Saturday, May 28, 2016

VICKY LONGOMBA ALIYEZALISHA VIPAJI VYA MUZIKI KATIKA FAMILIYA YAKE.

VICKY LONGOMBA ALIYEZALISHA VIPAJI VYA MUZIKI KATIKA FAMILIYA YAKE.

Huko nyuma niliwahi kuandika makala ikielezea familiya zilizojaliwa kuwa na vipaji katika fani mbalimbali.

Nilizitaja familiya hizo kuwa ni Uvuruge, Matumla na ile iliyouda kundi la Jackson Five na ile ya mzee Williams iliyo na nyota wa mchezo wa mpira wa tennis Venus na Serena Williams wa kutoka nchini Marekani.  

Makala haya yanamzungumzia mwanamuziki Vicky Longomba, aliyeweza kuibua vipaji vya muziki katika familiya yake vya Livi Longomba na Awilo Longomba.

Jina la Longomba halitakuwa geni kabisa kufuatia umaarufu wa wanamuziki waliomo katika familiya hiyo. 

Lovi Longopmba alikuwa kaka wa wanamuziki machachari Awilo Longomba ambaye kabla ya kuhodhi bendi yake alikuwa mcharazaji hodari wa drums katika bendi mbalimbali nchini humo na hatimaye akanza kutunga na kuimba.

Lovy naye pia alikuwa baba wa familiya yenye watoto wanamuziki akiwemo binti yake aliyerithi uimbaji, Elly Longomba na mapacha Christian na Lovy ambao wote ni nyota katika muziki  wa Hip-hop, wakimiliki Kampuni ya ‘Longambas’ huko Nairobi, nchini Kenya.

Vicky Longomba wasifu wake unaeleza kuwa majina yake kamili alikuwa ikiitwa Victor Besange Lokuli. 

Wengi walimjuwa kama ‘Vicky’.
Alikuwa mwanamuziki mahiri akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR) na kiongozi thabiti wa bendi yake.

Vicky alizaliwa mapema Desemba 13, 1932 huko DRC, na kwa mapenzi ya mungu alifariki Machi 12, 1988 akiwa katika jiji la Kinshasa.

Alianza fani ya muziki mwaka 1953, katika studio ya kurekodia za CEFA katika jiji hilo la Kinshasa ambalo wakati huo lilikluwa likiitwa Leopoldville.
Vicky alikuwa mwimbaji mwenye 
sauti ya kati ya kuhamasisha, mara nyingi alishirikiana na waimbaji wengine wa studio, akina Roger Izedi na Fracois  Engbodu ambapo waliweza kujilikana kama ‘Les Trois Caballeros’ kwa tafsiri ya Kiswahili ina maana ya ‘Waungwana Waspaniola Watatu’.

Longomba aliwahi kurekodi nyimbo nyingi katika mtindo wa rumba la Kikongo na wimbo uliokuwa umeibuka wakati huo ni ule uliopewa jina la ‘Cherie Awa, ikiwa na maana ya ‘Mpenzi Awa’.
 
Aliachia wimbo mwingien wa ‘Kongo ya Sika’ ikiwa na maana ya ‘Kongo Mpya’
Vibao hivyo vilikuwa ni miongoni mwa vibao vyake vya  kwanza.
Studio ya CEFA baadaye ilijikuta ikigubikwa na janga la kufilisika mwaka 1955, Vicky alihamia katika studio nyingine ya Longisa. 

Mwaka 1955 pamoja na kwamba alikuwa akipewa kazi nyingi katika Studio hapo Franco aliunda bendi akiwa na Jean Serge Essous iliyokuwa ikipigia katika Baa ya Ok. 

Akiwa na studio hiyo mwaka 1956 aliungana na mpiga gitaa Franco Luambo Luanzo Makiadi  pamoja na wanamuziki wengine wanne wakajiunga na bendi iliyokuwa imebadilisha jina la OK. Jazz ikawa T.P.OK.Jazz kuenzi sehemu ilipoanzia bendi hiyo yaani katika Bar yenye jila la OK (OK. Bar)
Vicky Longomba akiwa na mwimbaji  Eduado Gaga ‘Edo’aliyejiunga mwaka 1957 katika bendi hiyo, wakaonekana kama ‘Pacha’ walioweka mfumo mzuri wa uimbaji wa shule ya OK. Jazz, kwenda katika huo mtindo wa rumba la Kikongo. 

Mwaka 1960 Vicky na mwanamuziki mwingine aliyejulikana kwa jina  la Brazzos walijiunga na Josepph Kabasele ‘Grand Kale’ pamoja na wasanii wengine wa bendi ya African Jazz ambayo ilikuwa bendi hasimu na ile ya T.P.OK. Jazz, wakaenda kushiriki kurekodi kwenye maonesho ya kurekodi jijini Brussels nchini Ubelgiji. 

Hiyo ilikuwa ni baadhi ya harakati za Mkutano wa kutafuta Uhuru wa Kongo kutoka wa Wabelgiji waliokuwa wakiitawala nchi yao.

Vicky alichangia kwa kisai kikubwa katika wimbo  wa Joseph Kabasele unaoitwwa ‘Independence Cha Cha’ ulikuwa mmoja wimbo ulipata umaarufu mkubwa kuliko zote nchini humo.
Alitunga nyimbo nyingine zilikiwemo za ‘Vive Lumumba Patrice’  na
‘Sentiment Emonani’.

Kuondoka kwake kwenda Ubelgiji, kuliharibu uhusiano waka na bendi ya T.P.OK. Jazz hata alivyorejea kutoka huko aliungana na Dihunga ‘Djeskain’ Armando Brazzos aliyekuwa ametoka bendi ya T.P.OK Jazz, Johnny Pinnock na Leon Bholen Bombolo wakaunda bendi yao mpya waaiita Negro Success.

Wakiwa katika bendi hiyo Vicky Longomba alikuwa akiimba na Leon ‘Bholen’ Bombolo alikuwa akisimama kwenye upigaji wa gitaa la solo.

Negro Success ikajipata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi sana.

Sifa kubwa walizipata wanamuziki wa bendi hiyo, lakini ilipotimu mwaka 1962, matatizo ndani ya bendi yakaanza kujitokeza.

Vicky Longomba na Bohlen wakawa hawaelewani tena na kusababisha  Vicky kuondoka katika bendi hiyo, akaamua kwenda kumuangukia tena Franco Makiadi aliyekuwa kiongozi wa bendi ya T.P.OK. Jazz.

Negro Success haikuteteleka iliendelea kupiga muziki licha ya kuondokewa na Vicky Longomba.

Alipokubaliwa kurudi T.P.OK.Jazz aliendelea kuchangia katika uimbaji akiwa ‘back vocal’ kando ya Franco na Edo katika vibao vilivyoweza kushika chati vya ‘Ngai Marie Nzoto Ebeba’ ikiwa na maana ya Yaani mimi Marie ambaye mwili wangu unakwisha’, ambao ilikuwa ni hadithi ya kahaba wa Kinsahasa.

Vicky aliandika nyimbo nyingi akiwa na bendi ya T.P.OK. Jazz zikiwamo za  ‘Conseil d’Ami’ ikiwa na maana ya ‘ushauri wa rafiki’ uliopigwa katika mtindo wa polepole wanye ladha ya ‘bolero’ uliokuwa unapendwa sana na Vicky Longomba.  

Franco Makiadi na Vicky walikuwa viongozi wa T.P.OK. Jazz kwa takriban mwongo mmoja hadi walipofikia maafikiano kwamba bosi mmoja angelitosha kuongoza bendi yao na Makiadi akabakia kuwa kiongozi.

Mwaka 1971 Vicky Longomba aliicha bendi hiyo na kwenda kuunda bendi iliyoipa majina ya Lovy du Zaire. 

Kufuatia weledi wake katika muziki, Vicky aliweza kuwapandisha chati wanamuziki waliokuwa bado wachanga wakati huo akina Syran M’Benza ambaye baadaye alitokea kuwa mpiga gitaa mahiri wa kundi la Quatre Etoiles.

Vicky Longomba afya yake alianza kudorora siku hadi siku kulikopelekea kufa kwa shughuli zake katika muziki mwaka 1974.

Ugonjwa wa Kisukari kilimuathiri kwa kiasi kikubwa, hadi kukaribia kukatwa mguu wake. 

Longomba baadaye alipata nafuu ya kutosha akaendelea na Urais wa chama cha Wanamuziki cha wakati huo Zaire kilichokuwa kikijulikana kama UMUZA. 

Hiyo ilikuwa mwaka 1986 ambapo aliendelea na wadhifa huo hadi kifo kilipomfika Machi 12, 1988 akiwa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Longomba wakati wa uhai wake alikuwa ni mmoja wa waimbaji waliopendwa kuliko wote nchini humo, ameacha ‘himaya’ ya tungo za nyimbo alizorekodi.

Akishirikiana na Franco, waliweza kusaidia kuijenga T.P.OK. Jazz kufikia kuwa moja ya bendi mahir kuliko zote barani Adfrika.

Nyimbo zake aliziimba kwa mtindo wa wawili wawili, akiwa na Edo, hata waliomrithi Edo zilitengeneza uimbaji halisi wa bendi yao kwa zaidi ya miongo miwili.

Rais wa wakati huo Mobutu Seseseko Wazambanga kwa kuthamini mchango wake katika utamaduni wa Kongo, alimtunuku Vicky Longomba medali ya ‘National Order of the Leopard’, ikiwa ni medali ya juu kuliko zote  huko (Zaire) wakati huo.

Baadhi ya wanafamiliya ya Vicky Longomba walifuata mkondo wa Vicky katika kupiga muziki. 

Lovi Longomba ni mmojawapo aliyewahi kupiga muziki katika bendi ya Super Mazembe nchini Kenya hata hapa nchini mwetu aliwahi kujiunda bendi yake iliyokuwa na majina ya ‘Super Lovi’. 

Lovi alifariki mwaka 1996 hapa nchini. Wanawe Lovy Christian na Lovi wameunda kikundi kiitwacho Longombas, ambacho ni maarufu nchini Kenya.

Mwisho.

No comments: