PAPA WENDO MTUNZI WA 'MOKOLO
NAKOKUFA'
Yasemekena mwanamuziki Antoine Wendo
Kolosoy ndiye mtunzi halali wa wimbo wa Mokolo Nakokufa aliopigwa na bendi ya
African Fiesta National.
Katika makala haya itanamzungumzia
mwanamuziki nguli Antonie Wendo Kolosoy, historia ya maisha yake na
muziki.
Wasifi Wendo unaeleza kuwa alizaliwa
Aprili 25, 1925 katika Wilaya ya Mai-Ndombe Magharibi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Pamoja na kuwa alibatizwa kwa jina
la Antoine Kalosoyi, alipewa jina la Wendo kutokana na jina la mmoja wa
Watawala wa Uingereza aliyeitwa Duke of Windsor.
Hilo Windsor lilianza kubadilika na
kuwa Wendo Sor na hatimae likabakia Wendo peke yake.
Ni utaratibu wa Waafrika kuheshimu
wakubwa ndivyo ilivyokuwa kwa Wendo ambaye kwa utu uzima wake alikuja kuitwa
Papa Wendo.
Akiwa na umri wa miaka saba, baba
yake alifariki dunia. Lakini kwa mapenzi ya mungu muda mfupi baadae mama yake
ambaye nae alikuwa muimbaji akafariki pia.
Baada
ya matukio hayo makubwa, Wendo akapelekwa kuishi katika kituo cha watoto yatima
kilichokuwa kikiendeshwa na Society of the Missionaries of Africa. Alipofikisha
umri wa miaka 11 akaanza kupiga.
Alipofikisha umri kati ya miaka 12
na 13, akafukuzwa katika kituo hicho kutokana na kutunga nyimbo ambazo
hazikuwapendeza Wafadhili wake.
Wendo akaanza kupiga muziki wa
kuburudisha wasafiri katika Pantoni zilizokuwa zikifanya kazi katika Mto Kongo.
Mto Kongo ndio unaotenganisha nchi ya Kongo Brazzaville na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Kwenye mwaka 1941 alianza kupiga
muziki katika jiji la Leopordville (Kinshasa) akiwa na bendi yake ya Victoria
Bakolo.
Katika harakati za muziki
wakati huo alikutana na mmoja ya wale ndugu wawili wa Kigiriki walioanzisha
Record Label ya kwanza huko DRC, Nicolas Jeronimidis.
Walikubaliana kutoa nyimbo zake
chini ya label ya Ngoma.
Mwaka 1948 akiwa na mpiga gita Henri
Bowane, wakafyatua kibao ambacho kiliweza kupata umaarufu hata nje ya Kongo.
Kibao hicho kiliitwa Marie-Louise.
Kibao hicho kilitokea kupendwa sana
katika nchi za Afrika Magharibi.
Papa Wendo aliendelea kuimba nyimbo
nyingi kwa lugha mbalimbali ikiwemo ya Kiswahili.
Kuna kitendawili kikubwa
kilijitokeza cha nani aliyetunga wimbo wa Mokolo Nakokufa.
Kuna waliosema ni wimbo uliotungwa
na Wendo Kolosay maarufu kama Papa Wendo na aliuimba mwaka 1966 kwenye
msiba wa Paul Mwanga kule Kongo Brazzaville.
Kwa ushuhuda ni kwamba aliyempigia gita
katika wimbo huo alikuwa Honoré Liengo.
Kwa maelezo yalijiri kuhusu wimbo
huo ilikuwa kwamba Rochereau Tabu Ley alimkaribisha Papa Wendo auimbe wimbo huo
wa Mokolo Nakokufa katika bendi yake ya African Fiesta National.
Kwa kuwa Wendo alikuwa na matatizo
ya fedha wakati huo, akakubali haraka.
Tabu Ley Rochereau akamuahidi Papa
Wendo kumpa haki zake zote za utunzi.
Hatimae Rochereau akaurekodi wimbo
huo kwa jina lake na arrangement yake. Hili ni jambo ambalo hujitokeza mara
nyingi katika bendi za Afrika ambapo kiongozi huweka jina lake katika tungo
zilizorekodiwa.
Wendo aliendelea kuweko katika kundi
la African Fiesta National kwa miaka miwili mpaka pale lilipotokea tafrani
wakiwa katika jiji la Brussels nchini Ubelgiji. Bendi hiyo ilikuwa huko kwa
mwaliko wa Ubalozi wa DRC nchini humo, ambako bendi yao ikatapeliwa malipo ya
safari hiyo.
Tabu Ley Rochereau akawaacha
‘Solemba’ wanamuziki wengine huko wasijue la kufanya.
Mmoja wa wanamuziki hao Papa Wendo
ambae akaamua kuiacha bendi hiyo, akajiunga na mwanamuziki mwingine maarufu
Dewayon.
Mpaka mwaka 1990 alipokuwa akiulizwa
ni utunzi wake gani alioupenda kuliko wote, Papa Wendo daima alikuwa akisema
Mokolo Nakokufa.
Kwa
kipindi kirefu sana Wendo alipotea katika ulimwengu wa muziki. Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Laurent Kabila na baadae mwanae
Joseph Kabila kushika madaraka nchini humo, walimsaidia Papa Wendo kuanza
kurekodi tena sanjari na kuanza kufanya maonesho.
Aliwahi kufanya tamasha la MASA
Cultural Festival kabambe nchini Ivory Coast mwaka 1998, akiwa na kundi
lake alilokuwa bado akiliita Victoria Bakolo Miziki.
Onyesho lake la mwisho alilifanya
mwaka 2004 na hatimae kufariki 2008.
Mwaka
huohuo alifariki dunia Julai 28, 2008 wakati Tabu Ley alifariki Desemba 03,
2013.
Je,
wewe msomaji wa makala haya unaona ni nani mtunzi wa wimbo wa Mokolo Nakokufa?
Mungu
azilaze roho za Pawa Wendo Kalosoyi na Tabu Ley Rochereau pahala pema peponi,
Amina.
No comments:
Post a Comment