Saturday, April 16, 2016

JEAN ‘JOHNNY’ BOKELO ISENGE



 JEAN ‘JOHNNY’ BOKELO ISENGE

Jean Bokelo alizaliwa mwaka 1939 nchini Kongo, nje kidogo ya jiji la Kinshasa. 

Familia yake ilikuwa ni ya wanamuziki. Johnny alikuwa mdogo wa Paul Ebengo’Dewayon’ Isenge.

Mwanamuziki mwingine aliyekuwa mkubwa sana nchini Kongo toka mwanzoni mwa miaka ya 50. 

Huyu Dewayon alikuwa na bendi inaitwa Watam, hapa ndipo Johnny alipoanzia muziki akipiga na mtoto mwingine aliyekuja kutikisa ulimwengu wa muziki Franco Luambo Luanzo, wakati huo Franco akiwa na miaka 12 tu.

Johnny Bokelo aliendelea kupiga katika bendi alizoanzisha kaka yake kama vile Conga Jazz na Orchèstre Cobantu, lakini mwaka 1958 John akaanzisha bendi yake, Orchestre Conga Succès, akiwa na mdogo wake Mpia Mongongo maarufu kwa jina la Porthos Bokelo, ambaye alikuwa mpiga gitaa la rhythm mahiri sana. 

Kaka yao Dewayon, akaja kujiunga na kundi hilo1960 lakini miaka miwiwli baadae1962 Johny na kaka yake wakatengana. 

Bokelo alifanikiwa kulijenga kundi lake kuwa na nguvu na likawa kwa namna fulani linafanana sana na OK Jazz.
Hata tungo nyingine zilikuwa ni za kujibu tungo za OK Jazz au kuzungumzia mada ambayo imeanzishwa na OK Jazz. 

Kuna wakati Bokelo alianzisha kuimba nyimbo alizozipa jina la Mwambe no 1 na 2 mpaka 5 ambapo alikuwa akiongea na kushangaa jamii inaelekea wapi. 

Upigaji wa Bokelo Dewayon na Franco ulishabihiana, pengine ni kutokana na wote kuanzia Watam.

Mwaka 1968 Johnny Bokelo akabadili jina la kundi lake la “Conga success” na kulita “Conga 68” akaanzisha Label yake akaanza kutoa santuri, hii ilimuongezea kipato japo wanamuziki wake walitishia kuachana nae kwani walisema hawakuwa wanapata fedha zozote kutokana na mradi huo.

Santuri nyingi wakati huu alikuwa akiziachia kwanza kutoka Ufaransa ili kupata mapato zaidi. 

Kati ya 1972 mpaka 1974 Bokelo Isengo alikuwa anatumia muda mwingi zaidi akiwa studio, kwenye mwaka 1970, viwanda vya kutengeneza santuri vya Kinshasa vikawa vimechoka hivyo bokelo akaanza kupeleka master zake ili kutengeneza santuri. 

Mwaka 1980 Bokelo aliachana sana na shughuli za muziki.

Bokelo alifariki 15 January 1995 baada ya kuugua kwa muda mrefu
 Mwisho.
Mungu alilaze roho yake pahala pema peponi, amina. 

No comments: