UNAMKUMBUKA
SALUMU ABDALLAH WA CUBAN MARIMBA ?
Morogoro, moja ya miji iliyokuwa
maarufu kwa burudani katika miaka ya 1950, 1960 na ya 1970. Watu wengi walitoka
Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa
bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake
kupangwa kituo cha Morogoro.
Kati ya hizo bendi mbili shindani
Morogoro Jazz na Cuban Marimba Band. Bendi ya Cuban Marimba ilikuwa ndoto ya
mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah aliyezaliwa
Mei 5, 1928, mkoani humo.
Baba yake alikuwa mwarabu na mama
yake mwenyeji wa Morogoro. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na
akachaguliwa kuendelea na shule huko Dar es Salaam, maana wakati ule ililazimika
kwenda Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo. Pamoja na
kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za
biashara.
Katika kipindi hicho Salum alianza
kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa
maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika.
Pamoja na baba yake kutokupenda aina
ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya
kupigia hizo santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba
kujifunza muziki.
Alitoroka hadi Mombasa ili apande Meli
kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya
dunia na safari yake ikaishia Mombasa, nchini Kenya.
Baba yake alimrudisha Morogoro,
akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa
muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar
es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi
ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita
bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika
santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa
duniani kote.
Hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali
akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana. La
Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka
hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu, Salum
Abdallah –Band Master.
Katika kuiona Dar es Salaam Jazz
Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum
kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es
Salaam Jazz band.
Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi
rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka
Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza,
Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Nzige, Daulinge.
Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina
la Cuban Marimba Jazz Band ambalo lilianza kuwa maarufu kiasi cha kwamba mwaka
huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi
nyimbo za bendi hii.
Bendi ya Cuban
Marimba ikiwa na nguli hiyo iliwahi kurekodi vibao vingi vikiwamo vya Ngoma iko
huku, Naumiya,
Ubaya, Nalia Nalia, Wanipendeza, Cuba Chacha na Ndiyo hali ya Dunia. Zingine ni
Kazi Tanzania,Shemeji, Tanzania Twist, Sipati majibu, Salaam kwa jumla na
Wanawake Tanzania. Salumu Abdalaah hakuishia hapo alitoka na vibao vingine vya
Kachacha, Tulime Mashamba, Wabeberu, Kimanzi, Si kosa lako Unavunja Utu, Mpenzi
Wee na Maisha matamu
Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa
mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo
taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka
nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa
tarehe 19 Novemba 1965.
Cuban Marimba Band iliendelea kupiga muziki mjini humo
ikiongozwa na Juma Kilaza hadi naye alipofariki dunia.
Mwisho.
Nashukuru kupata msaada mkubwa kupitia Blog ya ‘Kijiwe cha
Kitime’
No comments:
Post a Comment