March , 2013
MAQUIS du ZAIRE ni bendi ambayo ‘iliwatesa’ Watanzania
kwa kuwaporomoshea burudani za muziki wa
dansi maridhawa katika kumbi mbalimbali hapa nchini.
Kwa wale
waliokuwa vijana kati ya miaka ya 1970 na 1990, katu hawawezi kuisahau bendi
hiyo ambayo iliingia hapa nchini kwa kishindo kikubwa ikitokea Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (Zaire)
wakati huo.
Mwaka
1981, niliwahi kufanya mahojiano maalumu na mmoja wa viongozi wa bendi hiyo
Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye alinipa wasifu wa bendi hiyo ya Maquis
du Zaire.
Kwa kuwa
wasifu huo uandikwa na kuchapishwa katika gazeti la serikali la Nchi Yetu la
kila mwezi, ambalo lilikuwa likuzwa kwa senti 30, likitolewa na mwajiri wangu
wakati huo, Idara ya habari (MAELEZO).
Hivyo
basi si vibaya nikirejea kuwapasha wale
ambao hawafahamu na kwa waliosahau, nichukue muda wenu kwa kuwapa wasifu wa
bendi hiyo tangia ilivyoanzishwa hadi kutoweka kwake katika taswira ya muziki.
Historia
ya bendi hiyo inaanzia mwaka 1960 kwa waliokuwa vijana wa wakati huo katika mji
wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(Zaire), walioungana na
kuunda bendi yao
wakaiita Super Theo.
Bendi
hiyo ilitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa Kamina
na vitongoji vinavyouzunguka mji huo, baadaye wakaibadilisha jina
kuwa Super Gabby.
Katika
kile kilichoelezwa na uongozi wa Super Gabby kuwa ni kuleta mageuzi katika
muziki, bendi hiyo mwaka 1972, ilibadili jina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.
Maquis du Zaire iliingia hapa Tanzania mwaka huohuo wa 1972, kwa
mwaliko wa mfanyabishara maarufu Mzee Batengas. Walianza kutumbuiza kwa mkataba
katika ukumbi wa Mikumi Tours uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao waliachana na Mzee
Batengas, wakaenda kupiga muziki katika
Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima
aliyekuwa akimiliki wa ukumbi wa Safari
Resort maeneo ya Kimara.
Mnamo mwaka 1977 Maquis du
Zaire waliamua kuongeza nguvu kwa
kuimarisha kikosi chao. Hivyo uongozi huo ulimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee
Paul’ kwenda Congo
kutafuta wanamuziki wapya.
‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukuwa akina Kikumbi Mwanza
Mpango ‘King Kiki’, Kanku Kelly, Ilunga
Banza ‘Mchafu’, Mutombo Sozy na mnenguaji
Ngalula Tshiandanda. Wakati huo walikuwa
wakicheza katika mtindo wa ‘Chakula Kapombe’ ambao kwa watanzania ulikuwa mpya
na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao
kulileta mabadiliko makubwa sana katika muziki
husuani tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ambaye yaelezwa kuwa ndiye
aliyeleta mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’,
mtindo uliowapagaisha wapenzi na wadau
toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam. Mpulizaji wa
Tarumbeta Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’
alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake akitoavibwagizo vya “cheza Kamanyolaa.. ,cheza ukijidai’
cheza Kamanyola bila jasho…”
Mwaka huo wa 1977 mwishoni Maquis walimaliza mkataba na wakaondoka
kwa Hugo Kisima. Bahati nyingine ikawaangukia tena kwani walisaini
mkataba mwingine na Mzee Makao
aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.
Wakiwa Savannah, walianzisha
mitindo ya Sanifu na Ogelea piga mbizi baadaye ukumbi huo ukaitwa White
House. Ikumbukwe kwamba wakati huohuo
Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi
wa Mpakani, maeneo ya Mwenge. Ukumbi wa
Mpakani baadaye ulibadilishwa
jina kuwa Silent Inn. Kisha kuishia kuwa Kanisa.
Mwishoni mwaka 1978 waliamua
kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka Congo ambao
ni akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Maquis du
Zaire ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu
Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula
‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo miaka ya 1980 mafanikio
makubwa yalionekana. Mojawapo ni lile la kuanzisha Orchestra Maquis Company
(OMACO). Kampuni hiyo ilikuwa ikimiliki shamba la matunda, wakilima kwa kutumia
matreka yao
maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao
walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko
Kuu la Kariakoo jijini Dar es
Salaam.
OMACO pia
ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa maeneo ya Sinza na pia
waliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.
Vijana wa
wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu
kila siku za Jumamosi, kuwashuhudia vijana wa Maquis du Zaire waliokuwa
watanashati na nidhamu ya hali ya juu wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.
Enzi hizo
ilikuwa ukiingia katika ukumbi huo wa White House, mbele yako macho lazima
yakutane na mbao zilizo nakshiwa kwa maandishi ya majina ya wanamuziki wote na
kukomelewa juu ya mwembe uliokuwa katikati ya ukumbi huo.
Maquis du
Zaire
ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa
manane, wanasisitisha muziki kwa muda na
kusikika kipaza sauti kikiuliza “Wapenzi mumekuja na miswakii? Wapenzi walikuwa wakijibu “ndiyooooo…”
Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo. Watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi
kurudi nyumbani kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima hadi alfajiri, muda ambao mabasi ya UDA ya
Ikarus yalikuwa yameanza kazi.
Bendi
hiyo ikiwa hapa nchini ilikuwa ikipiga na kucheza katika mitindo
mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya Chakula kapombe,
Kamanyola, Bishe Bishe, Zembwela, Chekecha na Ogelea Piga mbizi.
Mwema Mudjanga ‘ Mzee
Chekecha’ ndiye aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo. Alikuwa kivutio
kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya
kupuliza tarumbeta, aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza,
akitumia vibwagizo vya “Chekeee…. Chekechaaa”
“Tusangalaa”, “Aima imaa”, ‘Bishe
bishee”, “Saa… Sanifuu”, “cheza
Kamanyolaa” “cheza kwa maringo”, “
Cheza ukijidai” na mengine mengi.
Maquis du
Zaire
wakati huo ilikuwa imesheheni wanamuziki
zaidi ya 40 wenye vipaji vilivyopishana. Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki
katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.
Nina
uhakika kwamba msomaji wangu unashauku ya kujua au kukumbushwa kikosi kamili kilichokuwa
kinatengeneza Maquis du Zaire wakati huo. Nikianza na safu ya waimbaji
walikuwepo akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule
Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa.
Wengine
walikuwa Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo
Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’,
Tshimanga Kalala Assosa, Kabeya Badu, Masiya Radi ‘Dibakuba kuba’, Issa Nundu na waimbaji wa kike Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.
Wapiga
gita la solo alikuwepo Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye
kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo,
wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha ‘Field Marshal’.
Wengine
katika gitaa hilo walikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga
‘Vumbi’ na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.
Gitaa la
rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila
Mauffi. Bila kuwashau akina Mbambu
Kazadi, Mondo Mondonde na Nawayi
Kabwila.
Gitaa zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na
Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kulicharaza
gita hilo akiwa kajitwisha kwenye upara uliozungushiwa
simbi kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.
Kama nilivyokujuza hapo awali kwamba bendi hiyo ilikuwa
imejaza mseto wa vipaji mbalimbali. Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya
bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga/‘Super Sax’, Khatibu Iteyi
Iteyi, Kalamzoo, Alex Kanyimbo, Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna
‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na Majengo Selemani.
Wapuliza
tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku
Kelly, Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’,
Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’, Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde, Kaumba Kalemba, Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan
Machege na Ngenda Kalonga.
Madoido
na mbwembwe hizo, ziliwavutia wapenzi
wengi na kupenda kuhamishia viti vyao wakisogea sehemu iliyokuwa karibu, ili kushuhudia vijana
hao wakifanya maajabu ya kuchezea vyombo hivyo.
Pamoja na uimbaji
Mbuya Makonga ‘Adios’ alikuwa mbonyezaji wa kinada
huku Mutombo Sozzy akizicharaza drums akisaidiana na Matei Joseph.
Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu
Wabandoki Motto.
Walikuwepo
na wanenguaji mahiri ambao walikuwa wakitoa burudani za pekee
akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashid, Anna Mganga, Kinacho,
Mwajuma, Frida Shirima, Zuwena na Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.
Ikiwa
White House bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double,
Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Mwana yoka ya Babote, Ngalula, Nasononeka,
Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane wimbo ambao
ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.
Zingine
zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma,
Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini,
Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo
idadi.
Kuna
msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo”
msemo huo uliisibu bendi ya
Maquis du Zaire baada ya kiungia katika maelewano ‘hafifu’ na mmili wa ukumbi wa White House hadi kulazimika kuondoka
wakiacha ukumbi huo ukibadilishwa kuwa gereji hadi leo.
Baadaye bendi
hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Maquis Original wakipiga muziki katika kumbi za
Wapiwapi’s pale maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke, kabla ya kuhamia
ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata pale
Kinondoni.
Maquis
Original ilileta wanamuziki wengine toka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
muda mfupi kabla ya mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kuondoka kwenda
Stockholm nchini Sweden.
Wanamuziki
hao walikuwa Kivugutu Motona Chatcho (Solo), na waimbaji Freditto Butamu na
Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.
Walitikisa
ukumbi wa Lang’ata kwa nyimbo zao kali
za Mangolibo, Mayanga, Makumbele, zikisindikizwa na wimbo wa Ngalula ambapo
wakati wa chorus katika wimbo huo, Tshimanga Assosa alikuwa akimpandisha mori mpiga
gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ akimwita “vumbiii… Vimbiiii… Vumbiii…”
Nyimbo za Maquis Original zilikuwa zikipigwa
na kutamba kwa staili za ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.
Maquis Original ikiwa Lang’ata, kuna shabiki
mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’
ambaye alikuwa kivutio kikubwa kwa
wapenzi wa Maquis. Alikuwa akiachwa uwanja akionehsa uhodari wake wa kucheza
mtindo wa ‘Sendema’ huku akiwa kajitwisha chupa yenye Bia juu ya
kichwa chake.
Ni miaka takriban 23 toka jina la Maquis litoweke masikioni mwa wadau
na wapenzi wa muziki wa dansi baada ya kusambaratika katika miaka ya 1990, ikiwaachia simanzi na majonzi
wapenzi wake yasiyokwisha hadi leo.
Lakini Tshimanaga
Kalala Assosa ‘mtoto mzuri’ baadaye alitumia weledi wake katika muziki kwa
kuienzi jina la Maquis kwa kuanzaisha
bendi ya ‘Bana Maquis’ ambayo hupiga na
kukumbushia nyimbo zilizopigwa na Maquis
du Zaire na Maquis Original.
Ikumbukwe
kwamba idadi kubwa miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa humu, wameshatangulia
mbele za haki.
Wengine
ni wale wanaumwa maradhi mbalimbali akina Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’,
Mbombo wa Mboka na Mutombo Lufungula ‘Audax’
Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi
waliotangulia mbele za haki na awape tahfifu wanaoumwa, Amen.
Wapiga magita Dekula Kahanga 'Vumbi' na Ilunga Banza 'Mchafu' (kushoto) wakionesha manjonjo ya kupiga gita sakafuni.
Waimbaji wa Maquis du Zaire Kasongo Mpinda (katikati) na mapacha Kasalo Kyanga na Kyanga Songa (kulia)
Mpiga tumba Sidy Morris 'Super Konga' akionyesha mbwembwe za kupiga tumba hizo kwa mikono na mguu.
Mpulizaji wa Tarumbeta wa Maquis du Zaire, Nkashama Kanku Kelly akifanya vitu vyake.
Kiongozi wa Maquis du Ziare, Chinyama Chiyaza akicheza katika mtindo wa 'Chakula kapombe' unavyochezwa.
Wanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire wakiwa katika picha ya pamoja. Toka kushoto ni Suleiman Mbwana' Cox', Mbuya Makonga 'Adios', Mujos wa Bayeke, Steven Kaingila Mauffi na dekula Kahanga 'Vumbi'. Wengine ni Issa Nundu, Mukumbule Lolembo 'Parashi' na Roy Mukuna 'Mukuna wa Mukuna.
No comments:
Post a Comment