DEKULA KAHANGA AKIPIGA GITA KATIKA UKUMBI WA WHITE HOUSE UBUNGO DAR ES SALAAM, TANZANIA.
DEKULA KAHANA AKIWA KATIKA PICHA YA 'POZI' NA GITA LAKE.
'MAMBO YA ULAYA' VUMBI AKIWA NA FARASI.
DEKULA
KAHANGA ‘VUMBI’ ALIZIBA PENGO LA NGUZA
Na Kiyungi Moshy
January
28, 2013
KATI YA WANAMUZIKI WAAFRIKA waliopata
mafanikio makubwa kwa kuchacharika, jina la Dekula Kahanga haliwezi kukosa. Ni
mwanamuziki wa dansi, aliyefanikiwa kuanzisha bendi yake katika jiji la Stockholm nchini Sweden baada ya ‘kuitosa’ Maquis
Original.
Dekula
ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Vumbi’, anasisitiza kwamba mafanikio yoyote katika
maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, na dhamira ya dhati, hatimaye kufanya
maamuzi magumu.
Kabla
ya kwenda nchini Sweden,
‘Vumbi’ alikuwa mpigaji wa gita la solo katika bendi ya Maquis Original,
iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata Kindondoni jijini Dar es Salaam, miaka ya 1990.
Akiwa
katika mapumziko mafupi nyumbani kwake Mikocheni kwa Warioba jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Dekula
alitamka baadhi ya maamuzi magumu aliyoyafanya mojawapo ni lile la kondoka
katika bendi hiyo ya Maquis Original, na kutokomea kwenda Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa
nani huko ughaibuni.
Vumbi
anaeleza kwamba hivi sasa hajutii maamuzi yake kwakuwa amepata mafanikio
makubwa, ikiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake iitwayo Dekula Band. Amesema
bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala
Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.
Dekula
Band ina wanamuziki mahiri toka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo akina
Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na kucheza Show,
Sammy Kasule, huyo ni injinia pia huimba, kupiga gita la besi, drums na
kinanda. Wengine amewataja kuwa ni Joe Gerald Nnaddibanga, ambaye huimba,
kupiga konga na kucheza show, Christina Frank, na Marceline Kouakoua.
Mwenye
Dekula Kahanga, hulicharaza gila la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambaye
ni mbonyezaji wa kinanda. Safu hiyo kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika
kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya Sweden zikiwemo nchi za Ulaya, Asia, Marekani, Japan,
Falme za kiarabu na Afrika.
“
Hakuna kitu muhimu kama kuwa na mahusiano mema na baadhi ya watu toka nchi mbalimbali
ninazotembelea. Nimefikia kuweza kuongea kwa ufasaha lugha tano tofauti
za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa,
Lingala na Kiswidish” Anajigamba Dekula ‘Vumbi’.
Historia
ya Dekula Kahanga anailezea kwamba
alizaliwa mwezi Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera, Wilaya ya
Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ni baba
wa familia akiwa na mke na watoto watatu. Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya
watoto kadhaa wa Mzee Aloyce Obeid Dekula,
aliyekuwa mfanyakazi katika serikali ya Zaire iliyokuwa ikiongozwa na rais
Mobutu Seseseko.
Alipata elimu ya Sekondari katika shule mbili tofauti
za Bukavu na Uvira huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alihitimu kidato cha
nne mwaka 1979. Mwaka uliofuatia wa
1980, safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National,
na Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa
Nundu.
Akiwa
huko kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania
Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika wakati huo na alizitamani sana
nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz,
Tabora Jazz, Nyamnyembe Jazz, NUTA
Jazz, Mlimani Park, Maquis du Zaire na
Orchestra Safari Sound.
Kamwe
hatomsahau John Luanda katika historia
ya maisha yake, kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania.
Luanda alikuwa
akimiliki bendi ya Chamwino Jazz,
aliwachukua toka Kongo akiwa na wenzake
akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta kwa madhumuni ya kujiunga
katika bendi yake ya Chamwino. Bendi hiyo wakati huo ilikuwa ikipiga muziki maeneo ya Tandale huko
Manzese, jijini Dar es Salaam.
“Mwenye
bahati habahatishi” ndivyo anavyosema mkung’utaji mahiri wa gita la solo Dekula
Kahanga ‘Vumbi’, kwamba mwaka 1980 alikutana
na mwanamuziki Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika ofisi za ubalozi wa
Kongo hapa nchini.
Nguza
wakati huo alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa ni mmoja kati ya wanahisa wa Orchestra Maquis Comapy (OMACO) na
mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire. Katika
maongezi yao,
Chimbwiza Nguza alimpa mwaliko yeye na
wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya
Ubungo jijini Dar es Salaam.
Dekula
alikubali mwaliko huo na Weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha
kwa muda mfupi.
Walipopanda
jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika
ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.
Dekula
Kahanga baadaye aliitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu
Katai ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ wakimtaka
aandike barua ya kuomba kujiunga na bendi yao kwa mkataba usio na mshahara.
Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari
ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na akajiunga na Maquis du Zaire.
Vumbi
anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa Temeke Stereo, alimuona Nguza akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo
huku akisikiliza midundo inavyounguruma..
“Nilipomuona, nikaingiwa na hofu kubwa nikijihisi kama ninamvunjia heshima Nguza. Nikaomba nimpishe ili ashike nafasi yake” Anasema kwa
kujiamini Dekula Kahanga.
Lakini viongozi wake akiwemo Chibangu Katai ‘Mzee
Paul’ na Ilunga Lubaba, walimwamuru aendelee kushika ‘mpini’.
Kwa
amri hiyo, ilikuwa kama Fisi aliyeachiwa Bucha kuilinda. Aliweza kuzicharaza kwa
umahiri mkubwa nyimbo zote alizokuwa zikipigwa Field Marshal Nguza
zikiwemo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa
Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo
kutofautisha kati yake na Nguza.
Aliachiwa kulivurumisha gita hadi mwisho wa
onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya
hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipo naye hakusita
kumpa hogera kwa kazi nzuri.
“Mungu
mkubwa, siku hiyo Nyota yangu iling’ara
kiasi kwamba hata mimi mwenyewe sikuweza kuamini nilichokuwa nikikifanya
jukwaani hapo” Anasema Dekula Kahanga
‘Vumbi’ huku akitabasamu.
Taharuki
kati ya uongozi wa Maquis du Zaire na Nguza ‘Vicking’ ziliendelea
hatimaye aliondoka rasmi bendi hiyo, hadi kwenda kuanzisha bendi yake ya
Orchestra Sambulumaa akiwa na mwanamuziki wengine akiwemo mwanaye Papii Kocha.
Bendi hiyo ilikufa baada ya Nguza na mwanaye huyo kuhukumiwa kutumikia
kifungo cha maisha gerezani.
Miaka
ya 1989 na 1990 Dekula alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis
Original, jina lililozaliwa toka Maquis
du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi Lang’ata Kinondoni. Mtunzi na mwimbaji
Maquis Original Tshimanga Kalala Assosa,
alikuwa akipaza sauti ya kumpandisha mori kwa kumuita mara kwa mara
Vumbiii,Vumbiii,Vumbiii kama kibwagizo wakati wa chorus kwenye wimbo wa Ngalula.
Vumbi
wakati huo alikuwa na umri ambao unamruhusu kuhangaika kutafuta maisha yenye
maslahi mazuri. Hivyo maamuzi magumu yakaanzia hapo Lang’ata baada ya kuamua
kuicha bendi ya Maquis Original, iliyompa jina na kuchepukia katika jiji la Stockholm nchini Sweden.
Akiwa
Stockholm, Vumbi alianza kuchacharika mitaani akitafuta bendi ya
kupiga, hatimaye akakutana na mwanamuzi
toka Uganda, aitwaye Sammy Kasule. Mwaka 1993
wakaamua kuanzisha bendi yao
ikiitwa Makonde Group.
Mwaka
1999, Dekula Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni
nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘mpenzi Asha’
Dekula
Kahanga anajivunia kwamba yeye ni
mwanamuziki wa kwanza toka Afrika huko Sweden, kufyatua album. Alitoa album iitwayo ‘DEKULA Sultan Qaboos’
yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon,
Mayanga, Rozina, Mambo leo na Nostalgie nyimbo hizo anasema zinazopigwa mno katika vituo vingi
vya redio Duniani.
Ili
kupata unafuu wa maisha nchini Sweden, Dekula alilazimika kuomba uraia wa nchi hiyo
hivyo ilifuata taratibu zote. Alichukua maamuzi magumu mengine ya kuukana uraia
wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kupata uraia wa
nchi hiyo.
Hivi
sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni raia halali wa nchi ya Sweden
na wanaweza kusafiri kwenda nchi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo
kuomba VISA.
Dekula
ametoa mwito kwa wanamuziki chipukizi kujifunza kupiga ala za muziki ili
wafikie viwango vya kuwa wanamuziki. Pia amewaasa kuacha kulewa sifa
ndondogo pia kuepuka anasa zisizo na tija.
“Nawapenda
sana
Watanzania, walinipokea, wakanilea,
wakanithamini na wakanipenda. Ninatarajia kutoa zawadi endelevu kwa Watanzania siku za usoni kuanzisha bendi
ya vijana, itakayokuwa ikitumia ala za muziki wa kisasa” anamaliza Dekula
Kahanga Vumbi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment