Sunday, August 9, 2015

MUTOMBO LUFUNGULA NGUZO YA MAQUIS ILIYOTOWEKA



MUTOMBO LUFUNGULA NGUZO YA MAQUIS ILIYOTOWEKA
Kwa wale waliokuwa vijana wapenda muziki wa dansi kati ya miaka ya 1970 hadi 1990, jina la mwanamuziki Mutombo Lufungula ‘Audax’ haliwezi kuwa geni.

Alikuwa mtunzi na mwimbaji katika bendi za Maquis du Zaire na Maquis Original.

Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi na wanahisa  wa bendi hiyo pamoja na Kampuni ya Orchestra Maquis Company (OMACO).

Mutombo aliitumikia bendi hiyo kwa nguvu zake zote tangu akiwa kijana, hadi mauti yake yalipomfika akiwa na miaka takribani 70.

Kabla ya kifo chake aliugua kwa kipindi kirefu, hatimae akafariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi ya Aprili 23, 2015 akiwa nyumbani kwake Kimara Michungwani Jijini Dar es Salaam.

Lufungula alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Kiharusi tangu mwaka 2005, yaliyopelekea kupooza upande mmoja wa mwili.

Kipindi chote alikuwa akiuguzwa na wanawe ikizingatiwa kwamba mkewe, alikwisha tangulia mbele za haki miaka kadhaa kabla ya yeye kupatwa na maradhi hayo.

Ugonjwa huo ulimfanya ashindwe kuendelea na shughuli zake za muziki, akajikuta akiishi katika hali ngumu akiwategemea baadhi ya marafiki, jamaa na mabinti zake.

Audax alisikika akifanya mahojiano na mtangazaji wa TBC Taifa  ‘manju wa muziki’ Masoud Masoud, akaelezea hali yake ilivyo mbaya kimaisha.

Alitamka kwamba hakuwa na msaada wowote toka kwa watu aliokuwa akiwatarajia, ila wachache sana waliojaribu kwenda japo kumjulia hali nyumbani kwake.

Baada ya kifo maadalizi ya mazishi yakafanywa na ilipotimu Aprili 26, 2015, sala ya kuaga mwili wa Mutomba ilifanywa katika hospitali ya Mwananyamala kabla ya mwili wake kuwekwa katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mutombo ‘Audax’ ataendelea kukumbukwa na wakazi wengi wa Magomeni Mapipa, mtaa wa Mikumi, ambako aliishi kwa kipindi kirefu kabla ya kuweka makazi yake huko Kimara Michungwani.

Wasifu wake umeelezwa kwamba alizaliwa mwaka 1945 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyejiunga na bendi ya Maquis du Zaire katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bendi hiyo iliingia hapa nchini mwaka 1972, ikiwa na jina la  Maquis Du Zaire.

Kundi hilo lililokuwa na wanaanzilishi tisa, ilianza likiwa na jina la Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken Success na baadaye Super Gabby.

Bendi hiyo iliingia hapa nchini Tanzania mwaka 1972 likiwa na jina jipya la Orchestra Maquis Du Zaire.

Walipoingia nchini walipiga katika kumbi nyingi hususani Mikumi na White House pale Ubungo, jijini Dar es Salaam.
 
Walianza kwa mbewembwe nyingi wakitumia mtindo wa ‘Chakula chakula kapombe’ ukaja mtindo wa ‘Zembwela’ ukafutiwa na ‘Kamanyola bila Jasho’ 

Mzee Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ alikuwa kivutio kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya  kupuliza tarumbeta.

Aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia  vibwagizo vya “Chekechaa Chekeeee….  Chekechaaa”  “Tusangalaa”, “Aima imaa”, ‘Bishe bishee”, “Saa… Sanifuu”,  “cheza Kamanyolaa”  “cheza kwa maringo”, “ Cheza  ukijidai” na mengine mengi. 

Wanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘Kiki’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Nkashama Kanku Kelly, Chinyama Chiaza, Mukuna Roy na yeye Mutombo Lufungula, walikuwa kivutio kikubwa katika jukwaa wakionesha uchezaji wa mtindo wa Kamanyola.

'Audax' alikuwa mfano wa kuingwa na wanamuziki wengine wa bendi hiyo kwa jinsi alivyokuwa akijitoa kwa uwezo wake wote kutekeleza  majukumu yake ipasavyo. Hakuwahi kukosa onesho lolote ukumbini, ila kwa sababu ya msingi.

Kwa ushirikiano mkubwa wa  wanahisa waliokuwa chini ya uongozi wa Chinyama Chaiza bendi hiyo baadae ilifungua Kampuni iliyoitwa Orchestra Maquis Company(OMACO) 

Kampuni hiyo iliweza kuingia mkataba na Kampuni ya Scania pia ilikuwa na mashamba maeneo ya Mbezi wakilima mazao na kuyapeleka sokoni Kariakoo.

Wanahisa hao walikuwa akina Chinyama Chiaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mbuya Makonga ‘Adios’ pamoja na yeye Mutombo Lufungula ‘Audax’

Kifo cha Lufungula kiligeuza historia ya wanamuziki waanzilishi wa bendi hiyo.
Katika orodha ya hapo juu, ni mwanamuziki Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Vicking’, ambaye anatumikia  kifungo cha maisha jela ndiye aliye hai.

Mutombo Lufungula kwa nyakati tofauti alikuwa akishirikiana vyema na waimbaji wenzake akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Mbuya Makongo ‘Adios’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Mbombo wa Mbomboka, Kiniki Kieto, Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari,  Tshimanga Kalala Asossa na Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’.

Audax na bendi yao waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi wakitumia mitindo mingi iliyokuwa ikibadilika kila mara kufuatia ubunifu wa wanamuziki hao.

Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Chinyama Chiaza ‘Chichi’ akisaidiana na Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Vicking’.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, Mutombo alikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo.
Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na ‘Mpenzi Luta’, ‘Mimi’na nyingine nyingi alizotunga na kushiriki kuimba akiwa katika bendi ya Orchestra Maqis du Zaire.

Kila jema hukumbwa na matatizo, Maquis du Zaire baadae ilikutana na matatizo yaliyosababisha bendi hiyo kusambaratika. 

Audax na wanamuziki wengine wakauda bendi nyingine kwa jina la Maquis Original.
 
Lufungula aliungana na baadhi ya wanamuziki akina Tshimanga Kalala Asossa, Dekula Kahanga ‘Vumbi’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Mukuna Roy, Ilunga Banza ‘Mchafu’, Mujos wa Bayeke, Kaumba Kalemba, Mulenga Kalondji ‘Vata’ na wengine wengi wakaunda bendi hiyo.

Akiwa na Maquis Original Audax kwa kutumia talanta yake, aliweza kuachia kibao kilichoshika chati cha ‘Kisembengo’ wakati huo bendi hiyo ikiwa na jina la Maquis Original iliyokuwa na mako makuu yake katika ukumbi wa Lang’ata maeneo ya Kindondoni jijini Dar es Salaam.

Maquis Original iliongeza wanamuziki wengine toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akina Kivugutu ‘Motto na Chacho’ aliyekuwa akipiga gitaa la solo, Bobo Sukari na Freditto ‘Butamu’ waliokuwa watunzi na waimbaji.

Mutombo alishirikiana vyema na safu ya wanamuziki wa bendi hiyo akiwemo waimbaji wakipiga katika mtindo wao mpya wa ‘Sendema’ na ‘Washa washa’ .

Mungu iweke roho yake pahala pema peponi,  Amina.



No comments: