ANANIA NGOLIGA MWENYE UWEZO MKUBWA KATIKA
MUZIKI LICHA YA ULEMAVU WAKE WA MACHO.
Nchini Marekani yupo mwanamuziki Steve Wonder mwenye
ulemavu wa macho aliye na ukwasi mkubwa unaomuweka katika nafasi ya kuwa
miongoni wa wanamuziki matajiri duniani.
Miaka ya 1980 na 1990 alikuwepo mtunzi na mwimbaji
katika bendi ya Juwata raia wa kutoka nchini Kenya, Niko Zengekala, aliyekuwa
na ulemavu wa macho pia. Aliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa
muziki wa dansi kwa tungo halikadhalika uimbaji wake. Hii ni kudhihirisha kuwa
ulemavu siyo sababu ya kubweteka.
Makala haya yanamzungumzia mwanamuziki Anania Ngoliga,
mwenye talanta nyingi katika muziki. Amepitia vikwazo vingi vikiwamo vya
kubezwa na kufuatia ulofa na ulemavu wake wa macho.
Wasifu wa Ngoliga aliwahi kuelezea kuwa pamoja na kuwa
yeye ni mwanamuziki, hajui alikojifunza ala inayoitwa Kalimba, inayotumiwa na
wasanii wa eneo lao la Mpawapwa, mkoani Dodoma ila alijikuta tu analijua.
Alipozaliwa baada ya kupata
ufahamu, aliwaona baba pamoja na baba zake wadogo wote wakipiga ala hiyo.
Anania alisema kuwa hata dada zake watoto wa baba yake mdogo
walikuwa mabingwa wa kupiga Kalimba.
Kwa kawaida yeye ni mcheshi kila wakati,
anakumbuka wakati akiwa bado mdogo yeye na ndugu zake walikuwa wakishindana
kupiga chombo hicho.
Anania alizaliwa akiwa na udhifu wa kuona vizuri, tatizo
hilo liliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka mitano, macho yake yakaanza
kupoteza uwezo wa kuona kabisa.
Alipelekwa kwenda kuanza shule ya Wasioona ya Buigiri,
lakini anakiri na kutoa shukurani nyingi
kwa mwalimu wake Abel Mbata. Mwalimu huyo alikuwa anafundisha hapo Buigiri
ndiye aliyemshawishi babu yake ili aweze kujiunga na shule hiyo.
Baada ya ushawishi huo Ngoliga akafanya
mipango yote ya yeye kujiunga na shuleni hapo rasmi.
Katika shule ya Buigiri kulikuweko na magitaa na piano
na vyombo vingine vya kisasa, hivyo akajifunza pia kupiga vyombo hivyo.
Kufikia darasa la nne Anania tayari alikuwa kiongozi wa Kwaya
ya shule yake hiyo ya Buigiri.
Aliendelea na masomo shuleni hapo hadi alipomaliza
darasa la saba mwaka 1976.
Mara baada ya kumaliza shule alirudi kwao Mpwapwa mkoani
Dodoma.
Anania alipofika Mpwapwa akajiunga na Kwaya ya Kanisa
Kuu la Anglican la Mpwapwa, ambako hata huko baada ya muda mfupi akawa mwalimu
wa Kwaya hiyo.
Mwaka 1987 aliamua kwenda katika jiji la Dar es Salaam
akasindikizwa na rafiki yake kwenda kumsalimia dada yake aliyekuwa kaolewa
huko.
Dada yake alikuwa akiishi maeneo ya Msasani, lakini kwa
bahati nzuri jirani na alipofikia kukawa na jamaa aliyekuwa na gitaa.
Hivyo Anania Ngoliga akawa anaachiwa kupiga gitaa hilo
mara kwa mara, jambo ambalo likamfanya shemeji yake amuulize kwanini asijiunge
na mojawapo ya bendi.
Kwakuwa mmiliki wa hilo gitaa alikuwa anawafahamu baadhi
ya wanamuziki wa bendi iliyojulikana kama Jambo Stars, iliyokuwa mali ya Dk.
Vulata, ikiwa na makao makuu huko Komakoma maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Hivyo Anania akaenda kuonana na wanamuziki wa bendi hiyo
na kujitambulisha kama yeye anauwezo wa kuimba, huku akilazimika kuficha kuwa
anajua pia kupiga gitaa.
Alifanya hivyo baada ya kuingiwa na hofu baada ya
kuwasikia wapigaji wa magitaa waliokuwepo katika bendi hiyo wakati ule, ambao
walikuwa wazuri sana.
Ngoliga aliwakuta wanamuziki walikuwapo katika bendi
hiyo ya Jambos Stars akina Kazembe wa Kazembe, Cobra wa Bilumba ambao wote
walikuwa wapigaji wazuri wa magitaa.
Alikuwapo Omari Gendaeka aliyekuwa akiliungurumisha gitaa
la besi na mwingine aliyekuwa akijulikana kwa majina ya Cheo Ali.
Anania Ngoliga alifanyiwa usaili na akaonekana anafaa,
hivyo akawa mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo ya Jambos Stars.
Aliendelea kupiga katika bendi hiyo mpaka siku moja
ambapo mwanamuziki aliyekuwa raia toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lovy Longomba, alipita kuangalia mazoezi yao.
Baada ya kumshuhudia Ngoliga akabaini uwezo wake, Lovy
muda uleule akamtamani kumchukua awe katika bendi yake ya Afriso Ngoma.
Lovy Longomba akaenda kwa shemeji yake Anania, kumuomba
amshawishi Anania ajiunge na Afriso
Ngoma. Bendi hiyo ilikuwa ni mali ya mzee Mwendapole na Lovy akiwa kiongozi wa
bendi.
Anania alitamka kuwa kitendo hicho aliona kama ni ndoto, kwakuwa hakikupita
kipindi kirefu tangu afike katika jiji hilo akitokea Mpwapwa. Aidha alikuwa
hajawahi kupigia bendi yoyote, ikaona maajabu pale alipoombwa na mwanamuziki
kama Lovy Longomba kwenda kujiunga na bendi yake ilikuwa kama ndoto.
Anania Ngoliga hakufanya ajizi alienda kuripoti katika
bendi hiyo ya Afriso Ngoma lakini kwa bahati mbaya siku alipofika huko, ilikuwa
ndio siku Lovy alikuwa anasafiri. Hata hivyo Lovy aliacha maagizo kwa
wanamuziki wenzake kuwa wampokee Anania, na kwa uhakika zaidi wamfanyie
mahojiano.
Kama Waswahili wasemavyo kuwa “Hakika asiyekujuwa
hakuthamini…” hakuna mwanamuziki yeyote miongoni mwao aliyeshughulika nae.
Fikra tele zikamjaa Anania akidhani kuwa yawezekana
wenzake hao walimdharau kufuatia udhalili aliokuwa nao hapo. Hakuwa hana hata
viatu, alikuwa amevaa viatu vya matairi alivyotoka navyo Mpwapwa.
Alienda mbali zaidi akijihisi kuwa labda upofu wake
unamfanya wasimtilie maanani.
Baada ya wiki mbili Lovy alirejea akakuta mahojiano hajafanyiwa. Akamuomba aimbe, nae akaimba vizuri baadhi ya
nyimbo za Afriso, akajikuta yuko katika neema kubwa kwani baada ya jaribio
hilo akapata ajira mara moja.
Wakati huo huo waimbaji wawili wa bendi hiyo Kasavubu na
Anderson Supa wakaachishwa kazi.
Bendi ya Afriso Ngoma ilikuwa imesheheni wanamuziki
waliokuwa na uwezo mkubwa katika muziki. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja
na John Maida, Robert Tumaini Mabrish,
Mjusi Shemboza, Kasongo Kalembwe, Peter Kazadi wote hao walikuwa wakishika ala
za muziki.
Kwa upande wa waimbaji walikuwa Lovi Longomba, Ramadhani
Kinguti ‘Systeme’, Tofi Mvambe na mwenyewe Anania Ngoliga.
Bendi hiyo iliweza kurekodi nyimbo nyingi ikiwemo ya
‘Elly wangu’ vilevile ilipata fulsa ya kusafiri
karibu wilaya zote hapa nchini.
Ngoliga baadae aliamua ‘kuitosa’ Afriso Ngoma, akahamia
katika bendi ya Legho Stars iliyokuwa imeanzishwa.
Kwa mara ya kwanza bendi ya Legho Stars ilipoanzishwa
waimbaji walikuwa yeye Anania Ngoliga, Tshibanda Sonny, Marcelino Vitalis na
Lucy Emea. Kwa upande wa wapiga vyombo
walikuwapo akina Stamili Uvuruge, Chris Chiwaligo, George Mtully na Hemed
Mganga.
Bendi ya Legho Stars nayo ilionja hamahama ya wanamuziki
wake. Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki kuhamahama, Legho Stars iliondokewa na
wanamuziki wake akina Stamili Uvuruge pamoja na Tshibanda Sonny.
Ili kuiamarisha bendi hiyo, ilisajiri wanamuziki
wengine akiwemo mtunzi na mwimbaji Tshimanga Kalala Assosa Jemsia Msuya, John
Maeda na Shaaban Manyanya kwa pamoja wakaianza
Legho Stars ya awamu ya pili.
Ngoliga bado safari yake ya kutafuta ilikuwa
haijakamilika. Hakukaa sana katika bendi hiyo ya Legho Stars akaenda kujiunga
na kundi la Ram Choc Stars liliyokuwa linaongozwa na mwanamama Rukia Mtama.
Katika bendi hiyo ilikutana na waimbaji wengine ‘wakali’ akina Banza Tax,
Salim Shaaban, Adiel Makula, Chris Chiwaligo, Ado Mpoloto , Geofrey Charahani
na kwenye upigaji wa gitaa la rhythm, alikuwa ni Yahaya Mkango.
Ram Choc Stars ilipata mkataba katika Iringa
hotel,iliyopo mjini Iringa.
Wanamuziki takribani wote walitimka wote kwa pamoja siku
ya mwaka mpya 1991, wakaiacha bendi hiyo wakilalamika kutolipwa mishahara.
Ule msemo wa Waswahili kwamba “Usiache mbachao kwa msala
upitao” Ngoliga baada ya ‘mtiti’ wa wanamuziki wa bendi nzima kuhama Ram Choc
Stars, aliamua kurejea tena Legho Stars
wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ aliyekuwa
akilicharaza gitaa la solo.
Wanamuziki wengine waliokuwepo ni John
Maida, alikuwa akipiga gitaa la rhythm na Christopher Chiwaligo na gitaa
la besi lilikuwa likiungurumishwa na Adolf Mpoloto.
Waimbaji walikuwa Anna Mwaole, Banza Tax, Salim Shaban
na yeye Anania Ngoliga.
Lakini kama nilivyokujuza msomaji wa makala haya kwamba
Anania alikuwa mtafutaji. Kwa mara nyingine tena akaiacha
bendi hiyo na kuhamia kwenye bendi iliyokuwa mbioni kuanzishwa ya Ngoza
Makayota.
Juhudi za kuanzisha bendi hiyo ziligonga ukuta baada ya
danadana za ahadi zikawa nyingi bila kununuliwa vyombo vya muziki.
Wanamuziki hao wakawa wanafanya mazoezi bila kupiga
dansi. Hali hiyo ilipelekea yeye na wanamuziki wenzake wakaondoka tena
kundi zima na kwenda Iringa. Huko wakajiunga na bendi iliyokuwa inaendeshwa na Kanisa Katoliki la Mshindo iliyokuwa inaitwa VICO Stars (Vijana Catholic
Stars). Hata huko hawakukaa muda mrefu katika bendi hiyo kufuatia masharti
magumu na pia haikuwa na fedha za kuwalipa.
Aidha maonesho yake yalikuwa machache sana ambayo karibu yote yalifanywa
vijijini.
Wanamuziki hao watano wakakimbilia kwenda mji mkuu wa Tanzania Dodoma. Wakati walipokuwa
safarini kwenda Dodoma kujiunga na bendi ya Materu Stars, kwa bahati mbaya hawakupata
nafasi ya kufanya onyesho lolote kutokana na tatizo la kukosekana kwa vyombo.
Wakati wakihangaika siku moja wakatembelewa
na mwanamuziki Kasaloo Kyanga
wakiwa mazoezini. Kasaloo aliwaambia kuwa wanahitajika tena mjini Iringa ambako
kulikuwa na bendi ikitarajiwa kuazishwa.
“Mtafutaji hachoki, akichoka kaisha pata” msemo huu
ulijionesha wazi baada ya Ngoliga na wenzake wakaamua karudi Iringa,
wakaanzisha bendi ya Living Light mwaka 1993 mwishoni.
Bendi ihiyo ilianza kupiga katika hoteli ya Living Light,
iliyokuwepo eneo la Wilolesi mjini humo.
Bendi yao hatimaye ikapata mkataba wa kupiga muziki
Dodoma Hoteli. Tatizo likawa kwa mmiliki wa bendi aliyetoa amri kuwa wanamuziki wapige muziki bila
kulipwa chochote hadi pale atakaporudisha fedha alizonunulia vyombo.
Amri hiyo ikawa gumu wakikumbuka kuwa hakukuweko na
makubaliano yoyote kati ya wanamuziki na mwenye mali katika mkakati wa kununua
vyombo.
Kafuatia hali hiyo ikalazimu wanamuziki waondoke kwenye
bendi hiyo baada ya kufanyika ‘Varangati’ kubwa.
Wakapata taarifa kuwa kuna shirika lilioitwaTACOSODE
lilikuwa na vyombo vya muziki, hivyo kundi hilo lilijiunga na na kutengeneza
bendi ya TACOSODE mwaka 1995.
Anania aliweza kuendeleza bendi hiyo hadi mwaka 2002,
vyombo vyao vilipo chakaa kufika hali ya kutoweza kutumika tena.
Tahfif katika maisha yalianza kuonekana baada ya
kujiunga katika bendi ya Tango Stars, ambapo walikuwa wakilipwa mishahara.
Lakini ghafla mwenye bendi akaamua kushusha mishahara yao.
Wanamuziki hao wakawa hawana jinsi ila kuiacha bendi hiyo ambapo Anania akahamia
katika bendi ya Karafuu huko Zanzibar.
Anania Ngoliga aliamua kwenda kujiunga katika bendi ya
Kalunde inayoongozwa na Deo Mwanambilimbi ambako ndiko yuko mpaka sasa.
Kwa makala haya natumani mpendwa msomaji utakuwa umemfahamu
Anania Ngolinga, jinsi alivyofanya kila aina ya jitihada kutimiza malengo yake
ya kuwa mwanamuziki pasipo kukata tamaa. “Penye nia pana njia”
Hili ni fundisho tosha kwa wanamuziki wanaochipukia kuto
bweteka baada ya kutoa ka- single kamoja!
Mwisho.
No comments:
Post a Comment