Thursday, May 16, 2013

MIAKA 26 TANGU KIFO CHA AHMED KIPANDE WA KILWA JAZZ.





              Ahmed Kipande akiwa na Saxophone.
 Ahmed Kipande (kushoto) akiwa na wanamuziki wenzake wa Kilwa Jazz.

 Wanamuziki wa Kilwa Jazz wakiwa pembeni mwa gari lao liliohaibika njiani.

Kwa wale wale wapenda miziki ya zamani nikiaanza na sehemu ya ndogo ya mashairi ya wimbo huu, ninauhakika watang’amua ninani nitamzugumzia katika kipindi cha leo cha ‘Enzi hizo’  sikiliza wimbo huu…
“Napenda  nipate lau nafasii, nipate kusema nawe kidogo aah mamaa aah  rohoni  inaumiaa, hakika lakufanya bado sijaliona, nimeona leo bora nikuimbee, huenda punde roho yako ikadundaa ikaja siku ukaja nipoza moyo ooh mama rohoni naumia…” huyo ni marehemu Ahmedi Kipande akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.
Jumamosi ijayo ya tarehe  27, 2013 Ahmedi Kipande atatimiza miaka 26 tangu aiage dunia Aprili 27, 1987.
Wasifu wa mwanamuziki huyu  umeelezwa kwamba alikuwa mwanamuziki nguli aliyeshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigani Uhuru wa Tanganyika kupitia tasnia ya muziki akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.

Kilwa Jazz ilishiriki kikamilifu siku Tanganyika inapata Uhuru Decemba 09, 1961 kwa kuimba wimbo wa kusifia nchi yetu kupata Uhuru toka wa Wakoloni.

Chini ya uongozi wa Ahmed Kipande  Kilwa Jazz mwaka 1964,  ilishiriki kutoa burudani wakati mikakati ya kuandaa Mapinduzi ya Zanzibar kwenye maeneo ya makao makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam.

Ahmed Kipande na bendi yake waliteuliwa na serikali ya Tanganyika kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa nchi za Malawi na Uganda.

Ni miaka 26 imetimia tangu Ahmed Kipande alifariki  dunia Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kuharusi kwa kipindi kirefu, lakini ataendelea kukumbukwa kwa mazuri aliyofanya katika taifa hili.

Historia ya mwanamuziki huyu iliyotolewa na mwanawe wa mwisho Kipande Ahmed, ameeleza kwamba jina kamili la  baba yake alikuwa ikiitwa Ahmed Mohammed Kipande,  aliyezaliwa mwaka 1937 huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi.

Miaka michache baada ya kifo cha mama yake Ahmed Kipande alifuatana na Baba yake kuja Dar es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Wavulana ya Uhuru maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam ambapo alisoma hadi darasa la nne.

Katikati ya miaka ya 1950 Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo violin, katika bendi ya Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidasi. Bendi hiyo ilikuwa  na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao hivi sasa unaitwa mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale  wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.

Ahmed Kipande aliyekuwa akitoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi, akishirikiana na mwanamuziki mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Shamte nao wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958.

Kilwa Jazz ikaanza kujizolea umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbali mbali zikiwemo za siasa, mapenzi na za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.

Alitunga na kuimba nyimbo za ‘TANU yajenga nchi’, nchi yetu’  ‘enyi Vijana tujenga yetu, Doli na ‘It can be done, play your party’
Zingine zilikuwa za Nipate lau nafasi’ Rose waniuwa uwa’, ‘Nacheka cheka Kilwa leo’ na Maneno hayafai’

Wimbo wa Nacheka cheka ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kukopi wimbo wa John Bokelo na Tabu Ley wakiwa na bendi ya African Jazz  wa ‘Mokolo Nakokufa’ halikadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo, Rose waua na Maneno hayafai nazo walikopi na kupesti toka wimbo wa Course au Povouir  na Est ce Que za T.P.OK.  Jazz.

Mwaka 1973 Kilwa jazz ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz iliyefanya onyesho kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Luambo Makiadi baada ya kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake mkubwa wa ‘kokopi nyimbo hizo.

Kipande Ahmed alisema mwaka 1961 siku Tanganyika inapewa Uhuru toka kwa Wakoloni, bendi yake ya Kilwa Jazz ilikuwa Uwanja wa Taifa ikiporomosha muziki ambapo ilitoka na wimbo wa  kumshukuru mungu kwa Tanganyika kupata Uhuru.
Mtoto huyo wa marehemu Ahmed, aliimba mistari sehemu fupi ya wimbo huo.
 “Ewe mola tunakuomba uibariki Tanganyika yetu na jirani  zetu, Uhuru tumepata lakini Nyoyo zinasikitika,  wenzetu wanateseka  Wakoloni wamewashika…”

Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa na makao makuu yake katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako siku moja ilipiga muziki nje ya Ofisi yao na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana.

Lakini ilikuwa ni mipango kamambe ikipangwa na wazee toka Zanzibar maeneo hayo siku chache kabla ya mapinduzi ya Zanzibar. Wazee hao  walikuwa wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964, huko Zanzibar.

Bendi ya Kilwa Jazz baadaye haikueleweka miongoni mwa jamii. Wengine wakafika mbali zaidi wakizusha maneno kwamba ni bendi ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika shughuli nyingi za kitaifa.

Kilwa jazz pia ilialikwa kutoa burudani katika sherehe ya ndoa ya mmoja wa mawaziri wa serikali ya Tanganyika wakati huo, Oscar Kambona.

Katika hafla hiyo Ahmed Kipande alionesha kipaji chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao,  Oscar Kambona na mkewe.
Wakati Ahmedi Kipande akiimba wimbo huo, Bwana harusi  Kambona aliinuka toka kwenye kiti cha maharusi na  kwenda kumkumbatika kisha akamtunza kwa pesa.
Bendi hiyo ya Kilwa jazz ilikuwa chini ya udhamini mkubwa wa Mzee  Nangwanda Lawi Sijaona, ambaye anaelezewa kuwa alitoa mchango mkubwa mno wa hali  na mali.
Kilwa jazz ilikuwa na wanamziki wenye vipaji tofauti. Walikuwepo ambao walikuwa wakipiga ala za muziki zaidi ya moja pamoja na kuimba.

Ahemed Kipande alikuwa  kiongozi, mtunzi wa nyimbo, alikuwa akiimba pia alikuwa hodari  wa kupuliza ‘mdomo wa bata’ Saxophone. Duncan Njilima, Zuberi Makata, na Hassan Shabani ‘Kichwa’ wote walikuwa na uwezo wa kupiga gita la solo. Kwa taarifa yako msomaji wa gazeti hili kwamba  Hassan ‘Kichwa’ alikuwa kaka mkubwa wa Ahmedi Kipande.
Kwa upande wa saxophone walikuwepo akina Kisi Rajabu, Juma Town na Abbas. Waimbaji alikuwa yeye Ahmedi Kipande, Juma Mrisho’ Ngulimba wa ngulimba’ na Kassimu Mapili. Gita la kati lilikuwa likiungurumishwa na Abdull Ngatwa wakati Drum zilikuwa zikicharangwa na Said  na  Abdallah Kanjo.

Upigaji wao wa muziki ulikuwa ukiwakuna vilivyo viongozi wengi wa siasa na serikali, ilifikia kiongozi mkubwa wa nchi wakati huo, Mzee  Rashid Mfaume Kawawa alitoa ofa ya suti kwa wanamuziki wote wa Kilwa jazz.

Ahemed Kipande katika maisha yake alifanikiwa kupata watoto sita, lakini wawili kati yao, walikwisha tangulia mbele za haki.
Mzee Kassimu Mapili aliyejiunga na  bendi hiyo mwaka 1965, amelieleza gazeti hili kwamba Kilwa jazz wakati wa enzi zake haikuwa na mpinzani katika muziki licha ya kuwepo bendi kubwa za Dar Jazz na Western Jazz.

Kilwa jazz  miaka hiyo alitoka na vibao vingi vya Mapenzi yananivunja mgongo, Nipate lau nafasi, Nacheka cheka Kilwa leo, Rose waniuwa, Maneno hayafai na nyinginezo nyingi.
Nyimbo hizo baadhi yake hadi sasa  zinapigwa na baadhi ya bendi za muziki wa dansi, kwenye vituo vya Redio mbalimbali na wengine wameziweka kama miito ya simu zao.
Mtoto wa mwisho wa Ahmed Kipande, Kipande Ahemd  alisema kwamba pamoja na juhudi kubwa za baba yake za kufanikisha mambo mengi ya maendeleo toka Tanganyika hadi kuwa Tanzania, alipokuwa akiumwa nyumbani kwake hauonekana mtu yeyote wa kwenda kutoa msaada wala kumjulia hali.
Kipande akafika mbali zaidi kwa kusema kwamba licha ya mchango mkubwa wa baba yake Mzee Ahmed Kipande kwa taifa, bado hajamkumbukwa japo kwa kumpa tuzo ya heshima kama walivyofanyiwa wanamuziki wengine.

Ni miaka 26 tangu Ahmedi Mohammed Kipande afariki dunia  Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu. Alizikwa kwenye  makaburi ya Tandika Maguruwe, mkoani Dar es Salaam  Aprili 28,1987.

Mugu ailaze roho ya marehemu Ahmedi  Kipande  pahala pema peponi,  Amen.  

Mwisho.


No comments: