TUMSAIDIE MZEE MUHIDINI MAALIM GURUMO
Oktoba 2012.
Kuna wimbo ilioimbwa na bendi ya Mlimani Park ukiitwa ‘Nani
kaiona siku’ Wimbo huo mwimbaji Hassan Rehani Bichuka ameuimba kwa uchungu
akikemea baadhi ya watu ambao mtu akiwa anaumwa yu Hospitali au nyumbani, ndugu,
jamaa na marafiki hawajali kutoa msaada wowote kwa mgonjwa au familia.
Katika wimbo huo Bichuka anasema kwamba pindi mtu huyo
anapoaga dunia, siku ya msiba haohao hujitokeza vifua mbele kuchangia vifaa
mbalimbali ya vyakula vikiwemo mchele,unga,
maharage, mafuta, nyama hata maji ya kunywa huku wakitamba katika magari
yao ya kifahari, na Kamera za Video mazikoni.
Yawezekena baadhi yetu macho yalishindwa kusoma magazeti,
masikio yalishindwa kusikiliza redio na kuona Televisheni zetu zilizotujuza kwamba gwiji la muziki wa dansi hapa chini
Muhidini Maalimu Gurumo anateseka kwa maradhi
yanayomsibu muda mrefu sasa na hali yake si nzuri kiafya.
Mwaka huu wa 2012 tulishuhudia vifo vya aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
Haroun Mahundi, Msanii wa tasnia ya filamu Steven Charles Kanumba na
aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la wananchi Tanzania(CDF), Jenerali Ernest
Mwita Kyaro.Mungu aziweke pema roho zao pahala pema peponi, Amina.
Kifo cha ghafla cha msanii wa filamu Tanzania marehemu
Steven Charles Kanumba (28) ambaye hakuugua japo mafua bali yadaiwa kwamba aliuliwa na aliyekuwa ‘hawara’
yake ambaye ni msanii mwenzake maarufu
kwa jina la Elizabeth Michael ‘Lulu’
ambaye hivi sasa yupo kizuizini akisubiri kujibu mashitaka ya mauaji.
Kanumba alikuwa msanii maarufu katika tasnia ya filamu aliyejizolea
sifa lukuki alizostahili katika kutunga na kucheza filamu nyingi ndani na nje
ya nchi yetu.
Msiba huo ulichukua nafasi kubwa na kuleta taharuki kwa
waombolezaji wakati wa mizishi ya msanii huyo.
Kanumba akazikwa kwa heshima zote zilizoandaliwa. Wakati
wa maombolezo alisisika Kiongozi mmoja
wa dini akisema Kwa umati ule wa watu
ni mfano tosha kwa mazuri aliyoyafanya Kanumba hapa duniani! Tulitarajia
kusikia kauli toka kwa Kiongozi huyo japo ya kugusia au kukemea tabia ya
vijana kutofanya uzinzi hapa duniani.
Kama hiyo haitoshi baadhi ya watu waliulinganisha msiba wa
Kanumba kama ulivyokuwa wa rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ama wa aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Edward Moringe Sokoine!
Mmoja wa waombolezaji alifika mbali zaidi alisikika redioni akipendekeza kwamba eneo hilo la Sinza alipokuwa akiishi Kanumba mtaa
huo upewe jina la Kanumba The Great!
Ikumbukwe huko
nyuma Tanzania tumepoteza wasanii wengi wakubwa amabo hadi leo hawajakubukwa wala kupewa hadhi inayo
stahiki.Walikuwepo akina mzee Jongo, mzee Morris Nyunyusa, mzee Issa Matona,
Juma Mrisho, Ahmed Kipande, mzee Mayagilo, Salumu Abdallah, Mbaraka Mwinshehe
Mwaluka, Patrick Balisdya, Marijani Rajabu, mzee Kipara na wengine wengi. Je,
wote hao tutawaenzi kwa lipi?
Mzee Gurumo alizaliwa mwaka 1940, katika Kijiji cha Masaki Wilaya ya Kisarawe mkoa wa
Pwani ni mwanamuziki mkongwe mwenye historia ndefu katika tasnia ya muziki Afrika
Mashariki na hata nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara.
Hivi sasa ana umri wa zaidi ya miaka
70 ameshatoa mchango mkubwa katika
nchi hii kupitia tungo za nyimbo zake zilizojaa ujumbe mzito.
Amefikia hatua ya kuwatamani wanamuziki wa kizazi kipya na
taarabu kuwa wana mafanikio makubwa kimaisha kwa vile soko la sasa
limewapokea vyema na kujisikia wivu kuwaona vijana wakiendesha maisha mazuri
wakiwa na magari ya kifahari wakati yeye akitembea kwa miguu na hata kwenda
Hospitali kutibiwa hutumia usafiri wa daladala licha ya muda mrefu alioutumia
katika muziki.
Mke wa mzee Gurumo Pili Said Kitwana alitoa manung’uniko yake
kwa kusema kwamba yeye binafsi huwa anaumia roho wanapokuwa kwenye
daladala akimpeleka mumewe hospitali, abiria wengine huwashangaa. Lakini anasisitiza kwa
kusema wana haki ya kuwashangaa kufuatia jina kubwa la mume wake Gurumo ambaye
kwa hali ya kawaida hakustahili kutumia usafiri wa daladala.
Mama huyo ambaye aliolewa na mzee Gurumo mwaka 1967 na kupata
watoto wanne akina Mariamu, Mwalimu, Omar na Mwazani. Anamtaja Binti yao
wa kwanza Mariamu kwamba amefuata nyayo za Baba yake za usanii japo anaimba
nyimbo za kizazi kipya.
Mama Pili akasema laiti kama
angelikuwa na uwezo, angemtaka mumewe apumzike na masuala ya muziki baada ya
kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kupata mafanikio ya maana.
Kifo cha Kanumba tulishuhudia jinsi nguvu ya serikali
ikiongozwa na rais wetu Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, akifuatia na Waziri mkuu Mizengo Pinda jinsi walivyoshiriki ipasavyo katika msiba huo ambako
walitoa mkono wa pole kwa niaba ya serikari kwa kuubeba msiba huo hadi siku
ya mwisho wa mazishi. Mazishi hayo yakaongozwa na makamu wa rais Dkt. Mohammed
Ghalib Billar kwenye makaburi ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mzee Gurumo mwimbaji mwenye sauti isiyoigika anakiri fani
yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na watu wengi wakiwemo viongozi mbalimbali hapa nchini akiwemo rais Jakaya Kikwete anamuelezea kuwa
ni mmoja kati ya marafiki zake.
Mzee Gurumo alisema kitendo cha rais Kikwete kuacha kazi zake
akafuatana na mkewe mama Salma kuja kumjulia hali pia kumsaidia katika
matibabu wakati alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kulimfariji sana.
Anasema baada ya kutembelewa na rais Kikwete hapo
Muhimbili, huduma zilizofuatia toka kwa
madaktari na manesi zilikuwa ‘Baabu’ kubwa. Hivi sasa amepewa Daktari
maalumu wa kuiangalia Afya yake kila aendapo Hospitalini humo.
Mzee Gurumo mwenye uso wenye bashasha licha ya kudhoofu ki-
afya, hakukosa kutoa shukurani za dhati kwa mmiliki wa Kampuni ASET mama Asha
Baraka kwa kuandaa onyesho maalumu kwa
ajili ya kumchangia pesa.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’ ‘Sikinde’
na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park
na Orchestra Safari Sound (OSS). Mwenyewe anasema mitindo hiyo ilitokana na ngoma za asili ya kabila lake la Kizaramo
ambazo mama yake mzazi alikuwa gwiji
wa kuimba na kucheza enzi zake.
Gurumo alianza muziki akiwa na miaka 12 lakini muziki wa dansi alianza rasmi mwaka 1961 baada
ya kumaliza elimu ya Quraan katika
madrasa ambako alikuwa hodari wa kughani na kuimbaji kwa ustadi mkubwa Kaswida.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Kilimanjaro Chacha iliyokuwa ya ikiongozwa na Mkurugenzi wa bendi anamtaja kwa jina la Samwel Machango aidha anasema alipofika alipokelewa na Salumu Monde ambaye alikuwa mpigaji wa gita la rhythm. Anakiri kwamba wote wawili walimpa ujasiri wa jinsi ya kulitawala Jukwaa na vilevile kwa juhudi zake binafsi alijifunza kupiga Saxaphone. Bendi hiyo iliyokuwa na makao makuu katika ukumbi wa Amana jijini Dar-es-Salaam.
Mzee Gurumo anakumbuka anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba
katika bendi yake ya kwanza ukiwamo wa ‘Nilipoingia Bar watu walinionea
kijicho’ Anasema hawezi kuisahau siku ambayo
kwa mara ya kwanza alianza kupata pesa aliyoitolea jasho lake ilikuwa
ni shilingi Tano baada ya onyesho hilo.
Mwaka 1962 Kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz Ahmed Kipande alimrubuni kwa kumpa Shilingi mia mbili ili ajiunge na bendi yake. Anasema Shilingi mia mbili miaka hiyo ilikuwa na thamani kubwa sana naye alipokea na kukubali kujiunga na Kilwa Jazz. Mzee Gurumo anatabanaisha kwamba uongozi wa Ahmed Kipande, Duncan Njilima na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ hawakumtendea haki iliyostahili na baada ya mwaka kupita akaamua kutafuta bendi nyingine. Alifanikiwa kupata bendi ambayo ilikuwa ndogo kuliko Kilwa jazz ikiitwa Rufiji jazz mwaka 1963. Mawaka 1964 Gurumo aliitwa na uongozi wa NUTA Jazz ili akubali kuwa muanzilishi wa bendi hiyo na aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama , Mnenge Ramadhani na Wilfred Boniface.
Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa
Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine
zilikuwa Kilimo ni Kazi yetu na Mwenmgele.
Mzee Gurumo pamoja na uzee alionao bado kumbukumbu kichawani zijemjaa. Anakumbuka mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri John Simon alijiunga na bendi yao ya NUTA Jazz na anamtaja mpiga Solo Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa NUTA Jazz. NUTA jazz alikuwa ikimilikiwa Chama cha Wafanyakzi ambacho baadaye kikawa JUWATA, OTTU, TFTU hadi TUCTA.
Wakati wakiwa na TUCTA mishahara yao
ilikuwa duni kiasi cha kushindwa kijikimu kimaisha, hivyo kwa pamoja
wanamuziki hao wakajipanga kwa kununua vyombo vyao vya muziki kidogo kidogo
hadi wakatimiza adhma yao
ya kujitegemea. Ndipo bendi ya Msondo Ngoma Bendi ilopanzisha ikilibakiza jina la Msondo kwa kuienzi
staili iliyowapa umaarufu.
Mwaka 1978 Gurumo alihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra
‘Wana Sikinde ngoma ya Ukae’ na akawa Kiongozi wa bendi hiyo baada ya muda
mfupi alitunga nyimbo zikiwemo Baba na Mama na Weekend.
Akiwa na bendi hiyo maisha yake yalianza kubadilika na
kuwa mazuri kufuatia malipo na maslahi ya kuridhisha aliyokuwa akilipwa na
uongozi wa Mlimani
Park.
Anajigamba kwamba maslahi hayo ndiyo uliofikisha kujenga
nyumba yake na kunua eneo la shamba maeneo ya Masaki Wilayani Kisarawe mkoa
wa Pwani na kuwapeleka watoto wake
katika Shule nzuri.
Anasisitiza kwa kusema kwamba hatoweza kuwasahau wanamuziki alioshirikiana nao kwa karibu akiwemo aliyekuwa Kiongozi msaidizi Comas Tobias Chidumule ambaye hivi sasa ameokoka na anaimba nyimbo za Injiri, Joseph Bartholomew Mlenga ‘King Spoiler’ na Abdallah Gama
Pamoja na kipato alichokuwa akikipata Mlimani Park
Orchestra, ,mwaka 1985 mfanyabiashara maaraufu jijini Dar- es -Salaam Bwana Hugo Kisima akamshawishi kujiunga
katika bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) ambayo ilikuwa ikiongozwa
na Supreme Ndala Kasheba aliyekuwa akipiga
katika staili ya ‘Dukuduku’ Gurumo aliingia na staili ya Ndekule.
Alijiunga na OSS akifuatana na wanamuziki wawili toka Mlimani Park akina Abel Bartazar na Kassim Rashid ‘Kizunga’wakatoka na nyimbo za ‘Chatu mkali’ na ‘Bwana Kinyogoli’
Bendi ya OTTU ilikuwa bado inamuhitaji kurudi ndipo mwaka
1990 uongozi ulifaulu kumrudisha katika bendi hiyo ambayo tayari ilikuwa ilikuwa imebadili jina kuwa JUWATA.
Enzi za ujana wake ‘Bitozi’ wakati huo, Gurumo alipitia mambo mengi ya ujana ya kuvuta sigara na alikuwa mywaji wa pombe kupindukia ‘Cha Pombe’ Tabia hiyo ilikifikia kukorofishana na mama yake mzazi aliyetishia hata kumutolea ‘Radhi’ kama angeendekeza ulevi.
Mkewe Pili Siad Kitwana naye alikwaruzana kila mara juu ya
hiyo ya ulevi uliokithiri na aliwahi
kutishia kuomba talaka. Hatimaye mwaka 1982 akaamua kumshinda ‘Shetani’ akaachana
na ulevi kwa shinikizo la mama yake na mkewe.
Mzee huyu mwenye historia ndefu ya muziki na maisha yake
kwa ujumla, amekuwa kiongozi katika bendi hiyo akisaidiana na Said Mabela, anasema
furaha aliyonayo ni kuona pale pamoja na umri wake kuwa mkubwa akiwa na msondo
ngoma amekwisha tunga na kuimba nyimbo
nyingi na kuzirekodi katika Studio zikiwemo za ‘Mama nipeleke kwa Baba’ Mwanangu
acha Wizi, Wosi wa Baba na nyingine nyingi.
Muhidini Maalimu Gurumo amesema kwamba hana muda mrefu
kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya na
umri wake kutupa mkono.
Anasema atakapostaafu atajikita katika kuwasaidia vijanaili
atimize ndoto zake ni kujenga Chuo cha muziki katika shamba lake lililopo Masaki wilayani Kisarawe
iwapo atapata wafadhili wa kumsapoti adhma yake.
Kama walivyowahi kutamka wanamuziki wengine wa zamani,
mzee Gurumo naye amewasisitiza Vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza
kutumia Ala
za muziki ili kuweka kumbukumbu ya kazi zao ziwe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Mzee huyo anasema mazoezi ni muhimu kwa kila binadamu.
Yeye hulazimika kujikongoja kwenda kuimba katika bendi yake ya Msondo Ngoma
ambapo anasema kuna muda huimba akiwa amekaa kwenye Kiti. Mzee huyu ni muwazi
kwa kusema anapo imba na bendi yake pamoja na mazoezi pia huambulia posho
inayomuwezesha kujikimu kimaisha.
Gwiji huyu ametunga nyimbo zaidi ya 54 ambazo anasema
zinapendwa na watu japo yeye anasema kwamba hazina faida yeyote kwa kuwa
hapati hata senti tano ya nyimbo zake hizo. Hivyo anawaomba wadau na wasamaria wema kumsaidia ili aweze
kuzirekodi upya nyimbo hizo ili ziuzwe na yeye aweze kunufaika.
Mzee Gurumo anamalizia kwa kusema kama
tuliweza kujitoa katika msiba wa Kanumba na wengineo hivyo anaomba serikali, mawaziri,
wabunge na wadau wote wamuangalie kwa jicho la huruma, wamsaidie kufuatia hali yake kudhoofu na hana msaada mwingine.
|
Wednesday, October 31, 2012
TUMSAIDIE MZEE MUHIDINI MAALIM GURUMO Oktoba 2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment