Wednesday, February 27, 2013

MBILIA BELL ALIKATAA KUOLEWA NA WAZIRI.


           MBILIA  BELL
ALIKATAA KUOLEWA NA WAZIRI


 Na: Kiyungi  Moshy.

MBILIA BELL ni mwanamuziki alinyeonyesha ujasiri kwa kukataa kuolewa na Waziri katika serikali ya nchi ya Gabon huko Afrika  ya  Kati, aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.
 Bell ni mama aliyejaaliwa kuwa sura, umbo lililojengeka lenye  mvuto, sauti nzuri ya uimbaji na hata uchezaji wake katika jukwaa.

Ni mwanamuziki  mwenye sifa adimu ambazo pengine yawezekana zisisifikiwe na mwanamke mwingine.
Sifa  nyingine kubwa aliyonayo mwama mama huyo ni kwa aliolewa na mwanamuziki nguli Tabu Ley na ndoa yao ya kifahari iliyofungwa ndani ya ndege wakiwa hewani.

Jina lake halisi ni Marikirala Mboyo, ambaye kama walivyo watoto wengine wa kiafrika wafikiapo umri wa miaka  minane, hukaa na wazazi, Babu au nyanya zao na kulazimishwa kusikiliza hadithi pia  kuimba nyimbo za asili inayowazunguuka.

M’bilia alikuwa mmoja wa hao baada ya kuvutiwa na sauti ya babu yake ambaye alikuwa bingwa wa kuimba, wakati Bibi yake alikuwa mchezaji wa ngoma asiyeshindwa kijijini humo.

Marikirala M’bilia alizaliwa mwaka 1959 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 17 akiwa na mkongwe Abeti Massekini mwaka 1976.

Akiielezea historia yake Bell anasema alianza kupenda muziki baada ya kuangalia katika televisheni na kumuona mwanamuziki nyota toka nchi ya Togo, Bela Bello, ailiyekuwa akifanya onyesho katika mji wa Kinshasa  huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema alivutiwa na kipaji cha mwanamuziki huyo na kutamani siku moja aje kuwa kama Bello. Ansema siku aliyosikia kwamba amefariki, alilia kwa  siku kadhaa.

Baada ya siku saba kupita, akiangalia televisheni, alimuona mwanamuziki mwingine AbÈti Massekini. Baadaye akaamua kumuandikia barua Abeti ya kuomba kujiunga na bendi yake. Alishangazwa kuona  Abeti alipomualika kujianga naye. Hapo  ndipo historia katika muziki wake ilipoanzaia. Alijifunza kuimba akiwa karibu na Abeti kwa kipindi cha miaka minne.

M’bilia baada ya kujiamini amefuzu, aliondoka kwa AbÈti  na kwenda kuungana na Sam Mangwana, ambaye aliwasiliana naye  baada ya kumuona katika televisheni akifanya vitu vyake.  Lakini huko nako hukukaa sana kwani baada ya miaka miwili aliondoka na kujiunga na gwiji la muziki Afrika Tabu Ley Rochereau mwaka 1981.

Bell alipatwa na mshituko siku aliyokutana na kiongozi wa bendi ya Afrisa International Tabu Ley, akiwa na uso wa furaha katika mahojiano kwa njia ya televisheni.

Ley alimwambia kwamba hana mabilioni ya kumpatia lakini kama wakifanya kazi pamoja hatajuta kamwe.

M’bilia alitumia mwanya huo akajiunga na bendi ya Afrisa Internationale na ukizingatia sauti yake nyororo, uchezaji wake kupitia maungo yake yaliyojengeka kipekee, kwa kipindi kifupi M’bilia akawa gumzo katika jiji la Kinshasa. Juhudi zake hizo zilipelekea bendi hiyo kuongeza mapato kwa mauzo ya rekodi zao. 

Yaelezwa kwamba M’bilia Bell na Tabu Ley Rochereau walifunga ndoa kabambe ya kifahari wakiwa ndani ya ndege hewani. Katika maisha yao ya  ndoa walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Melodie Tabu, ambaye anasoma katika jiji la Paris na kufanya muziki na Baba yake.

M’bilia Bell anamuelezea Binti yake huyo kwamba anaongea kwa ufasaha lugha ya kiingereza, na kwamba ni mwimbaji mzuri aliyefuata nyayo za  wazazi wake na tayari amemshirikisha katika kuimba kwenye album yake mpya ya Belissimo.

Mwaka 1982 Bell alitoka na kibao  chake kiitwacho Mpeve  ya Longo, kikisimulia kisa cha mwanamke aliyetelekezwa na mumewe na kuachiwa watoto awalee peke yake. Kibao ambacho kiligusa hisia na kuwa simulizi kila kona za miji ya nchi hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani Zaire).

M’bilia aliipenda nchi ya Kenya, alipokuwa katika jiji la Nairobi alilazimika kujifunza lugha ya Kiswahili na kuweza kuimba nyimbo kadhaa kwa lugha hiyo.

Nyimbo zilizompatia chati M’bilia zalikuwa za  Nakei Nairobi, Boya ye,  Yamba ngay, Amour sans frantiere na   Biu Mondo.
Mbilia aliimba nyimbo nyingine zaidi za  Beyanga, Befosami, Faux Pas,Cadence Mudanda, Motema na Napika. Nyimbo za Kuteleza si kuanguka,  Faux  Pas, Iyolela, Bafosami na  Frontiere,. Zingine zilikuwa zaPhenomene, Manzil manzil, Mbanda na Nga, Nadina, Mayaval, Eswii yo Wapi, Biu Mondo, Nelson Mandela,Wende na Wende  na nyingine zasizokuwa na idadi zilimjengea heshima Mbilia Bell.

Karibia nyimbo zote alizoimba mwana mama huyo Bell akishirikiana na Rochereau hazichuji wala kukinai kuziangalia runingani au kuzisikiliza redioni, hadi leo.

Mbilia Bell aliwahi kuja hapa Tanzania akifuatana na mumewe  Tabu Ley Rochereau  na kundi zima la  Afrisa Internationale Bell alifanya kufuru katika maonyesho yao yote waloyoandaliwa hapa nchini.
Akiwa katika jiji la Dar es Salaam Bell aliweza kulitawala jukwaa mwanzo mwisho akitumia kuyachezesha  maungo yake sanjari na uzuri wake, akawa kivutio kikubwa.

Tabu Ley baadaye alimuongeza mwimbaji mwingine wa kike ‘Faya Tess’ ambaye jina lake halisi ni Kishila Ngoyi,  akiwa na nia ya  kuijenga vyema bendi yake. Lakini ujio wa Faya Tess ulimfanya  M’bilia  kuamua kuiacha Afrisa Internationale na kuondoka  kwenda jiji la Paris ambako alikutana na mwanamuziki wa sokous, mpiga gita Ringo ‘Star’ Bamundele mwaka 1983.

Sababu kubwa za kuondoka kwake ni kile kilichoelezwa kuwa wivu wa kimapenzi baina ya wana ndoa hao ulioingilliwa na Faya Tess.


Mbilia Bell aliwahi kuishi nchini Gabon,  ambayo inapakana na nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alikataa kuolewa na Waziri mmoja katika serikali ya nchi hiyo aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.

Anafurahia mafanikio yake na kujivunia kuwa yeye ni mmoja wa kati ya wanafunzi wa Rochereau  Tabu Ley ambaye alikuwa akimpa kipaumbele na kuwa mwanafunzi bora katika shule yake.

Marikirala Mboyo  M’bilia anasema haikuwa kazi rahisi kukubalika kuwa mwanamuziki mwanamke wa kimataifa katika maisha yake yote ya kazi za muziki. Watu wengi  hawakuwa wakimuamini na kuichukulia kazi yake kwamba haitakuwa endelevu.

Bell alikaririwa akisema kama wao wanawake wanawaamini waume zao na wala hawawalazimishi kuacha kazi zao, iweje wanaume wamfikirie yeye kila anapotikisa maungo yake kwamba huwa anawavutia?
Alitoa wito kwa wanawake wenzake kuungana na kufanya wanaume wawaone kwamba wao hawajirahisishi kama wanavyofikiria.

Marikirala Mboyo ‘M’bilia’ akiwa na muda wa ziada huutumia kufanya shghuli za kijamii zakiwa zile za kuwatembelea watoto wa mitaani, kurekebisha vituo vya watoto hao na kugawa msaada wa vyakula na nguo.

Mwana mama huyo kwa kawaida huamka kila siku saa 12:00 asuhuhi na kufanya maombi baadaye  huenda kwenye mazoenzi ya viungo. Anatoa siri ya kutochakaa mapema ni kuishi ukiwa na afya njema, wala si kwa kula nyama na kunywa pombe.

Ratiba yake ya asubuhi ni glasi moja ya maziwa isiyokuwa na mafuta, na glasi nyingine maji huwa ndiyo kifungua kinywa chake. Baada ya hapo hutumia muda mwingi katika kuandika nyimbo zake na kuangalia sinema katika televisheni.

Mbilia anasisitiza kwamba kazi ya muziki ni ya siku nzima na ni gumu sana hawezi kupata muda wa kutafuta kazi nyingine kwa kuwa hafikirii kuwa tajiri ila ameridhika na hali aliyonayo.

Bell ana mpango wa kuwahamsisha wanamuziki wa kike wa Afrika kuungana na wanamuziki wengine kulilia amani.

Mwisho.

MIAKA MIWILI BAADA YA KIFO CHA DK. REMMY ONGALA


MIAKA MIWILI BAADA YA KIFO CHA DK. REMMY


Desemba 15, 2012
                                                                             
SIKU HAZIGANDI nathubutu kusema hivyo  kwani jana Alhamisi Desemba 13, 2012 ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa Tanzania, Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla.
Ni miaka kamili imetimu toka tulivyoondokewa na kipenzi cha wengi, mwanamuziki nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’
Dk. Remmy aliyefariki usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kisukari.

Aliwaacha wapenzi wake wa muziki wa dansi na ijili pia wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka yetu.

Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye  viongozi wa serikali na dini watu kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk.Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani  tahadhari hiyo.

Alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele kinywani mwake  na akaonekana kana kwamba ni  mtoto wa ajabu. Aidha hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.

Dk. Remmy alijipatia umaarufu katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari yake ndogo ‘soloon’ lililokuwa la aina yake popote lipitapo watu walilishangaa, lenye maandishi nyuma ya gari hilo yakisema ‘ Baba yako analo’?

Historia ya maisha ya Dk.Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi  wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira. Baada ya kuzaliwa kwake haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko DRC.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia.

Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyompelekea kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.

Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na nywele ndefu namna ile, mpaka hapo baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Congo, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari.

Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.

Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia karo ya shule, Remmy ilibidi aache shule.

Ilipofika miaka ya1960, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa sio mwaka mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia.

Bila elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na  sehemu mbalimbali nchini ya Congo akiwa na bendi yake iliyokuwa imesheheni vijana wenzake iliyoitwa ‘Bantu Success’.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dk.Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Congo zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.

Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule  wa Franco ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy  ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.

Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka hapa nchini.

Mzee Makassy  aliamua kuihamishia bendi yake keipeleka nchini Kenya, kitendo kilichomfanya Dk. Remmy  kujiunga na bendi ya  Matimila baada ya kudumu kwa katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.

Jina la bendi hiyo ya  Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Kujiunga kwa  Remmy katika  bendi ya Matimila, alijiongezea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha  jina ikaitwa Orchestra  Super Matimila.

Miaka iliyofuatia Watanzania tulishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususani kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania na Afrika.

Dk.Remmy Ongala aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Alimpa kasseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.

Rafiki yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. Jamaa walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Matimila ilitoa album yenye jina la Nalilia Mwana ikiwa na  mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki.

Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa inaitwa Real World Studios.

Dk. Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya Kipenda Roho, aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye ni mzungu muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambapo walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’  ambayo ilikuwa na nyimbo kama hiyo ya Mambo ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No Money, No Life’ na ‘One World’.

Umaarufu wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa ‘Mambo Kwa Socks’ ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba hauwa na maadili ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Akiwa matimila Dk.Remmy alitoka na nyimbo ningi zikiwemo za Bibi wa mwenziyo, Kipenda roho, Asili ya muziki na Ngalula. Zingine  ni pamoja na Mwanza, Mama nalia, Harusi, Hamisa, Mnyonge hana haki, Ndumila kuwili na Mataka yote ambazo  zilimuongezea sifa kubwa Dk. Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi jamii.

Baadaye Dk. Remmy Ongala akaanza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na akaanza kumuimbia bwana.Kabla ya kifo chake Dk. Remmy alitoa albamu yake ya injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’. Remmy alikuwa katika hatua  za mwisho za kukamilisha albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13,2010 nyumbani Sinza. Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kufuatia umaarufu wake alipokuwa hai. 

Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.


Mwisho.

HASSAN SHAW KINANDA 'KIMEMTOA'


 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW AKIBONYEZA KINANDA HICHO KWENYE MOJA YA HOTEL YA KITALII  NCHINI THAILAND.

 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW AKIFANYA WINDOW SHOPING KATIKA MADUKA NCHINI THAILAND.


 MPIGAJI KINANDA WA BENDI YA JAMBO SURVIVORS, HASSAN SHAW  WAKIJIVINJARI  NA  MPULIZAJI  WA  TARUMBETA NKASHAMA KANKU KELLY (KUSHOTO) WALIPOKUWA NCHINI MALYSIA.

FEBRUARY 27, 2013

HASSAN SHAW alijulikana sana hapa nchini  hususan kwa wapenzi wa bendi ya Vijana Jazz ambao walimshuhudia kijana uyo wakati akibonyeza Kinanda.

Alibonyeza Kinanda hicho na kumjengea umaarufu katika nyimbo za  Shingo Feni, Penzi haligawanyiki na Wifi zangu mna mambo ambazo zilikuwa zikiimbwa kwa sauti nyororo na mwanadada Kida Waziri katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni Jijini Dasr es Salaam.

Jina lake kamili ni Hassan Shaw Rwambo, aliyezaliwa Septemba 25, 1959 jijini Dar es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gita na wenzie kando kando ya Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma, wakitumia magita ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi.

Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir Ally yaelezwa kwamba ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gita kiasi cha kukubaliwa kupiga gita la rhythm katika bendi yaya pili  Afro 70, iliyokuwa ikiitwa PAMA Band  iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya.

Ni chini ya malezi ya Patrick akajifunza kupiga Kinanda baadaye mambo ya muziki na kujiunga na cha Ufundi cha  Dar Technical College.
Mwaka 1980 alijiunga na bendi ya  Vijana Jazz kama mpiga Kinanda ambako akilikutana na  wanamuziki wengi akina John Kitime, Abuu Semhando kwa upande wa drums,  mwimbaji wa wa kike Kida Waziri, Saad Ally Mnara na Hamisi Mirambo. Wengime walikuwa akina   Rashidi Pembe,aliyekuwa kipuliza Saxophone,  Hassan Dalali na  Hamza Kalala walikuwa wapiga gita la Solo.
Ikimbukwe kwamba Hassan Dalali anyatajwa humu  ndiye yule baadaye  akawa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Sports.

Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound (OSS), chini ya  Muhidini Mwalimu  Gurumo na Abel Balthazar. Huko OSS alikutana na wanamuziki wengine akina  Benno Villa Anthony na Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ambao walikuwa waimbaji.

Hassan Shaw alikuwa na msimamo usiopindika pia  hakuwa mtu wa kuonewa ovyo. “Niliicha bendi ya hiyo baada ya miezi sitakutokana na  mhusika kutozingatia mkataba wangu…” anasema Shaw.

Katika kujitafutaia maisha Hassan Shaw akaamua kuhamia  Visiwani Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga katika Hoteli ya Mawimbini.

‘Chema chajiuza’  Sifa zake za kubonyeza Kinanda zilipelekea  kuitwa katika bendi ya Washirika Tanzania Stars. Alipotua hapo akakutana na wanamuziki wakali wakiwemo waimbaji mahiri akina  Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, na  Abdul Salvador ‘Faza kidevu’ ambaye alikuwa na ‘manjonjo’  ya kupiga kinanda akitumia kidevu chake. Ndiyo sababu ya kuitwa ‘Faza Kidevu’

Shaw katika maisha yake  abadan  hukupenda ‘Longolongo’ hivyo kwa bahati mbaya katika bendi hiyo kulitokea kutokuelewana baina ya wanamuziki. Yeye kama kiongozi wa bendi, ikambidi aachie ngazi ili kuepusha bendi kuzidi kujichanganya.

Baada ya hapo anamtaja mpulizaji mahiri wa  tarumbeta,  Nkashama Kanku Kelly  kuwa  alimuita ili ajiunge na bendi yake ya  The Kilimanjaro Connection. Kanku  Kelly na  Hassan Shaw wameona nyumba moja  Kanku  akiwa ni  mume wa dada wa mke wake.

 Anamsifia Kanku kwamba  alimvumilia sana kwa kuwa hapo awali  hakuwahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani. Akiwa Connection alijifunza kukopi nyimbo nyingi za wanamuziki  wa kimataifa duniani.

The Kilimanjaro Connection ilikuwa inazunguka kwenda  kupiga muziki kwenye  hoteli  mbalimbali katika nchi za Malaysia, Singapore, Indonesia, Thailand na Japan, jambo ambalo kwake yeye ilikuwa  faraja kubwa.

Pamoja na Kanku Kelly, Shaw anasema  kwamba alishirikiana vyema na wamanuziki wengine akina Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan,  Shomari Fabrice, Bob Sija, na Faliala Mbutu. Wengine  walikuwa Ray Sure boy, Delphin Mununga na Ramdhani Kinguti ‘System’

Baadaye Hassan  Shaw, na wanamuziki wenzake  Ramadhani Kinguti ‘ System’ na Burhan Muba wakafikia maamuzi ya kuanzisha kundi dogo la muziki  wakitumia ala iitwayo Sequencer keyboards, wakiicha The Kilimanjaro Connection ya Kanku Kelly.

Kundi hilo likajiita Jambo Survivors Band ambalo baadaye likaaza safari za  kuzunguka nchi mbalimbali kupiga muziki katika hoteli za kitalii.  Ilifanya kazi katika nchi za Oman, Fujairah, Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E), Singapore, Malaysia na Thailand.

Hassan  Shaw anasema wanamuziki ambao kamwe hatawasahau maishani mwake  ni pamoja na  Zahir Ally Zorro, Marehemu Patrick Balisdya, Waziri Ally, Ramadhani Kinguti ‘System’, Burhan Muba na Kanku Kelly kwa kuwa ni wao walomfikisha  hapo alipo.

Akielezea kituko ambacho hawezi kusahau ni pale walipokuwa nchini Malaysia,  alishindwa kupiga nyimbo baada ya kutoweka nyimbo zote  kichwani mwake.  “ Nililikuwa ninapiga muziki kwa mara ya kwanza nikiwa nimezungukwa na wazungu weupe wakiniangalia. Huwezi kuamini,  nyimbo zote  ziliyeyuka kichwani  nikawa sikumbuki hata nyimbo moja”  anasema Hassan Shaw.

Kama walivyo wanamuziki wengine wenye mafanikio, Shaw anawaasa vijana kujifunza kupiga ala za muziki ili kufikia ndoto zao za kuwa wanamuziki wa kukubalika kimataifa. Pia amewataka vijana kutokata tamaa pale wanapokutana na vikwazo bali watafute jinsi ya kujinasua.

Hassan Shaw hadi sasa yupo nchini Thailand akipiga muziki  na kundi zima la Jambo Survivors. 

Mwisho.





Tuesday, February 26, 2013

HISTORY of DEKULA KAHANGA 'VUMBI'

 DEKULA KAHANGA 'VUMBI'  AKICHARAZA NYUZI ZA GITA LA SOLO HUKO SWEDEN.


 DEKULA KAHANGA AKIPIGA GITA KATIKA UKUMBI WA WHITE HOUSE UBUNGO DAR ES SALAAM, TANZANIA.
 DEKULA KAHANA AKIWA KATIKA PICHA YA 'POZI' NA GITA LAKE.
 'MAMBO YA ULAYA' VUMBI AKIWA NA FARASI.

DEKULA  KAHANGA ‘VUMBI’  ALIZIBA PENGO LA NGUZA

Na Kiyungi Moshy
January 28, 2013

KATI YA WANAMUZIKI  WAAFRIKA waliopata mafanikio makubwa kwa kuchacharika, jina la Dekula Kahanga haliwezi kukosa. Ni mwanamuziki wa dansi, aliyefanikiwa kuanzisha bendi yake katika jiji la Stockholm nchini Sweden baada ya ‘kuitosa’ Maquis Original.
Dekula ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Vumbi’,  anasisitiza kwamba mafanikio yoyote katika maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, na dhamira ya dhati, hatimaye kufanya maamuzi magumu.
Kabla ya kwenda nchini Sweden, ‘Vumbi’ alikuwa mpigaji wa gita la solo katika bendi ya Maquis Original, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata  Kindondoni jijini Dar es Salaam, miaka ya 1990.
Akiwa katika mapumziko mafupi nyumbani kwake Mikocheni kwa Warioba  jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Dekula alitamka baadhi ya maamuzi magumu aliyoyafanya mojawapo ni lile la kondoka katika bendi hiyo ya Maquis Original, na kutokomea kwenda Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa nani huko ughaibuni.
Vumbi anaeleza kwamba hivi sasa hajutii maamuzi yake kwakuwa amepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake iitwayo Dekula Band. Amesema bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.

Dekula Band ina  wanamuziki mahiri toka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo akina Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na kucheza Show, Sammy  Kasule, huyo ni injinia pia huimba, kupiga gita la besi, drums na kinanda. Wengine amewataja kuwa ni Joe Gerald Nnaddibanga, ambaye huimba, kupiga konga na kucheza show, Christina Frank, na Marceline Kouakoua.
Mwenye Dekula Kahanga, hulicharaza gila la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambaye ni mbonyezaji wa kinanda. Safu hiyo kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya Sweden zikiwemo nchi za Ulaya, Asia, Marekani, Japan,  Falme za kiarabu na Afrika.
“ Hakuna kitu muhimu kama kuwa na mahusiano  mema na baadhi ya watu toka nchi mbalimbali ninazotembelea. Nimefikia kuweza kuongea  kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza,  Kifaransa, Lingala na Kiswidish” Anajigamba Dekula ‘Vumbi’.
Historia ya Dekula Kahanga anailezea kwamba  alizaliwa mwezi Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera, Wilaya ya Kivu  Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ni baba wa familia akiwa na mke na watoto watatu. Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa Mzee Aloyce Obeid Dekula,  aliyekuwa mfanyakazi katika serikali ya Zaire iliyokuwa ikiongozwa na rais Mobutu Seseseko.

Alipata  elimu ya Sekondari katika shule mbili tofauti za Bukavu na Uvira huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alihitimu kidato cha nne  mwaka 1979. Mwaka uliofuatia wa 1980, safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National, na Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa Nundu.
Akiwa huko kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika wakati huo na alizitamani sana nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz, Tabora Jazz, Nyamnyembe Jazz,  NUTA Jazz,  Mlimani Park, Maquis du Zaire na Orchestra Safari Sound.
Kamwe hatomsahau  John Luanda katika historia ya maisha yake, kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania. Luanda alikuwa akimiliki bendi ya Chamwino Jazz,  aliwachukua toka Kongo akiwa na wenzake  akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta kwa madhumuni ya kujiunga katika bendi yake ya Chamwino. Bendi hiyo wakati huo  ilikuwa ikipiga muziki maeneo ya Tandale huko Manzese,  jijini Dar es Salaam.
“Mwenye bahati habahatishi” ndivyo anavyosema mkung’utaji mahiri wa gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’,  kwamba mwaka 1980 alikutana na mwanamuziki  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika ofisi za ubalozi wa Kongo hapa nchini.
Nguza wakati huo alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa ni mmoja kati ya  wanahisa wa Orchestra   Maquis Comapy  (OMACO) na  mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire. Katika maongezi yao, Chimbwiza  Nguza alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Dekula alikubali mwaliko huo na Weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha kwa muda mfupi.
Walipopanda jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.
Dekula Kahanga baadaye aliitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ wakimtaka aandike barua ya kuomba kujiunga na bendi yao kwa mkataba usio na mshahara. Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na akajiunga na Maquis du Zaire.

Vumbi anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa  Temeke Stereo,  alimuona Nguza  akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo huku akisikiliza midundo inavyounguruma..
“Nilipomuona,  nikaingiwa na hofu kubwa nikijihisi kama ninamvunjia heshima Nguza. Nikaomba  nimpishe ili ashike nafasi yake” Anasema kwa kujiamini Dekula Kahanga.
Lakini  viongozi wake akiwemo Chibangu Katai ‘Mzee Paul’ na  Ilunga Lubaba, walimwamuru aendelee kushika ‘mpini’.
Kwa amri hiyo, ilikuwa kama Fisi aliyeachiwa  Bucha kuilinda. Aliweza kuzicharaza kwa umahiri mkubwa nyimbo zote alizokuwa zikipigwa Field Marshal  Nguza zikiwemo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha kati yake na Nguza.
Aliachiwa  kulivurumisha gita hadi  mwisho wa onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipo naye hakusita kumpa hogera kwa kazi  nzuri.
 “Mungu mkubwa,  siku hiyo Nyota yangu iling’ara kiasi kwamba hata mimi mwenyewe sikuweza kuamini nilichokuwa nikikifanya jukwaani hapo” Anasema  Dekula Kahanga ‘Vumbi’ huku akitabasamu.

Taharuki kati ya uongozi wa  Maquis du Zaire  na Nguza ‘Vicking’ ziliendelea hatimaye aliondoka rasmi bendi hiyo, hadi kwenda kuanzisha bendi yake ya Orchestra Sambulumaa akiwa na mwanamuziki wengine akiwemo mwanaye Papii Kocha. Bendi hiyo ilikufa baada ya Nguza na mwanaye huyo kuhukumiwa kutumikia kifungo  cha maisha gerezani.

Miaka ya 1989 na 1990 Dekula alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis Original,  jina lililozaliwa toka Maquis du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi Lang’ata Kinondoni. Mtunzi na mwimbaji Maquis Original Tshimanga Kalala Assosa,  alikuwa akipaza sauti ya kumpandisha mori kwa kumuita mara kwa mara Vumbiii,Vumbiii,Vumbiii kama kibwagizo wakati wa chorus kwenye  wimbo wa Ngalula.

Vumbi wakati huo alikuwa na umri ambao unamruhusu kuhangaika kutafuta maisha yenye maslahi mazuri. Hivyo maamuzi magumu yakaanzia hapo Lang’ata baada ya kuamua kuicha bendi ya Maquis Original, iliyompa jina na kuchepukia katika jiji la Stockholm nchini Sweden.
 
Akiwa Stockholm, Vumbi alianza kuchacharika mitaani  akitafuta bendi ya kupiga,  hatimaye akakutana na mwanamuzi toka Uganda,  aitwaye  Sammy Kasule. Mwaka 1993 wakaamua kuanzisha bendi yao ikiitwa  Makonde Group.
Mwaka 1999, Dekula Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘mpenzi Asha’

Dekula Kahanga anajivunia kwamba yeye ni  mwanamuziki wa kwanza toka Afrika huko Sweden, kufyatua album.  Alitoa album iitwayo ‘DEKULA Sultan Qaboos’ yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga, Rozina, Mambo leo na Nostalgie  nyimbo hizo  anasema zinazopigwa mno katika vituo vingi vya redio Duniani.
Ili kupata unafuu wa maisha nchini Sweden,  Dekula alilazimika kuomba uraia wa nchi hiyo hivyo ilifuata taratibu zote. Alichukua maamuzi magumu mengine ya kuukana uraia wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kupata uraia wa nchi hiyo.
Hivi sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni  raia halali wa nchi ya Sweden na wanaweza kusafiri kwenda nchi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo kuomba VISA.

Dekula ametoa mwito kwa wanamuziki chipukizi kujifunza kupiga ala za muziki ili wafikie viwango vya kuwa  wanamuziki. Pia amewaasa kuacha kulewa sifa ndondogo pia kuepuka anasa zisizo na tija.
“Nawapenda sana Watanzania, walinipokea,  wakanilea, wakanithamini na wakanipenda. Ninatarajia kutoa zawadi endelevu  kwa Watanzania siku za usoni kuanzisha bendi ya vijana, itakayokuwa ikitumia ala za muziki wa kisasa” anamaliza Dekula Kahanga Vumbi.

Mwisho.



HISTORIA YA DR.REMMY ONGALA


DK. REMMY ONGALA

Na: Kiyungi Moshy:

Desemba 15, 2012

Jumatano iliyopita ya Desemba 13, 2012 ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa Tanzania, Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla. Siku hiyo ilikuwa ni miaka miwili kamili toka kifo cha mwanamuziki nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’ aliyefariki usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam.

Alikuwa kipenzi cha watu aliyewaacha wapenzi wake na wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake zenye maudhui maridhawa, ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka yetu.

Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye  viongozi wa serikali,vyama na dini na wengine kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani  tahadhari hiyo.

Alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele kinywani mwake  na akaonekana kana kwamba ni  mtoto wa ajabu. Aidha hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.

Dk. Remmy alijipatia umaarufu katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari yake ndogo ‘soloon’ lililokuwa la aina yake popote lipitapo watu walilishangaa. Lilikiwa na maandishi nyuma ya gari hilo yakisema ‘ Baba yako analo’?

Historia ya maisha ya Dk.Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi  wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira. Baada ya kuzaliwa kwake haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko DRC.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia.

Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyompelekea kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.

Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na nywele ndefu namna ile. Lakini baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Congo, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari.

Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.

Kwa bahati mbaya baba yake huyo mwaka 1953 alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia karo za shule, Remmy ilibidi aache shule.

Ilipofika miaka ya 1960, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa.
Mwaka mmoja baada ya kifo cha Baba yake mzazi, mwaka uliofuatia wa 1964 ulikuwa si mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi naye alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia licha ya umri wake mdogo.

Bila elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na  sehemu mbalimbali nchini ya Congo akiwa na bendi yake iliyokuwa imesheheni vijana wenzake iliyoitwa ‘Bantu Success’.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dk. Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Congo zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.

Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa.

Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule  wa Franco Lwambo Makiadi ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy  ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.

Huo ukawa ndiyo mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka hapa nchini.

Mzee Makassy  aliamua kuihamishia bendi yake keipeleka nchini Kenya, kitendo hicho cha mjomba wake kilichomfanya Dk. Remmy  kujiunga na bendi ya  Matimila baada ya kudumu kwa katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.

Jina la bendi hiyo ya  Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Kujiunga kwa  Remmy katika  bendi ya Matimila, alijiongezea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha  jina ikaitwa Orchestra  Super Matimila.

Miaka iliyofuatia Watanzania tulishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususan kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Orchestra Super Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika.

Dk.Remmy Ongala aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Kasseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.

Rafiki yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. WOMAD  walivutiwa na nyimbo zao, hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Super Matimila ilitoa album yenye jina la ‘Nalilia Mwana’ ikiwa na  mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile ‘Ndumila Kuwili’ na ‘Mnyonge Hana Haki’

Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ya Stud Real World Studios,
ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel.

Dk. Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya ‘Kipenda roho’ aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye ni ‘mzungu’ muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambako walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’  ambayo ilikuwa na nyimbo kama hiyo ya ‘Mambo’ ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No money, no life’ na ‘One World’.

Umaarufu wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa ‘Mambo kwa soksi’ ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili mema kwa jamii, ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Akiwa Super Matimila Dk. Remmy alitoka na nyimbo ningi zikiwemo za ‘Bibi wa mwenziyo’, ‘Kipenda roho’, ‘Asili ya muziki’ na ‘Ngalula’. Zingine  ni pamoja na ‘Mwanza’, ‘Mama nalia’, ‘Harusi’, ‘Hamisa’, ‘Mnyonge hana haki’, ‘Ndumila kuwili’ na ‘Mataka yote’ ambazo  zilimuongezea sifa kubwa Dk. Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi jamii.

Baadaye Dk. Remmy Ongala akaanza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani.
Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na akaanza kupiga muziki akimuimbia bwana.
Kabla ya kifo chake Dk. Remmy alitoa albamu yake ya Injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’. Remmy alikuwa katika hatua  za mwisho za kukamilisha albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza. Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kufuatia umaarufu wake alipokuwa hai.

Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.


Mwisho.