Mwimbaji mashuhuri Thsimanga Kalala Assosa akiimba katika moja ya maonyesho alipokuwa Maquidu Zaire.
Novemba 05,2012.
Tshimanga Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu
aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo za Negro Success, Les Kamalee,
Lipua Lipua na Fuka Fuka.
Assosa ni mwenye kipaji cha kutunga na kuimba nyimbo za muziki dansi pia ni kiongozi wa Bendi ya Bana Maquis iliyopo
jijini Dar es Salaam.
Kwa hali isiyokuwa ya
kawaida, Tshimanga Assosa amekuwa akikataa Ofa lukuki za kwenda ‘kula maisha’ Ulaya
na Marekani na kuamua kuishi katika Jijini la Dar es Salaam
hapa Tanzania.
Akiwa katika bendi hizo alishirikiana
wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na Kiamuangana Mateta Wazola Mbongo ‘ Verckies’
Historia ya maisha yake
inaanzia siku aliyoiona dunia baada ya kuzaliwa katika mji wa Kamina uliopo
Jimbo la Shaba
huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Aprili 04, 1949.
Alipata elimu ya Sekondari
katika Shule iliyojulikana kama Charles
Ruangwa hapo Kamina.
Akielezea
historia hiyo Tshimanga Assosa anasema alianza kuimba akiwa bado mdogo na
kwamba aliyejipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina
ambako maPadri walimsaidia kumfundisha muziki.
Pamoja na juhudi zake hizo, Baba
yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye
ajitumbukize katika muziki na kumtaka afuate masomo yake shuleni.
Baada kumaliza kidato cha nne,
Baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Assosa Muziki ulikuwa ndani ya
damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo
hapo Kamina ya Super Gabby.
Anasema mazoezi ya hiyo yalimtia
hamasa kubwa ya kupenda muziki. Anaeleza kwamba siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa
kuimba katika bendi hiyo. Assosa
alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla Baba
yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko.
Waswahili wanasema ‘Sikio la kufa halisikii dawa’ Baba yake mwisho wake alikubali
ombi la mwanaye baada ya kubaini kuwa hashikiki
wala habadiliki kitabia, akamruhusu afanye muziki aupendao.
Mwaka 1969 Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana
na mwanamuziki Bavon Marie Marie na akampeleka
kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo
aliyejulikana kama Didi Kalombo.
Assosa aliitumia vyema nafasi
hiyo ya kujaribiwa sauti. Mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza
kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika bendi hiyo.
Assosa anazikumbuka changamoto
alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko
yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti na
wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo)
Anasema sauti yake ndiyo
iliyomuokoa na kupewa heshima kama wanamuziki wengine.
Tshimanga Kalala Assosa anafafanua
kwamba kufa kwa Kiongozi ‘Star’ yeyote katika bendi, mara nyingi husababisha
bendi aliyoiacha kuteteleka hatimaye kufa. Akitolea mifano ya Bendi za T.P.OK. Jazz na Empire Bakuba
ziliondoka katika sura muziki baada ya vifo vya Franco Lwambo Lwanzo
Makiadi na Pepe Kalle Yampanya.
Anasema ndivyo ilivyoitokea kwa
Negro Success baada ya kufariki kiongozi
wao Bavon Marie Marie kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye
ikafa.
Mwaka 1974 Assosa alikutana
na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa Bendi ya Lipua
Lipua, aliyejulikana kwa jina Kiamuangana Mateta Wazo la Mbongo‘Verckies’
Alipofika huko alitakiwa
kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka.
Anasema hajui ujasiri uliupata
wapi siku hiyo pale alipomtamkia mmiliki
huyo kwamba hayuko tayari kuimba sauti
ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.
Aliungana na wanamuziki wengine
wakali akina Chizunga Ricks (Solo), Mutembu
Chibau, Basikita na Kayembe waliokuwa wamemtangulia katika bendi hiyo.
Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka
na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya
Mombasa,
Nikibwe na Amba.
Mwaka 1975
bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na
wanamuziki. Aliamua kuondoka na kwenda
kujiunga na Bendi ya Les Kamalee.
Akiwa na Les Kamalee walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa
bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na zingine
nyingi.
Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa
sifa na kujiamini kupita kiasi. Walilipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao
vya muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo.
Mbwembwe zikazidi na kusababisha
kusahau wajibu wao katika kazi. Bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975.
Mwenye bahati habahatishi, Assosa
alikaribishwa katika Bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma.
Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tannzania.
Fuka Fuka ilipoingia Dar es
Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga
Funga ambazo anazielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa jiji la Dar es Salaam wakati huo.
Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga
muziki kwa miezi sita na Chama cha mateksi
Dereva cha Tanzania Transport, Tax and
Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park.
Baada ya kumaliza mkataba
Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi
nchi Kenya na Kampala huko Uganda.
Wakiwa Kampala kwa bahati
mbaya nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani,
ikipigana na Tanzania
mwaka 1979.
Vita hivyo viliiwaathiri kwa
kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia,
wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ili hali kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha
yake.
Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa
alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania
aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi
ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita.
Akiwa Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa
muziki wa Tanzania,
akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew
Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule.
‘Mungu hamtupi mja wake’ Baada
ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Assosa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy
katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986. Akiwa hapo
alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani.
Mwaka huo huo aliamua kuanzisha
bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga
kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na
maadili mema.Bendi hiyo ilijengewa mizengwe
na kusababisha kasambaratika baada ya
muda mfupi.
Assosa alichukuliwa na bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa
na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987.
Alipigia bendi ya Maquis hadi
ilipo sambaratika ikipiga kayika ukumbu wa Lang’ata, Kinondoni miaka ya 1990.
Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia
utanashati wake.
‘Chema chajiuza kibaya
chajitembeza’ Mwanamuziki huyu alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala
kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya
Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi.
Baada ya kumaliza mkataba aliungana
na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya
Bana Maquis.
Anawataja akina Kasongo
Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza
‘Banza Mchafu’. Hadi sasa bado yuko na bendi hiyo ya Bana Maquis.
Mwanamuziki Tshimanga anasema
amekuwa alikataa mialiko lukuki ya kwenda kuishi na kufanya kazi ya muziki
Ulaya na Marekani. Anakiri kuipenda Tanzania kwa vile anaona maisha
yake yanamyookea vyema.
Anasema uhakika anao kwamba yeye
yuko vizuri kimaisha kuliko ya hao waliopo huko Ulaya na kwengineko. Anabeza
kwa kusema kwamba baadhi yao
tayari wameanza kurejea Kongo baada ya kushindwa kumudu maisha.
‘Mtoto mzuri’ Assosa ni Baba
wa familia ya mke na watoto kadhaa. Hakukosa kusifia muziki wa kizazi kipya kwa
kusema kwamba wanafanya vizuri.
Lakini akatoa angalizo kwamba
muziki wao wa kutumia CD ni wa muda mfupi
hauwezi kudumu kwa kipindi kirefu,vilevile makosa kubwa kwa vijana hao kutojifunza
kupiga Ala za
muziki.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment