Sunday, March 10, 2013

‘BABA GASTON’ MWANAMUZIKI ASIYESAHAULIKA KILA KRISMASI


                              BABA GASTON’

MWANAMUZIKI ASIYESAHAULIKA KILA KRISMASI

Desemba 17, 2012

‘KAKOLELE VIVA KRISMAS’ ni wimbo  ambao unatamba katika vituo vingi vya redio hapa nchini nyakati hizi za sikukuu ya Krimasi. Ni utunzi wake mwanamuziki nguli wa  bendi iliyokuwa ikiitwa ‘Baba Nationale’,  Ilunga Omer ‘Baba Gaston’  aliyejizolea sifa endelevu kwa wapenzi wa muziki na  waaumini wa dini ya Kikristo Afrika ya Mashariki na Kati ambao hivi sasa wapo katika maandalizi ya sikukuu ya Krismasi.
Wimbo huo uliopangiliwa kiufundi,  hutangulizwa kwa gita la solo na kupokelewa na sauti za waimbaji mahiri wakiongozwa na Kasongo wa Kanema,  wakiwa na bendi ya Baba Nationale.
Hapana ubishi kwamba maneno yanayotamkwa katika wimbo huo, wengi wetu hatuyajui kabisa kwa kuwa ni ya lugha ya Lingala. Ingawa kuna  kipande kidogo cha mwishoni kinasikika kwa Kiswahili cha ‘Viva Krismasi mtoto wa Yesu, Yesu   anakuya’
Sauti ya Kasongo wa Kanema ambaye  bado yupo katika mji wa Naiorobi, hunogeshwa kwa vyombo vya muziki vilivyopigwa kwa mpangilio murua wa kiongozi wa bendi hiyo,  Ilunga Omer ‘Baba Gaston’
Kati ya nyimbo ambazo haziigiki, basi  ‘Kakolele’ ni mmoja wapo kwani sijapata kusikia bendi yeyote ikiwa ‘imeuchakachua’ katika kumbi mbalimbali nilizowahi kuzitembelea hapa nchini.

Mpenzi msomaji leo ninakupa historia fupi ya  gwiji hilo, ambayo inaeleza kuwa alizaliwa July 5, 1936 katika mji wa Likasi, jirani na mji wa Lubumbashi uliopo jimbo la Shaba Kusini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na akapewa jina la Ilunga Omer.
Ilunga Omer alikuwa mwanamuziki wa kwanza toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuishi katika  nchi za Afrika ya Mashariki katika miaka ya 1970 ikiwemo Tanzania.
 Amri ya rais Mobutu wa Zaire (wakati huo) ya kuwataka raia wote wa nchi hiyo ya kubadilisha majina yao kuwa ya kiafrika,  Ilunga Omer ‘Baba Gaston’ alibadilisha jina lake na  kuwa  Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda.
Waswahili wanasema ‘Ukitaka uhondo wa ngoma, ni  uingie ucheze’ ndivyo alivyofanya  rais huyo,  kwa kuwaonyesha mfano wananchi wake kwa  yeye mwenyewe  kubadilisha jina lake la  Joseph Mobutu kuwa Mobutu Sese Seko Kuku Ng’endu Wazambanga.
 Kipaji cha kupiga muziki cha ‘Baba Gaston’ kilianza kuonekana muda mfupi baada kufundishwa na mpiga Piano toka nchi ya Ugiriki, Leonides Rapitis. Alitoka na wimbo wa  ‘Barua kwa mpenzi Gaston’ wakati huo akiwa bado mwanafunzi.
Alipofikiisha umri wa miaka 20, Gaston aliunda bendi yake ya Orchestra Baba Nationale. Bendi hiyo ilipanda chati na kufanya safari nyingi kupitia Zambia, Zimbabwe na nchi nyingine za Ulaya, kabla ya kuwa mwanamuziki wa kwanza kuishi nchi za Afrika ya Mashariki katika miaka ya 1970.
Mmoja wa wanamuziki wakali wa bendi hiyo alikuwemo Kabila Kabanze ‘Evany’ ambaye aliimba kwenye  bendi hiyo ya Orchestra Baba Nationale katika mji wa  Lubumbashi baadaye akawa nyota katika bendi ya  Les Mangelepa katika mji wa Nairobi nchini Kenya.

Kwa mujibu wa  Kabila Kabanze ‘Evany’ aliyenukuliwa akisema kwamba bendi hiyo ya Orchestra Baba Nationale,  ilifanya safari toka Lubumbashi  kwenda  Kinshasa kwa ajili ya kurekodi.
 Akitoa ushuhuda huo alisema mwaka 1971 kufuatina  miundo mbinu ya barabara kuwa mibovu walilazimika kupitia njia ya  Kisangani hadi Kalemi, iliyopo mpakani na Tanzania.
Safari yao hiyo badala ya kuelekea Kinshasa, wakaamua  kuingia Afrika ya Mashariki na kujikuta wakiweka makazi katika jiji la Dar es Salaam, na kupiga muziki katika kumbi mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne.
Wakati huo nchi yetu ya Tanzania kulikuwa na Studio moja ya kurekodi miziki ya Redio Tanzania Dar es Salaa (RTD) Baba Gaston na bendi yake kwa kutaka kurekodi kwa haraka nyimbo za bendi yao,  waliamua kuvuka mpaka kwenda  Nairobi kwa minajiri ya kurekodi.
Jiji la Nairobi wakati huo kulikuwa na ushindani mkubwa wa bendi nyingi zikiwemo za  Les  Wanyika, Super Mazembe, Shika Shika, na nyingine nyingi. Ushindani huo uliifanya bendi hiyo kudumu katika jiji hilo kwa takribani miaka minne, baadaye mwaka 1975 Baba Gaston aliamua kulikacha jiji hilo la Naorobi baada ya kubaini kuwa bendi yake  haikuwa na wapenzi wengi wanaoishabikia.
 Maelewano mabaya miongoni mwa wanamuziki na uongozi wa bendi hiyo ulisababisha wanamuziki wengi wa Baba Nationale kuikimbia bendi  hiyo mwezi  July 1976 na kusababisha kusambaratika bendi hiyo.

Wanatajwa wanamziki waliomkimbia Baba Gaston ni akina Bwami Walumona, Kasongo Wakanema, Kabila Kabanze ‘Evan’, Kalenga Nzaazi Vivi. Wengine ni pamoja na Lutulu Kaniki Macky na Twikale wa Twikale  wakaenda kuunda bendi ya Orchestra Les Mangelepa.

Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda ‘Baba Gaston’, ataendelea kukumbukwa daima pamwe na wimbo wake wa ‘Kakolele Viva Krismasi’ ambao ataendelea kutamba kila nyakati za Krismasi miaka nenda rudi.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii toka Nairobi, aliyekuwa mwanamuziki wa bendi hiyo Kabila Kabanze ‘Evany’ amesema kwamba  ‘Baba Gaston’ alifariki dunia mwaka 1977 akiwa  jijini Arusha na aliacha mke na watoto saba.

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.  


 Mwisho.

No comments: