Tuesday, January 1, 2013

MJUE MKONGWE ABUBAKAR KASONGO MPINDA 'CLAYTON'

Abubakar Kasongo Mpinda akiimba kwenye moja ya
maonyesho na bendi ya  Maquis du Zaire enzi hizo
ABOUBAKAR KASONGO MPINDA ‘Clayton’ ni mwanamuziki mkongwe katika tasnia ya muziki aliyezaliwa wakati vita kuu vya pili vya dunia vikikaribia kumalizika.

Kasongo Mpinda ‘Clayton’anatoka katika ukoo wa ki Chifu. Baba wa Babu yake alikuwa Chifu akiitwa Chifu Kasongo huko Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kasongo ni mtoto wa kwanza kati ya wanane aliyezaliwa Februari 02, 1945, katika  mji wa Lubumbashi jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baba yake mzazi mzee Boniface Mpinda Kasongo, alikuwa mfanyabiashara maarufu katika mji wa Lubumbashi, wakati mama yake Kanku wa Mokendi alikuwa muumuni na  mwimbaji mashuhuri katika  Kanisa la kikatoliki mjini humo.

Mpinda anamuelezea mama yake kwamba ndiye chanzo cha yeye kupenda kuimba kwa kuwa kila mara alikuwa akifuatana na mama yake kwenda Kanisani  kuimba.

Kasongo Mpinda ‘Clayton’ hakuweza kuendelea na masomo ya  Sekondari baada ya wazazi wake wote  kufariki dunia akiwa kidato cha kwanza.

‘Clayton’ ni mtunzi na mwimbaji mwenye sauti nyororo isiyochusha masikioni, anaeleza kwamba kamwe hawezi kuisahau siku aliyoshikana mikono na rais Alli Hassan Mwinyi.

Anasema hakuwa na ndoto hata siku moja ya kuja kushikana mikono na rais katika maisha yake yote, lakini siku hiyo ikatokea.

 Bendi ya M.K.Group ilishinda kupitia wimbo wake wa ‘Uwajibikaji’ katika shindano la Top Ten Show mwaka 1988.

Uwajibikaji ilikuwa ni kauri mbiu ya rais wa awamu ya pili, Alhaj Alli Hassan Mwinyi kwa wantanzania akiwataka kuwajibika katika kazi ipasavyo.

Kasongo alianza safari yake katika muziki kwa  kujiendeleza kidogo kidogo katika bendi mbalimbali zikiwemo za Ode Jazz na Lupe Jazz mjini Lubumbashi.

Mwaka 1965 alikwenda Kinshasa na akajiunga na mkongwe wa muziki wakati huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Dokta Nico Kasanda wa Mikalaia aliyekuwa akimiliki bendi ya L'Africa Fiesta Sukisa.

Mwaka 1968 aliachana na Dokta Nico akaamua kuvuka mpaka akaingia mji wa Lusaka nchini Zambia. Mwaka uliofuatia wa 1969 na kuanzisha bendi yake ya The Wings Brother’s.

The Wings Brother’s ilijumuisha vijana toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokuwa wamechipukia katika  muziki wakati huo.
Anawataja kuwa ni akina Kibambe Ramadhani, Lomani, Jozee, Lushiku wa Lushiku na Kayembe Trumbloo.

Chini ya uongozi  wake bendi, hiyo ilisafiri kwenda kupiga muziki katika nchi za Botswana, Zambia hatimaye wakatua hapa nchini Tanzania mwaka 1979.

Walipofika hapa nchini wanamuziki wa bendi hiyo  waligawanyika. Wengine wakajiunga na Orchestra Safari Soud (OSS) na baadhi wakajiunga na Maquis du Ziare akiwemo yeye.

Baada ya ujio wa vijana hao kukawa na ushidani mkali kati ya bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa ikipiga muziki wake kwenye ukumbi wa Kimara resort na Maquis du Zaire iliyokuwa imejikita ukumbi wa White House Ubungo.

Pamoja na umri wake kuwa mkubwa, Kasongo bado ana kumbukumbu akizitaja nyimbo alizotunga na kuimba akiwa Maquis du Zaire za Angelo, Mwana Malole, Nasononeka, Baharia, Siri ya Mkoko na zingine kibao.

Kasongo alifunga ndoa ya kiisilamu na Bi. Habiba….. mwaka 1984, jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kupata watoto kadhaa kati yao wawili ndiyo waliofuata nyao za Baba yao. Kabla ya kufunga ndoa alilazimika kuingia dini ya kiislamu,  hivyo alisilimishwa na kupewa jina la Abubakar Kasongo Mpinda.

Anawataja wanaye hao kuwa ni Idd Kasongo ‘Clayton’ na Kiloman Kasongo. Idd ‘Clayton’ yupo katika kikosi cha Twanga Pepeta Academy akifanya vizuri katika muziki wa dansi wakati Kiloman anapiga muziki wa kizazi kipya.

Abubakar Kasongo ‘Clayton’ akisaidiana na Mbombo wa Mbomboka walikuwa waanzilishi wa bendi ya M.K. Group iliyokuwa ikiporomosha muziki wake katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ya M.K.Group ndiyo iliyozaa bendi za M.K. Beat na M.K .Sound zikimilikiwa kwa pamoja wafanayabiashara wawili  Mayalu na Kilomoni.

Abubakar   Kasongo Mpinda aliwakusanya wanamuziki mahiri ili kuunda kikosi cha mashambulizi dhidi ya bendi zingine hapa nchini.

Safu hiyo ilikuwa ni ya waimbaji mahiri akiwemo Kalala Mbwembwe, Paul Vitangi, Issa Nundu, Green Simutowe (nyimbo za kizungu), Rahma Shaari  na yeye Kasongo Mpinda. Upande wa gita alikuwepo Monga Stanie na Kasongo Ilunga (solo), Omari Makuka (rhythm) na Andy Swebe (besi). Saxophone ilikuwepo Mafumu Billari ‘Bombenga’ na trumpet zilipulizwa na Abdallah Tuba na Kayembe Ndalabuu.

Kinanda kilikuwa kikipapaswa na Asia Darwesh ‘Mama lao’ na upande wa tumba alikuwepo Sidy Morris ‘Super Konga’

Wakiwa na M.K. Group walitoka na nyimbo za Kibera, Nishike mkono, Kitendawili,  Nipe ukweli, Habiba, Waniumbua, Mwintunpe na nyingine nyingi zilizokuwa zikikonga nyoyo za wapenzi wa ‘ngoma za maghorofani’

Ili kuongeza nguvu katika bendi hiyo,  waliamua kuwachukuwa wapiga magita wengine wakali Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’, Kawelee Mutimwana na baadaye Miraji Shakashi ambaye wakati huo alikuwa bado akijifunza ‘Lena’.

Bendi hiyo ilijizolea sifa kubwa ambapo kila mwisho wa wiki wapenzi na washabiki wa bendi hiyo walisikika wakihimizana kwamba  leo twende ‘ngoma za maghorofani’ Ndiyo sababu ya bendi hiyo kupachikwa jina la ‘Ngoma za maghorofani’

Kasongo anaeleza jinsi alivyo ibua kipaji cha mpiga solo Miraji Shakashia ‘Shakazulu’ambaye kwa sasa anatamba katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’

Ansema kuna kipindi mpiga gita Joseph Mulenga alikuwa akiumwa kila mara na Kawelee Mutimwana alikuwa katimkia Ulaya wakiiacha M.K. Group bila ya  mpiga wa gita la Solo.

Bahati nzuri mkataba wao na Hoteli ya New Afrika ukamalizika na kupata mkataba mwingine mjini Morogoro wa kupiga muziki katika Hoteli za Morogoro na Luna.

Msemo wa ‘ukishikwapo shikamana’ ulijidhihirisha baada ya kufika Morogoro ambapo Kasongo alimlazimisha Miraji  Shakashia kupiga gita la solo nyimbo zote.

Abubakar Kasongo anamsifia Shakashia kwa kipaji alichojaaliwa na mwenyezi mungu, kwa kuweza kuokoa jahazi lililokuwa likienda mrama. Alizipiga nyimbo zote pasipo kugundua dosari yeyote.

‘Clayton’ alidumu na M.K. Group kwa takribani miaka minane na baadaye akajiunga na bendi ya Zaita Muzika ya Ndala Kasheba ambapo walisafiri na bendi hiyo kwenda London nchini Uingereza kwa mwaliko wa watanzania waishio nchini humo.

Kasongo ansema yeye ni mithiri ya ‘Panga kukuu lenye, makali yaleyale’  pale anapotababaisha kwamba baadaye alikuwa akisaidia kupiga muziki katika bendi ya Bakulutu kabla ya kujiunga katika bendi ya Bana Maquis  ambayo inayoongozwa na Tshimanga Kalala Asssosa hadi sasa.

Abubakar  Kasongo hivi sasa afya yake si njema sana anasumbuliwa na maradhi ya kisukari na  gazi iliyotanda maungoni mwake, kiasi kwamba humfanya wakati mwingine asifike kupiga muziki pindi  anapozidiwa.

Mkewe Bi. Habiba Kasongo anasema mumewe  siku zingine hataka kujilazimisha kwenda kupiga muziki hata kama hali yake si nzuri. Lakini kama mke anayejua majukumu yake, humkataza akihofia kuzidiwa akiwa mbali naye.  

Kasongo Mpinda ‘Clyaton’ ameusifia muziki wa kizazi kipya kwa kusema kwamba ‘Hakuna muziki mbaya ili mradi  unapendwa na jamii’ Akawasisitiza wakaze Buti.
 Abubakar Kaosngo Mpinada akiimba. Kushoto ni Abdalah Tuba na Kayembe Ndalabuu (Trumapet)
 Kaongo Mpinda (katikati), akiwa na mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa
 Mpina akiimba Nyuma Ilunga Kalinji ' Vata'


  

No comments: