DEKULA KAHANGA “VUMBI”
Mafanikio katika maisha ni
lazima mtu kuwa na malengo, nia na dhamira ya dhati, kujiamini na hatimaye kufanya maamuzi magumu. Maneno
haya yametamkwa na mwanamuziki wa dansi Dekula Kahanga maarufu kwa jina la ‘vumbi’ambaye
safari yake ya kwenda kupiga muziki huko Ulaya ilitokea katika bendi ya Maqius
Original ya hapa Tanzania.
Moja kati ya maamuzi magumu
aliyoyafanywa mwanamuziki huyo lile la kondoka bendi hiyo iliyompa chati iliyokuwa
ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni jijini Dar
es Salaam na kutokomea hadi Sweden bila
kujua atakuwa mgeni wa nani huko ugenini.
Anaeleza kwamba hivi sasa
hajutii maamuzi yake kwa vile tayari amepata mafanikio makubwa akiwa ni pamoja
na kumiliki bendi yake iitwayo Dekula Band. Bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika
ukumbi wa Lala Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.
Bendi hiyo ina wanamuziki mahiri wenye vipaji vingi toka nchi mbalimbali hapa
duniani wakiwemo akina Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ (kuimba na Show),
Sammy Kasule (Injinia, kuimba, Bass,Drums
na Keyboard), Joe Gerald Nnaddibanga(kuimba, Conga na Show),Christina Frank, na
Marceline Kouakoua.
Wengine ni yeye Dekula
Kahanga(Solo na rhythm), Arne Winald (Keyboard) kwa pamoja huufanya muziki wao
kukubalika kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya nchi
ya Sweren zikiwemo za Ulaya, Asia, Marekani,
Japan, Falme za kiarabu na Afrika.
Anaelezea mafanikio mengine
ni kutengeneza mahusiano mema kwa baadhi ya watu toka nchi mbalimbali wanazotembelea
na sasa anaweza kuongea kwa ufasaha
lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Lingala na Kiswidish.
Dekula Kahanga ni alizaliwa Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera,
Wilaya ya Kivu Kusini mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Ni baba wa familia akiwa na mke na watoto watatu na yeye
ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa mzee Aloyce Obeid Dekula aliyekuwa
mfanyakazi wa Shirika la reli katika serikali iliyokuwa ikiongozwa na rais
Mobutu Seseseko Kuku Ng’endu wa Zabanga.
Alipata elimu Sekondari hadi
kidato cha nne karika miji Bukavu na
Uvira.
na kumaliza elimu hiyo mwaka 1979.
Mwaka uliofuatia wa 1980
safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National, na
Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa
Nundu.
Akiwa Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa
msikilizaji mzuri wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa
ikisikika vyema wakati huo na alizitamani nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na
bendi za Morogoro Jazz, Tabora Jazz, Cubzn Marimba, JUWATA Jazz, Mlimani Park
na Orchestra Safari Sound.
Anamtaja John Luanda
aliyekuwa akimiliki bendi ya Chamwino Jazz kuwa ndiye chanzo cha yeye kuingia hapa
Tanzania
baada ya kuwachukua toka Kongo yeye na wenzake akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga
na Baposta ili kujiunga katika bendi
yake iliyokuwa ikipiga muziki Manzese maeneo ya Tandale jijini Dar es Salaam.
‘Mewenye bahati habahatishi’
ndivyo anavyosema mkung’utaji huyu wa gita la Solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kwamba
mwaka 1980 alikutana na mwanamuziki Chimbwiza
Nguza Mbangu ‘Viking’ katika Ofisi za Ubalozi wa Kongo hapa nchini.
Nguza Viking
wakati huo alikuwa mpiga gita la Solo pia akiwa mmoja kati ya wanahisa na viongozi wa bendi ya Orchestra
Maquis du Zaire, hapo alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye
ukumbi wa White House uliokuwa maeneo ya Ubungo Kibo jijini Dar es Salaam.
Dekula alikubali mwaliko huo kisha
weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha kwa muda mfupi ambapo waliutumia
vyema na kuweza kuzikonga nyoyo za wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis na wapenzi wa muziki waliokuwa mamefurika wakishuhudia
vijana hao.
Baada ya kuburudisha usiku
huo hazikupita siku nyingi Dekula akaitwa
na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai (mzee Paul),
Mutombo Lufungula (Audax) na Mbuya Makonga (Adios) wakimtaka aandike barua ya
kuomba ajiunge na bendi yao kwa mkataba wa kazi isiyo na mshahara ili kuziba
nafasi ya Nguza Vicking ambaye tayari alikuwa ameanza mgomo baridi.
Naye aliona kama
ngekewa imemshukia kwa kuitwa katika bendi kubwa ya Maquis du Zaire. Hakufanya
ajizi alikubali kaunndika barua na akajiunga na bendi hiyo.
Vumbi anakumbuka siku mmoja
wakipiga muziki ukumbi wa Temeke Stereo, alimuona kwa mbali Nguza Vicking akiwa
kajibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo akisikiliza nyuzi alivyokuwa akizicharaza.
Baada ya kumuona anasema aliingiwa
na tashwishwi isiyo mfano na kujiona kama anamvunjia
heshima Nguza na kuomba ampishe ili aje kushika nafasi yake. Lakini viongozi
wake akiwemo Chibangu Katai (mzee Paul) na Ilunga Lubaba, walimtaka aendelee kupiga gita hilo.
Dekula Kahanga anasema
alimudu akizipiga nyimbo zote alizokuwa zikipigwa na Nguza zikiwemo za
Makumbele, Ngalula, Seya, Malokelee, Karubandika, Dora mtoto wa Dodoma,
Nimepigwa Ngwala na nyingine nyingi kiasi kwamba wapenzi wa muziki walishindwa kutofautisha
upigaji wa gitaa la Solo kati yake na Nguza katika mitindo yao ya Bishe bishe,
Kamanyola, Ogelea piga mbizi na Zembwela.
Aliendelea kulivurumisha gita
hadi mwisho wa onyesho na baada ya hapo
kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipokuwa kajibanza, naye
hakusita kumsifia kwa kazi nzuri.
Taharuki kati ya uongozi wa Maquis du Zaire na Nguza ziliendelea kupamba moto hatimaye aliondoka rasmi bendi
hiyo na akaanzisha bendi yake ya Orchestra Sambulumaa akiwa na wanamuziki
wengine akiwemo mwanaye Papii Kocha.
Bendi hiyo haikudumu kwa kipindi kirefu kufuatia matatizo
yaliyomikumba familia yake akiwemo yeye na watoto wake wote wa kiume kwa kufunguliwa
kesi ya ubakaji wa wanafunzi wa shule ya msingi maeneo ya Sinza jijini
Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilichukua muda
mrefu kusikilizwa hatimaye mahakama Kuu aliwatia
hatiani yeye Nguza na mwanaye Papi Kocha
na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha
maisha gerezani.
Miaka ya 1989 na 1990 Dekula alikuwa
kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis Original. Maquis Original lilikuwa jina jipya
lililo badilishwa toka Maquis du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi Lang’ata,
Kinondoni.
Dekula alivutia wapenzi wake
kwa upigaji wa gita hasa pale wimbo wa
Ngalula ulipokuwa ukipigwa huku mwimbaji
Tshimanga Kalala Assosa akimpandisha mori, akipaza sauti kwa kumuita
Vumbiii,Vumbiii,Vumbiii kila mara kama kibwagizo cha wimbo huo.
Vumbi anawakumbuka baadhi
wanamuziki aliokuwanao katika bendi ya
Maquis du Zaire na Maquis Original kwa wakati huo wakiwemo waimbaji akina Mbuya Makonga ‘Adios’
Mutombo Lufungula ‘Audax’ Mukubule Lulembo ‘Parashi’, Kiniki Kieto, Tshimanga
Kalala Assosa, Issa Nundu, Kasalo Kyanga.
Wapiga gita la Solo walikuwemo
akina Chimbwiza Nguza Mbangu”Nguza Vicking”, Ilunga Lubaba na Suleiman Mbwana
‘Cocks’.
Anawataja wapigaji wa gita la kati walikuwepo akina Mulenga Kalonji ‘Vata’ Omari
Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Gita
zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ na Mujjos
wa Bayeke.
Wapuliza midomo ya Bata walikuwa
Mafumu Billar ‘Bombenga’ Majengo Bakari,
Mukuna Roy ‘ Mukuna wa Mukuna’, Akulyake Suleiman ‘King Maluu’, Alex Kanyimbo na
Khatibu Iteitei.
Wengine anawataja Kanku Kelly Ilunga Bizoo, Mpoyo Kalenga, Kaumba Kalemba
na Ngenda Kalonga kwa upande wa Trampet na Drums walikuwepo Mbuya Makonga
‘Adios’ na Matei Joseph.
Pia hakumsahau Kiongozi wa wacheza shoo, Nkulu Wabangoi na wapiga
Tumba akina Siddy Morris na Pulukulu Wabandoki Motoo ambao wote kwa pamoja
waliifanya Maquis kuwa tishio kwa bendi zingine hapa nchini.
Dekula anaeleza kwamba alipofika
Stockholm alianza
kuchacharika mitaani akitafuta bendi ya
kupiga. Kwa bahati nzuri mwaka 1993 akakutana
na mwanamuzi toka Uganda
aitwaye Sammy Kasule nao kwa pamoja wakaamua
kuanzisha bendi yao
ikiitwa Makonde Group.
Mapema mwaka 1999, Dekula
Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia
kuna mambo’ na ‘Mpenzi Asha’
Dekula anajivunia kuwa
mwanamuziki wa kwanza mwaafrika huko Sweden
baada ya kufyatua Album iitwayo DEKULA
Sultan Qaboos, yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga, Rozina, Mambo leo na
Nostalgie nyimbo ambazo hupigwa katika vituo vingi vya redio duniani.
Usemi wa ‘Mtaka cha
Uvunguni sharti ainame’ ulimpata Dekula pale alipotaka kupata unafuu wa maisha nchini Sweden ambao ni lazima uwe raia wa
nchi hiyo. Hivyo alilazimika kuomba uraia kwa kufuata taratibu zote.
Dekula alitoa mfano wa Shubiri
kwamba ni chungu lakini ni dawa, hivyo alifikia maamuzi mengine magumu zaidi ya kuukana uraia
wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).
Hivi sasa yeye na wanamuziki
wenzake wa bendi hiyo ni raia halali wa nchi
ya Sweden
na wanaweza kusafiri kwenda nchi nyingi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo
kubughuziwa kwa kuomba VISA.
Mwanamuziki huyo ambaye kwa
tabia ni mpole japo ni mcheshi, ametoa mwito kwa Vijana chipukizi katika muziki kujifunza kupiga Ala ili wafikie
viwango vya kuwa wanamuziki na kuwaasa kaachana
na anasa za dunia sisizo na maslahi kwao.
Vilevile amewaonya kuondokana na ulevi wa sifa toka kwa washabiki ambazo huwavimbisha
vichwa na kusababisha kijisahau majukumu yaliyo mbele yao.
Dekula kwa kuona vijana wa
kizazi hiki hawana munkari wa kujifunza kupiga Ala
za muziki, ametoa ahadi kwamba atajitahidi
kwa kadri ya uwezo wake siku za usoni kuanzisha bendi hapa nchini itakayokuwa
ikitumia Ala za muziki za kisasa ili vijana wa
Tanzania
wajifunze.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment