GWIJI
LA TAARABU SITI BINTI SAADI
Ukitaka
kuzungumzia historia ya muziki wa taarabu, jina la Siti binti Saadi kamwe haliwezi kukosa kutajwa.
Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha
pekee cha uimbaji.Alipokuwa akiimba sauti
yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi.
Mama huyo ilifikia wakati ambapo
sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo Jukwaani kutumbuiza.
Mara alipozaliwa alipewa jina la
'Mtumwa'. Hii ni kwa kuwa alizaliwa katika kipindi cha Utumwa wa Kiarabu waliomuwa wakatwala
visiwa hivyo.
Jina la Siti alipewa na Kabaila mmoja
wa Kiarabu wakati huo.
Baba yake bwana Saad alikuwa ni wa
kabila la Kinyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga.
Wazazi wote hao walizaliwa Zanzibari.
Yaelezwa kwamba hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana.
Walijishughulisha zaidi katika kilimo
na ufinyanzi, kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.
Kama waswahili wasemavyo “kuzaliwa
masikini si kufa masikini” Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha
uimbaji. Kipaji hicho kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani
alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia
kuvitembeza.
Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa
na kusafiri kwa umbali maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua
kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo.
Alifananishwa kuwa na mapafu yenye
nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila
kuachia pumzi.
Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto
wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya
Koraani.
Mnamo mwaka 1911, aliona ni bora ahamie
mjini Unguja, ili kubooresha maisha yake
zaidi. Ujio wake wa mjini humo ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja
wa kundi la muziki wa Taarabu la ‘Nadi Ikhwani Safaa’ aliyeitwa Muhsin Ali.
Katika kipindi hicho kundi hilo ndilo
lilikuwa pekee la muziki wa taarabu, lililoanzishwa na Sultani aliyekuwa akipenda
starehe na anasa, bwana Seyyid Barghash Said.
‘Nadi Ikhwani Safaa’ lilikuwa ni la
wanaume peke yake, wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa
vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni.
Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee
cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki
na lugha ya kiarabu.
Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha
kwa wanamuziki wenzie wa ‘Nadi Ikhwani Safaa’ ambao bila kusita wakaanza
kufanya naye maonesho mbalimbali katika jamii.
Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa
Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika harusi na sherehe zingine
mbalimbali.
Siti alikuwa ni ‘moto’ wa kuotea mbali,
jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la
Afrika. Punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa
kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.
Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa
si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928 Kampuni
ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master's voice yenye makazi yake huko Mumbai nchini India, ilisikia
umaarufu wa Siti binti Saadi. Hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda
kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika.
Kampuni hiyo haikuweza kuamini jinsi
muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza
kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo. Hadi kufikia 1931 santuri
72,000 zilikuwa zimeuzwa.
Kutokana na kusambaa kwa santuri hizo,
umaarufu wa Siti ulizidi kuongezeka mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za
dunia walikuwa wakija Zanzibar kumuona.
Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti
hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya
kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.
Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza
wengi wenye wivu. Wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumpunguzia kasi hasa
walitumia kigezo kwamba hakuwa na uzuri wa sura.
Nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio
uliovuma sana:
Siti binti Saadi kawa mtu lini,
Kaja mjini na kaniki chini,
Kama si sauti angekula nini?
Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake,
akaona isiwe taabu akajibu shambulio kwa namna hii:
Si hoja uzuri,
Na sura jamali,
Kuwa mtukufu,
Na jadi kebeli,
Hasara ya mtu,
Kukosa akili.
Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna
yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifuatafuata.
Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza
mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla. Katika
kipindi chake watu waliokuwa matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na
walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru, halafu wewe
uliyeshitaki ndiye unayefungwa.
Utunzi wake wa wimbo wa ‘Kijiti’
ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta
mwanamke mmoja mgeni kutoka Bara. Mwanamke huyo alipofika alikutana na tajiri
mmoja ambaye alijifanya amempenda. Hivyo akamchukua na kulala naye halafu
baadaye akamuua.
Tajiri yule alishitakiwa kwa bahati
nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile. Lakini kwa vile ni
tajiri huyo alitoa hongo, kesi ikawageukia wale mashahidi na wakafungwa.
Siti akatoa wimbo huu :
Tazameni tazameni,
Eti alofanya Kijiti,
Kumchukua mgeni,
Kumcheza foliti,
Kenda naye maguguni,
Kamrejesha maiti.
Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo
zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa
ajili yake.
Siti aliendelea na shughuli zake za
muziki hadi uzeeni. Muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi
maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert,
ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita
"Wasifu wa Siti binti Saadi" Wasifu huo unaonekana kuwa ndio bora
zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hicho kinatumika kufundishia shule za sekondari
za Tanzania.
Ilipotimu Julai 08, 1950 Siti binti Saadi
alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu.
Japo pengo hilo haliwezi kuzibika,
lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia
kwake, mfano hai ni marehemu Bi. Kidude.
Hata baada ya kifo chake jina lake bado
linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake. Chama cha Waandishi wa habari
wanawake Tanzania
(TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya
Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa
Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika
mashariki kurekodi muziki katika santuri.
Mungu ailaze roho yake pahala pema
peponi amina.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment