KASSIM
MPODA ‘De la Chance’ ATIMIZA MIAKA 14 KABURINI
Wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi hususani katika jiji la Dar
es Salaam, jina la Kassim Mponda ‘De la Chance’ lilikuwa maarufu mnamo miaka ya 1980 na 1990,
akipiga katika bendi za Juwata na Mlimani Park.
Mwanamuziki huyo alikuwa mpiga gitaa
mashuhuri hapa nchini, Juni mwaka huu 2016, imetimia miaka 14 tangu alipofariki
mwezi Juni 2002 akiwa katika jiji la Dar es Salaam.
Wakati wa uhai wake alijizolea sifa
lukuki kwa kulicharaza gitaa la besi na solo kwa nyakati tofauti.
Alionesha makali yake hususani
alipokuwa katika bendi ya Juwata. Gitaa lake hilo lilisikika kwenye wimbo wa
Sogea Karibu.
Katika wimbo huo Waziri Alli
alibofya kinanda kwa umahiri mkubwa sana.
Wasifu wa Mponda unaleleza kuwa alikuwa
wa kabila Kindengereko aliyezaliwa mwaka 1945, barabara ya Mwanza mjini Tabora.
Mwaka huo una historia kubwa duniani kote kwani ulikuwa mwaka ambao Vita vikuu
vya pili vya dunia vilipomalizika.
Majina yake halisi alikuwa akiitwa
Kassim Mponda Mbwana. Baba yake mzazi Mbwana Mponda aliyekuwa na asili ya
Kabila la Kindegereko toka mkoa wa Pwani. Mzee Mponda alifika Tabora na
kuwa mfanyabiashara ndogondogo.
Kassim Mponda alipata elimu ya
msingi katika shule ya Town, iliyopo mjini humo, baadaye alijiendeleza mwenyewe
kujifunza lugha ya Kiingereza.
Alifunzwa kupiga gitaa la besi akiwa
nyumbani kwa Hassani Athumani, aliyekuwa mwanamuziki katika bendi za Tabora
Jazz, Kiko Kidds, Nyanyembe Jazz na Milambo ‘ Wana Sona sona’ kwa nyakati
tofauti.
Hassan Athumani ambaye hivi sasa ni
mjasiliamali akitengeneza Samani za ndani nyumbani kwake Barabara ya Mwanza
mjini humo, aliunda kikundi kidogo cha vijana waliokuwa wanapenda kufundishwa
muziki.
Kikundi hicho kilikuwa kikipiga
muziki ‘mkavu’, vyombo vya muziki vilivyokuwa vikitumika ni magitaa makavu na
ngoma.
Baadhi ya vijana walioshiriki kwenye
kikundi hicho ni pamoja na yeye Hassani Athumani, aliyekuwa akilicharaza gitaa
la solo, Kassim Mponda akiliungurumisha gita zito la besi na ngoma zilidundwa
na Mavumbi Alli. Kwa upande wa waimbaji walikuwapo Hassani Athumani, Bozeni na
Moshi Alli.
Baadaye Mponda alikwenda kujiunga na
bendi ya Kiko Kidds, iliyokuwa ikiongozwa na Salim Zahoro, mjini Tabora. Wakati
huo huo mwalimu wake Hassani Athumani alikwenda kujiunga katika bendi ya Tabora
Jazz.
Baada ya miezi takribani mitatu,
Kassim Mponda aliicha bendi hiyo na kuchepukia katika bendi ya Tabora Jazz,
akamfuata mwalimu wake Hassani Athumani.
Akiwa katika bendi hiyo, Mponda
alionesha makali yake vilivyo kwa kuliungurumisha gitaa la besi wakati huo.
Kati ya mwaka 1968 na 1966,
aliondoka katika bendi ya Tabora Jazz, akaenda katika jiji la Dar es Salaam
ambako huko alijiunga katika bendi ya Western Jazz hadi mwaka 1967, aliporejea
tena Tabora.
Alipofika mjini humo alimkuta Hassan
Athumani akiwa mbioni kuanzisha bendi mpya ya Nyanyembe Jazz. Aliungana naye
kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo.
Akiwa na Nyanyembe Jazz, Mponda
ndipo alianza kupiga gitaa la solo hadi Juni 1967, alipoondoka kwenda Dodoma
kujiunga katika bendi ya Central.
Alikuwa na sifa kubwa ya utafutaji
maendeleo latika muziki hivyo baada ya miezi miwili alikwenda Dar es Salaam
kujiunga katika bendi ya Polisi Jazz. ‘Wana Vangavanga’.
Akiwa katika bendi ya Polisi Jazz
alikokutana na aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo Kassim Mapili. Licha ya kuwa
kiongzi Mapili pia alikuwa ni mtunzi, mwimbaji na uwezo mkubwa wa kupiga gitaa.
Hukaa sana katika bendi hiyo baada
ya kipindi kifupi Mponda aliondoka akaenda kujiunga katika bendi ya Vijana Jazz
iliyokuwa ikiongozwa na Hemed Maneti wakati huo.
Hata huko Viajana Jazz nako
hakutumikia kwa kipindi kirefu kwani alitimka kwenda kujiunga katika bendi ya
Safari Trippers, ambako katika wimbo wa Salama alikung’uta gitaa ‘kinoma’
likisindikiza sauti nyororo ya Marijani Rajabu wakati huo.
Baadaye akawa mmoja kati ya
wanamuziki waloihama Safari Trippers, wakaenda kuanzisha bendi ya Dar
International.
Bendi ya Juwata ‘Wana Msondo ngoma’
ilimyakuwa Kassim Mponda kuongeza nguvu katika bendi yao.
Wakati huo bendi ya Juwata ilikuwa
ikipiga kwenye ukumbi za Kigongo Bar, maeneo ya Buguruni na Argentina maeneo ya
Manzese jijini Dar es Salaam.
Mnamo miaka ya 1980 Kassim Mponda
alijiunga katika bendi ya Orchestra Mlimani Park akitokea Msondo ngoma na
baadaye alichukuliwa kwenda kupiga muziki katika bendi ya African Sound
Orchestra (Afriso Ngoma).
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na
mtunzi na mwimbaji mahiri toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lovy Longomba.
Longamba aliwahi kukiri umahiri wa
Kassim Mponda tangu akiwa katika jiji la Nairobi miaka ya 1980, alimuelezea
kuwa ni mmoja wa wapiga solo wa Kitanzania anaowaheshimu sana pamoja na kwamba
alikuwa hajawahi kukutana nae.
Sifa hizo ndizo ilielezwa kuwa
yawezekana ndio zilimfanya Lovi amchukue kujiunga katika bendi ya Afriso.
Wakati huo Lovi Longomba alikuwa ni
,wanamuziki katika bendi ya Super Mazembe, iliyokuwa na makazi yake katika
jiji la Nairobi nchini Kenya.
Kwa upande wake Mponda hakuwa
akitarajia sifa kubwa toka mwimbaji na mtunzi katika bendi ya Super Mazembe.
Akisimulia wasifu wa Mponda, Hassani
Athuani alisema kuwa kuondoka kwa Mponda katika bendi ya Juwata, kulipelekea
bendi hiyo kumchukua mwanamuziki chipukizi Abdu Ridhiwani Pangamawe kujaza
nafasi yake.
Pangamawe aliingia katika bendi hiyo
akiwa na vipaji vingi kikiwemo cha kulicharaza gitaa la solo na kubofya
kinanda. Ikumbukwe kwamba hata wakati mbofya kinanda wa bendi hiyo Waziri Alli
‘Kissinger’ alipoondoka kwenda katika bendi ya Kilimanjaro ‘Wana Njenje’,
Ridhiwani aliziba nafasi yake pasipo shaka.
Mponda aliyepachikwa jina la bandia
la ‘De la Chance’, likiwa na maana ya ‘mtu mwenye bahati’.
Ndiye aliyepiga gitaa solo katika
nyimbo nyingi ukiwemo wa wa Kiu ya Jibu, Ashibai, Sogea Karibu na vingine vingi
akiwa na bendi ya Mlimani Park Orchestra.
Nyota ya Mponda ilianza kufifia
baada ya kuondoka katika bendi ya Juwata hata alipokwenda kujiunga na bendi
za Mlimani Park, Bima Lee na hatimaye Afriso Ngoma.
Aidha gitaa lake linasikika vizuri
katika wimbo wa ‘Dawa ya Pendo ni Pendo’ uliofyatuliwa na bendi ya DDC Mlimani
Park Orchestra.
Mponda alikuwa ni miongoni mwa
wanamuziki waliochukuliwa na Shirika la Bima la Taifa kwenda kuongeza nguvu
katika bendi ya Shirika hilo ya Bima Lee Orchestra. Bima Lee ilikuwa ikitumia
mtindo wa ‘Magneto tingisha’
Baadhi ya wanamuziki alioungana nao
wakati huo walikuwa ni Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shabani Dede, Joseph
Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’, Maximilian Bushoke na wengine.
Katika wimbo wa ‘Busu pande tatu’
ulioghaniwa kwa umahiri mkubwa na Jerry Nashon, Mponda aliyelikung’uta gitaa la
rhythm linalosikika, likitanguliwa na solo la Joseph Mulenga.
Aidha kwa kipindi kifupi aliwahi
kupiga muziki katika bendi ya Shikamoo Jazz inayoongozwa na Salim Zahoro katika
jiji la Dar es Salaam.
Sifa nyingine za Mponda aliyokuwa
nayo ambayo wanamuziki wengine wameikosa ni utanashati wake. Alikuwa akionekana
maridadi muda na popote utakapokutana naye.
‘De la Chance’ alikuwa akipendelea
kuvaa kofia ya aina ya ‘Kapelo’, wakati akishika ‘mpini’ alikuwa akifuata
miserebuko ya mashabaki utadhani anawaona rohoni.
Faida ya kuwa na mtoto mwenye hekima
aliionja pale mwanae mmoja alipoamua kumnunulia vyombo va muziki
vilivyomuwezesha kuanzisha bendi yake ya Afriswezi.
Bendi hiyo iliwahi kufanya ziara
mkoani Lindi ambako mara walipowasili mjini humo, Mponda alipatwa na matatizo
ya kuziba mkojo yaliyopelekea kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Lindi
wakati huo.
Juhudi za kumtibu ziliedelea hata
kupelekwa Kisiwani Mafia, mkoani Pwani kwa matibabu zaidi. Hata hivyo
ilishindikana akarejeshwa jijini Dar es Salaam, ambako aliendelea kupatiwa tiba
japo hazikumsaidia hatimaye mwaka 2002, akafariki.
Mungu ailaze roho yake pahala pema
peponi, Amina.
Mwandishi wa makala haya anapatikana
kwa namba 0784331200 na 0767331200.
No comments:
Post a Comment