Sunday, March 10, 2013

MUHIDINI GURUMO ‘JEMBE’ LINAUMWA’


MUHIDINI  MAALIM  GURUMO

               JEMBE’ LINAUMWA’


December 30, 2012.


MUHIDINI MAALIM GURUMO ni mwanamuziki aliyetumikia nchi hii kwa ufanisi mkubwa toka miaka ya 1960, lakini hadi leo yupo katika dimbwi la ufukara uliokithiri.
Katika kipindi chote hicho Mzee Gurumo ametunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani pamoja na kuwaasa wazazi kutumiza wajibu wao kwa kulea watoto  na vijana  kutimiza wajibu wao.
Licha ya sifa zilizoainishwa hapo juu, mzee Gurumo hakuwahi kukumbukwa kwa lolote pamoja na mchango wake mkubwa kwa taifa hili tangia uhuru wa nchi hii mwaka 1961.

Hatimaye kwa mara ya kwanza Mzee Gurumo amekumbukwa kwa kutunukiwa nishani ya heshima ya Muungano na rais Jakaya Kikwete, siku ya maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye uwanja wa uhuru Desemba 09, 2012 Jijini Dar es Salaam.



Gurumo alivishwa nishani hiyo na rais Jakaya Kikwete ambaye aliwatunuku pia wanamuziki wengine watatu, msanii wa maigizo na mwanariadha mkongwe katika viwanja vya Ikulu, jiji Dar es Salaam.

Wasanii wengine waliotunukiwa siku hiyo ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Dar. International, Marijani Rajabu, mwimbaji mkongwe wa taarabu, Fatuma Baraka ‘Bi. Kidude’, msanii wa maigizo ya filamu Fundi Said ‘Mzee Kipara’ na  mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.

Baada ya kuvishwa nishani hiyo, Mzee Gurumo alionyesha furaha yake na kumshukuru rais Kikwete na wananchi kwa ujumla kwa kutambua kazi yake ambayo alisema iwe changamoto kwa vijana kutambua kuwa muziki  si  kwa ajili mapenzi pekee, bali kila kitu kinachoihusu jamii.

Mwandishi wa  habari hii  alifika nyumbani kwa Mzee Gurumo  huko  Makuburi, Ubungo ambapo alielezea historia yake na akasema haijui tarehe kamili aliyozaliwa, japo anafahamu kuwa alizaliwa katika  Kijiji cha Masaki, Wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani mwaka 1940.

Ni  mwanamuziki mkongwe mwenye historia  ndefu katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki   na hata nchi  zilizo chini ya Jangwa la Sahara.
Sifa kubwa aliyonayo Mzee Gurumo ni ile ya toka aanze kupiga muziki miaka 52 iliyopita, hakuwahi kupumzika ila mwezi wa mtukufu wa Ramadhani ama awe anaumwa. Kila siku za kazi hakukosa jukwaani.
Rekodi ya sifa hiyo ingeliweza kuvunjwa na mkongwe Salimu Zahoro, ambaye alimtangulia Gurumo katika muziki, akipiga katika bendi ya Kiko Kids ya mjini Tabora. Lakini baada ya bendi hiyo kufa, Mzee Salimu Zahoro  alipumzika mambo ya muziki kwa takriban miaka 20, hadi alipojiunga na bendi ya  Shikamoo Jazz.

Hivi sasa Mzee huyu  ana umri wa zaidi ya miaka 70,  ameshatoa mchango mkubwa katika nchi hii kupitia tungo za nyimbo zake zisizopungua  1, 000 zilizojaa ujumbe mzito kwa jamii.

Mzee Gurumo anailezea afya yake kwa sasa kuwa si nzuri, akisumbiliwa na maradhi yaliyopelekea yeye  kulazwa katika kitengo cha wagojwa mahututi (ICU) katika hosiptali ya Muhimbili.

Kwa masikitiko makubwa mzee huyo anasema ufukara alionao, amefikia hatua ya kuwatamani wanamuziki wa kizazi kipya na taarabu, kuwa wana mafanikio makubwa kimaisha.

Gurumo akafika mbali zaidi kwa kusema mafanikio yao ni  kwa vile soko la sasa limewapokea vyema na yeye kujisikia wivu kuwaona vijana wakiendesha maisha mazuri wakiwa na magari ya kifahari wakati yeye akitembea kwa miguu.

“Hata kwenda Hospitali Muhimbili kutibiwa, ninatumia  usafiri wa daladala licha ya muda mrefu nilioutumia katika muziki” anasikitika mzee Gurumo.
Mke wa mzee Gurumo  Pili  Kitwana alitoa dukuduku lake akisema kwamba yeye binafsi huwa anaumia roho wanapokuwa kwenye daladala  akimpeleka mumewe  hospitali, abiria  wengine huwashangaa. Lakini anasisitiza kwa kusema wana haki ya kuwashangaa  kufuatia jina kubwa la mume wake ambaye kwa hali ya kawaida hakustahili kutumia usafiri wa daladala.
Mama huyo ambaye aliolewa na Muhidini Maalimu  Gurumo mwaka 1967, walipata watoto wanne akina Mariamu, Mwalimu, Omar na Mwazani. Anamtaja  Binti yao wa kwanza Mariamu kwamba amefuata nyayo za Baba yake za usanii japo anaimba nyimbo za kizazi kipya.
Mkewe Pili, akaenda mbali zaidi akisema kwamba  laiti  kama angelikuwa na uwezo, angemtaka mumewe apumzike na masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kupata mafanikio ya maana.

Mzee Gurumo mwimbaji mwenye sauti isiyoigika, anakiri fani yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na watu wengi  wakiwemo viongozi  mbalimbali hapa nchini  akiwemo rais Jakaya Kikwete.


Anakiri kitendo cha rais Kikwete kuacha kazi zake akifuatana na mkewe, mama Salma kuja kumjulia hali, pia kumsaidia katika matibabu wakati alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kwamba kulimfariji  sana.
Muhidini Gurumo anasema baada ya ujio wa rais Kikwete hapo Muhimbili, huduma zilizofuatia toka kwa  madaktari na manesi zilikuwa ‘Baabu’ kubwa.
Hivi sasa amepewa Daktari maalumu wa kuiangalia afya yake kila aendapo hospitalini humo.
Gurumo mwenye uso wenye bashasha licha ya kudhoofu kiafya, hakukosa kutoa shukurani za dhati kwa mmiliki wa Kampuni African Stars Entertainment Tanzania (ASET),  Asha Baraka  kwa kuandaa onyesho maalumu kwa ajili ya kumchangia pesa.
“Asha Baraka namshukuru sana aliniletea shilingi milioni mbili ambazo zilinisaidia sana katika matibabu”  anasema Mzee Gurumo.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’ ‘Sikinde’ na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, JUWATA, OTTU, Mlimani Park na Orchestra Safari Sound (OSS).
Mwenyewe anasema mitindo hiyo ilitokana  na ngoma za asili ya kabila lake la Kizaramo ambazo mama yake mzazi  alikuwa gwiji wa kuimba na kucheza enzi zake.
Gurumo alianza muziki akiwa na miaka 12 lakini muziki  wa dansi alianza rasmi mwaka 1961, baada ya  kumaliza elimu ya koroani katika madrasa ambako alikuwa hodari wa kughani na kuimbaji kwa ustadi mkubwa Kaswida.

Bendi yake ya kwanza ilikuwa Kilimanjaro Chacha iliyokuwa ya ikiongozwa na Mkurugenzi  wa bendi anamtaja kwa jina la  Samwel Machango. Aidha  anasema alipofika hapo, alipokelewa na Salumu Monde ambaye alikuwa mpigaji wa gita la rhythm. Anakiri kwamba wote wawili walimpa ujasiri wa jinsi ya kulitawala Jukwaa na vilevile kwa juhudi zake binafsi alijifunza kupiga Saxophone.
Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu katika ukumbi wa Amana maeneo ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Mzee Gurumo anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba katika bendi yake ya kwanza ukiwamo wa ‘Nilipoingia Bar watu walinionea kijicho’ Anasema  hawezi kuisahau siku ambayo kwa mara ya kwanza alianza kupata pesa aliyoitolea jasho lake ilikuwa ni shilingi  tano  baada ya onyesho hilo.

Mwaka 1962 kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz Ahmed Kipande alimrubuni kwa kumpa Shilingi mia mbili ili ajiunge na bendi yake. Anasema Shilingi mia mbili miaka hiyo ilikuwa na thamani kubwa sana naye alipokea na kukubali kujiunga na Kilwa Jazz.

Mzee Gurumo anatabanaisha kwamba uongozi  wa  Ahmed Kipande, Duncan Njilima na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ hawakumtendea haki iliyostahili na  baada ya  mwaka kupita  akaamua kutafuta bendi nyingine. Alifanikiwa kupata bendi ambayo ilikuwa ndogo kuliko Kilwa jazz  ikiitwa Rufiji jazz mwaka 1963.

Mwaka 1964  Gurumo aliitwa na uongozi wa NUTA Jazz ili akubali kuwa muanzilishi wa bendi hiyo na aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama, Mnenge Ramadhani na Wilfred  Boniface.
Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine zilikuwa Kilimo ni kazi yetu na Mwengele.

Mzee Gurumo pamoja na uzee alionao bado kumbukumbu kichawani zijemjaa. Anakumbuka mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri John Simon alijiunga na bendi yao ya NUTA Jazz na anamtaja mpiga Solo, Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa NUTA Jazz.

NUTA jazz alikuwa ikimilikiwa   Chama cha Wafanyakzi  ambacho baadaye kikawa JUWATA, OTTU, TFTU hadi TUCTA.
Wakati wakiwa na TUCTA mishahara yao ilikuwa duni kiasi cha kushindwa kijikimu kimaisha, hivyo kwa pamoja wanamuziki hao wakajipanga kwa kununua vyombo vyao vya muziki kidogo kidogo hadi wakatimiza adhma yao ya kujitegemea. Ndipo bendi ya Msondo Ngoma ilopanzisha  ikilibakiza jina la Msondo kwa kuienzi staili iliyowapa  umaarufu.

Mwaka 1978 Gurumo alihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde ngoma ya ukae’ na akawa kiongozi wa bendi hiyo baada ya muda mfupi alitunga nyimbo zikiwemo Baba na Mama na Weekend.
Akiwa na bendi hiyo maisha yake yalianza kubadilika na kuwa mazuri kufuatia malipo na maslahi ya kuridhisha aliyokuwa akilipwa na uongozi wa Mlimani Park.
Anajigamba kwamba maslahi hayo ndiyo uliofikisha kujenga nyumba yake na kunua eneo la shamba maeneo ya Masaki Wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani  na kuwapeleka watoto wake katika Shule nzuri.

Anasema hatoweza kuwasahau wanamuziki alioshirikiana nao kwa karibu akiwemo aliyekuwa kiongozi msaidizi Comas  Tobias Chidumule, Joseph Bartholomew Mlenga ‘King Spoiler’ na Abdallah Gama.
Pamoja na kipato alichokuwa akikipata Mlimani Park Orchestra, mwaka 1985 mfanyabiashara maaraufu jijini Dar- es -Salaam  Hugo Kisima, akamshawishi kujiunga katika bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) ambayo ilikuwa ikiongozwa na Supreme  Ndala Kasheba aliyekuwa akipiga katika staili ya ‘Dukuduku’ nay eye Gurumo akaingia na staili ya ‘Ndekule’

Alijiunga na OSS akifuatana  na wanamuziki wawili toka  Mlimani Park akina Abel Bartazar na Kassim Rashid ‘Kizunga’ na kutoka na nyimbo za ‘Chatu mkali’ na ‘Bwana Kinyogoli’
Bendi ya OTTU ilikuwa bado inamuhitaji kurudi ndipo mwaka 1990 uongozi ulifanikiwa kumrudisha katika bendi hiyo ambayo tayari  ilikuwa ilikuwa  imebadili jina kuwa  JUWATA.

Enzi za ujana wake ‘Ubitozi’ wakati huo, Gurumo alipitia mambo mengi ya ujana yakiwemo ya  kuvuta sigara na  alikuwa mywaji wa pombe kupindukia ‘cha Pombe’  Tabia hiyo ilikifikia kukorofishana na mama yake mzazi aliyetishia hata kumutolea  ‘radhi’ kama angeendekeza ulevi.
Mkewe Pili naye alikwaruzana kila mara juu ya hiyo ya ulevi uliokithiri  na aliwahi kutishia kuomba talaka.
Hatimaye mwaka 1982, akaamua kumshinda ‘Shetani’ akaachana na ulevi kwa shinikizo la mama yake na mkewe.
Mzee huyu mwenye historia ndefu ya muziki na maisha yake kwa ujumla, amekuwa kiongozi katika bendi hiyo na anasema furaha aliyonayo ni kuona pale pamoja na umri wake kuwa mkubwa akiwa na msondo ngoma, amekwisha tunga  na kuimba nyimbo nyingi na kuzirekodi katika Studio zikiwemo za ‘Mama nipeleke kwa Baba’ Mwanangu acha Wizi, Wosi wa Baba na nyingine nyingi.
Muhidin Maalimu Gurumo amesema kwamba hana muda mrefu kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya halikadharika umri wake kumtupa mkono.
Anasema atakapostaafu atajikita katika kuwasaidia vijana ili atimize ndoto yake ya kujenga Chuo cha muziki katika shamba lake  lililopo Masaki wilayani Kisarawe, iwapo atapata wafadhili wa kumsapoti adhma yake.
Mzee huyo anasema mazoezi ni muhimu kwa kila binadamu. Yeye hulazimika kujikongoja kwenda kuimba katika bendi yake ya Msondo Ngoma. Wakati mwingine hulazimika huimba akiwa amekaa kwenye kiti. “Nja kali, nikienda huko pamoja na mazoezi ninayopata, pia huwa ninaambulia posho, inayoniwezesha kujikimu kimaisha” Mzee Gurumo  anasema kwa uwazi.

Gwiji huyu ametunga nyimbo zaidi ya 54 ambazo anasema zilizong’ara na kupendwa na watu japo yeye anasema kwamba hazina faida yeyote. Analalama  kwa kusema kuwa hapati hata senti tano ya nyimbo zake hizo. Hivyo anawaomba wadau na  wasamaria wema kumsaidia ili aweze kuzirekodi upya nyimbo hizo ili ziuzwe na yeye aweze kunufaika.

Kama walivyowahi kutamka wanamuziki wengine wa zamani, Mzee Gurumo naye amewasisitiza vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kutumia ala za muziki, ili kuweka kumbukumbu ya kazi zao kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.
Mzee Gurumo anamalizia kwa kusema anaomba serikali, mawaziri, wabunge na wadau  wote  wamuangalie kwa jicho la  huruma, kwa kumsaidia kufuatia  hali yake ya maradhi yanayomkabiri, na kwamba hana msaada mwingine, akisisitiza kuwa  wasisubiri hadi afe.

Mwisho.

No comments: