MTAMBUE MWANZILISHI WA WESTERN JAZZ
MZEE
IDD NHENDE
Febr. 2013.
BENDI YA WESTEN JAZZ ilikuwa kongwe ambayo ilianzishwa mwaka 1959, kabla ya
nchi yetu haijapata Uhuru.
Umaarufu wa bendi hiyo
ulipanda ‘chati’ zaidi baada ya wimbo
wake wa Vigelegele kuibwa na bendi kongwe toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
ya Soukos Stars.
Jina la Idd Nhende ni geni masikioni wa wapenzi wa muziki wa
dansi hasa kwa kizazi kilichoiona dunia baada ya miaka ya 1970.
Western jazz ikajipatia
umaarufu mkubwa hapa nchini na nje ya mipaka yetu hadi ilipotoweka katika
medani ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1970.
Pamoja na umaarufu wote huo,
historia ya bendi hiyo ya Western Jazz haiwezi kukamilika iwapo utaliweka pembeni jina la Mzee Idd Nhende ambaye ndiye aliyepata wazo
la kuazisha bendi ya hiyo mwaka 1959.
Wasifu wa Mzee Idd Nhende anaeleza
kwamba alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule ya msingi huko
Nzega. Mwaka 1944 alichaguliwa kujiunga katika shule ya Sekondari ya wavulana ya
Tabora, huko akakuta kikundi cha blass
band, akajiunga nacho akipiga ala iliyojulikana kwa jina la Cornet.
Baada ya kumaliza masomo ya
Sekondari, alikwenda Dar es Salaam na akajiunga
na Chuo cha Afya, Sewa
Haji Medical
Training Center.
Baada ya kumaliza mafunzo
akaajiriwa katika Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili.
Upenzi wake wa muziki
ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na bendi ya Rufiji Jazz kama
mpiga tarumbeta.
Bendi hiyo kwa wakati huo
ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo
linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi
wa Arnatougro.
Kutokana na miji ndio kwanza ilikuwa
ikianza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu
kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au
kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali.
Wakoloni waliokuwa wanatawala
nchi yetu ya Tanganyika wakati huo, waliigawa katika
majimbo mbalimbali. Majimbo hayo yalikuwa ya Northern
Province, Southern Highlands Province na Western Province
Wanamuziki wa wakati huo walianzisha
bendi wakizipa majina ya maeneo yale
wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo
ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Kwa vile Nhende alitoka Nzega huko Tabora ulikuwa
katika jimbo la Magharibi yaani Western
Province, akaamua
kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi ndipo alipoanzisha bendi ya Western Jazz
mwaka 1959.
Mzee Idd aliweza kupata fedha
baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mama yake na kufanikiwa kununua vyombo aina ya
Grampian toka duka la vyombo vya muziki lililojulikama kama Souza Junior
lililokuwepo mtaa wa Mkwepu, jijini Dar
es Salaam.
Wakati huo katika bendi za
aina yake, ni Dar es Salaam
Jazz pekee ambayo ilikuwa na magita ya
umeme. Kufuatia hali hiyo, Mzee Nhende
akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gita la umeme wa
kwanza Haus Dibonde ‘msukuma’, aliyekuwa anapigia bendi ya Dar es Salaam Jazz iliyokuwa chini ya Mzee Muba.
Baada ya hapo akawapata
wanamuziki wengine kutoka bendi ya Ulanga Jazz. Wakati huo chombo cha Banjo
kilikuwa muhimu, hivyo akamtafuta mpiga Banjo toka bendi ya Cuban Marimba ambayo wakati huo ilikuwa na tawi jijini Dar
es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu.
Mwaka mmoja baadae alipata
uhamisho wa kwenda mji wa Morogoro, akalazimika kuongeza wasanii wengine ili kuimarisha bendi wakati yeye akiwa hayupo.
Akampata mwimbaji mahiri
wakati huo David Makwaya, Ally Rashid (huyu
ameacha muziki karibuni akiwa Msondo) na mpiga Saxophone toka Zanzibar.
Kwa bahati mbaya yule mpiga
gita Haus akapatwa na kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina
kutokana na ushindani mkubwa wa bendi uliokuwepo.
Hivyo basi walifuatwa
wanamuziki watatu toka Tabora Jazz. Wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja
katika bendi iliyokuwa na makazi huko Mwanza, ikiitwa Kimbo Twist Band na
wakahamia Tabora Jazz. Waliochukuliwa kutoka Tabora Jazz kwenda Western Jazz walikuwa
akina Rashid Hanzuruni, Kassim ponda na Omary Kayanda.
Baada ya kazi nzuri sana, Rashid Hanzuruni
ambaye alikuwa mkung’utaji wa gita la solo, nae akarukwa na akili katika
mazingira yaleyale ya yule mpiga solo wa kwanza Haus Dibonde. Bendi ikalazimika kumrudisha Hanzuruni Tabora
ambako alikaa mpaka mauti yake yalipomfika.
Baadaye Wema Abdallah
akachukua nafasi ya Hanzuruni ya kupiga
solo.
Nidhamu ilikuwa ni moja ya kigezo
cha kuwa mwanamuziki katika bendi ya Western wakati huo. Haikujali umaarufu wa
mtu kwani mwanamuziki yeyote alikuwa na
nafasi kubwa ya kutimliwa kwa utovu wa nidhamu. Hivyo tatizo la utovu wa
nidhamu lilifanya Wema Abdallah kuondolewa
katika bendi hiyo ya Western Jazz.
Bendi ikiapata ‘kifaa’
kingine baada ya kumnyakua mpigaji mzuri
wa gita la solo, Shamba Abdallah kuziba pengo la Wema.
Shamba alionesha umahiri
mkubwa kwa kushiriki katika kupiga solo kwenye nyimbo za Rosa
na zingine nyingi.
Ukumbi wa nyumbani wa bendi
ya Western Jazz ulikuwa ukiitwa Alexander Hall, ambalo baadaye ukaja kuitwa
Ukumbi wa DDC Kariakoo.
Ushindani wa bendi na bendi
uliendelea miaka hiyo, hivyo iliilazimu
bendi ya Western kununua drums baada ya wenzao wa bendi ya Kilwa Jazz kuzipitisha
drums zao walizonunua kwa minajiri ya kuwaringishia.
Walinunua toka kwa bendi moja
ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini
ya mkataba waliyousaini kwa Lebo ya
Phillips ya Kenya.
Hatimae Western jazz akipiga katika mtindo wao wa Saboso, walitoweka katika anga za muziki mwishoni mwa miaka ya 1970.
Wetern kabla ya hapo ilitoka
na vibao vingi vilivyopendwa na mashabiki wake hapa nchini. Baadhi ya nyimbo
zao hizo zilikuwa za Rosa, Jela ya Mapenzi, Helena no 1& 2 na Vigelegele.
Kwa ruhusa yako msomaji wa
makala haya naomba nikudonyolee kipande cha wimbo wa Vigelegele. Unanza
hivi “Vigelegele
ndiyo furaha jamaa hehehe!!! utamu wa
ngoma ni kushangiliwa jamaa hehehe!!!
chereko chereko na mayowe mengi, hehehe!!!
mkofi mengi na vibwebwe, ndiyo
furaha, hayo, hutokea ? pamoja!! Western, mayowe!! kwa wingi,,
njoo uonee, furaha furaha…”
Wimbo huo wa Vigelegele
uliwatoa ‘udenda’ wakongwe wa muziki
toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
ya Soukous Stars, na kujiamlia kuukwiba pamoja na ule wa Dada Asha wa Tabora
jazz. Kwa utaalamu mkubwa walionao, Soukous
wakazichakachua nyimbo hizo pamoja na nyingine na kuziweka katika album
moja iitwayo Nairobi
by Night.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment