Wednesday, December 24, 2014

MAJENGO ALIANZA KUPIGA MUZIKI TANGU MIAKA YA 1950

 MAJENGO ALIANZA MUZIKI MIAKA YA 1950


Majengo Bakari ni mwanamuziki aliyeuthibitisha usemi usemao kuwa “Ujuzi hauzeeki”. Alianza kupiga muziki  tangu miaka ya 1950, lakini hadi sasa anaendelea na fani hiyo.

Majengo anapiga muziki katika bendi ya Shikamoo Jazz 'Wana Chelachela Beat'.

Hilo ni kundi la muziki wa dansi lililoanzishwa mwaka 1993 kwa kujumuisha baadhi ya Wakongwe wa miondoko hiyo kutoka katika bendi nyingine kadhaa.

Wakongwe hao hufanya ‘vitu’ vyao kwa kupiga nyimbo za zamani ambazo zilitamba katika bendi zao.

Salum Zahor ni kiongozi wa bendi hiyo akiwa na nguli wenzake akina John Simon, Ally Adinani, Athuman Manicho, Kassim Mapili na wengine ambao wameshatangulia mbele za haki, akina Mohammed Tungwa, Ally Rashid, Kassim Mponda na Mariam Nylon.

Mbali ya hao, kuna mwanamuziki ambaye makala hii inamuongelea ambaye ni nguli katika upulizaji wa Saxophone ‘mdomo la Bata’ aliyepitia bendi kadha wa kadha za muziki wa dansi, Majengo Bakari.

Majengo akiwa ni mmoja wa waasisi wa Shikamoo Jazz, amechangia mafanikio makubwa ndani ya bendi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuiongezea mashabiki na kuvuta mapromota nje ya nchi.

Aliwahi kumtaja mzungu aitwaye Ronnie Graham aliyekuwa anafanyakazi katika shirika la HelpAge Tanzania, kuwa ndiye chanzo cha Shikamoo Jazz.

Ronnie akiwa HelpAge alikuwa na kamati iliyokuwa na wajumbe akina John Kitime, Mariam Hamdani na marehemu Godigodi.

Kamati hiyo  ndiyo iliyowezesha uletwaji wa vyombo vya muziki kutoka Uingereza.

Baada ya hapo Godigodi na Kitime ndio walienda nyumbani kwa Mzee Salum Zahoro huko Buguruni kumuomba akusanye wakongwe wenzake watengeneze kundi litakalokuwa chini ya Helpage.

Hii ikiwa ni njia mojawapo ya Shirika hilo kuwezesha Wazee kujitegemea.

Majengo amesema kwamba tangu ajiunge na bendi hiyo ameshasafiri nayo kwenda nchi kadhaa, zikiwamo Kenya na Uingereza.

Shikamoo Jazz awali ilikuwa na  maskani yake katika jingo la Tanzania Region, maeneo ya Faya jijini Dar es Salaam.

Baada ya kipindi Ronnie aliamua kujiengua katika bendi hiyo kutokana na vituko vilivyofanywa na mmoja wa wazee hao bendi ilipokwenda nchini Uingereza.

Kutokana na waanzilishi wengine kuwa wameshafariki, ni wanamuziki wanne tu wanaoiendesha Shikamoo Jazz Band sasa, ambao ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani na yeye mwenyewe.

Wasifu wa mwanamuziki huyu unaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya 1949 na 50.
Mwaka 1955 ilipoanzishwa shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane mwaka 1962.

Akizungumzia historia yake kimuziki, Majengo anasema kuwa, mwaka 1954 ndipo alipoanza kujiingiza kwenye fani hiyo kwa kujiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz, akiwa mkung'utaji Tumba.

Kabla ya hapo, Majengo amesema kuwa, alikuwa akipiga ngoma kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe mbalimbali za kichama, kwenye ofisi za TANU.

Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz, ni pamoja na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumnoa kwenye chombo hicho.

Ilipofika mwaka 1963, marehemu King Michael Enock aliingia Dar Jazz na kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.

Mwaka 1968 aliondoka Dar Jazz akiwa keshashiriki kupiga Saxophone kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, 'Mtoto Acha Kupiga Mayowe', akajiunga na bendi ya Wakongoman watupu iliyoitwa King Afrika.

Mwaka 1969 alijiunga na bendi nyingine ambayo nayo ilikuwa ya Wakongoman, iliyoitwa 60 Zaire.

Mwaka 1970 aliamua kujiunga katika bendi ya  Nova Success iliyokuwa ikiongozwa na Papa Micky toka Zaire wakati huo. Alishiriki kupuliza saxophone katika nyimbo kadhaa mojawapo ni Chlorida.

Aliachana na Nova Success mwaka 1974, bendi hiyo ilipopata safari ya Swaziland ambapo yeye alishindwa kwenda kutokana na ajira aliyokuwa nayo katika kiwanda cha BATA Shoes, jijini Dar es Salaam.

Alifanyakazi kazi kwenye kiwanda cha BATA tangu mwaka 1963. Mwaka 1975 aliingia katika bendi ya Maquis du Zaire 'Wana Kamanyola' iliyokuwa chini ya mpulizaji Saxophone hodari, Chinyama Chiaza. Huko alishiriki kurekodi vibao vingi vya bendi hiyo, huku mwenyewe akijisifu kazi aliyoifanya katika wimbo 'Nimepigwa Ngwala'.

Mwaka 1986 Majengo aliamua kusimama kufanyakazi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifua. Baada ya kupata nafuu alikwenda kumsaidia mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki' aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.

Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumsihi kurejea Maquis du Zaire.

Hakuwa mbishi alikubali na siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuwani.

"Nilisalimiana naye kama kawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani kupiga muziki, alinizuia akiniamuru ‘nimsujudie’ kumuomba kwa vile yeye ndiye Kiongozi. “Baada ya majibizano makali nilisusa na kusimama kupigia bendi hiyo…," amesema Majengo.
Amesema kuwa alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku moja alitembelea onesho la pamoja na Orchestra Safari Sound (OSS) 'Wana Power Iranda' na mmiliki wake alikuwa mfanyabiashara Huggo Kisima.
Kwa bahati njema Hugo alikuwemo ukumbini humo na alipomuona akamvuta kwake, na Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki katika bendi hiyo ya OSS.

Kiongozi wa bendi wakat huo alikuwa Muhidin Gurumo aliyekuwa na safu nzuri ya wanamuziki wakiwemo akina Skassy Kasambulla, Mobali Jumbe na Abdallah Kimeza, aliyekuwa akipuliza Saxophone.

Alishiriki kikamilifu  kurekodi vibao vingi akiwa na OSS. Baadhiya vibao hivyo vilikuwa vya 'POP' na 'Mbu'.

Mwaka 1990 alirudi tena Maquis na kushiriki nao hadi mwaka 1993 alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz.
Tofauti na wanamuziki wengi wenye tabia ya kuvitupia lawama kwa vyombo vya habari kuhusiana na kudidimia kwa dansi, Majengo anaweka wazi kuwa, ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo.
Majengo anasema kuwa, kila mmoja kwenye muziki wa dansi anajijali yeye mwenyewe na wanamuziki wake tu na kwamba ushirikiano uliopo ni wa mdomoni si wa vitendo.
Kwa kawaida kazi yeyote ile ni muhimu ilete faida. Kwa upande wa Majengo faida aliyonufaika nayo katika muziki anayo ielezea kuwa ni ngumu kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Yeye amefanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa familiya, Majengo Bakari anaonesha kutofurahishwa jinsi watoto wake kushindwa kurithi kazi yake ya muziki.
Majengo na mke na watoto watano, ambao ni Selemani, Kassim, Juma, Zubeda na Tunu.

Mwisho.

MIAKA 50 YA MSONDO NGOMA.

MIAKA 50 YA MSONDO NGOMA.



Bendi ya Msondo ngoma Oktoba 10, 2014 imeadhimisha miaka 50 toka ianzishwe mwaka 1964.
Mapema mwaka 1963 Muhidini Gurumo aliitwa kujiunga na NUTA Jazz akitokea katika bendi ya Rufiji Jazz, na kuwa mmoja wa waasisi wa bendi hiyo.
Katika mahojiano maalumu na Mzee Gurumo aliwahi kusema kuwa mpiga solo Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechagualiwa kuwa kiongozi wa NUTA Jazz wakati huo.

Walipoanza walikuwa chini ya udhamini wa Chama cha Wafanyakazi Tanzania (National Union of Tanzania) kwa kifupi NUTA. Hivyo bendi ikapewa jina la NUTA Jazz.
Wakati huo iliongozwa na mpuliza Tarumbeta, Joseph Lusungu akisaidiana na Mnenge Ramadhani aliyekuwa akipuliza Saxophoni ‘mdomo wa Bata’.
Miaka michache ya nyuma Chama cha Wafanyakazi kilijitoa kuidhamini na kuwaacha wanamuziki kujitegemea na sasa inaitwa Msondo Ngoma Band, ikiwa ni kuenzi mtindo ilioipa  umaarufu.
Alipojiunga  na bendi hiyo Mzee Gurumo alionesha cheche zake za kwanza kwa kurekodi nyimbo akiwa na NUTA Jazz.  Nyimbo hio zilikuwa za ‘Baba Nyerere’  uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine ni  ‘Kilimo ni Kazi yetu’ , ‘Mwengele’ na nyingine nyingi.

Nyimbo nyingine zilizotamba zilikuwa za Mpenzi Sofia, Tumeishi toka zamani, na Walinicheka. Zingine zilikuwa Aziza, Tukiwa na Monica shuleni, Sakina , Maneno ya Nyerere, Mipacha Ngui na nyingine nyingi.

Bendi hiyo baadaye ikabadili jina na kuwa ‘JUWATA Jazz’ baada ya jina la Chama cha NUTA kubadilishwa kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania JUWATA. Hivyo bendi ikawa JUWATA Jazz.

Wakati huo huo mpiga Solo Saidi Mabera alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi hi. Bendi hiyo ikatunga nyimbo nyingi kati ya miaka ya 1980 wakitumia mtindo wa Msondo Ngoma ‘Magoma Kita Kita’
Baadhi ya wanamuziki waliounda JUWATA ni pamoja waimbaji  Muhidin Gurumo aliyeingia katika bendi hiyo iakitokea katika bendi ya Rufiji Jazz, Hassani Rehani Bichuka, na mpiga Kinanda  Waziri Alli ambaye hivi sasa ni mmoja kati ya viongozi wa bendi ya The Kilimanjaro Band. (Wana Njenje).
Ushindani kati ya bendi za muziki wa dansi ulipoongezeka, wanamuziki wawili Muhidini Gurumo na  Hassani Rehani Bichuka waliiacha bendi hiyo na kwenda kujiunga na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra.
Mzee Gurumo alirejea tena JUWATA mwaka 1991 akateuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo. Nyimbo walizotoka nazo zilikuwa za Nidhamu ya kazi, Ete, Queen Kasse, Mariamu ninakujibu, Usia wa baba, Msafiri kafiri, Tupa tupa, Ndugu Kassimu na nyingine lukuki.

Baadaye bendi hiyo ilibadilishwa tena jina na kuwa OTTU Jazz kufuatia kubadilika kwa jina la Chama cha Wafanyakazi JUWATA kuwa OTTU.
OTTU Jazz au kwa jina lingine wakajiita ‘Baba ya Muziki’ ilitikisa jiji la Dar es Salaam na sehemu nyingine hapa nchini na kuwa tishio kwa bendi zingine.
Wakiwa Dar es Salaam walikuwa wakipiga muziki kwenye ukumbi wa Amana uliopo Ilala. Ilisheheni wanamuziki kabambe akina  TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’,  Athuman Momba, Abdull Ridhiwan na Roman Mng’ande ‘Romario’
Wengine ni Salehe Bangwe, na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera mpiga solo mahiri ambaye tangia ajiunge katika  bendi hiyo hajathubutu kuiondoka.
Shabani Dede alirejea tena katika bendi hiyo akitokea bendi ya Mlimani Park Orchestra (Wana Sikinde).
Kufuatia Hospitali ya Ilala kupanuka, OTTU Jazz walitakiwa kuondoka kwa kile kilichodaiwa ni kuwabughudhi wagonjwa kwa makelele ya vyombo vya muziki wao.
Walilazimika kuhamia ukumbi wa AfriCenter uliopo barabara ya Kigogo, ambako nako hawakudumu kipindi kirefu. Hivi sasa wanapiga muziki wao katika ukumbi wa Max Bar uliopo Ilala Bungoni.
Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’ na OTTU Jazz zilikuwa za Kicheko, Mawifi mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama katika dimbwi, Mti mkavu na Mizimu. Zingine ni Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la mlemavu, Piga ua talaka utatoa, Tuma, Wapambe, Asha mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya kusikitisha, Mwana mkiwa,  Kalunde, Kaza moyo, Jesca, Kwenye penzi, Binti maringo, Dalili na nyingine nyingi.
Chama cha Wafanyakazi Tanzania baadaye kijiondoa katika ufadhili wa bendi hiyo, kikawaachia vyombo wajitegemee. Walijikusanya kutengeneza mikakati na kuamua kuipa jina jipya la Msondo Ngoma Band.
Bendi ya Msondo Ngoma imesheheni wanamuziki wengi wakiwemo wa zamani na wapya, wanaofikisha idadi yao kuwa 18 na fundi mitambo mmoja.
Safu nzima ya wanamuziki hao ni Kiongozi wao ni Saidi Mabera ambaye  pia ni mpigaji wa gita la Solo. Waimbaji akaina Juma Katundu, Shabani Dede, Twaha Mohamed, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.
Wakung’utaji magita ya solo na rhythm ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge. Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’ hupiga gita la Rhythm. Kwa upande wa gita zito la besi wapo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’. Drums huchanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe. Tarumbeta hupulizwa na kijana machachari Roamn Mng’ande na Hamis Mnyupe.
Dorice George hupiga Tumba, Drums pia ni Mwimbaji wakati Amiri Said Dongo naye ni mpigaji wa Tumba.

Dorice George ni mwanamuziki mpya wa kike mwenye vipaji vingi. Ni tunda la Chuo cha Sanaa Bagamoyo, bado yupo kwenye majaribio.
Fundi wao wa mitambo anajulikana kwa jina la Mifupa.
Katika orodha ya wanamuziki wa bendi hiyo imewaacha akina Eddo Sanga ambaye ni mwimbaji na Shabani Lendi mpulizaji wa  Saxophoni, kwa kuwa kulikuwa na fununu kwamba wamejiunga na katika bendi ya Victoria Sound.


Baadhi ya wanamuziki wanaotajwa katika makala hii, wamekwisha tangulia mbele za mungu akiwemo Mzee Muhidini Gurumo. Wengine ni TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’,  Athuman Momba na mpulizaji wa saxophoni Alli Rashidi aliyefariki dunia siku ambayo bendi hiyo ikitimiza miaka 50, Oktoba 10, 2014.

Mwisho.

MUUNGURUMISHA WA SOLO NENE TCHAKOU.



MUUNGURUMISHA WA SOLO NENE TCHAKOU.

Nene Tchakou ni jina ambalo halijazoweleka sana kwa wapenzi wengi wa muziki wa dansi. Ni mkung’utaji wag it la solo aliyepitia katika bendi nyingi huko jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jina lake halisi ni Nene Mbedi, kwa sasa ni mtu mzima wa umri wa miaka 57 hivi sasa. Alizaliwa Februari 1957, katika eneo lililojulikana kama Banana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vipaji vingi vya wanamuziki huibukia wakati wakiimba Kanisani au kupiga ala ya muziki na wengine hutokea kwenye Madrasa wakiimba Kaswida. Lakini kwa Nene Tchakou kwake ilikuwa tofauti kabisa.

Mbendi Tchakou yeye alianza kujihusisha na maswala ya muziki akicharaza gita kwenye kundi lililokuwa linaundwa na watoto wa Askari jijini Kinshasa.

Nuru njema ya mafanikio katika muziki ilianza kung’aa mwaka 1973 akiwa na bendi ya Bella Negrita. Mafanikio hayo yalipelekea kuanza safari ndefu ya kuzunguka kwenye bendi kadha wa kadha.

Weledi wake katika muziki alifanywa mithiri ya Kito cha thamani kwa kuwa kila alikotuwa, alikubalika vilivyo. Safari yake ya mwaka ya 1981, ilimfikisha katika kundi lililokuwa maarufu la ‘Langa Langa Stars mahali alikopewa jina la ‘Tchakou,’ likiwa na maana ya Parrot kwa lugha ya Kilingala. Kwa Kiswahili ni ndege ajulikanaye kama Kasuku.

Tchakou hakuwa mtu wa kukata tamaa wakati akitafuta mfanikio zaidi. Aliendeza safari  mwaka 1983 alipojiunga katika bendi ya Grand Zaiko, ikiwa chini ya uongozi wa Pepe Manwaku.

Alitoa mchango mkubwa mno katika bendi hiyo hususani katika e kibao cha ‘Mbongo’. Baadaye akaamua kupiga muziki akijitegemea na kufanikiwa kufyatua wimbo wa ‘Niger’ mwaka 1987.

Ni kawaida kwa wanamuziki toka nchi za Afrika ya Kati pindi wanapokaribia mafanikio, hukimbilia kwenda nje ya nchi yao. Nene naye alifanya kwenda katika jiji Paris nchini Ufaransa mwaka 1988.

Alipokuwa katika jiji hilo aliandika historia kwa kutoa mchango mkubwa kwa nguli wa muziki barani Afrika, Kofi Olomide na kutoa albamu ya ‘Papa Bonheur’.

Alipenda sana kushiriki na wanamuziki wakubwa hivyo baada ya muda alijiunga na kundi la Soukous Stars linaloongozwa na Lokassa ya Mbongo. Hapo walianza matayarisho ya albamu iliyokuja kutamba vilivyo ya ‘Lagos Knight’.

Utaratibu wa kushirikiana na wanamuziki wakubwa aliuendeleza ambapo kwa mara nyingine alishirikiana na mwanamuziki Lala Nomotoki (kutoka Togo) Shi Loving (Kutoka Nigeria), Papa Wemba (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, walitoa albamu ya ‘For idole.’

Ili atengeneze muziki mzuri Nene akashirikiana na mwimbaji mahiri Aurlus Mabele kutoka Congo Brazzavile, kwa pamoja wakaandaa albamu ya ‘Dossirr X’.

Nene Tchakou alitengeneza albamu yake ya kwanza akiwashirikisha Madame (Bongo), Patience Dabani (Kutoka Gabon), 3615 Code Niawu (Kutoka DRC.

Mwaka mmoja baadaye akiwa katika Jiji la California nchini Marekani, alirekodi albamu moja iliyotoka mwaka 2001.

Alimshirikisha mwimbaji wa Soukous Stars Shimmita mapema mwaka 2002, kuanzisha kundi la Afro Muzika.

Mwaka 2003 Nene Tchakou alijiunga na Lembo ya ‘Rowa Records’ kama msanii mkaazi. Huko ndiko alikotengeneza na kufyatua CD ya ‘Cesse Le Fou’ Pendin.

Tchakou vilevile anajishirikisha na kupiga muziki wa kiasili akishirikiana na wanamuziki wengine wa Kiafrika chini ya uongozi wa Injinia na Produza Rick Scott.

Nene Tchakou ameongeza idadi ya wanamuziki kwa Kiafrika wanaoishi nchini Marekani, na kwa idadi yao hadi sasa wamepatikana wanamuziki watatu.

Wanamuziki hao ni pamoja na Sam Mangwana, Diblo Dibala na  yeye Nene Tchakou.

Amesema bado wanahitaji wanamuziki wengi ili waendelee kuutangaza muziki wa Kiafrika Ulimwenguni kote.

Mwisho.





Sunday, June 29, 2014

UNAMKUMBUKA SALUMU ABDALLAH WA CUBAN MARIMBA ?




UNAMKUMBUKA SALUMU ABDALLAH WA CUBAN MARIMBA ?

Morogoro, moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya 1950, 1960 na ya 1970. Watu wengi walitoka Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro.

Kati ya hizo bendi mbili shindani Morogoro Jazz na Cuban Marimba Band. Bendi ya Cuban Marimba ilikuwa ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah aliyezaliwa Mei 5, 1928, mkoani humo.

Baba yake alikuwa mwarabu na mama yake mwenyeji wa Morogoro. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule huko Dar es Salaam, maana wakati ule ililazimika kwenda Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo.  Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara.

Katika kipindi hicho Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika.

Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki.

Alitoroka hadi Mombasa ili apande Meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia Mombasa, nchini Kenya.

Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote.
Hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana.  La Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah –Band Master.

Katika kuiona Dar es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es Salaam Jazz band.

Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Nzige, Daulinge.

Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band ambalo lilianza kuwa maarufu kiasi cha kwamba mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hii.

Bendi ya Cuban Marimba ikiwa na nguli hiyo iliwahi kurekodi vibao vingi vikiwamo vya Ngoma iko huku, Naumiya, Ubaya, Nalia Nalia, Wanipendeza, Cuba Chacha na Ndiyo hali ya Dunia. Zingine ni Kazi Tanzania,Shemeji, Tanzania Twist, Sipati majibu, Salaam kwa jumla na Wanawake Tanzania. Salumu Abdalaah hakuishia hapo alitoka na vibao vingine vya Kachacha, Tulime Mashamba, Wabeberu, Kimanzi, Si kosa lako Unavunja Utu, Mpenzi Wee na Maisha matamu

Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba 1965.

Cuban Marimba Band iliendelea kupiga muziki mjini humo ikiongozwa na Juma Kilaza hadi naye alipofariki dunia.

Mwisho.

Nashukuru kupata msaada mkubwa kupitia Blog ya ‘Kijiwe cha Kitime’