MWEZI HUU FRANCO LUAMBO LUANZO MAKIADI anatimiza
miaka takriban miaka 23 toka kifo chake kilichotokeea tarehe 12, Oktoba1989.
Franco ambaye alizaliwa Tarehe 6 Julai,
1938, katika Kijiji cha Sona Bata Magharibi ya Kongo, atakumbukwa na watanzania
wakati alipofanya onyesho kweye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwaka 1973.
Baba yake Joseph Emogo alikuwa
mfanyakazi wa Shirika la reli wakati mama yake alikuwa mama wa nyumbani akioka
mikate na kuuza Sokoni wakati akiwa bado mdogo wazazi wake walihamia katika
Jiji la Kinshasa.
.
Franco alipofikisha umri wa miaka Saba alitengeneza gitaa la kienyeji ambalo alilitumia
kupiga na akiwavutia wateja pembeni mwa
mama yake wakati akiuza mikate.
Kipaji chake kiligunduliwa na mpiga gita
Paul Ebengo Dewayon ambaye alijitolea kumfunza Franco jinsi ya kupiga vyema Ala hiyo.
Mwaka 1950, wakati huo akiwa na umri wa
miaka 12, alitengeneza jina akiwa katika bendi ya Watam ya Ebengo Dewayon ambaye
alikuwa kiongozi wa bendi hiyo.
Alizikonga nyoyo za wapenzi kwa uwezo wakemkubwa wa kupiga gita ambalo
lilikuwa kubwa kuliko yeye.Miaka mitatu baadaye Franco alirekodi wimbo wake wa kwanza uliokuwa na jina la
Bolingo na Ngai na Beatrice.(mpenzi wangu Beatrice) baada ya kukubalika kuwa mmoja
wa wana bendi ya Loningisa Studio, kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane alitoa
nadhiri kwamba ataishi na Franco katika maisha yake yote yaliyosalia.
Chini ya Henri Bowane Franco akawa mpiga
gita la solo ambapo alikuwa kipiga staili ya Sebene na akaanza kutunga na kuimba yeye mwenyewe
kwa staili za rumba na za kiafrika na hata za kilatini.
Mwaka 1955 pamoja na kwamba alikuwa
akipewa kazi nyingi katika Studio hapo Franco aliunda bendi akiwa na Jean Serge
Essous iliyokuwa ikipigia katika Baa ya Ok.
Huko Kinshasa.
Mwaka uliofuatia bendi hiyo
ilibadilishwa jina na kuwa Ok Jazz na baadaye ikaitwa T.P.Ok. Jazz kuenzi
sehemu ilipoanzia bendi hiyo yaani katika Bar yenye jila la OK (OK. Bar)
Katika kipindi cha mwaka mmoja bendi
yake ya T.P.Ok Jazz ikagundulika kwamba inataka kumpiku Vicky Longomba ambaye
alikuwa katika bendi ya Grand Kale ya African Jazz ambayo ndiyo ilikuwa bendi
kubwa nchini Kongo.
Franco alishadai kwamba bendi yake ya Ok.Jazz
ilitoa zaidi ya album 150 katika kipindi cha miaka 30.
Mwaka 1958 Franco alifungwa kwa kosa la ajali ya barabarani.
Purukushani za kisiasa katika nchi yake
ya Kongo Franco alilazimika kuhamia Ubelgiji kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake.
Baada ya nchi kutulia ikiwa chini ya
uongozi wa rais Mobutu Seseseko Kuku Ng’endu Wazabanga ambaye alibadilisha jina
la Kongo kuwa Zaire, Franco alirudi nchini mwake na kafanya tamasha kambambe la
Festival Ok. Jazz f African Arts lililofanyika Kinshasa mwaka 1966.
Ok Jazz iliisaidia sana Serikali ya Mobutu katika mambo ya
kisiasa kupitia nyimbo zake zilizokuwa na mafunzo mengi.Franco hakuona soni
katika kusifia mazuri wala kuonya mabaya pamoja na kwamba aliwekwa lupango mara
nyingi alipokiuka taratibu za nchi.
Mwaka
1970 Franco alipata pigo kubwa kwa kufiwa na mdogo wake Bavon Marie Marie amabaye kifo chake
kilitokana na ajali ya gari alipokuwa akiendesha kwa hasira baada ya
kukorofishana na kaka yake Franco juu ya mwanamke ambaye pia alikufa katika
ajali hiyo.
Mwaka
1980 Serikali ya Kongo (Zaire)
ilimtunuka hadhi ya kuwa Babu wa muziki wa Kongo kama
heshima kwa juhudi zake za kufufua uchumi amabo ulikuwa ukiyumba nchini humo.
Wakati wa maisha yake aliwahi kuongeza
uzito ghafla na kufikia paundi 300 ambazo ni sawa na kilo 136.
Franco alifyatua wimbo mkali mwaka 1985,
uliotikisa nchi wa Mario. Lakini mwaka 1987 fununu zikaanza kuzagaa kwamba Franco
yu mgonjwa.
Wimbo aliotengeneza mwaka huo kabla ya
kifo chake ulikuwa wa ‘Attention na SIDA’(Jihadhari kwa Ukimwi / AIDS)
Franco alifariki tarehe 12, Oktoba 1989
akiwa katika hospitali mojawapo huko Ubelgiji na mwili wake ulisafirishwa
kupelekwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire zamani) ambako jeneza lake
lilipitishwa mitaani kuagwa na wananchi likisindikizwa na ulinzi mkali wa
Polisi na baadaye serikali ikatangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa.
Wakati wa siku hizo za maombolezo radio
ya taifa hilo ilikuwa ikipiga nyimbo za Franco hadi tarehe 17, Oktoba 1989 alipozikwa kwa heshima zote za kitaifa.
Mungu aiweke pahala pema peponi Amen.
Imeandaliwa na Mr. Kaiyungi
No comments:
Post a Comment