ALFA NA OMEGA
YA MAQUIS
March , 2013
MAQUIS du ZAIRE ni bendi ambayo ‘iliyowatesa’ Watanzania
kwa kuwaporomoshea burudani za muziki wa
dansi maridhawa katika kumbi mbalimbali hapa nchini.
Kwa wale
waliokuwa vijana kati ya miaka ya 1970 na 1990, kamwe hawawezi kuisahau bendi
hiyo ambayo iliingia hapa nchini kwa kishindo kikubwa ikitokea Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (Zaire)
wakati huo.
Mwaka
1981 niliwahi kufanya mahojiano maalumu na mmoja wa viongozi wa bendi hiyo,
Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye alinipa wasifu wa bendi hiyo ya Maquis
du Zaire.
Wasifu
huo niliuandika na kuchapishwa katika gazeti la serikali la Nchi Yetu la kila
mwezi, ambalo lilikuwa likuzwa kwa senti 30, likitolewa na Idara ya habari
(MAELEZO).
Hivyo
basi si vibaya nikarejea kuwapasha wale
ambao hawaifahamu bendi hiyo na kwa waliosahau, niwakumbushe kwa kuwapa wasifu wa bendi ya Maquis du Zaire
tangia ilivyoanzishwa hadi kutoweka kwake
katika taswira ya muziki.
Historia
ya bendi hiyo inaanzia mwaka 1960 kwa vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina
huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(Zaire), walioungana na
kuunda bendi yao
wakaiita Super Theo.
Bendi
hiyo ilitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa Kamina
na vitongoji vinavyouzunguka mji huo, baadaye wakaibadilisha jina
kuwa Super Gabby.
Katika
kile kilichoelezwa na uongozi wa Super Gabby kuwa ni kuleta mageuzi katika
muziki, bendi hiyo mwaka 1972, ilibadili jina tena na kuitwa Maquis du Zaire.
Bendi hiyo ya Maquis du
Zaire iliingia hapa Tanzania
mwaka huohuo wa 1972, kwa mwaliko wa mfanyabishara maarufu Mzee Batengas.
Walianza kutumbuiza kwa mkataba katika ukumbi wa Mikumi Tours uliokuwa maeneo
la Tazara, Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao waliachana na Mzee
Batengas, wakaenda kupiga muziki katika
Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima
aliyekuwa akimiliki wa ukumbi wa Safari
Resort maeneo ya Kimara.
Mnamo mwaka 1977 Maquis du Zaire
waliamua kuongeza nguvu kwa kuimarisha
kikosi chao. Hivyo uongozi huo ulimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ kwenda Congo
kutafuta wanamuziki wengine wapya.
‘Mzee Paul’ alibahatika
kuwachukuwa akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Nkashama Kanku Kelly,
Ilunga Banza ‘Mchafu’, Mutombo Sozy
na mnenguaji mahiri, Ngalula
Tshiandanda. Wakati huo walikuwa wakipiga na kucheza katika mtindo wa
‘Chakula Kapombe’ ambao kwa watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na
mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao
yaelezwa kuwa kulileta mabadiliko
makubwa sana katika muziki husuan tungo nzuri za
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ambaye ndiye aliyeleta mapinduzi makubwa ya
muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire ilikuwa
na wanamuziki wenye ubunifu kwa ajili ya kuboresha bendi yao. Waliazisha mtindo
mwingine wa ‘Kamanyola’ mtindo uliowapagaisha
wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Wakati huo ‘rapa’ wa bendi hiyo, Mwema Mudjanga
‘Mzee Chekecha’ alikuwa akiwahamasisha wapenzi
wake kwa kutamka “cheza Kamanyola…
Kamanyola bila jasho… cheza ukijidai…”
‘Mwenye bahati habahatishi’
usemi huo ulijodhhirisha mwaka wa 1977 mwishoni, ambapo bendi ya Maquis du Zaire ilipoangukiwa na bahati
nyingine tena. Walisaini mkataba
mwingine na Mzee Makao aliyekuwa
akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Baada ya kumaliza mkataba na
mfanayabiashara Hugo Kisima
ilimaliza mkataba na kuondoka kwa Hugo Kisima.
Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya Sanifu na Ogelea piga mbizi, haikuchukua kipindi
kirefu ukumbi huo ukabadilishwa jina na kuitwa White House. Ikumbukwe
kwamba wakati huohuo Maquis pia ilikuwa
ikipiga muziki kwenye ukumbi wa Mpakani,
maeneo ya Mwenge. Ukumbi wa Mpakani baadaye ulibadilishwa jina kuwa Silent Inn.
Kisha kuishia kuwa Kanisa.
Mwishoni mwaka 1978 waliamua
kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka Congo ambao
ni akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Maquis du
Zaire ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu
Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula
‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo miaka ya 1980 mafanikio
makubwa yalionekana. Mojawapo ni lile la kuanzisha Orchestra Maquis Company
(OMACO). Kampuni hiyo ilikuwa ikimiliki shamba la matunda, wakilima kwa kutumia
matreka yao
maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao
walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko
Kuu la Kariakoo jijini Dar es
Salaam.
OMACO pia
ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa maeneo ya Sinza na pia
waliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.
Vijana wa
wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu
kila siku za Jumamosi, kuwashuhudia vijana wa Maquis du Zaire waliokuwa
watanashati na nidhamu ya hali ya juu wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.
Enzi hizo
ilikuwa ukiingia katika ukumbi wa White House, mbele yako macho lazima yakutane
na mbao zilizo nakshiwa kwa kuandikwa majina
ya wanamuziki wote na kukomelewa juu ya mwembe uliokuwa katikati ya ukumbi huo.
Maquis du
Zaire ambayo ilikuwa ikipiga
muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha
muziki na kusikika kipaza sauti kikiuliza kama wapenzi wao kama
wamekuja na miswaki? Wapenzi walikuwa
wakijibu ndiyooooo… Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo. Muziki ulikuwa unapigwa
hadi alfajiri.
Bendi
hiyo ikiwa hapa nchini ilikuwa ikipiga na kucheza katika mitindo
mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya Chakula Kapombe,
Kamanyola, Bishe Bishe, Zembwela, Chekecha na Ogelea Piga mbizi.
Mwema Mudjanga ‘ Mzee
Chekecha’ ndiye aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo. Alikuwa kivutio
kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya kupuliza
tarumbeta, alikuwa ‘rapa’ aliyeweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza,
akitumia vibwagizo vya ‘Chekeee…. Chekechaaa’
‘Tusangalaa’, ‘aima imaa’, ‘Bishe
bishee’, ‘cheza Kamanyolaa’, ‘cheza kwa maringo’, ‘ Cheza ukijidai’ ‘ Sanifuu Saa... Sanifu, Ongeleaa piga mbizi …
na mengine mengi.
Maquis du
Zaire
wakati huo ilikuwa imesheheni wanamuziki
zaidi ya 40 wenye vipaji vinavyopishana. Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki
katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.
Nina
uhakika kwamba msomaji wangu unashauku ya kujua au kukumbushwa kikosi kamili kilichokuwa
kinatengeneza Maquis du Zaire wakati huo. Nikianza na safu ya waimbaji
walikuwepo akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule
Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa.
Wengine
walikuwa Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo
Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’,
Tshimanga Kalala Assosa, Kabeya Badu, Masiya Radi ‘Dikuba kuba’, Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari
na Anna Mwaole.
Wapiga
gita la solo alikuwepo Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye
kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo,
wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha ‘Field Marshal’.
Wengine
katika gitaa hilo waalikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga
‘Vumbi’ na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.
Gitaa la
rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila
Mauffi. Bila kuwashau akina Mbambu
Kazadi, Mondo Mondonde na Nawayi
Kabwila.
Gitaa zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na
Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kwa kulicharaza gita
hilo akiwa kajitwisha kwenye upara kichwani kwake.
Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.
Kama nilivyokujuza hapo awali kwamba bendi hiyo ilikuwa
imejaza mseto wa vipaji mbalimbali. Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya
bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga/‘Super Sax’, Khatibu Iteyi
Iteyi, Alex Kanyimbo, Kalamazoo, Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna
‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na Majengo Selemani.
Wapuliza
tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku
Kelly, Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’,
Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’ Mpoyo Kalenga,
Berry Kankonde, Kaumba Kalemba, Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan
Machege na Ngenda Kalonga.
Vijana
hao kwa pamoja walikuwa wakitoa burudani maridadi wakiwa wamejitwisha tarumbeta zao vichwani wakilishambulia
jukwaa, huku wakicheza kwa staili za aina yake ukumbini.
Madoido
na mbwembwe hizo, ziliwavutia wapenzi
wengi na kupenda kuhamishia viti vyao wakisogea sehemu iliyokuwa karibu, ili kushuhudia vijana
hao wakifanya maajabu ya kuchezea vyombo hivyo.
Mbonyezaji wa Kinada
alikuwa Mbuya Makonga ‘Adios’ huku Mutombo
Sozzy akizicharaza drums akisaidiana na Matei Joseph.
Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu
Wabandoki Motto.
Walikuwepo
na wanenguaji mahiri ambao walikuwa wakitoa burudani za pekee
wakati huo akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashidi, Anna
Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima,
Zuwena na Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.
Ikiwa
White House bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara,
Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Mwana yoka ya Babote, Ngalula, Nasononeka,
Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane wimbo ambao
ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.
Zingine
zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma,
Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya
nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo
idadi.
Kuna
msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo”
msemo huo uliisibu bendi ya
Maquis du Zaire baada ya kiungia katika maelewano ‘hafifu’ na mwenye
ukumbi, hadi kulazimika kuondoka wakiacha ukumbi huo ukibadilishwa kuwa Gereji
hadi leo.
Baadaye bendi
hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Maquis Original wakipiga katika kumbi za
Wapiwapi’s pale maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke, kabla ya
kuhamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata pale Kinondoni.
Maquis
Original ilileta wanamuziki wengine toka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo muda mfupi kabla ya mpiga gitaa la solo, Dekula
Kahanga ‘Vumbi’ kuondoka kwenda Stockholm nchini
Sweden.
Wanamuziki
hao walikuwa Kivugutu Motona Chatcho (Solo), na waimbaji Freditto Butamu na
Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.
Walitikisa
ukumbi wa Lang’ata kwa nyimbo zao kali
za Mangolibo, Mayanga, Kisebengo, Makumbele, zikisindikizwa na wimbo wa Ngalula
ambao mwimbaji Thsimanga Kalala Assosa alikuwa akitoa kibwagizo wakati wa
chorus akiita “ Vumbiii Vumbiii Vumbiii.
Nyimbo zote zilipigwa na kutamba kwa mitindo ya ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.
Maquis Original ikiwa Lang’ata, kuna shabiki
mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’
ambaye alikuwa kivutio kikubwa kwa
wapenzi wa Maquis, kwa kuonyesha uhodari wa kucheza ‘Sendema’ akiwa kajitwisha chupa ya Bia juu ya kichwa
chake.
Ikumbukwe
kwamba idadi kubwa mno miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa humu, wameshatangulia
mbele za haki.
Wengine
ni wagonjwa akina Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mmbombo wa Mmboka na
Mutombo Lufungula ‘Audax’
Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi
waliotangulia na awape tahfifu wanaoumwa, Amen.
MPIGA GITA LA SOLO CHIMBWIZA MBANGU NGUZA 'VICKING' AKIWA NA KASONGO MPIDA 'CLAYTON' NYUMA.
MUTOMBO LUGUNGULA 'AUDAX'(kushoto) NA KASONGO MPINDA
KASONGO MPINDA (katikati) NA MAPACHA KYANGA SONGA NA KASALO KYANGA.
NKASHAMA KANKU KELYY AKIPULIZA TARUMBETA.
CHINYAMA CHIYAZA AKIYARUDI KATIKA STAILI YA CHAKULA KAPOMBE.
ILUNGA BANZA ' MCHAFU' (kushot) NA DEKULA KAHANGA WAKIYACHARAZA MAGITA.
BAADHI YA WANAMUZIKI WA MAQUIS DU ZAIRE TOKA KUSHOTO, SULEIMA MBWANA 'COX', MBUYA MAKONGA 'ADIOS', MUJOS WA BAYEKE, KSTEVEN KAINGILILA MAUFFI, DEKELA KAHANGA 'VUMBI' ISSA NUNDU MUKUMBULE LOLEMBO 'PARASHI' NA ROY MUKUNA.
MPIGA TUMBA WA MAQUIS DU ZAIRE SIDY MORRIS AKIZIDUNDATUMBA KWA STAILI YA AINA YAKE.
No comments:
Post a Comment