Saturday, April 16, 2016

WAMKUMBUKA MKONGWE JIMMY MONIMAMBO?



WAMKUMBUKA MKONGWE JIMMY MONIMAMBO?
Wapenzi wa muziki wa dansi hapa nchini wanatakumbuka wimbo wa Sisili ulioimbwa kwa umahiri mkubwa na bendi ya Orchestra Shika Shika.
Ilikuwa ikiongozwa na mwanamuziki Jimmy ikiwa na  makao makuu yake katika jiji la Nairobi, nchini Kenya.
Shika Shika ilikuwa ikichuwana vikali na bendi zingine kubwa zikiwemo za Super Mazembe, Les Mangelepa, Baba Gaston, Les Wanyika na nyingine nyingi.
Akiwa na bendi hiyo ya Shika Shika walitoa album yao ya kwanza mwaka 1982, iliyotikisa jiji la Nairobi na mbili zaidi alizitoa mwaka uliofuatia.
Katika safu ya waimbaji alikuwepo Lovy Longomba ambae alitunga wimbo wa Tika Nalela, ulioibeba kwa kaisi kikubwa Shika Shika  na yingine zikiwemo za  "Sisili," "Amba," na "Inyo"
Wasifu wa Jimmy Monimambo anaeleza kuwa alizaliwa katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Wazazi wake wake walikuwa raia wa  Angola, waliokuwa miongoni mwa raia walioikimbia nchi yao ya Angola na kwenda kuishi nchini Kongo wakitafuta kazi.
Monimambo pia alifahamika kwa majina ya Jimmy Monimambo Mfumu Ntoto “Mfalme wa dunia”, aliyewahi kupiga muziki katika bendi ya Ochestra Maquis du Zaire, ilikuwa na makao yake makuu katika ukumbiwa wa White House , maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Baadae akajiunga katika bendi ya Orchestra  Shika Shika, pia alikwenda kujiunga katika bendi za  Special Liwanza, Boma Liwanza, na Viva Makale iliyokuwa ikiongozwa na Kalombo Mwanza George.
Baadhi ya wanamuziki waliounda Shika Shika walikuwa Jimmy Monimambo  Vicky Longomba "Lovy" na Moreno Batamba, aliyekuwa mwimbaji mwenye sauti nzito yenye mvuto. Wengine walikuwa ni pamoja na Bwami Walumona  na Kasongo Kanema.
Wengi wa wanamuziki hao kabla ya kujiunga katika bendi ya Orchestra Shika Shika walikuwa katika bendi ya Baba Gaston Nationale, iliyokuwa ikiongozwa na  Baba Gaston Ilunga wa Ilunga.
Safu hiyo ilinogeshwa zaidi na wanamuziki akina Lawi Somona, Sammy Mansita, mpiga gitaa Mwalimu Siama Matuzungidi, na aliyekuwa mcharanga  drums Lava Machine.
Hao kwa pamoja walitoka katika bendi ya Virunga iliyokuwa ikiongozwa na Samba Mapangala.
Safari ya mwanamuziki Monimambo ilimfikisha kuungana na Lovy Longomba kurekodi nyimbo katika studio iliyokuwa ikimilikiwa na bendi za Orchestra Mos Mos na Orchestra Pole Pole.
Safu ya wanamziki waliiuda bendi ya Shika Shika ilikuwa ni waimbaji Jimmy Monimambo, Dago Mayombe na Lovy Longomba wakati kwa upande wa wapiga magitaa walikuwepo Siama Matuzungidi, aliyekuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi, aliwahi kupigia katika beni ya Cavacha katika jiji la Kinshasa mnamo miaka ya 1970.

Chery Matumona,Tabu Frantal, Manitcho na kwenye besi alikuwa Silu Waba Nsilu.
Mpiga gitaa Chery Matumona  ambae baadae aliiacha bendi hiyo mwaka 1981, akaenda nchini Uganda na baadae Zambia. Hivi sasa anaishi nchini Canada.
Bendi yake Cavacha iliundwa na waimbaji  Dona Mobeti na Mopero wa Maloba. Mopero baadae aliicha bendi hiyo na kwenda kuunda kundi lake akalipa jina la Orchestra Cavacha de Mopero, ambayo nayo iliingia katika migogoro.
Hatimae nguli wa muziki huo huko DRC Franco Luambo Makiadi, aliingilia kati na kumshawishi Mopero kubuni jina jipya.
Binti ailiyekuwa akiitwa Vicky Shama Shama alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mopero wa Maloba, ambae aliamua jia la binti huyo liwe jina la bendi hiyo ikaitwa Orchestra Shama Shama.
Shama Shama iliundwa ikiwa na wanachama toka bendi ya Cavacha, ambayo hata Mopero Wa Maloba alikuwa mwimbaji katika bendi hiyo.
Bendi hiyo ya Shama Shama, alikuja kugawanyika muda mfupi kabla ya safari yao ya kwenda nchini U Uganda.
Hapo ndipo busara za Mopero zilionekana baada ya kusajili wanamuziki wengine wapya aliokwenda na Uganda.
Ule usemi kuwa “La kuvunda halina ubani” ulijionesha wazi pale bendi hiyo ikiwa nchini Uganda  ikasambaratika tena.
Mwanamuziki KoKo Zigo alimshawishi Jimmy Monimambo kuondoka nchini Uganda, wakaunda bendi ya Orchestra Kombe Kombe mwaka 1978 wakiwa na na mwimbaji Koko Zigo. Walifika nchini Kenya wakiwa na bendi hiyo mpya ya Orchestra Kombe Kombe, lakini waliingia mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi uliopo Garden Square katika jiji la Nairobi wakiwa wamebadilisha jina la bendi kuwa Orchestra Viva Makale.
Bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki mahiri waliokuwa wakitoa burudani maridadi kwa wapenzi wake. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na George Kalombo Mwanza aliyekuwa kipuliza saxophone na kuimba, Buami Walumona  na Chery Matumona walikuwa akicharaza gitaa la solo, Siama Matuzungidi, alikuwa akisimama kwa upande wa gitaa la kati la rhythm pamija na Tabu Frantal akiliungurumisha gitaa.
Wengine walikuwa akina Thomy Kabea Lomboto aliyekuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi, Coco Zigo, Moreno Batamba, Jimmy Monimambo, Tambwe Mandola wakiwa waimbaji.
Tarumbeta ilikuwa ilipulizwa na Tshamusoke na drums zilicharangwa na Lava Machine.

Jimmy Monimambo alikisha tangulia mbela za haki mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, amina.

Mwisho.


Sunday, November 1, 2015

NENE TCHAKOU MUUNGURUMISHA WA SOLO



NENE TCHAKOU MUUNGURUMISHA WA SOLO

Nene Tchakou ni jina ambalo halijazoweleka sana kwa wapenzi wengi wa muziki wa dansi. Ni mkung’utaji wa gitaa la solo aliyepitia katika bendi nyingi huko jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jina lake halisi ni Nene Mbedi, kwa sasa ni mtu mzima wa umri wa miaka 57 hivi sasa. 

Alizaliwa Februari 1957, katika eneo lililojulikana kama Banana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vipaji vingi vya wanamuziki huibukia wakati wakiwa  Kanisani  wakiimba au kupiga ala ya muziki na wengine hutokea kwenye Madrasa wakiimba Kaswida. Lakini kwa Nene Tchakou kwake ilikuwa tofauti kabisa.

Mbendi Tchakou  alianza kujihusisha na maswala ya muziki akicharaza gita kwenye kundi lililokuwa linaundwa na watoto wa Askari jijini Kinshasa.

Nuru njema ya mafanikio katika muziki ilianza kung’aa mwaka 1973 akiwa na bendi ya Bella Negrita. Mafanikio hayo yalipelekea kuanza safari ndefu ya kuzunguka kwenye bendi kadha wa kadha.

Weledi wake katika muziki alifanywa mithiri ya kito cha thamani kwa kuwa kila alikotuwa, alikubalika vilivyo.

Safari yake ya mwaka ya 1981, ilimfikisha katika kundi lililokuwa maarufu la ‘Langa Langa Stars mahali alikopewa jina la ‘Tchakou,’ likiwa na maana ya Parrot kwa lugha ya Kilingala. Kwa Kiswahili ni ndege ajulikanaye kama Kasuku.

Tchakou hakuwa mtu wa kukata tamaa wakati akitafuta mfanikio zaidi. Aliendeza safari  mwaka 1983 alipojiunga katika bendi ya Grand Zaiko, ikiwa chini ya uongozi wa Pepe Manwaku.

Alitoa mchango mkubwa mno katika bendi hiyo hususani katika e kibao cha ‘Mbongo’. Baadaye akaamua kupiga muziki akijitegemea na kufanikiwa kufyatua wimbo wa ‘Niger’ mwaka 1987.

Ni kawaida kwa wanamuziki toka nchi za Afrika ya Kati pindi wanapokaribia mafanikio, hukimbilia kwenda nje ya nchi yao. Nene naye alifanya kwenda katika jiji Paris nchini Ufaransa mwaka 1988.

Alipokuwa katika jiji hilo aliandika historia kwa kutoa mchango mkubwa kwa nguli wa muziki barani Afrika, Kofi Olomide na kutoa albamu ya ‘Papa Bonheur’.

Alipenda sana kushiriki na wanamuziki wakubwa hivyo baada ya muda alijiunga na kundi la Soukous Stars linaloongozwa na Lokassa ya Mbongo. 

Hapo walianza matayarisho ya albamu iliyokuja kutamba vilivyo ya ‘Lagos Knight’.

Utaratibu wa kushirikiana na wanamuziki wakubwa aliuendeleza ambapo kwa mara nyingine alishirikiana na mwanamuziki Lala Nomotoki (kutoka Togo) Shi Loving (Kutoka Nigeria), Papa Wemba (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, walitoa albamu ya ‘For idole.’

Ili atengeneze muziki mzuri Nene akashirikiana na mwimbaji mahiri Aurlus Mabele kutoka Congo Brazzavile, kwa pamoja wakaandaa albamu ya ‘Dossirr X’.

Nene Tchakou alitengeneza albamu yake ya kwanza akiwashirikisha Madame (Bongo), Patience Dabani (Kutoka Gabon), 3615 Code Niawu (Kutoka DRC.

Mwaka mmoja baadaye akiwa katika Jiji la California nchini Marekani, alirekodi albamu moja iliyotoka mwaka 2001.

Alimshirikisha mwimbaji wa Soukous Stars Shimmita mapema mwaka 2002, kuanzisha kundi la Afro Muzika.

Mwaka 2003 Nene Tchakou alijiunga na Lembo ya ‘Rowa Records’ kama msanii mkaazi. Huko ndiko alikotengeneza na kufyatua CD ya ‘Cesse Le Fou’ Pendin.

Tchakou vilevile anajishirikisha na kupiga muziki wa kiasili akishirikiana na wanamuziki wengine wa Kiafrika chini ya uongozi wa Injinia na Produza Rick Scott.

Nene Tchakou ameongeza idadi ya wanamuziki kwa Kiafrika wanaoishi nchini Marekani, na kwa idadi yao hadi sasa wamepatikana wanamuziki watatu.

Wanamuziki hao ni pamoja na Sam Mangwana, Diblo Dibala na  yeye Nene Tchakou.

Amesema bado wanahitaji wanamuziki wengi ili waendelee kuutangaza muziki wa Kiafrika Ulimwenguni kote.

Mwisho.





JOSEPH KABASELE ALIYETAMBA KWENYE MUZIKI WA DANSI



JOSEPH  KABASELE ALIYETAMBA KWENYE MUZIKI WA DANSI
                      

MUZIKI WA DANSI UNA HISTORIA NDEFU PIA UNA WAPENZI WENGI HAPA TANZANIA NA AFRIKA KWA UJUMLA.

PASIPO KUWATAJA BAADHI YA MAGWIJI UTAKUWA HUJAKAMILISHA HISTORIA NA MAELEZO YA MUZIKI UPASWAVYO KUSIMULIA.

JOSEPH KABASELA TSHAMA ‘GRAND KALLE’ NI MIONGONI MWA HAO ALIYEKUWA GWIJI WA MUZIKI HUO HAPA AFRIKA. 

HUYO NDIYE ALIYESAIDIA MUELEKEO WA MUZIKI WA KISASA HUKO JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO.

KABASELE 'GRAND KALLE' NDIYE ALIYEKUWA MUANZILISHI NA KIONGOZI WA BENDI YA AFRICAN JAZZ.

BENDI HIYO ILITOA WANAMUZIKI MAHIRI AKIWAMO MPIGA GITAA MAHIRI, DK. NICO KASANDA. AIDHA ILISHEHENI NGULI WENGINE AKINA TABU LEY ALIYEKUWA MTYUNZI NAMWIMBAJI WA BENDI HIYO. MPULIZAJI WA SAXOPHONE ‘MDOMO WA BATA’ MAARUFU MANU DIBANGO.

JOSEPH KABASELE ALIKUWA AKIITWA BABA WA MTINDO WA RUMBA PIA KINARA WA MUZIKI WA KIAFRIKA NA MIONGONI MWA WAIMBAJI NA WATUNZI WAKUBWA KATIKA BARA HILI LA AFRIKA YA WATU WEUSI WANAOZUNGUMZA KIFARANSA.


ALIZALIWA  KONGO - MATADI   KATIKA FAMILIA MAARUFU ILIYOMJUMUISHA JOSEPH MALULA AMBAYE ALITOKEA KUWA ASKOFU WA KANISA KATOLIKI. 

KABASELE ALIONDOKEA KUWA MIONGONI MWA WATU WA ZAMA HIZO WALIOELIMIKA. ALIMALIZA ELIMU YA SEKONDARI NA AKAAJIRIWA KAZI YA MPIGA MASHINE (TYPIST) KWENYE KAMPUNI ZA BIASHARA KATIKA JIJI LA LEOPOLDVILLE (KINSHASA).

MUZIKI ULIKUWA KAMA WITO WAKE NA AKAGUNDUA MWANYA WA KUUFUATILIA NA KWENYE MWAKA 1950 AKAWEPO KATIKA STUDIO MPYA ILIYOJULIKANA KWA JINA LA OPIKA.


KATIKA STUDIO HIYO, ALIUNGANA NA  WANAMUZIKI WA MUDA AMBAO WALIYEJULIKANA KWA JINA LA JIMMY ‘ZACHARIE ELENGA’ AMBAYE ALIKUWA NDIYE NYOTA WA WAKATI HUO. 

PIA WALIKUWEPO WAPIGA MAGITA MASHUHURI GEORGES DOULA NA ALBERT YAMBA YAMBA. BENDI HIYO HAIKUBAGUA WAPIGAJI WACHANGA AMBAO KAMA ALIVYOKUWA KWAKE YEYE, MWENYEWE WALIONA MUZIKI NDIO UFUNGUO WA MAFANIKIO BAADAYE WAKIWA NJE YA MIHANGAIKO YA KAZI NA PIA BAADA YA MAONEVU YA UKOLONI.


MSETO WA HUO KABASELE, DOULA NA YAMBA YAMBA, ULIIGWA NA BENDI NYINGINE  ILIYOJULIKANA KWA JINA LA OTC BAADA YA KUFANYA ‘PROMOSHENI’ YA FILAMU KWA AJILI YA RADIO STESHENI YA HAPO KINSHASA AMBAYO ILIKUWA IKITUMIA HERUFI HIZO – OTC.


KABASELE ALIWEZA KUBUNI MTINDO WAKE BAADA YA KUHAMASIKA NA KUMUONA MUIMBAJI MACHACHARI ‘TINO ROSI’ AMBAYE SAUTI YAKE YA KUGHANI NA YENYE MVUTO KWENYE NYIMBO ZAKE, ILIKUWA KIVUTIO KIKUBWA KWA WAKAZI WA MJI WA KINSHASA.

‘GRAND KALLE’ NYIMBO ZAKE ZA MWANZONI ZILIZO ZILIKUWA MITHIRI YA MOTO MKALI  WA KUOTE MBALI. ILIKUWA KAZI MARIDADI ILIYOTOKANA NA MJUMUIKO WA WANAMUZIKI VIJANA WA OPIKA, HUSUSANI MPIGA GITAA DK. NICO KASANDA NA MCHEZA GITAA LA KATI (RHYTHM), KAKA YAKE NICO, CHARLES ‘DECHAUD’ MWAMBA.

WIMBO PARAFIFI ULIOFYATULIWA MWAKA 1952, ULIKUWA NA  MAUDHUI YAKE YA KUMSIFIA MTANGAZAJI WA RADIO ALIYEKUWA KONGO  BRAZZAVILLE.

UTUNZI WA KABASELE ULIOWEZA KUTIA FORA  PAMOJA NA ULE ‘KALE KATO’ WA MWAKA 1952, ULIHADITHIA JUU YA PENZI LA KABASELE KWA KIMWANA MMOJA ALIYEJULIKANA KWA JINA LA ‘KATHERINE’.

WIMBO HUO ULIKUWA WA KWANZA WA KIKONGO KUCHEZWA KWA ALA YA ‘SAXOPHONE’, IKIMTUMIA MPULIAJI WA KUAZIMA ‘FUD CANDRIX’.


KATIKA KIPINDI CHA KWENYE MIAKA YA 1953 HADI 1955 BENDI MPYA ILIYOWAJUMUISHA JOSEPH KABASELE, DK. NICO KASANDA NA DECHAUD ILIIBUKA KUTOKA KUWA WANAMUZIKI WA MUDA WA STUDIO YA OPIKA WAKAJIITA AFRICAN JAZZ, WAKIAZIMA JINA HILO AMBALO HALIKUSHABIHIYANA NA MTINDO WA MUZIKI WA KIMAREKANI WA ‘JAZZ’ KAMA JINA LILIVYO.

AFRICAN JAZZ ILIPIGA MUZIKI WA NYIMBO ZAKILATINI NA BENDI ILICHANGIA KWA KIASI KIKUBWA KUKUA KWA RUMBA LA KIKONGO LILILOIBUKA KIPINDI HICHO.


KABASELE AKAJULIKANA KAMA ILIYEJULIKANA KAMA ‘LE GRAND KALLE’, UMAARUFU WAKE UKAWA HAUNA MFANO.

WAIMBAJI WENGINE KADHAA WALIANZA KUMUIGA STAILI ZAKE KIASI KWAMBA WATU WAKAANZA KUZUNGUMZIA KUANZISHWA KWA SHULE (MCHAPUO) WA KABASELE AU WA AFRICAN JAZZ.

AIDHA BAADHI YA NYOTA WENGINE ALIOKUWA NAO KATIKA AFRICAN JAZZ WALIKUWEPO WAIMBAJI JOSEPH MULAMBA MUJOS, BOMBENGA NA MPIGA GITA TINO BAROZA AMBAPO BENDI HIYO YA AFRICAN JAZZ ILIWEZA KUWEKA FURSA NZURI KUWA NI UWANJA WA MAFUNZO KWA WANAMUZIKI VIJANA WA KIZAZI KILICHOFUATIA KONGO.

HADI KUFIKIA MWAKA 1960 AFRICAN JAZZ ILIKUWA BENDI YA JUU NCHINI HUMO NA KUWEZA KUFYATUA MAELFU KADHAA YA SANTURI ZILIZOTOLEWA KATIKA NEMBO YA ‘DECCA’ NA KUWEZA KUWAPATA MASHABIKI WENGI KATIKA KUMBI MBALI MBALI.


JOSEPH KABASELE ALIKUWA KARIBU SANA NA KUNDI LA ROCK MAMBO, HIYO ILILETA MUUNGANO MZURI NA KUNDI LAKE LA AFRICAN JAZZ.

ALISHIRIKIANA NAO NA KUWEZA KUTOA VIBAO VYENYE VIWANGO VIZURI HASA ALIPOKUWA AMESHIRIKIANA NA JEAN SERGE ESSOUS, NINO MALAPET, ROSSIGNOL NA PANDI.


ILIPOTIMU MWEZI JANUARI 1960, KABASELE NA KUNDI LAKE LA AFRICAN JAZZ PAMOJA NA WAJUMBE WAWAKILISHI WA ILIYOKUWA ‘BELGIAN CONGO’ WALIFANYA KITU CHA KIHISTORIA AMBACHO NI KONGOMANO LA UTAMBULISHO  LA KISISASA HUKO BRUSSELS.

MIONGONI MWA TUNGO ZAKE ALIZOZIFANYA KATIKA KONGOMANO HILO LA KISIASA LA MWAKA HUO, NI UTUNZI WAKE ULIOJULIKANA KAMA ‘INDEPENDENCE CHA CHA’ NA ULE WA ‘LE TABLE RONDE’ AMBAO KWA PAMOJA ULITAMBULIKA KAMA WIMBO WA KITAIFA KUFIKIA UHURU.


UTUNZI MWINGINE WA KABASELE ‘BILOMBE BA GAGNE’ (WENYE MAANA WENYE KUJIAMINI WAMESHINDA). 

WIMBO HUO ULIELEZEA MAISHA YA MADHILA CHINI YA UTAWALA WA WABELGIJI KIPINDI AMABAPO UHURU ULIBADILIKA NA KUELEKEA KWENYE VURUGU.

KABASELE ALITOA KIBAO KINGINE ‘TOYOKANA TOLIMBISANA NA KONGO’ (WENYE MAANA TUELEWANE NA TUSAMEHE YALIYOPITA) UKIHIMIZA KUUNGANA WAKONGOMANI.

MWAKA 1960 KABASELE  ALIREKODI KIBAO KILICHOJULIKANA ‘OKUKA LOKOLE’ AMBACHO NI KWA HESHIMA YA MWANAMUZIKI ‘LOUIS ARMSTRONG’ (SATCHMO) AMBAYE ALITEMBELEA KONGO KWA ZIARA ILIYODHAMINIWA NA SERIKALI YA AMERIKA.

MWAKA 1961 KUNDI LA AFRICAN JAZZ LIKIONGOZWA NA JOSEPH KABASELE LILIFANYA ZIARA NDEFU KATIKA NCHI ZA AFRIKA MAGHARIBI NA KUSAMBAZA MTINDO WAO ILIOKUWA UMECHANGANYA MAHADHI YA KIAFRIKA.

KWA WASIKILIZAJI WA CHANA, NIGERIA, IVORY COAST, SIERRA LEONE NA GUINEA ILILETA ATHARI KUBWA KWA WANAMUZIKI WA HUKO. KWA MFANO BENDI YA BEMBEYA JAZZ YA NCHINI GUINEA, ILIWEZA KUFAIDIKA KWA ZIARA HIYO YA KABASELE YA MWAKA 1961 NA KUWEZA KUZALIWA MUZIKI MCHANGANYIKO WA AFRIKA MAGHARIBI NA LATIN AMERIKA KWA KUPATIKANA MITINDO YA HIGH-LIFE, JUJU NA AFRO-BEAT.


KABASELE BAADAYE ALIIBUKA NA KUWA KIONGOZI MKALI, TABIA AMBAYO ILIPELEKEA WANAMUZIKI WOTE KUHAMA KATIKA BENDI YA AFRICAN JAZZ MWAKA 1963.

ALIJIUNGA NGUVU NA KUSHIRIKIANA NA MWIMBAJI JEAN BOMBENGA. BOMBENGA ALIKUWA MWANAFUNZI WAKE ALIYEKUWA KATIKA BENDI YA VOX AFRICA.

KUNDI HILO LA VOX AFRICA MARA NYINGINE LILITAMBULIKA KAMA AFRICAN JAZZ. 

HATA HIVYO HALIKUFANIKIWA KUFIKIA KIWANGO CHA ILIYOKUWA AFRICAN JAZZ HALISI.

BAADA YA KUNDI HILO KUFANYA KUREKODI KWAO PAMOJA NA MAONESHO KUWA MACHACHE, LILIKUFA MWAKA 1969.

BAADAYE KABASELE AKAFANYA SAFARI YA KWENDA ULAYA KUREKODI AKIWA NA KUNDI LA WANAMUZIKI WALIKUWEPO STUDIO NA KULIPA JINA ‘AFRICAN TEAM’.

KUNDI HILO LILIKUWA NA WANAMUZIKI, WAPULIZAJI WA SXOPHONE, MKAMERUNI MANU DIBANGO NA JEAN SERGE ESSOUS TOKA KONGO BRAZZAVILLE. 

ALIKUWEPO PIA MPIGA FLUTI MCUBA DON GONZALO AMBAO KWA PAMOJA WALICHEZA MIONDOKO YA AFRO-LATIN JAZZ.


MWANZONI  MWA MIAKA YA 1970, KABASELE AKAWA RAISI WA CHAMA CHA HAKI MILIKI CHA KONGO KINSHASA (SONEKA).

AIDHA ALIONEKANA JUKWAANI MARA CHACHE SANA KUTOKANA NA MARADHI YA ‘HYPERTENSION’ SUGU(SHINIKIZO LA DAMU) AMBAYO YALIMUANDAMA SANA.

ALIWAHI KWENDA PARIS MARA MBILI KWA MATIBABU AMAKO ALIKUWA AKIPATA NAFUU YA MUDA.

MWAKA 1980 KABASELE ALITUNIKIWA NISHANI YA ‘MWALIMU MKUU’ WA MUZIKI WA ZAIRE NA UMOJA WA WANAMUZIKI – UMUZA.

LAKINI KWA MAPENZI YA MUNGU, MIAKA MITATU BAADAYE FEBRUARY 11, 1983 KABASELE  AKAFARIKI  DUNIA AKIWA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO.

KABASELE ANAKUWA MMOJA WA WANAMUZIKI WAKUBWA WA KARNE YA ISHIRINI. ALIKUWA NA SAUTI PAMOJA NA STAILI KIGEZO, AMBAYO WAIMBAJI WOTE WA KONGO WANGEWEZA KUPIMWA KWA HIYO. BENDI YAKE YA AFRICAN JAZZ ILIKUWA NI MFANO KWA KILA KUNDI LA BENDI ZA WAKONGO WALIOFUATIA.

MCHANGO WAKE KATIKA MUENDELEZO WA RUMBA LA KONGO ULIWAFANYA WAKONGO WOTE KUMWITA ‘BABA WA MUZIKI WA KONGO’.

MUNGU AIPUMZISHE ROHO YAKE PAHALA PEMA PEPONI, AMINA.


 MWISHO.