Tuesday, May 12, 2015

GWIJI LA TAARAB SITI BINTI SAADI



GWIJI LA TAARABU SITI BINTI SAADI
 
Ukitaka kuzungumzia historia ya muziki wa taarabu, jina la Siti binti Saadi kamwe haliwezi kukosa kutajwa.
Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji.Alipokuwa akiimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi.
Mama huyo ilifikia wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo Jukwaani kutumbuiza.
Alizaliwa mwaka 1880 katika kijiji cha Fumba huko visiwani Zanzibar.
Mara alipozaliwa alipewa jina la 'Mtumwa'. Hii ni kwa kuwa alizaliwa katika kipindi cha Utumwa wa Kiarabu waliomuwa wakatwala visiwa hivyo.
Jina la Siti alipewa na Kabaila mmoja wa Kiarabu wakati huo.
Baba yake bwana Saad alikuwa ni wa kabila la Kinyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga.
Wazazi wote hao walizaliwa Zanzibari. Yaelezwa kwamba hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana.
Walijishughulisha zaidi katika kilimo na ufinyanzi, kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.
Kama waswahili wasemavyo “kuzaliwa masikini si kufa masikini” Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hicho kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza.
Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo.
Alifananishwa kuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.
Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Koraani.
Mnamo mwaka 1911, aliona ni bora ahamie mjini  Unguja, ili kubooresha maisha yake zaidi. Ujio wake wa mjini humo ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la muziki wa Taarabu la ‘Nadi Ikhwani Safaa’ aliyeitwa Muhsin Ali.
Katika kipindi hicho kundi hilo ndilo lilikuwa pekee la muziki wa taarabu, lililoanzishwa na Sultani aliyekuwa akipenda starehe na anasa, bwana Seyyid Barghash Said.
‘Nadi Ikhwani Safaa’ lilikuwa ni la wanaume peke yake, wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni.
Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu.
Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa ‘Nadi Ikhwani Safaa’ ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonesho mbalimbali katika jamii.
Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika harusi na sherehe zingine mbalimbali.
Siti alikuwa ni ‘moto’ wa kuotea mbali, jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika. Punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.
Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928  Kampuni ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master's voice yenye makazi yake huko Mumbai nchini India, ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi. Hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika.
Kampuni hiyo haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo. Hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa.
Kutokana na kusambaa kwa santuri hizo, umaarufu wa Siti ulizidi kuongezeka mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibar kumuona.
Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.
Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu. Wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumpunguzia kasi hasa walitumia kigezo kwamba hakuwa na uzuri wa sura.
Nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio uliovuma sana:
    Siti binti Saadi kawa mtu lini,
    Kaja mjini na kaniki chini,
    Kama si sauti angekula nini?
Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio kwa namna hii:
   Si hoja uzuri,
   Na sura jamali,
   Kuwa mtukufu,
   Na jadi kebeli,
   Hasara ya mtu,
   Kukosa akili.
Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifuatafuata.
Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla. Katika kipindi chake watu waliokuwa matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru, halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.
Utunzi wake wa wimbo wa ‘Kijiti’ ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka Bara. Mwanamke huyo alipofika alikutana na tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda. Hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua.
Tajiri yule alishitakiwa kwa bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile. Lakini kwa vile ni tajiri huyo alitoa hongo, kesi ikawageukia wale mashahidi na wakafungwa.
Siti akatoa wimbo huu :
   Tazameni tazameni,
    Eti alofanya Kijiti,
    Kumchukua mgeni,
    Kumcheza foliti,
    Kenda naye maguguni,
    Kamrejesha maiti.
Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.
Siti aliendelea na shughuli zake za muziki hadi uzeeni. Muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert, ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita "Wasifu wa Siti binti Saadi" Wasifu huo unaonekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hicho kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.
Ilipotimu Julai 08, 1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu.
Japo pengo hilo haliwezi kuzibika, lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni marehemu Bi. Kidude.
Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake. Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.
Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi amina.

Mwisho.


BURIANI MUTOMBO LUFUNGULA 'AUDAX' NYOTA YA MAQUIS.




BURIANI MUTOMBO LUFUNGULA NYOTA YA MAQUIS.
JINA LA MWANAMUZIKI MUTOMBO LUFUNGULA ‘AUDAX’ SIYO NGENI KWA WALE WAPENZI WA MUZIKI WA DANSI ULIOKUWA UKIPOROMOSHWA NA BENDI ZA MAQUIS DU ZAIRE NA MAQUIS ORIGINAL.

MAREHEMU AUDAX ALIKUWA MMOJA KATI YA VIONGOZI NA WANAHISA  WA BENDI YA MAQUIS DU ZAIRE NA KAMPUINI YAO ORCHETSRA  MAQUIS COMPAY (OMACO).

MUTOMBO ALIITUMIKIA BENDI HIYO KWA NGUVU ZAKE ZOTE  TANGU AKIWA KIJANA HADI MAUTI YAKE YALIOMFIKA AKIWA NA MIAKA TAKRIBANI 70.
BAADA YA KUUGUA KWA KIPINDI KIREFU, HATIMAE AUDAX ALIFARIKI DUNIA USIKU WA KUAMKIA ALHAMISI YA APRILI 23, 2015 AKIWA NYUMBANI KWAKE KIMARA MICHUNGWANI JIJINI DAR ES SALAAM.

KABLA YA KUFIKWA NA MAUTI HAYO, MUTOMBO ALIKUWA AKISUMBULIWA NA UGONJWA WA KIHARUSI TANGU MWAKA 2005 YALIYOPELEKEA KUPOOZA UPANDE MMOJA WA MWILI.

ALIKUWA AKIUGUZWA NA WANAWE KATIKA KIPINDI CHOTE HICHO IKIZINGATIWA KWAMBA MKEWE, ALIKWISHA TANGULIA MBELE ZAHAKJI HATA KABLA YA YEYE KUPATWA NA MARADHI HAYO.

MARADHI HAYO YALIMFANYA ASHINDWE KUENDELEA NA SHUGHULI ZA MUZIKI.
AUDAX ALIWAHI KUFANYA MAHOJIANO NA MTANGAZAJI WA TBC ‘MANJU WA MUZIKI’ MASOUD MASOUD, AKAELEZEA HALI YAKE ILIVYO MBAYA KIMAISHA.

HAKUWA NA MSAADA WOWOTE TOKA KWA WATU ALIOKUWA AKIWATAJIA. ALISEMA NI WACHACHE SANA WALIOJARIBU KWENDA KUMJULIA HALI NYUMBANI KWAKE.

BAADA YA KIFO, MAADALIZI YA MAZIKO YAKAFANYWA NA ILIPOTIMU SIKU YA JUMAPILI YA APRILI 26, 2015, IBADA YA KUUUGA MWILI WAKE ZILIFANYWA KATIKA HOSPITALI YA MWANANYAMALA KABLA YA MWILI WAKE KUWEKWA KATIKA NYUMBA YAKE YA MILELE  KATIKA MAKABURI YA KINONDONI, JIJINI DAR ES SALAAM.

UMATI MKUBWA ULIKUSANYIKA KATIKA MAZISHI HAYO MIONGONI MWAO WAKIWA WANAMUZIKI ALIOWAHI KUFANYA NAYE KAZI.


‘AUDAX’ ATAKUMBUKWA KWA WAKAZI WENGI WA MAGOMENI MAPIPA,  MTAA WA MIKUMI AMBAKO ALIISHI KWA KIPINDI KIREFU KABLA YA KUJENGA MAKAZI YAKE HUKO KIMARA MICHUNGWANI.

AMEIGA DUNIA AKIWA NA UMRI WA MIAKA INAYOKARIBIA 70, ALIZALIWA MWAKA 1945 HUKO JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO.

LUFUNGULA AUDAX ALIKUWA MMOJA WA WANAMUZIKI WA KUNDI LA BENDI YA MAQUIS DU ZAIRE. BENDI HIYO ILITOKEA KATIKA MJI WA KAMINA, JIMBO LA SHABA, HUKO  JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO.

AWALI KUNDI HILO LILIANZA KWA KUITWA SUPER TEO, KISHA KUBADILI JINA NA KUITWA ROCKEN SUCCESS NA BAADAYE SUPER GABBY.

BENDI HIYO ILIINGIA NCHINI TANZANIA MWAKA 1972, IKIWA NA JINA LA  MAQUIS DU ZAIRE. KUNDI HILI LA AWALI LIKUWA NA WANAMUZIKI TISA.

MUTOMBO ALIKUWA MFANO WA KUINGWA NA WANAMUZIKI WENGINE WA BENDI HIYO KWA JINSI ALIVYOKLUWA AKIJITOA KWA UWEZO WAKE WOTE KUTEKELEZA  MAJUKUMU YAKE IPASAVYO.

ALIKUWA MTUNZI NA MWIMBAJI ALIYEMUDU VYEMA KULISHAMBULIA JUKWAA LA MAQUIS SAMBAMBA NA WAIMBAJI WENZAKE AKINA MBUYA MAKONGO ‘ADIOS’, MUKUMBULE LOLEMBO ‘PARASHI’, TSHIMANGA KALALA ASSOSA NA ABOUBAKAR KASONGO MPINDA.

HATA KULE MAQUIS ORIGINAL, MUTOMBO ALISHIRIKIANA VYEMA NA WAIMBAJI WENZAKE AKINA MUKUMBULE LOLEMBO PARASHI’, TSIMANGA KALALA ASSOSA, ISSA NUNDU, FREDITO ‘BUTAMU NA BOBO ‘SUKARI’

MPENDWA MSOMAJI WA MAKALA HAYA ITAKUWA  NI VIZURI UIJUE HISTORIA FUPI YA BENDI YA MAQUIS DU ZAIRE.

BENDI HIYO INAANZIA MWAKA 1960 KWA WALIOKUWA VIJANA WA WAKATI HUO KATIKA MJI WA KAMINA HUKO JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO (ZAIRE), WALIOUNGANA NA KUUNDA BENDI YAO WAKAIITA SUPER THEO.

BENDI HIYO ILITOA BURUDANI TOSHA KWA WAPENZI WA MUZIKI  WA KAMINA  NA VITONGOJI VINAVYOUZUNGUKA MJI HUO, BAADAYE WAKAIBADILISHA JINA KUWA  SUPER GABBY.

BAADAE  BENDI HIYO IKABADILI JINA KUWA ROCKEN SUCCESS. UONGOZI WA BENDI HIYO KWA KUWA NI KULETA MAGEUZI, ILIBADILI JINA TENA KUWA SUPER GABBY.

KUNDI LA HILO LILIINGIA NCHINI TANZANIA MWAKA 1972 LIKIWA NA JINA LA ORCHESTRA MAQUIS DU ZAIRE.

MAQUIS DU ZAIRE WALIPOINGIA NCHINI, KUWA WALIPIGA KATIKA KUMBI NYINGI HUSUSANI MIKUMI NA WHITE HOUSE PALE UBUNGO, JIJINI DAR ES SALAAM.

BENDI HIYO BAADAE ILIFUNGUA KAMPUNI ILIYOITWA ORCHESTRE MAQUIS COMPANY (OMACO ) IKIONGOZWA NA WANAHISA AKINA CHINYAMA CHIAZA ‘CHICHI’, CHIBANGU KATAYI ‘MZEE PAUL’, CHIMBWIZA MBANGU NGUZA ‘NGUZA VICKING’, MBUYA MAKONGA ‘ADIOS’ PAMOJA NA YEYE MUTOMBO LUFUNGULA ‘AUDAX’

KIFO CHA LUFUNGULA KIMEGEUZA HISTORIA YA WANAMUZIKI WAANZILISHI WA BENDI HIYO. KATIKA ORODHA YA HAPO JUU, NI MWANAMUZIKI CHIMBWIZA MBANGU NGUZA ‘VICKING’ NDIYE  ALIYE HAI, LICHA YA KUTUMIKIA KIFUNGO CHA MAISHA JELA.

BENDI HIYO ILIWEZA KUKONGA NYOYO ZA WAPENZI NA MASHABIKI WA MUZIKI WA DANSI WAKITUMIA MITINDO MINGI ILIYOKUWA IKIBADILIKA KILA MARA KUFUATIA UBUNIFU WA WANAMUZIKI HAO.

WALIPOTUA WKAANZA KWA MBEWEMBWE NYINGI WAKITUMIA MTINDO WA ‘CHAKULA CHAKULA KAPOMBE’ UKAJA MTINDO WA ZEMBWELA UKAFUTIWA NA ‘KAMANYOLA BILA JASHO’.

MZEE MWEMA MUDJANGA ‘MZEE CHEKECHA’ ALIKUWA KIVUTIO KIKUBWA UKUMBINI LICHA YA KAZI YAKE YA  KUPULIZA TARUMBETA, ALIWEZA KUWAINUA VITINI WAPENZI KWENDA KUCHEZA, AKITUMIA  VIBWAGIZO VYA “CHEKECHAA CHEKEEEE….  CHEKECHAAA”  “TUSANGALAA”, “AIMA IMAA”, ‘BISHE BISHEE”, “SAA… SANIFUU”,  “CHEZA KAMANYOLAA”  “CHEZA KWA MARINGO”, “ CHEZA  UKIJIDAI” NA MENGINE MENGI.

MTINDO WA OGELEA PIGA MBIZI ULITIA FORA KWA MASHABIKI AMBAO WALICHEZA MITHIRI WATU WAMO BAHARINI, BWAWANI, MTONI AMA ZIWANI WAKIONESHA JINSI YA KUOGELEA’.

KAMA ILIVYOELEZWA HAPOO JUU, MUTOMBO ALIKUWA MTUNZI MZURI WA NYIMBO. BAADHI YA NYIMBO HIZO NI PAMOJA NA ‘MPENZI LUTA’, ‘MIMI’NA NYINGINE NYINGI ALIZOTUNGA NA KUSHIRIKI KUIMBA AKIWA KATIKA BENDI YA ORCHESTRA MAQIS DU ZAIRE.

ALICHIA KIBAO KINGINE KILICHOSHIKA CHATI CHA ‘KISEMBENGO’ WAKATI HUO BENDI HIYO IKIWA NA JINA LA MAQUIS ORIGINAL.

MSOMAJI WA MAKALA HAYA NAKUOMBA NIKUKUMBUSHE BAADHI YA WANAMUZIKI WA ENZI ZA BENDI YA MAQUIS DU ZAIRE. 
ALIKUWEPO MWAMAMA TABIA MWANJELWA, ALIYEKUWA MWIMBAJI PEKEE WA KIKE WAKATI HUO. ALIIMBA PEKE YAKE KWA HISIA KALI WIMBO ULIOHUSU ‘KIFO’.

ALIIMBA HIVI. “MWISHO WA MAISHA NI KIFOOO... KWELI MAISHA NI SAFARI NDEFU.... AMBAYO HAINA MWISHOOOO.... MWISHO WAKE NI KIFOOO.....DUNIA HAINA MWISHOOO….. MWISHO WAKE NI KIFOOO....”
ULIKUWA NI WIMBO WENYE MANENO YA KUTAHADHARIFA JUU KIFO,  JAPO WATU HAWAKUTILIA MAANANI, ILA WALIKUSAKATA RUMBA PASIPO HOFU.

MAQUIS DU ZAIRE WAKATI HUO ILIKUWA IKIONGOZWA NA  CHINYAMA CHIAZA ‘CHICHI’ AKISAIDIANA NA CHIMBWIZA NGUZA MBANGU ‘VICKING’.

KULIKUWA NA MPULIZAJI TARUMBETA, MWEMA MUJANGA ‘MZEE CHEKECHA’. CHEKECHA NDIE ALIYEKUWA ‘MFOKAJI’ MAARUFU WA BENDI HIYO. NA  NKULU WABANGOI, ALIYEKUWA KIONGOZI WA WANENGUAJI.

WENGINE WALIKUWA KANKU NKASHAMA KELLY, NGOI MUBENGA,ILUNGA NGOI, KAUMBA KALEMBA, NGENDA KALONGA, MAFUMU BILALI NA KHATIBU ITEI ITEI. PALIKUWEPO NA WAPIGA GITA LA SOLO AKINA ILUNGA LUBABA NA DEKULA VUMBI KAHANGA ‘VUMBI’. ILUNGA KALONDJI, MUJOS WA BAYEKE PIA NI MIONGONI WA KIKOSI HICHO.

WALIPOKWENDA KATIKA UKUMBI WA LANG’ATA, KINONDONI, MAQUIS ORIGINAL ILIONGEZA WANAMUZIKI WATATU TOKA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO. WALIINGIA MPIGA GITA LA SOLO KIVUGUTU MOTTO NA TCHATCHO, WATUNZI NA WAIMBAJI WALIKUWA BOBO SUKARI’ NA  FREDITTO ‘BUTAMU’.
WAKIWA KATIKA UKUMBI HUO, WAKAANZISHA MITINDO YA ‘SENDEMA’ NA ‘WASHA WASHA’ .
MWISHO.
MUNGU IWEKE ROHO YA MUTOMBO LUFUNGULA ‘AUDAX’ PAHALA PEMA PEPONI, AMINA.

MWISHO.