DK. REMMY ONGALA
Na: Kiyungi Moshy:
Desemba 15, 2012
Jumatano iliyopita ya Desemba
13, 2012 ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa Tanzania,
Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla. Siku hiyo ilikuwa ni miaka
miwili kamili toka kifo cha mwanamuziki nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’
aliyefariki usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza,
jijini Dar es Salaam.
Alikuwa kipenzi cha watu
aliyewaacha wapenzi wake na wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi
yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake zenye maudhui maridhawa, ambazo
hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya
mipaka yetu.
Dk. Remmy alikuwa wa kwanza
kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini
jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa serikali,vyama na dini na wengine
kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy, wakaanza kuhubiri
majukwaani tahadhari hiyo.
Alizaliwa akiwa na meno
mawili ya mbele kinywani mwake na
akaonekana kana kwamba ni mtoto wa
ajabu. Aidha hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja
kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.
Dk. Remmy alijipatia umaarufu
katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari yake
ndogo ‘soloon’ lililokuwa la aina yake popote lipitapo watu walilishangaa.
Lilikiwa na maandishi nyuma ya gari hilo
yakisema ‘ Baba yako analo’?
Historia ya maisha ya
Dk.Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala.
Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Baba yake alikuwa ni
mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira.
Baada ya kuzaliwa kwake haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji
wa Kisangani
huko DRC.
Ipo habari kwamba kabla ya
kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya
kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda
kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa
asiiage dunia pia.
Bila kusita mganga wa kienyeji
akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia
hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto
akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha
Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyompelekea
kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.
Mwenyewe aliwahi kusema
kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana
kwa kuwa na nywele ndefu namna ile. Lakini baadaye jina na taswira ya mfalme wa
reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Congo,
ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza
kuikubali na kuionea ufahari.
Pia inasemekana Remmy
alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji.
Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana
hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.
Baba yake ndiye aliyeanza
kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini
kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine
wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili
awe mwanamuziki.
Kwa bahati mbaya baba yake
huyo mwaka 1953 alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa
tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama
yake hakuweza kuendelea kumlipia karo za shule, Remmy ilibidi aache shule.
Ilipofika miaka ya 1960,
Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa.
Mwaka mmoja baada ya kifo cha
Baba yake mzazi, mwaka uliofuatia wa 1964 ulikuwa si mzuri kwa Remmy kwani mama
yake mzazi naye alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa
kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia licha ya umri
wake mdogo.
Bila elimu na ujuzi mwingine
wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake
wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha
kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na sehemu mbalimbali nchini ya Congo akiwa na bendi yake iliyokuwa
imesheheni vijana wenzake iliyoitwa ‘Bantu Success’.
Kwa miongo kadhaa iliyofuatia
Dk. Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za
wakati huo nchini Congo
zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.
Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy
alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka
nchini Cuba
ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia
katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa.
Kwa upande wa uimbaji anasema
uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule
wa Franco Lwambo Makiadi ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.
Mwaka 1978 Remmy aliingia
jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati
huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.
Huo ukawa ndiyo mwanzo wa
maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania.
Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana
kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika
kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa
na kujulikana kwa haraka hapa nchini.
Mzee Makassy aliamua kuihamishia bendi yake keipeleka
nchini Kenya,
kitendo hicho cha mjomba wake kilichomfanya Dk. Remmy kujiunga na bendi ya Matimila baada ya kudumu kwa katika bendi ya
Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.
Jina la bendi hiyo ya Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja
kilichoko kusini mwa Tanzania.
Kujiunga kwa Remmy katika bendi ya Matimila, alijiongezea umaarufu
katika anga za muziki nchini Tanzania
wakati huo. Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na
kuibadilisha jina ikaitwa Orchestra Super Matimila.
Miaka iliyofuatia Watanzania
tulishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususan kutokana na mashairi ya
nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.
Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la
Orchestra Super Matimila hayakuishia nchini Tanzania
kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya
mipaka ya Tanzania
na Afrika.
Dk.Remmy Ongala aliwahi
kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama
mchezo tu. Kasseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa
akiondoka nchini Tanzania
kurejea kwao Uingereza.
Rafiki yake huyo alipofika
huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) shirika
linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za
dunia ya tatu. WOMAD walivutiwa na
nyimbo zao, hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.
Baada ya kurudi kutoka Ulaya
bendi ya Super Matimila ilitoa album yenye jina la ‘Nalilia Mwana’ ikiwa
na mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo
nyimbo zilizopendwa sana kama
vile ‘Ndumila Kuwili’ na ‘Mnyonge Hana Haki’
Mwaka 1989 Remmy na Matimila
walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo
ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ya Stud Real
World Studios,
ambayo ilikuwa inamilikiwa na
mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel.
Dk. Remmy aliwahi kufafanua
kuwa wimbo maarufu ya ‘Kipenda roho’ aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye
ni ‘mzungu’ muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto
watatu.
Mwaka 1990, Remmy na bendi
yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambako
walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’ ambayo ilikuwa na nyimbo kama
hiyo ya ‘Mambo’ ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya
wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No money, no life’ na
‘One World’.
Umaarufu wake ulizidi
kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa ‘Mambo kwa soksi’ ingawa baadhi ya watu
waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili mema kwa jamii, ingawa kimsingi
alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na
maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Akiwa Super Matimila Dk. Remmy
alitoka na nyimbo ningi zikiwemo za ‘Bibi wa mwenziyo’, ‘Kipenda roho’, ‘Asili
ya muziki’ na ‘Ngalula’. Zingine ni
pamoja na ‘Mwanza’, ‘Mama nalia’, ‘Harusi’, ‘Hamisa’, ‘Mnyonge hana haki’, ‘Ndumila
kuwili’ na ‘Mataka yote’ ambazo
zilimuongezea sifa kubwa Dk. Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi
jamii.
Baadaye Dk. Remmy Ongala
akaanza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na
muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani.
Remmy akaokoka, akatubudu
dhambi zake na akaanza kupiga muziki akimuimbia bwana.
Kabla ya kifo chake Dk. Remmy
alitoa albamu yake ya Injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’. Remmy alikuwa
katika hatua za mwisho za kukamilisha
albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13,
2010 nyumbani kwake Sinza. Eneo hilo
alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kufuatia umaarufu wake
alipokuwa hai.
Mungu
aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment