Saturday, October 10, 2015

JE, UNAFAHAMU KAMA ILIKUWEPO BENDI YA WANAWAKE NCHINI?



JE, UNAFAHAMU KAMA ILIKUWEPO BENDI YA WANAWAKE NCHINI? 

Ule usemi kwamba “Wanawake wanaweza” inaelekea kwamba ulikuwepo tangu zamani. Mnamo miaka ya 1960, hapa nchini ilianzishwa bendi ya wanawake watupu ikiwa na jina la ‘ Women Jazz Band.
Bendi hiyo haikufahamika sana kwa kuwa haikudumu sana na pia nyimbo zake hakuendelea kupigwa katika vituo vya redio licha ya kuvirekodi katika redio ya taifa wakati huo ya Radio Tanzania Dar es Salaam(RTD).
Kama ilivyo kwa historia kwamba huwa haifutiki, inaeleza kuwa mwaka 1965, kundi jipya la aina yake lilianzishwa nchini humu lilikuwa ni bendi ya akina mama watupu. Bendi hiyo iliitwa Women Jazz.
Akina mama hao wengine walikuwa ni wafanyakazi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali (Government Press), ambao walijichaguana wakaanza kuhudhuria mafunzo ya muziki chini ya yule mwanamuziki mahiri Mzee Mayagilo.
Mayagilo kipindi hicho alikuwa kiongozi wa kitengo cha muziki Brass band katika Jeshi la Polisi, waanza mazoezi kwa nguvu.

Bendi hiyo ilikuwa chini ya Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League) wakati ule. Sasa ni UVCCM.
Kina mamam hao walipokuwa wakianza shughuli hiyo walikuwa hawana ujuzi wowote wa katika muziki. Kutokana na jitihada zao wakajitengenezea utaratibu wa kuanza kufanya maonesho yao hasa kwenye hafla za serikali na Chama tawala cha TANU wakati huo.
Dhamira yao ilitimia Mei 31, 1966 ambapo bendi yao iliingia katika studio za RTD zilizopo jijini Dar es Salaam na kurekodi nyimbo zao sita.
Nyimbo hizo zilikuwa za Tumsifu mheshimiwa, Leo tunafuraha, Mwalimu kasema, Women Jazz, Sifa nyingi tuwasifu viongozi na TANU yajenge nchi.
Nathubutu kutamka kwamba nyimbo za akina mama hao hazifahamiki kwa kizazi hiki kwa kuwa hazisikika zikipigwa katika kituo cha redio chochote hata TBC taifa iliyo na maktaba kubwa ya muziki!
Ka mantiki hiyo basi itakuwa ni busura zikatumika kwa uongozi bora wa TBC Taifa, kuzikumbuka kupiga nyimbo hizo ili kuweka changamoto kwa kizazi hiki hususani kwa akina dada wanao chipukia kimuziki.
Women Jazz alikuwa ikiundwa na akina Mary Kilima, Juanita Mwegoha, Rukia Hassan na Siwema Salum ambao walikuwa waimbaji katika bendi hiyo.
Wengine ni Kijakazi Mbegu aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo, Mwanjaa Ramadhani alikuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi na Chano Mohammed, aliyekuwa akipiga gitaa la kati la rhythm.
Kwa upande wa ‘mdomo wa bata’ walikuweapo Tatu Ally na Anna Stewart waliokuwa wakipuliza Alto Saxophone wakati Mina Tumaini na Rukia Mbaraka wakipuliza Tenor Saxophone.
Mama aliyejulikana kwa jina la Lea Samuel alikuwa akichangaya Bongos, wakati huohuo Josephine James alikuwa akidunda  drums.
Miaka hiyo kulikuwa na zana nyingi za muziki tofauti na miaka hii. Kulikuwepo na chombo kikiitwa Maracass kilichokuwa ambacho katika bendi hiyo kilichezwa na Zainabu Mbwana wakati kile cha Timing alikuwepo Tale Mgongo.
Kwa wale wasioijuwa ama kukumbuka historia ya chama cha TANU, kirefu chake ni Tanganyika African National Union. Hicho ndicho kilikuwa chama kilichotawala Tanganyika na Tanzania hadi muungano wa chama hicho na Chama cha Afro-Shirazi cha Zanzibar, vilipounda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.
Chama cha TANU kilianzishwa 7 Julai, 1954, kabla yake kulikuwepo na chama cha Tanganyika African Association (TAA).
TAA ilikuwa na mwelekeo wa kitamaduni zaidi ya siasa. Mwenyekiti wa kwanza wa TANU alikuwa Julius Kambarage Nyerere.
TANU ilikuwa ikishinda kila uchaguzi chini ya utawala wa kikoloni ikawa chama cha kuongoza Tanganyika hadi ilipopata uhuru wake mwaka 1961.
Katiba ya Taifa ya mwaka 1962 ilifanya TANU kuwa chama cha pekee nchini ikifuata mfano wa nchi za kijamaa zenye muundo wa siasa ya chama kimoja.
Bendi ya Women Jazz ilipata umaarufu kiasi cha kuanza kufanya safari nje ya Tanzania, na kuweza kufanya maonesho katika miji ya Nairobi na Mombasa, baada ya kutembelea miji kadhaa hapa nchini.
Baada ya waaamuziki wa bendi hiyo kujiona hawapati faida yeyote kutokana na mapato ya bendi yao, wakiwa katika maandalizi ya kufanya ziara ya kwenda nchini China, bendi hiyo ilisambaratika.
Hii chamngamoto kwa Wanawake wa hapa nchini kuiga mfano wa wenzao waliowatangulia wakathubutu, wakafanikiwa kuwa na bendi yao.

Mwisho.




No comments: