MIAKA MIWILI BAADA YA KIFO CHA DK.
REMMY
Desemba 15, 2012
SIKU HAZIGANDI nathubutu
kusema hivyo kwani jana Alhamisi Desemba
13, 2012 ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa
Tanzania, Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla.
Ni miaka kamili imetimu toka tulivyoondokewa
na kipenzi cha wengi, mwanamuziki nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’
Dk. Remmy aliyefariki usiku
wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam
baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kisukari.
Aliwaacha wapenzi wake wa
muziki wa dansi na ijili pia wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi
yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake ambazo hadi leo zinarindima
katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka yetu.
Dk. Remmy alikuwa wa kwanza
kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini
jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa serikali na dini watu kwa ujumla walielewa
nini alichokuwa akisema Dk.Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani tahadhari hiyo.
Alizaliwa akiwa na meno
mawili ya mbele kinywani mwake na
akaonekana kana kwamba ni mtoto wa
ajabu. Aidha hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja
kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.
Dk. Remmy alijipatia umaarufu
katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari yake
ndogo ‘soloon’ lililokuwa la aina yake popote lipitapo watu walilishangaa,
lenye maandishi nyuma ya gari hilo
yakisema ‘ Baba yako analo’?
Historia ya maisha ya
Dk.Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala.
Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Baba yake alikuwa ni
mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira.
Baada ya kuzaliwa kwake haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji
wa Kisangani
huko DRC.
Ipo habari kwamba kabla ya
kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya
kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda
kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa
asiiage dunia pia.
Bila kusita mganga wa
kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia
hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto
akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha
Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyompelekea
kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.
Mwenyewe aliwahi kusema
kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa
kuwa na nywele ndefu namna ile, mpaka hapo baadaye jina na taswira ya mfalme wa
reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Congo,
ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali
na kuionea ufahari.
Pia inasemekana Remmy
alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji.
Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana
hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.
Baba yake ndiye aliyeanza
kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini
kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine
wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili
awe mwanamuziki.
Kwa bahati mbaya baba yake
huyo alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa tayari
ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake
hakuweza kuendelea kumlipia karo ya shule, Remmy ilibidi aache shule.
Ilipofika miaka ya1960, Remmy
tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa sio
mwaka mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi alifariki dunia jambo ambalo
lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa
mkuu wa familia.
Bila elimu na ujuzi mwingine
wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake
wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha
kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na sehemu mbalimbali nchini ya Congo akiwa na bendi yake iliyokuwa
imesheheni vijana wenzake iliyoitwa ‘Bantu Success’.
Kwa miongo kadhaa iliyofuatia
Dk.Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za
wakati huo nchini Congo
zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.
Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy
alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka
nchini Cuba
ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia
katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji
anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule wa Franco ulimsaidia kupata staili yake ya
uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai
wake.
Mwaka 1978 Remmy aliingia
jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati
huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.
Huo ndio ukawa mwanzo wa
maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania.
Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana
kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika
kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa
na kujulikana kwa haraka hapa nchini.
Mzee Makassy aliamua kuihamishia bendi yake keipeleka
nchini Kenya,
kitendo kilichomfanya Dk. Remmy kujiunga
na bendi ya Matimila baada ya kudumu kwa
katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.
Jina la bendi hiyo ya Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja
kilichoko kusini mwa Tanzania.
Kujiunga kwa Remmy katika bendi ya Matimila, alijiongezea umaarufu
katika anga za muziki nchini Tanzania
wakati huo. Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na
kuibadilisha jina ikaitwa Orchestra Super Matimila.
Miaka iliyofuatia Watanzania
tulishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususani kutokana na mashairi ya
nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.
Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la
Matimila hayakuishia nchini Tanzania
kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania
na Afrika.
Dk.Remmy Ongala aliwahi
kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama
mchezo tu. Alimpa kasseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa
akiondoka nchini Tanzania
kurejea kwao Uingereza.
Rafiki yake huyo alipofika
huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) shirika
linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za
dunia ya tatu. Jamaa walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa mwaliko kushiriki
katika maonyesho yao
barani Ulaya ya mwaka 1988.
Baada ya kurudi kutoka Ulaya
bendi ya Matimila ilitoa album yenye jina la Nalilia Mwana ikiwa na mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo
zilizopendwa sana kama
vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki.
Mwaka 1989 Remmy na Matimila
walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo
ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa
inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa
inaitwa Real World Studios.
Dk. Remmy aliwahi kufafanua
kuwa wimbo maarufu ya Kipenda Roho, aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye
ni mzungu muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto
watatu.
Mwaka 1990, Remmy na bendi
yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambapo
walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’ ambayo ilikuwa na nyimbo kama
hiyo ya Mambo ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya
wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No Money, No Life’ na
‘One World’.
Umaarufu wake ulizidi
kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa ‘Mambo Kwa Socks’ ingawa baadhi ya watu
waliupinga kwa kusema kwamba hauwa na maadili ingawa kimsingi alikuwa anawaasa
watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa
ukimwi.
Akiwa matimila Dk.Remmy
alitoka na nyimbo ningi zikiwemo za Bibi wa mwenziyo, Kipenda roho, Asili ya
muziki na Ngalula. Zingine ni pamoja na
Mwanza, Mama nalia, Harusi, Hamisa, Mnyonge hana haki, Ndumila kuwili na Mataka
yote ambazo zilimuongezea sifa kubwa Dk.
Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi jamii.
Baadaye Dk. Remmy Ongala
akaanza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na
muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Remmy
akaokoka, akatubudu dhambi zake na akaanza kumuimbia bwana.Kabla ya kifo chake
Dk. Remmy alitoa albamu yake ya injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’. Remmy
alikuwa katika hatua za mwisho za
kukamilisha albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba
13,2010 nyumbani Sinza. Eneo hilo
alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kufuatia umaarufu wake
alipokuwa hai.
Mungu aiweke roho yake pahala
pema peponi, Amina.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment