LOVY LONGOMBA ALIYETOKEA KATIKA
FAMILIYA YA WANAMUZIKI.
“Mwana
wa Nyoka ni Nyoka…” usemi huu wa wahenga unajionesha wazi kwa baadhi ya
familiya zilizo jaaliwa vipaji vikubwa.
Kuna familiya zilizojaaliwa kuwa za wacheza
mpira wa miguu, nyavu, na michezo mingine.
Mifano halisi ni kwa wanadada wawili
Wamarekani weusi, Serena na Vunus Williams, ambao ni mabingwa Kimataifa katika
kucheza mpira wa Tennis.
Hapa nchini familya ya Uvuruge ilikuwa na
watoto waliokuwa na vipaji vya kutunga
nyimbo na kupiga muziki. Ndugu
hawa Jumanne, Stamili, Huluka na Maneno, walijijengea sifa tele katika muziki
hapa nchini.
Familiya ya akina Kihwelu nayo ilikuwa na
viaji vya kucheza mpira wa miguu, ambapo walikuwepo akina Mtwa, Jamhuri
‘Julo’ na ndugu zao wengine.
Kwa upande wa ngumi, familiya ya Matumla
imerithisha kucheza mchezo wa ndondi takribani familiya nzima.
Katika makala hii ambayo itamzungumzia
Familiya ya Longomba, toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Vicky Longomba ndye
aliye kuwa baba wa familiya ya watoto wengi waliojaaliwa vipaji vingi vya
muziki.
Huyo Mzee Vicky Longomba alikuwa mmoja kati ya wanamuziki waliokuwa
waanzilishi wa bendi ya T.P.OK. Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luanzo
Makiadi.
Pia ikumbukwe kwamba Vicky ndiye aliyekuwa
mwanzilishi wa bendi ya Lovy du Zaire, iliyotamba kwa muziki nchini
Kongo mwaka 1971.
Kwa kuwa familiya hiyo ina wanamuziki wengi
leo katika makala hii itamzungumzia mmoja wa watoto wake Lovy Longomba.
Wasifu wa mwanamuziki huyo unaelezea kwamba
alianza muziki katika bendi ya Orchestra Macchi mwaka 1976, akiwa na mwimbaji
mwenzake Dindo Yogo.
Aidha walikishirikiana na mpiga gita Nseka
Huit, waliondoka katika bendi ya Macchi na wakaunda bendi yao ya Etumba na Ngwaka wakiwa na waimbaji wengine
akina Lofanga, Gaby Yau-Yau na Mukolo, aliyekuwa akiimba sauti ya kwanza.
Wanamuziki wengine waliokuwepo katika bendi
hiyo ni pamoja na Huit Kilos, ambaye baadaye alikwenda kuwa nyota katika bendi
ya Afrisa International ya Tabu Ley Rochereau.
Mwanamziki Ricardo aliondoka na
kwenda katika bendi ya Lemvo in Makina Loca, iliyo na makao yake huko Los Angeles, Marekani.
Inaelezwa kwamba Lovy Longomba alikuwa
mtunzi na mwimbaji mahiri. Alikuwa kaka wa wanamuziki machachari Awilo Longomba.
Awilo kabla ya kuanza kutunga na kuimba, alikuwa mcharazaji hodari wa drums
katika bendi mbalimbali nchini humo.
Lovy naye pia
alikuwa baba wa familiya yenye watoto wanamuziki akiwemo binti yake aliyerithi
uimbaji, Elly Longomba na mapacha Christian na Lovy ambao wote ni nyota katika
muziki wa Hip-hop, wakimiliki Kampuni ya
‘Longambas’ huko Nairobi, nchini Kenya.
Baadaye
Agosti 1978, Lovy aliicha bendi ya Orchestra Macchi, na kuamua
kuondoka Kinshasa. Alitiga katika jiji
la Nairobi nchini Kenya ambako alijiunga katika bendi ya Les Kinois.
Kwa kuwa ‘Kiu’ chake hakikuwa kimekidhiwa,
Lovy alidumu kwa miezi mitatu pekee,
akatimkia katika bendi ya Boma Liwanza.
“Maisha ni kutafuta” mbio za kutafuta maisha
zikaendelea. Baada ya miezi sita Lovy alitimka na kuiacha Boma Liwanza,
akajiunga na bendi ya Super Mazembe iliyokuwa ikiongozwa na Mutonkole Longwa Didos.
Akiwa katika bendi hiyo alionesha uhodari wa
kutumia sauti yake ilivyokuwa nyembemba na nyororo, ambayo ndiyo iliyopelekea
kwa yeye kupachikwa jina bandia la ‘Ya Mama’. Sababu kubwa ni kwamba alikuwa na
uwezo wa kuimba sauti ya juu ambayo alipashwa aimbe mwanamke.
Katika bendi hiyo alikutana na wanamuziki wenzake mahiri akina Joseph Okello
Songa, Kasongo wa Kanema, Musa Olokwiso Mandala na Fataki Lokassa ‘Masumbuko ya
duniya’ aliyekuwa ametokea katika bendi ya Les Noirs.
Baadhi ya nyimbo alizoachia katika bendi
Super Mazembe ni pamoja na ‘Lovy’, ‘Yo mabe’, ‘Ndeko’, ‘Nanga’, ‘Mokano’ na
‘Elena’.
Sauti yake nyororo mara nyingi husikika
katika baadhi ya nyimbo za bendi hiyo, akibwagiza akitamka “Vuta sigara SM,
maana yake Super Mazembe…”
Hata hivyo umahiri wa kutunga na kuimba
katika bendi hiyo, ilisababisha kuhitajika takribani na kila bendi.
Kwa mara nyingine tena Lovy aliondoka Super
Mazembe mwaka 1981 akaenda kuimba katika bendi ya Shika Shika, iliyokuwa
ikiongoza na Jimmy Monimambo, kwa miaka miwili.
Ndoto zake za kumiliki bendi yake zilitimia
baada ya yeye na wanamuziki wenzake alipounda bendi yake Super Lovy ikiwa na
Nembo ya AIT.
Lakini kwa kile alichokieleza ni kuepuka
mkanganyiko na mvutano aliamua kutumia jina Bana Likasi wakati aliporekodi katika
Kampuni ya Audio Productions Ltd.
Akiwa na bendi hiyo, Lovy alipachikwa jina
bandia la ‘Ya Mama’ kwa kile
kilichoelezwa kwamba alikuwa anauwezo
mkubwa wa kuimba sauti nyembamba ambayo
ingelistahili kuimbwa na mwanamke.
Mnamo mwaka 1988 Lovy aliingia Tanzania
katika jiji la Dar es Salaam na akapigia katika bendi Orchestra Afriso Ngoma.
Maisha ya nguli huyo yalikatishwa ghafla
katika ajali iliyopelekea kufariki dunia nchini Tanzania mwaka 1996.
Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi,
amina.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa
namba:
0784331200, 0767331200 na 0713331200.
No comments:
Post a Comment