TABORA JAZZ ‘Wana
Segere Matata’ ni bendi pekee ya muziki wa dansi inayojulikana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo.
Kauli
hiyo nzito ilitolewa na mkongwe wa muziki wa dansi toka Jamhuri na Kidemokrasia ya Congo, Tabu Ley Rochereau.
Akiwa ziarani hapa Tanzania,
Tabu Ley aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa
habari katika hoteli Kilimanjaro. Moja kati ya
maswali aliyoulizwa ni kutaka kufahamu ni bendi gani hapa Tanzania
wanayoijua huko kwao DRC. Tabu Ley pasipo kupepesa macho, alikiri kwa kujibu
kwamba ni Tabora Jazz pekee ndiyo
inayojulikana huko.
Tabora Jazz
ni bendi kongwe iliyoanzishwa mwaka 1954, ambao katika historia ya Tanzania
ndiyo mwaka ambao chama cha TANU kilianzishwa.
Bendi
hiyo ilikuwa ikiongozwa na waanzilishi
akina Hamis Ali Songo na Mlekwa
Selemani, ikiwa na makazi yake mjini Tabora ikipiga na kutoa burudani murua za muziki
wa dansi katika kumbi za Lumumba kwenye
kona ya mitaa ya Usagara na Rufita ambako ndiko yalikuwa makao makuu yake. Pia
walikuwa wakipiga katika Baa za Bizeta, Maua
na nje ya mji wakialikwa.
Miaka ya nyuma Tabora Jazz ilikuwa na upinzani mkubwa na
bendi ya Western Jazz ya jijini Dar es
Salaam. Upinzani huo ulijiri baada ya Bendi ya Western
Jazz kukwapua kwa nyakati tofauti nguli wawili toka Tabora Jazz., kwa ambao
walihamisha ‘melody’ yao
kuipeleka huko.
Wanamuziki hao walikuwa
akina Wema Abdallah na Rashidi Hanzuruni ambao walikuwa mahiri kwa
kulicharaza gitaa la solo,ambao walihamisha ‘melody’ kuzipeleka Western Jazz.
Nyimbo nyingi
za bendi hiyo zilipigwa mno katika kituo
cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kusikika sehemu kubwa Afrika ya Mashariki na Kati.
Huko nchini
Rwanda kulikuwepo redio Rwanda
iliyokuwa na kipindi cha muziki nyakati za jioni kikiendeshwa na mtangazaji
Kabendera Shinani, ambaye alikuwa akizipiga nyimbo za Tabora Jazz kila mara.
Redio hiyo ilikuwa ikisikika hapa nchini maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kigoma,
Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera (Ziwa Magharibi) wakati huo.
‘Wana
Segere matata’ waliwika sana miongoni mwa bendi kubwa hapa nchini zikiwemo Morogoro
Jazz, Cuban Marimba, Western Jazz, NUTA Jazz, Dar. Jazz, Kilwa Jazz, Urafiki
Jazz, Jamhuri Jazz na nyingine nyingi.
Mji wa
Tabora wakati huo ulikuwa na ushindani mkubwa katika muziki kati ya Tabora Jazz
na bendi zingine zilizokuwepo wakati huo za Kiko Kids iliyokuwa ikiongozwa na
Salimu Zahoro na Nyanyembe Jazz iliyoibuka na kibao chake cha ‘Rangi ya Chungwa’
wimbo ambao hadi sasa bado unarindima kwenye vituo vingi vya redio na kumbi
nyingi za burudani hapa nchini.
Pia mji
wa Tabora enzi hizo kulikuwa na umkumbi mkubwa wa Disco uliokuwa ukijulikana
kwa jina la ‘Mwana Isungu’ uliokuwa ikiteka kundi kubwa la vijana wa mji huo kwa kuporomosha muziki
maridhawa, zikiwemo nyimbo za Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz.
Kama
nilivyokudokeza hapo awali kwamba bendi hiyo ilianzaishwa kabla ya Tanganyika kupata Uhuru, hivyo
iliendeleza mfumo wa kikoloni. Mfano mmoja ni kwamba katika miaka ya 1960
ilikuwa ni marufuku kwa mpenzi au shabiki kuingia ukumbini kucheza muziki
pasipo ‘kunyonga’ Tai shingoni, licha ya pesa zake. Hii ilikuwa ni moja ya njia
ya kuzingatia utanashati na nidhamu kwa
ujumla.
Bendi
hiyo ilipiga katika mitindo ya Segere matata, Segua Segua, na Mambo
Milekana, ikiwazingua wapenzi wa muziki mjini humo.
Miaka hiyo Tabora Jazz alitoka na nyimbo
zao ngingi zikiwemo za Usijifanye mwewe, Mariam mpenzi, Zabibu No.2, Anna, Regina, Mambo
Mileka, Tucheza Segere, Dada Mwantumu, Serafina,Tamaa yako, Alhamdulilah,
Nashukuru sana, na Dada Asha.
Zingine
ni pamoja na Zabibu, Halima, Dada Helena, Lucie, Farida na Dada Mwantumu.
Kufuatia
ushindani mkubwa uliokuwepo mjini humo
kati yake na Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, Tabora Jazz ilifumua vibao ingine
vikali vya Chakula kwa Jirani, Mapenzi
hayana mganga, Mambo Mileka, Ujana una mwisho. Salima, Dada Remmy, Tucheze
Segere na Rukia wajidanganya.
‘Segere
matata’ wakati huo ilikuwa na mashabiki waliokubuhu. Kwa wakazi wa Tabora mjini
hawawezi kumsahau shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mzee Segua’ ambaye
alikuwa hakosi onyesho lolote la bendi hiyo akicheza ‘Segua Segua, mtindo
aliokuwa aikiumudu hadi kufikia kupachikwa jina la ‘Mzee Segua’
Alikuwa
ni Mzee mwenye vituko ukumbini, akiwa na mfanyakazi katika Ofisi moja ya serikali
mjini humo kama
dereva. ‘Mzee Segua kwa mapenzi yaliyopitiliza mbele ya tabora Jazz, alidiriki
kukakataa uhamisho kwenda Wilaya ya Urambo, akitoa sharti ili aende huko basi Bendi
hiyo nayo ihamishiwe Urambo. Yaelezwa kwamba baadaye alifukuzwa kazi.
Kikosi kamili cha wanamuziki waliokuwa wakiunda kikosi
kamili cha bendi hiyo kilikuwa cha akina Athumani Tembo kwa upande wa gitaa la
Soloakisaidiana na Shem Ibrahim Karenga
aliyekuwa akipiga gitaa la solo, akitunga na kuimba. Salumu Luzira alikuwa akiliungurumisha gitaa zito besi na ugeweza kulilingalinisha na alivyokuwa akipiga
Suleiman Mwanyiro ama Lofombo wa Empire
Bakuba.
Wengine katika safu hiyo walikuwa Kassim Kaluwona, aliyekuwa akilicharaza gitaa
la rhythm akisaidiana na Issa Ramadhani
‘Baba Isaya’ Waimbaji walikuwa ni akina Ramadhani
Hamis Nguligwa, Ismail Mwangoko, na Msafiri Haruob, ambaye baadaye alijiunga na Mwenge
Jazz ya Jijini Dar es Salaam.
Kuna
msemo wa waswahili usemao kwamba ‘ Vizuri huigwa na Vitamu huonjwa’ Msemo huo ulijidhihirisha wazi kwa Bendi
kubwa toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Soukos Stars, ambayo iliiba
nyimbo za Dada Asha wa Tabora Jazz na Vigeregere wa Western Jazz.
Kwa
umahiri mkubwa wa bendi hiyo ya Soukous
Stars ilitoka na mseto wa nyimbo nyingi zikiwemo za Dada Asha na
Vigeregere katika album moja ya ‘ Nairobi by Night’
Shem Karenga
alijaribu kufuatilia haki miliki yake
pasipo mafanikio kwa kuwa nchi yetu ilikuwa bado haijatunga sheria ya haki
miliki.
Tabora
Jazz iliposambaratika mwaka 1980, sanjari na Bendi za Nyanyembe Jazz na Kiko
Kids, nazo zilienda mrama na baadaye kuondoka katika taswira ya muziki hapa
nchini.
Kutoweka
kwa Bendi hizo kuliwaacha wapenzi wa muziki wa dansi wa mji huo ambao
waliupachika jina la ‘Mboka’ wakijawa na simanzi tele, licha ya kuanzishwa kwa
bendi nyingine ya Tabora Jazz ‘Sensema Malunde’ ambayo imeibuka miaka ya
karibuni ikiwapa burudani.
No comments:
Post a Comment