UNAMKUBUKA BINGWA WA DRUMS ABUU SEMHANDO?
Miaka, miezi, wiki na siku hazigandi. Unakaribia mwaka
wa tano sasa tangu mwanamuziki mashuhuri hapa nchini, Abuu Semhando kufariki
dunia.
Kila mwanadamu hujipangia mambo yake akitaraji
kukamilisha mipango hiyo. Lakini juhudi zote hizo hupanguliwa kwa uwezo wake
mungu, kwa kuyakatisha maisha yako hata kabla ya kutimiza ndoto alizojiwekea.
Abuu Semhando
alifariki dunia kwa ajali ya Pikipiki aliyokuwa aikiindesha mwenyewe usiku wa Jumamosi ya Desemba 18, 2010
akitokea kazini.
Semhando katika maisha yake alichangia mafanikio ya
African Star Entertainment Tanzania (ASET), kwa asilimia kubwa kutokana na
kujitoa kwa kila hali.
Alidumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo toka
alipojiunga na vijana hao wa Twanga Pepeta mwaka 1998 akitokea bendi ya Diamond
Sound wana Kibinda Nkoi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ASET Asha Baraka alimuelezea
Abuu kuwa aliitumikia Twanga kama mali yake binafsi.
Kifo cha Semhando kilimitia simanzi yeye binafsi pamoja
na wapenzi wote wa Twanga Pepeta ndani na Nje ya Nchi.
Alitamka kuwa Semhando alikuwa ni chachu ya mafanikio ya
albamu zote 10 ambazo wamezitoa kutokana na kushiriki katika kuandaa muziki na
kusimamia nidhamu ya bendi.
Kifo cha Abuu Semhando katika familia yake kilimgusa
sana binti yake Sharifa, ambaye siku ambayo alikuwa anatakiwa kufungishwa ndoa
na baba yake ndiyo mauti yalipomkuta na kufanya sherehe hizo kugeuka msiba.
Wasifu wa nguli huyo unaeleza kuwa jina lake kamili
lililkuwa Abuu Ally Semhando maarufu ‘Lokassa’ au ‘Baba Diana’
Alikuwa mcharazaji mahiri wa drum wakati huohuo alikuwa ndiye Meneja wa bendi
ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Abuu Ally Semhando “Lokassa” alizaliwa mwaka 1953 Kijiji
cha Kibanda Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
Alianza shughuli za muziki mwanzoni mwa miaka 1970 akiwa
katika bendi ya Tanga International na baadaye kwenda kuwa mmoja kati ya
waasisi wa bendi za Tanza Muzika na Orchestra Tomatoma kabla ya kutua Safari
Sound Orchestra (OSS)
Abuu Ally Semhando na Hamza Kalala ni miongoni mwa
wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Super Matimila na ndio waliomkaribisha
Mosese Fanfan na marehemu Dk. Remmy Ongala.
Baadae Semhando alijiunga na bendi ya Vijana Jazz ‘Pamba
Moto’, ambapo kwa uwezo wake wa kuongoza alikabidhiwa nafasi ya kuwa Katibu wa
bendi.
Abuu alishiriki kupiga drums kwa kiwango kikubwa katika
nyimbo nyingi ambazo ziliiletea mafaniko ya bendi hiyo.
Akiwa katika bendi hiyo, mwimbaji maarufu toka Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo Kasaloo Kyanga, alimpachika jina bandia la Lokassa.
Licha ya kuwa mpiga drums, Sembando alikuwa ni
mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa cha uongozi wa bendi (Music Band Management)
na kushiriki katika kuandaa muziki ili kuhakikisha bendi yoyote aliyopitia
inapata mafanikio. Jambo hilo lilimjengea umaarufu katika kila bendi
aliyopitia.
Historia inaonyesha kuwa kila bendi alizowahi kupitia
akiwa kiongozi baada ya kuondoka, ziliyumba na zingine kutokomea kabisa katika
medani ya muziki wa dansi.
Lakini si Matimila pekee yake hata alipokuwa na Vijana
Jazz ‘Saga Rhumba’ ambako alikuwa Katibu chini ya uongozi wa Hemed Maneti,
alikuwa mmoja wanamuziki walioshiriki katika kuiletea mafanikio kwa miaka yote
hiyo kabla ya kujiondoa.
Yaelezwa kuwa Abuu pia alikuwa muasisi wa ‘Vijana Day’.
Katika bendi hiyo ya Vijana alishiriki kwa kiwango
kikubwa kutengeneza nyimbo akiwa na waimbaji kina Hemed Maneti, Saidi Hamis,
Fred Benjamin, Cosmas Chidumule na Kida Waziri.
Aidha wapiga vyombo wakati huo walikuwa akina Kurwa wa
Milonge, Hamza Kalala, Hassan Dalali, Aggrey Ndumbalo na Disfa Semhando (mdogo
wake), aliyekuwa akiliungurumisha gitaa la besi. Alikuwepo mpiga gita la solo
Shabani Yohana “Wanted” na wengine wengi.
Akiwa na wanamuziki hao ambao ni baadhi tu ya kundi
alilokuwa nalo, walishiriki kutengeneza nyimbo kali kama ‘Bujumbura’, ‘Mary
Maria’, ‘Tambiko la Pambamoto’, ‘Mundinde’, ‘Ali Hassan Mwinyi apewe Kura za
Ndiyo’, ‘Wifi Zangu Wananinyanyasa’, Stella, ‘Penzi Haligawanyiki’ na nyingine
nyingi nzuri kupindukia.
Nyimbo hizo zilitikisa anga ya muziki chini ya uongozi
shupavu wa Hemed Maneti aliyekuwa Kiongozi, Hamza Kalala alikuwa ni Kiongozi
msaidizi na Abuu Semhando mwenyewe
aliyekuwa Katibu.
Katika kudhihirikisha uwezo aliokuwa nao alipojing’atua
Vijana Jazz, ndipo jinamizi na anguko la bendi hiyo lilipoanza kuinyemelea.
Tangu hapo bendi hiyo haijafanya vyema katika medani ya muziki nchini.
Baadhi ya wanamuziki aliofanya nao kazi walimzungumzia
marehemu Semhando akiwemo John Kitime
ambaye alisema kuwa ataendelea kumkumbuka Abuu Semhando kwa ucheshi wake, na
vilevile alimpokea na kumtafutia malazi jijini mwaka 1989, wakati anajiunga na
Vijana Jazz akitokea Tuncut Almasi ya Iringa.
Kwa upande wake mkung’utaji wa gitaa la solo Aldof
Mbinga ambaye naye alisema tasnia ya muziki wa dansi imepoteza Jemedari ambaye
alikuwa hayumbi katika misimamo yake jambo ambalo liliiletea mafanikio Vijana
Jazz akiwa Katibu na ASET.
Mbinga alifanya kazi na Semhando kwa kutengeneza albamu
ya kwanza ya Twanga Pepeta ya ‘Kisa Mpemba’ na ‘Jirani’.
Wengine waliomzungumzia marehemu ni Waziri Ally ambaye
ni mwanamuziki wa bendi The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’ akimtaja Semhando kama
nguzo iliyokatika ghafla wakati watu wakihitaji huduma na ukongwe wake katika
muziki.
Ushuhuda mwingine ulitolewa Isihaka Kibene, ambaye
alisema, Twanga Pepeta imepoteza mpiganaji na mtawala mahiri kutokana na kuwa
kiungo katika kufanya majukumu ya kila siku ya bendi. “Huyu jamaa ni rafiki
yangu sana ambaye niliwahi kufanya naye kazi kiwanda cha uchapaji cha Printpak
miaka ya 1970, na hata alipoanza shughuli za muziki tuliendelea kuwa
marafiki..." alisema Kibene.
Abuu Ally Semhando ameacha mke na watoto 10 na kaburi
lake lipo kijiji cha Kibanda Wilaya ya Muheza alipozaliwa.
Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment