongwe mwenye historia ndefu katika
tasnia ya muziki Afrika Mashariki na
hata nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara.
Sifa kubwa aliyonayo Mzee Gurumo ni ile ya toka aanze kupiga
muziki miaka 52 iliyopita, hakuwahi kupumzika ila mwezi wa mtukufu wa Ramadhani
ama awe anaumwa. Kila siku za kazi hakukosa jukwaani.
Rekodi ya sifa hiyo ingeliweza kuvunjwa na mkongwe Salimu
Zahoro, ambaye alimtangulia Gurumo katika muziki, akipiga katika bendi ya Kiko
Kids ya mjini Tabora. Lakini baada ya bendi hiyo kufa, Mzee Salimu Zahoro alipumzika mambo ya muziki kwa takriban miaka
20, hadi alipojiunga na bendi ya
Shikamoo Jazz.
Hivi sasa Mzee huyu ana umri wa zaidi ya miaka 70, ameshatoa mchango mkubwa katika nchi hii
kupitia tungo za nyimbo zake zisizopungua 1, 000 zilizojaa ujumbe mzito kwa jamii.
Mzee Gurumo anailezea afya yake kwa sasa kuwa si nzuri,
akisumbiliwa na maradhi yaliyopelekea yeye kulazwa katika kitengo cha wagojwa mahututi
(ICU) katika hosiptali ya Muhimbili.
Kwa masikitiko makubwa mzee huyo anasema ufukara alionao,
amefikia hatua ya kuwatamani wanamuziki wa kizazi kipya na taarabu, kuwa wana
mafanikio makubwa kimaisha.
Gurumo akafika mbali zaidi kwa kusema mafanikio yao ni kwa vile soko la sasa limewapokea vyema na yeye
kujisikia wivu kuwaona vijana wakiendesha maisha mazuri wakiwa na magari ya
kifahari wakati yeye akitembea kwa miguu.
“Hata kwenda Hospitali Muhimbili kutibiwa, ninatumia usafiri wa daladala licha ya muda mrefu nilioutumia
katika muziki” anasikitika mzee Gurumo.
Mke wa mzee Gurumo
Pili Kitwana alitoa dukuduku lake akisema
kwamba yeye binafsi huwa anaumia roho wanapokuwa kwenye daladala akimpeleka mumewe hospitali, abiria wengine huwashangaa. Lakini anasisitiza kwa
kusema wana haki ya kuwashangaa kufuatia
jina kubwa la mume wake ambaye kwa hali ya kawaida hakustahili kutumia usafiri
wa daladala.
Mama huyo ambaye aliolewa na Muhidini Maalimu Gurumo mwaka 1967, walipata watoto wanne akina
Mariamu, Mwalimu, Omar na Mwazani. Anamtaja
Binti yao
wa kwanza Mariamu kwamba amefuata nyayo za Baba yake za usanii japo anaimba
nyimbo za kizazi kipya.
Mkewe Pili, akaenda mbali zaidi akisema kwamba laiti kama angelikuwa na uwezo, angemtaka mumewe apumzike na
masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kupata
mafanikio ya maana.
Mzee Gurumo mwimbaji mwenye sauti isiyoigika, anakiri fani
yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na watu wengi wakiwemo viongozi mbalimbali hapa nchini akiwemo rais Jakaya Kikwete.
Anakiri kitendo cha rais Kikwete kuacha kazi zake akifuatana
na mkewe, mama Salma kuja kumjulia hali, pia kumsaidia katika matibabu wakati alipokuwa
amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kwamba kulimfariji sana.
Muhidini Gurumo anasema baada ya ujio wa rais Kikwete hapo
Muhimbili, huduma zilizofuatia toka kwa
madaktari na manesi zilikuwa ‘Baabu’ kubwa.
Hivi sasa amepewa Daktari maalumu wa kuiangalia afya yake
kila aendapo hospitalini humo.
Gurumo mwenye uso wenye bashasha licha ya kudhoofu kiafya,
hakukosa kutoa shukurani za dhati kwa mmiliki wa Kampuni African Stars Entertainment
Tanzania (ASET), Asha Baraka kwa kuandaa onyesho maalumu kwa ajili ya
kumchangia pesa.
“Asha Baraka namshukuru sana
aliniletea shilingi milioni mbili ambazo zilinisaidia sana katika matibabu” anasema Mzee Gurumo.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’ ‘Sikinde’
na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, JUWATA, OTTU, Mlimani Park
na Orchestra Safari Sound (OSS).
Mwenyewe anasema mitindo hiyo ilitokana na ngoma za asili ya kabila lake la Kizaramo
ambazo mama yake mzazi alikuwa gwiji wa
kuimba na kucheza enzi zake.
Gurumo alianza muziki akiwa na miaka 12 lakini muziki wa dansi alianza rasmi mwaka 1961, baada
ya kumaliza elimu ya koroani katika
madrasa ambako alikuwa hodari wa kughani na kuimbaji kwa ustadi mkubwa Kaswida.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Kilimanjaro Chacha iliyokuwa
ya ikiongozwa na Mkurugenzi wa bendi
anamtaja kwa jina la Samwel Machango. Aidha anasema alipofika hapo, alipokelewa na Salumu
Monde ambaye alikuwa mpigaji wa gita la rhythm. Anakiri kwamba wote wawili
walimpa ujasiri wa jinsi ya kulitawala Jukwaa na vilevile kwa juhudi zake binafsi
alijifunza kupiga Saxophone.
Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu katika ukumbi wa Amana maeneo
ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Mzee Gurumo anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba katika
bendi yake ya kwanza ukiwamo wa ‘Nilipoingia Bar watu walinionea kijicho’
Anasema hawezi kuisahau siku ambayo kwa
mara ya kwanza alianza kupata pesa aliyoitolea jasho lake
ilikuwa ni shilingi tano
baada ya onyesho hilo.
Mwaka 1962 kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz Ahmed Kipande
alimrubuni kwa kumpa Shilingi mia mbili ili ajiunge na bendi yake. Anasema
Shilingi mia mbili miaka hiyo ilikuwa na thamani kubwa sana naye alipokea na kukubali kujiunga na
Kilwa Jazz.
Mzee Gurumo anatabanaisha kwamba uongozi wa
Ahmed Kipande, Duncan Njilima na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ hawakumtendea
haki iliyostahili na baada ya mwaka kupita
akaamua kutafuta bendi nyingine. Alifanikiwa kupata bendi ambayo ilikuwa
ndogo kuliko Kilwa jazz ikiitwa Rufiji
jazz mwaka 1963.
Mwaka 1964 Gurumo
aliitwa na uongozi wa NUTA Jazz ili akubali kuwa muanzilishi wa bendi hiyo na
aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama, Mnenge Ramadhani na
Wilfred Boniface.
Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa
Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika.
Nyingine zilikuwa Kilimo ni kazi yetu na Mwengele.
Mzee Gurumo pamoja na uzee alionao bado kumbukumbu
kichawani zijemjaa. Anakumbuka mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri John
Simon alijiunga na bendi yao
ya NUTA Jazz na anamtaja mpiga Solo, Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechaguliwa kuwa
Kiongozi wa NUTA Jazz.
NUTA jazz alikuwa ikimilikiwa Chama cha Wafanyakzi ambacho baadaye kikawa JUWATA, OTTU, TFTU
hadi TUCTA.
Wakati wakiwa na TUCTA mishahara yao
ilikuwa duni kiasi cha kushindwa kijikimu kimaisha, hivyo kwa pamoja wanamuziki
hao wakajipanga kwa kununua vyombo vyao vya muziki kidogo kidogo hadi
wakatimiza adhma yao
ya kujitegemea. Ndipo bendi ya Msondo Ngoma ilopanzisha ikilibakiza jina la Msondo kwa kuienzi staili
iliyowapa umaarufu.
Mwaka 1978 Gurumo alihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra
‘Wana Sikinde ngoma ya ukae’ na akawa kiongozi wa bendi hiyo baada ya muda
mfupi alitunga nyimbo zikiwemo Baba na Mama na Weekend.
Akiwa na bendi hiyo maisha yake yalianza kubadilika na
kuwa mazuri kufuatia malipo na maslahi ya kuridhisha aliyokuwa akilipwa na
uongozi wa Mlimani
Park.
Anajigamba kwamba maslahi hayo ndiyo uliofikisha kujenga
nyumba yake na kunua eneo la shamba maeneo ya Masaki Wilayani Kisarawe mkoa wa
Pwani na kuwapeleka watoto wake katika
Shule nzuri.
Anasema hatoweza kuwasahau wanamuziki alioshirikiana nao
kwa karibu akiwemo aliyekuwa kiongozi msaidizi Comas Tobias Chidumule, Joseph Bartholomew Mlenga
‘King Spoiler’ na Abdallah Gama.
Pamoja na kipato alichokuwa akikipata Mlimani Park Orchestra,
mwaka 1985 mfanyabiashara maaraufu jijini Dar- es -Salaam Hugo Kisima, akamshawishi kujiunga katika
bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) ambayo ilikuwa ikiongozwa na
Supreme Ndala Kasheba aliyekuwa akipiga
katika staili ya ‘Dukuduku’ nay eye Gurumo akaingia na staili ya ‘Ndekule’
Alijiunga na OSS
akifuatana na wanamuziki wawili
toka Mlimani Park
akina Abel Bartazar na Kassim Rashid ‘Kizunga’ na kutoka na nyimbo za ‘Chatu
mkali’ na ‘Bwana Kinyogoli’
Bendi ya OTTU ilikuwa bado inamuhitaji kurudi ndipo mwaka
1990 uongozi ulifanikiwa kumrudisha katika bendi hiyo ambayo tayari ilikuwa ilikuwa imebadili jina kuwa JUWATA.
Enzi za ujana wake ‘Ubitozi’ wakati huo, Gurumo alipitia
mambo mengi ya ujana yakiwemo ya kuvuta
sigara na alikuwa mywaji wa pombe
kupindukia ‘cha Pombe’ Tabia hiyo
ilikifikia kukorofishana na mama yake mzazi aliyetishia hata kumutolea ‘radhi’ kama
angeendekeza ulevi.
Mkewe Pili naye alikwaruzana kila mara juu ya hiyo ya
ulevi uliokithiri na aliwahi kutishia
kuomba talaka.
Hatimaye mwaka 1982, akaamua kumshinda ‘Shetani’ akaachana
na ulevi kwa shinikizo la mama yake na mkewe.
Mzee huyu mwenye historia ndefu ya muziki na maisha yake
kwa ujumla, amekuwa kiongozi katika bendi hiyo na anasema furaha aliyonayo ni
kuona pale pamoja na umri wake kuwa mkubwa akiwa na msondo ngoma, amekwisha
tunga na kuimba nyimbo nyingi na
kuzirekodi katika Studio zikiwemo za ‘Mama nipeleke kwa Baba’ Mwanangu acha
Wizi, Wosi wa Baba na nyingine nyingi.
Muhidin Maalimu Gurumo amesema kwamba hana muda mrefu
kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya halikadharika
umri wake kumtupa mkono.
Anasema atakapostaafu atajikita katika kuwasaidia vijana
ili atimize ndoto yake ya kujenga Chuo cha muziki katika shamba lake lililopo
Masaki wilayani Kisarawe, iwapo atapata wafadhili wa kumsapoti adhma yake.
Mzee huyo anasema mazoezi ni muhimu kwa kila binadamu.
Yeye hulazimika kujikongoja kwenda kuimba katika bendi yake ya Msondo Ngoma.
Wakati mwingine hulazimika huimba akiwa amekaa kwenye kiti. “Nja kali, nikienda
huko pamoja na mazoezi ninayopata, pia huwa ninaambulia posho, inayoniwezesha
kujikimu kimaisha” Mzee Gurumo anasema
kwa uwazi.
Gwiji huyu ametunga nyimbo zaidi ya 54 ambazo anasema zilizong’ara
na kupendwa na watu japo yeye anasema kwamba hazina faida yeyote. Analalama kwa kusema kuwa hapati hata senti tano ya
nyimbo zake hizo. Hivyo anawaomba wadau na
wasamaria wema kumsaidia ili aweze kuzirekodi upya nyimbo hizo ili
ziuzwe na yeye aweze kunufaika.
Kama walivyowahi kutamka wanamuziki
wengine wa zamani, Mzee Gurumo naye amewasisitiza vijana wa muziki wa kizazi
kipya kujifunza kutumia ala za muziki, ili kuweka kumbukumbu ya kazi zao kuwa
endelevu kwa vizazi vijavyo.
Mzee Gurumo anamalizia kwa kusema anaomba serikali, mawaziri,
wabunge na wadau wote wamuangalie kwa jicho la huruma, kwa kumsaidia kufuatia hali yake ya maradhi yanayomkabiri, na kwamba
hana msaada mwingine, akisisitiza kuwa wasisubiri hadi afe.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment