Wednesday, February 27, 2013

HASSAN SHAW KINANDA 'KIMEMTOA'


 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW AKIBONYEZA KINANDA HICHO KWENYE MOJA YA HOTEL YA KITALII  NCHINI THAILAND.

 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW AKIFANYA WINDOW SHOPING KATIKA MADUKA NCHINI THAILAND.


 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW  WAKIJIVINJARI  NA  MPULIZAJI  WA  TARUMBETA NKASHAMA KANKU KELLY (KUSHOTO) WALIPOKUWA NCHINI MALYSIA.

FEBRUARY 27, 2013

HASSAN SHAW alijulikana sana hapa nchini  hususan kwa wapenzi wa bendi ya Vijana Jazz ambao walimshuhudia kijana uyo wakati akibonyeza Kinanda.

Alibonyeza Kinanda hicho na kumjengea umaarufu katika nyimbo za  Shingo Feni, Penzi haligawanyiki na Wifi zangu mna mambo ambazo zilikuwa zikiimbwa kwa sauti nyororo na mwanadada Kida Waziri katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni Jijini Dasr es Salaam.

Jina lake kamili ni Hassan Shaw Rwambo, aliyezaliwa Septemba 25, 1959 jijini Dar es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gita na wenzie kando kando ya Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma, wakitumia magita ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi.

Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir Ally yaelezwa kwamba ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gita kiasi cha kukubaliwa kupiga gita la rhythm katika bendi yaya pili  Afro 70, iliyokuwa ikiitwa PAMA Band  iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya.

Ni chini ya malezi ya Patrick akajifunza kupiga Kinanda baadaye mambo ya muziki na kujiunga na cha Ufundi cha  Dar Technical College.
Mwaka 1980 alijiunga na bendi ya  Vijana Jazz kama mpiga Kinanda ambako akilikutana na  wanamuziki wengi akina John Kitime, Abuu Semhando kwa upande wa drums,  mwimbaji wa wa kike Kida Waziri, Saad Ally Mnara na Hamisi Mirambo. Wengime walikuwa akina   Rashidi Pembe,aliyekuwa kipuliza Saxophone,  Hassan Dalali na  Hamza Kalala walikuwa wapiga gita la Solo.
Ikimbukwe kwamba Hassan Dalali anyatajwa humu  ndiye yule baadaye  akawa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Sports.

Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound (OSS), chini ya  Muhidini Mwalimu  Gurumo na Abel Balthazar. Huko OSS alikutana na wanamuziki wengine akina  Benno Villa Anthony na Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ambao walikuwa waimbaji.

Hassan Shaw alikuwa na msimamo usiopindika pia  hakuwa mtu wa kuonewa ovyo. “Niliicha bendi ya hiyo baada ya miezi sitakutokana na  mhusika kutozingatia mkataba wangu…” anasema Shaw.

Katika kujitafutaia maisha Hassan Shaw akaamua kuhamia  Visiwani Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga katika Hoteli ya Mawimbini.

‘Chema chajiuza’  Sifa zake za kubonyeza Kinanda zilipelekea  kuitwa katika bendi ya Washirika Tanzania Stars. Alipotua hapo akakutana na wanamuziki wakali wakiwemo waimbaji mahiri akina  Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, na  Abdul Salvador ‘Faza kidevu’ ambaye alikuwa na ‘manjonjo’  ya kupiga kinanda akitumia kidevu chake. Ndiyo sababu ya kuitwa ‘Faza Kidevu’

Shaw katika maisha yake  abadan  hukupenda ‘Longolongo’ hivyo kwa bahati mbaya katika bendi hiyo kulitokea kutokuelewana baina ya wanamuziki. Yeye kama kiongozi wa bendi, ikambidi aachie ngazi ili kuepusha bendi kuzidi kujichanganya.

Baada ya hapo anamtaja mpulizaji mahiri wa  tarumbeta,  Nkashama Kanku Kelly  kuwa  alimuita ili ajiunge na bendi yake ya  The Kilimanjaro Connection. Kanku  Kelly na  Hassan Shaw wameona nyumba moja  Kanku  akiwa ni  mume wa dada wa mke wake.

 Anamsifia Kanku kwamba  alimvumilia sana kwa kuwa hapo awali  hakuwahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani. Akiwa Connection alijifunza kukopi nyimbo nyingi za wanamuziki  wa kimataifa duniani.

The Kilimanjaro Connection ilikuwa inazunguka kwenda  kupiga muziki kwenye  hoteli  mbalimbali katika nchi za Malaysia, Singapore, Indonesia, Thailand na Japan, jambo ambalo kwake yeye ilikuwa  faraja kubwa.

Pamoja na Kanku Kelly, Shaw anasema  kwamba alishirikiana vyema na wamanuziki wengine akina Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan,  Shomari Fabrice, Bob Sija, na Faliala Mbutu. Wengine  walikuwa Ray Sure boy, Delphin Mununga na Ramdhani Kinguti ‘System’

Baadaye Hassan  Shaw, na wanamuziki wenzake  Ramadhani Kinguti ‘ System’ na Burhan Muba wakafikia maamuzi ya kuanzisha kundi dogo la muziki  wakitumia ala iitwayo Sequencer keyboards, wakiicha The Kilimanjaro Connection ya Kanku Kelly.

Kundi hilo likajiita Jambo Survivors Band ambalo baadaye likaaza safari za  kuzunguka nchi mbalimbali kupiga muziki katika hoteli za kitalii.  Ilifanya kazi katika nchi za Oman, Fujairah, Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E), Singapore, Malaysia na Thailand.

Hassan  Shaw anasema wanamuziki ambao kamwe hatawasahau maishani mwake  ni pamoja na  Zahir Ally Zorro, Marehemu Patrick Balisdya, Waziri Ally, Ramadhani Kinguti ‘System’, Burhan Muba na Kanku Kelly kwa kuwa ni wao walomfikisha  hapo alipo.

Akielezea kituko ambacho hawezi kusahau ni pale walipokuwa nchini Malaysia,  alishindwa kupiga nyimbo baada ya kutoweka nyimbo zote  kichwani mwake.  “ Nililikuwa ninapiga muziki kwa mara ya kwanza nikiwa nimezungukwa na wazungu weupe wakiniangalia. Huwezi kuamini,  nyimbo zote  ziliyeyuka kichwani  nikawa sikumbuki hata nyimbo moja”  anasema Hassan Shaw.

Kama walivyo wanamuziki wengine wenye mafanikio, Shaw anawaasa vijana kujifunza kupiga ala za muziki ili kufikia ndoto zao za kuwa wanamuziki wa kukubalika kimataifa. Pia amewataka vijana kutokata tamaa pale wanapokutana na vikwazo bali watafute jinsi ya kujinasua.

Hassan Shaw hadi sasa yupo nchini Thailand akipiga muziki  na kundi zima la Jambo Survivors. 

Mwisho.





No comments: