SAUDA ANNA MWAOLE AKIMBA KATIKA MOJA YA MAONESHO YAKE.
SAUDA MWAOLE AKISEREBUKA BAADA YA KUIMBA.
MUUMIN MWINJUMA NA ANNA MWAOLE WAKIIMBA KWA KUPOKEZANA,
ANNA MWAOLE ni mwanamuziki aliyepanda na kushuka milima na
mabonde hadi kukubalikana na wapenzi wa muziki wa dansi na taarabu hapa nchini.
Mwaole
katika kutimiza malengo yake aliruka majaribu
mengi aliyokumbana nayo hususan
katika tasnia hiyo ya muziki hatimaye aliweza kushinda na akafika hapo alipo.
Ni
mama aliyejaaliwa vipaji vingi vikiwemo vya utunzi, uigizaji, uimbaji wa nyimbo za dansi na taarabu. Mwaole
ukimwangalia kwa wasiwasi hauwezi kuamini kama
anaweza kulishambulia jukwaa kwa kucheza hasa ukizingatia tambo lake la mwili
lilojaa minofu kila maeneo.
Uzoefu
na vipaji vyake viliendelea kukua, akivipata toka bendi mbalimbali za muziki wa
dansi alizopitia.
Mwaole
anasema ameshapiga katika bendi zaidi ya nane hapa nchini akitafuta maisha na
harakati za kujiedeleza kimuziki.
Historia
ya maisha ya Mwaole mwenye asili ya mkoa wa Iringa, inaanzia katika mji wa Mpwapwa
mkoani Dodoma, ambako mama huyo ndiko alikozaliwa mwaka 1965.
Anna
akiwa yu ngali kigori, alikuwa akihusudu sana sauti
na uimbaji wa mwanamuziki wa kike toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,
Mbilia Bell. Anasema kila mara alikuwa akinunua kanda za Mbilia na akanza
kujifunza kuimba nyimbo zake.
Mwaole
alijiunga katika kwaya ya Kanisa mjini Mpwapwa 1989, akiwa na mwanamuziki Rahma
Shaari. Anasimulia kuwa yeye na Rahma Shaari walikuwa waimbaji wakutegemewa katika kwaya ya
Kanisa hilo.
Anna
Mwaole anafafanua kwamba kabla ya hapo yeye na Ramha Shaari walikuwa waumini wa
dini wa kikristo. Anamuelezea Rahma kwamba alikuwa akiitwa Grace. Lakini baada ya
kuolewa na mwiisilamu, akalazimika kubadili dini na kusilimishwa akapewa
jina hilo la
Rahma.
Halikadharika
yeye Anna naye aliolewa na mwanamume mwiislamu aliyemtaja kwa jina la Rashidi
Nyambya. Huyo ndiye aliyesababisha kusilimu
na kuingia dini ya kiislamu, akachagua jina la Sauda.
Sauda
Mwaole anamtaja Rahma Shaari kuwa ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kwa yeye
kuingia katika muziki wa dansi muda
mfupi baada ya kufika jijini Dar es Salaam mwaka 1988.
Anasema
wakati huo alimkuta Rahma akiimba katika
bendi ya Maquis du Zaire ambapo alimuombea
nafasi ya kuimba katika bendi hiyo mwaka 1989.
Sauda
anafafanua kwamba ushawishi wa Rahma kwa uongozi wa Maquis ulifankiwa. Aliitwa na
akafanyiwa usaili kwa kuimba wimbo wa ‘Nakei
Nairobi’ wa Mbilia Bell na ule wa ‘Kama umenichoka mpenzi ’ ulioimba
na Issa Nundu.
Wimbo
wa ‘Nakei Nairobi’ kwake ilikuwa kama ‘kumsukuma mlevi’ kwani tayari alikuwa
amezifanyia mazoezi nyimbo zote za Mbilia Bell
toka wakati akiwa Mpwapwa.
Kwa
majigambo Sauda Mwaole anasema aliuimba wimbo huo kwa kujiamini hadi uongozi wa bendi
hiyo wakiwemo akina Chibangu Katayi ‘mzee Paul’, Chinyama Chiyaza, Nguza Mbangu
‘Vicking’ na Tshimanga Kalala Assosa, hawakuamini
masikio yao, walimkubali papo hapo na kumapa ajira.
Siku
ya kwanza kupanda stejini akiwa na Maquis du Zaire, Mwaole anaeleza kwamba alitetemeka mno mara alipoambiwa
kuimba mbele ya wapenzi na mashabiki kwa
mara ya kwanza katika ukumbi wa Wapi wapi’s Bar iliyokuwa Chang’ombe maduka
mawili.
“Nilitamani
ardhi ipasuke, nitumbukie humo. Nilihofu
hasa baada ya kuona jinsi wapenzi na mashabiki wa Maquis waliokuwa wamefurika
ukumbini humo wakinianagalia mimi ” anatamka Mwaole.
Lakini anamshukuru
mungu kwamba ni mwema aliyempa ujasiri akaimba kwa umahiri mkubwa wimbo wa ‘Kama
umenichoka mpenzi’ akishirikiana na Issa
Nundu.
Sauda
Mwaole anasema alipoimba wimbo wa ‘Nakei Nairobi’,
watu waliinuka kwenye viti vyao wakishangilia na kumtunza pesa huku wakitamka
kwamba wamepata Mbilia Bell wa Tanzania.
Walitamka hayo kwa vile sauti na uimbaji wake haukutofatiana na wa Bell.
Mwaole
anasema hatoweza kuisahau siku hiyo katika maisha yake, kwa kuwa ndiyo ilikuwa
imemfungulia ukurasa mpya wa maisha yake katika fani ya muziki.
Mwezi
Septemba 1989, alichukuliwa katika bendi ya Polisi Jazz, ambako alilazimika
kwenda ‘depo’ za kijeshi kwa miezi mitatu, Kilwa road jijini Dar es Salaam.
Akiwa
katika bendi hiyo alikutana na wanamuziki wengine anawataja kwa majina ya akina Mobari Jumbe, Maimuna Ramadhani, Hamza
Mwanamasingi, Ali Moshi na wengine wengi.
Akiwa
na Polisi Jazz alitoka na wimbo wa ‘Sitaki sitaki visa vyako’ wimbo uliotungwa
na Mobari Jumbe.
Mwaole alipenda kujiendeleza zaidi katika fani hiyo ya
muziki, hivyo akaondoka kwenda kujiunga na Bantu Group iliyokuwa ikiongozwa na
‘mzee wa madongo’ Hamza Kalala.
Akiwa
Bantu Group alikutana na vijana wengine chipukizi akina Muumini Mwinjuma, Musemba
wa Minyungu, Rogers
na wapiga gitaa Magele Sange na Ali Adinani.
Anasema
hakutarajia kwamba ipo siku angelikuja kuingia katika studio kurekodi nyimbo.
Lakini kwa mara ya kwanza aliweza kuingia studio kurekodi wimbo wa ‘Emma tupunguze
matumizi yasiyo ya lazima’
.
Safari
ya Mwaole haikuishia hapo, kwani mwishoni mwa 1991, alijiunga katika bendi ya Mzee Kitenzogu Makassy. Baada
ya mwaka mmoja kupita ‘alichupa’ na kwenda
kujiunga na bendi ya Lego Stars, iliyokuwa na wakali akina Joseph Bartholomew
Mulenga ‘King Spoiler’(solo), Anania Ngorika, Kapaya Vivi na Chibanda Sonny
(waimbaji)
Bendi
ya Legho iliposambaratika, Mwaole akaenda kujiunga na Kikumbi Mwanza Mpango
‘King Kiki’ na bendi yake ya La Capitale, wakati huo akipiga muziki katika jiji la Mbeya mwaka 1992.
Nyota
yake ikamuangazia zaidi kwani mwezi Januari 1993 alijiunga katika bendi ya
Washirika ‘Watunjatanjata’ Bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki wakubwa ambao
waliweza kumsaidia kuinua kipaji chake cha kuimba.
Aliwataja
wanamuziki hao kuwa ni pamoja na Madaraka Morris, Adam Bakari ‘Sauti ya zege’,
Eddy Sheggy na Christian Sheggy na Muhina Panduka’ Toto tundu’
Hapo
napo akaona hapatoshi, akajiengua kati ya mwaka 1993 hadi 1995 alipiga katika
bendi ya Tanza Muzika iliyokuwa ikimilikiwa na Elvis Musiba. Elvis Musiba kwa
vijana wa zamani watamkumbuka kwa utunzi wake wa kitabu chake cha ‘Simu ya
Kifo’
Anafafanua
kuwa katika bendi hiyo aliwakuta wanamuziki wenye asili ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo,
François Makassy ‘Makassy Junior’,
Kasongo Ilunga, na Chibanda Sonny. François Makassy ni mtoto wa Mzee Kitenzogu Makassy.
Msemo
usemao kwamba ‘Wazee dawa’ Sauda Mwaole alioufanyia
kazi pale alipoamua kwenda kuchota mawazo, fikra na ujuzi toka kwa wazee wa bendi ya Shikamoo Jazz ya jijini Dar es Salaam.
Wanamuziki
wazee aliowakuta katika bendi hiyo anawataja baadhi yao kwamba ni akina Salimu Zahoro, John
Simon, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Majengo Selemani.
Akiwa
na Shikamoo Jazz, alibahatika kusafiri akiambatana na bendi hiyo iliyofanya
ziara na kupiga muziki katika mji wa Kampala
nchini Uganda.
Miezi
sita ilitosha kuyapata aliyoyadhamiria, hivyo aliondoka kwa wazee wa Shikamoo Jazz na kutimkia bendi ya Matimila ya
Dokta Remy Ongalla kwa kipindi kifupi
kabla ya kujiunga na bendi ya Binti ya Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, Taji Mbaraka.
Sifa
zake za kupitia Jeshi la Polisi zilipelekea yeye apate kazi kiulaini katika
bendi ya Magereza, Februari 1998. Akiwa
Magereza Jazz alitoka na wimbo wake wa ‘Samahani Baba watoto’ akishirikiana
kuimba na akina Makoye Kwirukwira, Sharifa Bernard na wengine.
Sauda
katika juhudi za kuhangaika kutafuta kujiendeleza zaidi katika tasnia ya muziki, alikwenda kujiunga na bendi ya Vijana
Jazz anayomilikiwa na Jumuiya ya Vijana Tanzania, ambako alikutana na
waimbaji ambao anasema nao walimuongezea chachu katika kipaji chake cha kuimba.
Anawataja
wanamuziki hao kuwa ni Suleiman Mbwembwe, Freddy Benjamin, Abdallah Mgonahanzelu,
na mwana dada wakati huo Nuru Muhina’ Baby White’ Kwa upande wa ala za muziki, walikuwepo Miraji Shakashia
‘Shakazulu’ Kulwa wa Milonge, Mawazo Hunja na Rashid Pembe. Wote hao
anawashukuru kwa kumuongezea ujuzi katika muziki.
Ilikuwa
mwaka 2001 ambapo msanii maarufu wa kucheza
na Nyoka, Norbert Chenga, alipomchukuwa
mwanamama huyo kwenda kujiunga katika
kikudi cha Muungano dancing troupe.
Alipofika
hapo akaambiwa azifanyie mazoezi nyimbo za taarabu za alizokuwa akiziimba Nasma
Hamis ambaye alikuwa tayari katimkia kundi lingine.
Nyimbo
hizo anazitaja kuwa ni za ‘Mtu mzima ovyo’, ‘Hata mkisema’, ‘Sanamu ya
michelini’ na nyingine nyingi.
Kipaji
cha Sauda Mwaole kilijoinyesha mapema hapo Muungano, baada ya kuzitendea haki
nyimbo hizo. Aliweza kuziimba huku wapenzi wakisema kumbe pengo laweza kuzibika.
Aliimba nyimbo zote za Nasma pasipo mtu kubaini kuwa anayeimba hakuwa Nasma.
Mashabiki papo hapo walimpachika jina la Nasma Junior.
Akiwa
Muungano dancing troupe, Mwaole licha ya
kuimba taarabu pia aliweza kucheza sarakasi na ngoma za asili zalizokuwa zikichezwa
na kikundi hicho.
Mwaole
alikuwa mtafutaji ikizingatiwa msemo
usemao ‘atafutae hachoki, na akichoka kaisha pata’ Ndivyo ilivyokuwa kwa mama
huyo ambaye mwaka 2004 aliachana na Muungano baada ya kutokuelewana katika mpango
mzima wa maslahi.
Mwaka
2006 aliomba kurudi kwa King Kiki ‘Bwana Mkubwa’ katika bendi ya La Capitale. Sauda alikubaliwa japo alikaa na bendi hiyo kwa
muda mfupi sana, akaamua kwenda kupiga muziki
katika hoteli mbalimbali mjini Zanzibar
mwaka 2007.
Mkataba
ulipomalizika huko Zanzibar,
alikwenda katika bendi ya Bana Maquis inayoongozwa na Thsimanga Kalala Assosa
ambako aliungana na mwimbaji mkongwe Abubakar Kasongo Mpainda ‘Clayton’
Kama
nilivyo kujuza kuwa historia ya Mwaole katika mzuziki haichoshi kuisikia au
kuisoma, aliitwa kujiunga na bendi ya Super Kamanyola ya jijini Mwanza ‘Rocky City’.
Huko
nako alikutana na wakali wengina katika uimbaji akina Mukumbule Lolembo
‘Parash’ na Benno Villa Anthony.
Alipiga
muziki na bendi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili baadaye akarejea katika bendi
yake ya Bana Maquis hadi kipindi hiki.
Sauda
Mwaole tayari amekwisha tengeneza album
ambayo anasema bado ipo jikoni ikikolezwa viungo kabla ya kupakuliwa hivi karibuni.
Anazitaja
nyimbo zilizo katika album hiyo kuwa ni ‘Penye penzi pana mengi’, ‘Penzi la
ukweli’, ‘Shoka la bucha’, ‘Siyo kama nina wivu’, ‘Huyu ni chaguo langu’ na
‘Sitaki visa vyako’
Mwaole alibahatika kupata watoto watatu, mmoja kati yao alitangulia mbela za
haki. Anawataja watoto walio hai kuwa ni Mariam Rashid (20) na Kassim Farid (26),
Kassim anamuelezea kuwa amefuata nyayo zake za kuimba nyimbo za muziki wa dansi,
akitumia jina la kisanii la ‘Farid Lokuwa’
Kama
mzazi, anatoa wito kwa vijana kufuata
maadili mema na kutoiga utamaduni wa nje
wa kuvaa nguo nusu uchi hadharani, kuvaa hereni na vipini kwa vijana wa kiume
na mengine mengi ya kuudhi.
“Ni
kujivunjia heshima mbele ya kadamnasi, aibu kubwa kwa jamii kwa kuwa ni
kujidharirisha pasipo sababu” kwa
masikitiko anatamka Sauda Mwaole.
Kwa
upande wa muziki wa kizazi kipya Mwaole anasema muziki wao ungelikuwa mzuri zaidi
kama baadhi yao
wasingelikuwa wanatamka maneno ya matusi katika nyimbo zao.
Anawasihi
maproduza wenye studio za kurekodi miziki, kuzichuja nyimbo za wasanii hao
pindi wanapobaini kwamba lugha iliyotumika katika nyimbo hizo haziendani na
utamaduni wa Mtanzania.
Mwisho.
Mwandishi wa makala haya anapatika ka simu:
0713331200, 0784331200, 0773331200 na 0767331200
No comments:
Post a Comment