AHMED KIPANDE NA KILWA JAZZ.
AHMEDI KIPANDE ni mwanamuziki nguli aliyeshiriki
kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigani Uhuru wa Tanganyika
akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.
Kilwa Jazz ilishiriki
kikamilifu siku Tanganyika
inapata Uhuru Decemba 09, 1961 kwa kimba wimbo wa kusifia nchi yetu kupata
Uhuru toka wa Wakoloni.
Chini ya uongozi wa Ahmedi
Kipande, Kilwa Jazz ilishiriki
kikamilifu kutoa burudani wakati mikakati ya kufanya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye meneo ya makao
makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam mwaka 1964.
Ahmedi Kipande na bendi yake
waliteuliwa na serikali ya Tanganyika
kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa nchi za Malawi
na Uganda.
Historia ya mwanamuziki huyu
iliyotolewa na mwanawe wa mwisho Kipande Ahmed, ameeleza kwamba jina kamili
la baba yake alikuwa ikiitwa Ahmed
Mohammed Kipande, aliyezaliwa mwaka 1937
huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi.
Miaka michache baada ya kifo
cha mama yake Ahmed Kipande alifuatana na Baba yake kuja Dar
es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Uhuru Wavulana ilikuwa
maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam.
Katikati ya miaka ya 1950
Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo Violin, katika bendi ya
Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidosi. Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao
hivi sasa unaitwa mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz
walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Ahmed Kipande aliyekuwa
ametoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi nae akishirikiana na mwanamuziki mwenzake
aliyetajwa kwa jina moja la Shamte nao wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka
Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958.
Kilwa Jazz ikaanza kujizolea
umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbali mbali zikiwemo za siasa, mapenzi na
za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.
Aliunga na kuimba wimbo wa
‘TANU yajenga nchi’, nchi yetu’ ‘enyi
Vijana tujenga yetu Doli na ‘It can be done, play your party’
Zingine zilikuwa za ‘Roza
waniuwa uwa’, ‘Nipate lau nafasi’, ‘Nacheka cheka Kilwa leo’ na ule wa Maneno hayafai’
Wimbo wa Nacheka cheka
ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kukopi wimbo wa Tabu Ley na John Bokelo wa ‘Mokolo nokokufa’
halikadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo na Maneno hayafai ambazo walizikopi
na kupesti toka wimbo wa Course au Povouir wa T.P.OK. Jazz.
Mwaka 1973 Kilwa jazz
ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco
Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz
iliyefanya onyesho kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Luambo Makiadi baada ya
kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake
mkubwa wa ‘kokopi na kupesti’ pasipo kukosea.
Akimsifia baba yake Kipande
Ahmed alisema kwamba mwaka 1961 siku Tanganyika inapewa Uhuru toka kwa
Wakoloni, bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa Uwanja wa taifa ikiporomosha muziki
ambapo ilitoka na wimbo wa kumshukuru
mungu kwa kupata Uhuru.
Mtoto huyo wa marehemu Ahmed,
aliimba mistari michache ya wimbo huo “ Ewe
mola tunakuomba uibariki Tanganyika
yetu na jirani zetu, Uhuru tumepata lakini
Nyoyo zina sikitika wenzetu wanateseka
Wakoloni wa mewashika…”
Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa
na makao makuu yake katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako siku moja
ilipiga muziki nje ya Ofisi yao
na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana. Lakini ilikuwa mipango
kamambe ikipangwa maeneo hayo kwa viongozi wanamapinduzi siku chache kabla ya
mapinduzi ya Zanzibar viongozi walikuwa
wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964
huko Zanzibar.
Bendi ya Kilwa Jazz baadaye haikuelewa na jamii. Wengine wakafika mbali zaidi
wakizusha maneno kwamba ni bendi ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa
burudani katika sherehe nyingi za kitaifa.
Kilwa jazz pia ilialikwa
kutoa burudani katika sherehe za ndoa ya mmoja wa mawaziri wa serikali ya Tanganyika
wakati huo, Oscar Kambona.
Ahmed Kipande katika sherehe hiyo alionesha kipaji
chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa papo kwa papo wa kuwasifia
wanandoa hao Oscar Kambona na mkewe.
Yaelezwa kwamba Kambona
aliinuka toka kwenye kiti cha maharusi na kwenda kumkumbatika Kipande kisha akamtunza
kwa pesa.
Ni miaka 27 sasa tangu Ahmedi Mohammed
Kipande afariki dunia Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa
kiharusi kwa kipindi kirefu. Alizikwa kwenye makaburi ya Tandika
Maguruwe, mkoani Dar es Salaam Aprili 28,1987. Mugu ailaze roho ya marehemu Ahmedi Kipande pahala pema peponi, Amen.
No comments:
Post a Comment