MIAKA 50 YA MSONDO NGOMA.
Bendi ya Msondo ngoma Oktoba 10, 2014 imeadhimisha miaka
50 toka ianzishwe mwaka 1964.
Mapema
mwaka 1963 Muhidini Gurumo aliitwa kujiunga na NUTA Jazz akitokea katika bendi
ya Rufiji Jazz, na kuwa mmoja wa waasisi wa bendi hiyo.
Katika
mahojiano maalumu na Mzee Gurumo aliwahi kusema kuwa mpiga solo Ahmed Omar kuwa
ndiye aliyechagualiwa kuwa kiongozi wa NUTA Jazz wakati huo.
Walipoanza
walikuwa chini ya udhamini wa Chama cha
Wafanyakazi Tanzania (National Union of Tanzania) kwa kifupi NUTA. Hivyo bendi
ikapewa jina la NUTA Jazz.
Wakati huo iliongozwa
na mpuliza Tarumbeta, Joseph Lusungu akisaidiana na Mnenge Ramadhani aliyekuwa
akipuliza Saxophoni ‘mdomo wa Bata’.
Miaka
michache ya nyuma Chama cha Wafanyakazi kilijitoa kuidhamini na kuwaacha
wanamuziki kujitegemea na sasa inaitwa Msondo Ngoma Band, ikiwa ni kuenzi mtindo
ilioipa umaarufu.
Alipojiunga na bendi hiyo Mzee Gurumo alionesha cheche
zake za kwanza kwa kurekodi nyimbo akiwa na NUTA Jazz. Nyimbo hio zilikuwa za ‘Baba Nyerere’ uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kuleta
Uhuru wa Tanganyika. Nyingine ni ‘Kilimo
ni Kazi yetu’ , ‘Mwengele’ na nyingine nyingi.
Nyimbo nyingine zilizotamba
zilikuwa za Mpenzi Sofia, Tumeishi toka zamani, na Walinicheka. Zingine
zilikuwa Aziza, Tukiwa na Monica shuleni, Sakina , Maneno ya Nyerere, Mipacha
Ngui na nyingine nyingi.
Bendi hiyo
baadaye ikabadili jina na kuwa ‘JUWATA Jazz’ baada ya jina la Chama cha NUTA
kubadilishwa kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania JUWATA. Hivyo bendi ikawa
JUWATA Jazz.
Wakati huo huo mpiga Solo Saidi Mabera alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi hi.
Bendi hiyo ikatunga nyimbo nyingi kati ya miaka ya 1980 wakitumia mtindo wa Msondo Ngoma ‘Magoma Kita Kita’
Baadhi ya wanamuziki waliounda JUWATA ni pamoja waimbaji Muhidin Gurumo aliyeingia katika bendi hiyo
iakitokea katika bendi ya Rufiji Jazz, Hassani Rehani Bichuka, na mpiga
Kinanda Waziri Alli ambaye hivi sasa ni
mmoja kati ya viongozi wa bendi ya The Kilimanjaro Band. (Wana Njenje).
Ushindani kati ya
bendi za muziki wa dansi ulipoongezeka, wanamuziki wawili Muhidini Gurumo
na Hassani Rehani Bichuka waliiacha bendi
hiyo na kwenda kujiunga na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra.
Mzee Gurumo alirejea tena
JUWATA mwaka 1991 akateuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo. Nyimbo walizotoka nazo zilikuwa za Nidhamu
ya kazi, Ete, Queen Kasse, Mariamu ninakujibu, Usia wa baba, Msafiri kafiri,
Tupa tupa, Ndugu Kassimu na nyingine lukuki.
Baadaye bendi
hiyo ilibadilishwa tena jina na kuwa OTTU Jazz kufuatia kubadilika kwa jina la
Chama cha Wafanyakazi JUWATA kuwa OTTU.
OTTU Jazz au kwa
jina lingine wakajiita ‘Baba ya
Muziki’ ilitikisa jiji la Dar es Salaam na sehemu nyingine hapa nchini
na kuwa tishio kwa bendi zingine.
Wakiwa Dar es Salaam walikuwa wakipiga muziki kwenye ukumbi wa Amana uliopo
Ilala. Ilisheheni wanamuziki kabambe akina
TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustafa
John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’, Athuman Momba, Abdull
Ridhiwan na Roman Mng’ande ‘Romario’
Wengine ni Salehe
Bangwe, na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera mpiga solo
mahiri ambaye tangia ajiunge katika bendi hiyo hajathubutu kuiondoka.
Shabani Dede alirejea
tena katika bendi hiyo akitokea bendi ya Mlimani Park Orchestra (Wana Sikinde).
Kufuatia
Hospitali ya Ilala kupanuka, OTTU Jazz walitakiwa kuondoka kwa kile
kilichodaiwa ni kuwabughudhi wagonjwa kwa makelele ya vyombo vya muziki wao.
Walilazimika
kuhamia ukumbi wa AfriCenter uliopo barabara ya Kigogo, ambako nako hawakudumu
kipindi kirefu. Hivi sasa wanapiga muziki wao katika ukumbi wa Max Bar uliopo
Ilala Bungoni.
Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’
na OTTU Jazz zilikuwa za Kicheko, Mawifi mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama
katika dimbwi, Mti mkavu na Mizimu. Zingine ni Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi
la mlemavu, Piga ua talaka utatoa, Tuma, Wapambe, Asha mwana Sefu, Ajali,
Mtanikumbuka, Barua ya kusikitisha, Mwana mkiwa, Kalunde, Kaza moyo, Jesca, Kwenye penzi,
Binti maringo, Dalili na nyingine nyingi.
Chama cha Wafanyakazi Tanzania
baadaye kijiondoa katika ufadhili wa bendi hiyo, kikawaachia vyombo
wajitegemee. Walijikusanya kutengeneza mikakati na kuamua kuipa jina jipya la
Msondo Ngoma Band.
Bendi ya Msondo
Ngoma imesheheni
wanamuziki wengi wakiwemo wa zamani na wapya, wanaofikisha idadi yao kuwa 18 na fundi mitambo
mmoja.
Safu nzima
ya wanamuziki hao ni Kiongozi wao ni Saidi Mabera ambaye pia ni mpigaji wa gita la Solo. Waimbaji
akaina Juma Katundu, Shabani Dede, Twaha Mohamed,
Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.Wakung’utaji magita ya solo na rhythm ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge. Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’ hupiga gita la Rhythm. Kwa upande wa gita zito la besi wapo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’. Drums huchanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe. Tarumbeta hupulizwa na kijana machachari Roamn Mng’ande na Hamis Mnyupe.
Dorice George hupiga Tumba, Drums pia ni Mwimbaji wakati Amiri Said Dongo naye ni mpigaji wa Tumba.
Dorice George ni mwanamuziki mpya wa kike mwenye vipaji vingi. Ni tunda la Chuo cha Sanaa Bagamoyo, bado yupo kwenye majaribio.
Fundi wao wa mitambo anajulikana kwa jina la Mifupa.
Katika orodha ya wanamuziki wa bendi hiyo imewaacha akina Eddo Sanga ambaye ni mwimbaji na Shabani Lendi mpulizaji wa Saxophoni, kwa kuwa kulikuwa na fununu kwamba wamejiunga na katika bendi ya Victoria Sound.
Baadhi ya wanamuziki wanaotajwa katika makala hii, wamekwisha tangulia mbele za mungu akiwemo Mzee Muhidini Gurumo. Wengine ni TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’, Athuman Momba na mpulizaji wa saxophoni Alli Rashidi aliyefariki dunia siku ambayo bendi hiyo ikitimiza miaka 50, Oktoba 10, 2014.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment