Wednesday, December 24, 2014

BURIANI ISSA NUNDU

 BURIANI ISSA NUNDU.
“Kwa vyovyote vile kifo hakizoweleki” usemi huu ulitamkwa na mzee Kassim Mapili katika moja ya misiba jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo nikaiweka kichwani na hivi karibuni wapenzi mashabiki wa muziki wa dansi wamempoteza mwanamuziki Issa Nundu.

Nundu alikuwa mtunzi na mwimbaji mashuhuri aliyepiga muziki katika bendi tofauti kwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hapa nchini.

Nundu aliugua maradhi yaliyopelekea kulazwa kwa kipindi kifupi katika hospitali ya KCMC ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ambako Oktoba 25, 2014 aliiga dunia.

Akizungumza kwa simu toka Stockholm nchini Sweden,  mwanamuziki Dekula Kahanga ‘Vumbi’
alimuelezea Nundu kuwa alizaliwa Julai  23, 1954 huko Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

kiwa Uvira Nundu alifanya kazi katika hospitali ya Uvira kama Mfamasia. Akiwa katika hospitali hiyo alikuwa akifanya kazi asubuhi hadi mchana, ambapo usiku alikuwa akienda kupiga muziki katika bendi ya Bavy National. 

Issa mungu  alimjaalia sauti nyororo iliyopelekea kupendwa hususani kwa wapenzi na mashabiki wa bendi ya Bavy National.

Alikuwa na uwezo wa kukariri kisha kuimba nyimbo za wanamuziki wakongwe mbalimbali zikiwemo za akina Dk. Nico Kasanda wa Afrcan Jazz.

Dekula akizungumzia wasifu wa Nundu amesema kwamba aliwahi kufanya naye kazi katika bendi mbili za Bavy National mjini Uvira DRC mwaka 1981 hadi 1983.
Nundu aliondoka Uvira huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuja Tanzania akifuatana na mtunzi na mwimbaji Kyanga Songa.

Walikutana tena katika bendi ya Maquis du Zaire mwaka1986, ambako anakiri kuwa Nundu alimpokea vizuri hadi alipoanza  na mipango ya kuhamia MK. Group 1990.

Baba yake Issa Nundu alikuwa  Chifu wa kijiji cha Nundu katika Wilaya ya Fizi Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ndiyo sababu hata alipotuwa hapa Tanzania, alitumia hadhi na kujiita ‘mtoto wa mfalme’ Prince Jaques Nundu.

Prince Nundu alipokuwa katika jiji la Dar e Salaam, aliwahi kupiga muziki katika bendi za Orchestra Makassy, Orchestra Super Matimila,  Maquis du  Zaire, MK. Group, Bana Maquis,  Super Kamanyola ya jijini Mwanza na La Capitale ‘Wazee Sugu’ inayoongozwa na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’
Prince Nundu alipokuwa katika bendi ya Makassy alikutana na waimbaji mahiri akiwemo Mbombo wa Mbomboka, Mzee Makassy na Maliki Star na wengine weingi.

Alipojiunga na bendi ya Maquis du Zaire wakati huo ikipiga katika ukumbi wa White House Ubungo, alikutana na miamba ya uimbaji akina Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mbuya Makonga ‘Adios’ Tshimanga Assosa,  Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na  Kyanga Songa.

Wengine walikuwa  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Tshimanga Kalala Assosa, Masiya Radi ‘Dikuba kuba’, Rahma Shaari, Anna Mwaole na  Mary Mwanjelwa.

Aliwahi kuimba wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Sikutegemea’ambao aliimba peke yake kwa sauti yenye simanzi tele. 

Alipokwenda katika bendi ya MK. Group iliyokuwa ikipiga muziki katika hoteli ya New Afrika, Nundu alikutana na waimbaji akiwemo kiongozi wa bendi hiyo Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’ Kapaya Vivi na wengine wengi.

Nundu alijiunga na bendi ya Bana Maquis anayoongozwa na Tshimanga Kalala Assosa, huko akakutana na waimbaji akiwemo Assosa, Anna Mwaole na Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’
Nundu alikuwa mtafutaji hivyo alichepika katika jiji la Mwanza ‘Rocky City’ akajiunga na bendi ya Super Kamanyola. Aliimba kwa kushirikiana na  mtunzi na mwimbaji mahiri Mukumbule Lolembo ‘Parashi’ na Anna Mwaole. 

Aidha ‘Vumbi’ alitaja moja ya tungo zake ni wimbo wa Marusu ambao naye alishiriki kupiga gita ka solo waliporekodi katika studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) mwaka 1989.

Hadi mauti yalipomfika alikuwa mtunzi na mwimbaji katika bendi ya La Capitale. 

No comments: