Thursday, May 16, 2013

JUMA UBAO 'KING MAKUSA'



UNAMKUMBUKA ‘KING MAKUSA’ JUMA UBAO?

JUMA UBAO ‘KING MAKUSA’ halitakuwa jina geni hususani kwa  wale waliokuwa vijana na wapenzi wa muziki wa dansi kati ya miaka ya 1970 na 1990 hapa nchini.

Ubao  ni mwanamuziki  mwenye vipaji vya pekee, ambavyo sitakosea nikitamka kwamba wanamuziki wengine hawakujaaliwa kuvipata. Kubwa zaidi ni lile la kuwa na uwezo wa kitumia kila aina za ala za muziki.

Juma Ubao aliwahi kuonesha maajabu wakati akirekodi nyimbo katika kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) wakati huo,  ambapo alirekodi (single track) ndani ya dakika 8, akishiriki katika sehemu sita tofauti Studioni.

Nguli huyu alikuwa mastari wa mbele katika uhamasishaji wa wananchi kwenda kujiunga katika vijiji vya Ujamaa, ukimbizaji wa mbio za Mwenge, na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kupitia tasnia ya muziki.

Akieleza Wasifu wake anasema jina lake halisi ni Juma Salim Laizer, aliyezaliwa mkoani Dodoma mwaka 1950.

“Kabila langu na Mmasai, ni mzaliwa wa Dodoma lakini asili yangu ni kijiji cha Mabebu kilichopo Longido, mkoani Arusha…” anasema Ubao.
Akisimulia asili yake ya Arusha anasema babu wa babu zake walikuwa watu wa kuhamahama kama ilivyokwaida ya kabila lao la Masai. Walihamia Kondoa mkoani Dodoma, ambako ndiko mababu hao  wakasilishwa kuingia dini ya Kiislamu, baadaye wakafanya makazi yao Dodoma mjini.
Anawataja wazazi wake kuwa ni  Mama Sheila Sindano  na Mzee Salim Laizer, aliyeishia elimu ya msingi ya darasa la tano. Alikuwa mhasibu katika Shirika la Reli la Afrika ya Mashariki (EAR) akifanyika kazi katika mji wa Iringa.
Mzee Laizer alishatangulia mbele za haki.

Jina la Ubao si halisi, bali alipachikwa na wapenzi na mashabiki wa muziki wake  baada ya kuridhishwa na upigaji wa ala nyingi kwa wakati mmoja, wakimlinganisha na ubao ambao hutumiwa katika  kufanya kazi nyingi.

Juma Ubao alipata elimu yake katika shule ya msingi ya  Wamissionari ya Konsolata mjini Iringa hadi alipomaliza darasa la nane mwaka 1965.
Alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi  wa shule hiyo waliofaulu mtihani  wa darasa la nane,  akachaguliwa kwenda kujiunga katika shule ya  Sekondari ya Tosamaganga ya mkoani humo  hadi alipomaliza kidato cha nne mwaka 1969.
Miaka hiyo hapa nchini wasomi hawakuwa wengi, elimu ilikuwa mithiri  ya ‘lulu’.  Hivyo elimu yake ya kidato cha nne ilimpatia kazi  nzuri mwaka 1970 kwenye kitengo cha Colito Barracks iliyopo Lugalo jeshini, akijifunza muziki katika bendi ya blass.
Munkari wa muziki ukaanzia hapo kwani mwaka 1972, alijiunga na bendi ya Polisi Jazz. Ubao baadaye akijiunga katika bendi ya King Afrika iliyokuwa na wanamuziki mchanganyiko toka nchi za Zambia na Frolie, Monga Stanii na Tomaa‘Kabotolo’Congo.
Bendi hiyo ilikuwa ikiporomosha muziki wake katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa ukimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Mzee Fadhili Batengas, maeneo ya  Tazara, Buguruni.
Mwaka 1973 kulipoanzishwa vijiji vya Ujamaa hapa nchini,  Juma Ubao alishiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika vijijini hivyo. “tulinusurika kuliwa na Simba tukiwa porini  huko Mkongo wilaya ya Rufiji,  wakati wa oparasheni ya vijiji vya ujamaa…” anatamka Juma Ubao.
Safari yake katika muziki iliendelea kwa kujiunga katika bendi ya STC Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Umma la (State Trade Corporation) mwaka 1975.

Baadaye Shirika hilo la STC ikabadilishwa kuwa Bodi ya Biashara ya ndani(Board of Internal Trade.) halikadhalika bendi nayo ikawa Biashara Jazz. Juma Ubao alipigia bendi hiyo hadi mwaka 1982 bendi ilipotoweka katika taswira ya muziki.


Ikumbukwe kwamba miaka ya 1970 baadhi ya mashirika ya umma yalianzisha vitengo vya michezo na burudani. Shirika la usafiri Dar es Salaam lilikuwa na bendi ya UDA Jazz waliokuwa wakipiga katika mtindo wao wa  ‘Bayankata’, Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilikuwa na bendi ya Urafiki Jazz ‘wakitamba na mtindo wa ‘Chakachuwa’ Shirika la Bima la Taifa (NIC), nalo lilikuwa na bendi ya Orchestra Bima Lee, wakitamba katika mtindo wao wa ‘Magneti tingisha’

Akielezea kisa cha kuitwa   ‘King Makusa’  Ubao anasema
“mwaka 1976 tulikwenda Studio za Redio Tanzania (RTD), kurekodi nyimbo zetu. Niliwaacha midomo wazi watayarishaji na watangazaji wa wakati huo akina Khalid Ponela, John Luanda, Charles Hirali, Frank Kirumbi, Gilbert Boma na fundi mitambo wao  James Mhillu na Crispin Lugongo,  wakinishuhudia nikipiga sehemu sita katika wimbo mmoja ndani ya dakika nane…”

Juma Ubao ambaye ni mcheshi na mwenye  masihara mengi, anasimulia zaidi jinsi alivyofanya ‘vimbwanga’ siku hiyo akisema
“nilitayarisha wimbo, nilipiga solo, niliimba, nilipapasa kinanda, nilipuliza saxophone, na kutwanga tumba katika ‘single track’ ndani ya dakika nane…”
Kwa Watangazaji hao, ilikuwa ni kitu kipya ambacho  hakikuwahi kufanywa na mwanamuziki mwingine yeyote.

Ndipo hapo walipompachika jina la King Mkusanya, likiwa na maana ya Mfalme(King) wa kukusanya. Lakini wakashauriana na kufupisha kuwa ‘King Makusa’ jina linalovuma hadi leo.
Ubao anasema enzi zake wakati akipiga muziki ukumbini, alikuwa apiga gita,   na  kinanda,  kila ala kwa wakati wake.
“Wakati ninaimba gita huliweka mbavuni, saxophone huliweka mgongoni na Kinanda pembeni huku watu wakinishangaa…” anajisifia Juma Ubao.

Nguli huyo mwaka 1987 aliwahi kuteuliwa kuwa miongoni mwa wanamuziki 57 waliounda kundi la Tanzania All Stars, waliotoka na wimbo wa ‘Fagio la Chuma’ ukiwa ni kauli mbiu ya rais wa awamu ya pili  Alli Hassan Mwinyi, juu ya uwajibikaji.

Juma Ubao mwaka 1989, alikuwa muasisi wa bendi ya Six Manyara akiwa na wanamuziki wakongwe akina Suleiman Mwanyiro, Hassan Bichuka, Kassim Rashid ‘Kizunga’ Kasola Rajabu na Manicho Athumani. Wakiwa katika bendi hiyo walifumua vibao vya Batuli na Salama zikiwa ni tungo za Juma Ubao. Zingine ni Maselina, Fatuma Samahani sana na Tabu.

Bendi hiyo ya Six Manyara iliundwa kwa madhumuni ya kutangaza fahari za Utalii wa nchi yetu zikiwemo mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro na vivutio vingine vilivyopo hapa nchini.
Bendi hiyo ilisafiri kwenda kutangaza utalii katika nchi za Uganda na Kenya mwaka 1991.
Wakiwa huko Kenya walifanikiwa kurekodi nyimbo nne katika kampuni ya PolyGram nchini humo  kwenye Long Play.
Waliporejea toka Kenya, wanamziki wake wengine walirudi katika bendi zao za zamani ila yeye ‘akakomaa’ na bendi  hiyo hadi sasa.

Juma aliamua kupumzika mambo ya muziki kwa muda.  Akuamua kuutumia muda huo kwenda kusoma  masomo ya jioni akiwa na lengo la kuendeleza elimu yake. Alisoma masomo ya Uhasibu na Biashara na kupata cheti.
Cheti chake kilimpa nafasi ya kupata ajira katika shirika la ndege la Tanzania (ATC),  kama mhasibu katika klabu ya Jet.

Baadaye alihamishiwa kwenda Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambako alipewa kitengo cha kusimamia vyakula vya kwenye ndege.
Katika kitengo hicho, Ubao alilipunguzia kwa kiasi kikubwa gharama za malipo zilizokuwa zikilipwa na Shirika la ATC. Yeye aliweza kusimamia ipasavyo vyakula vyote kuandaliwa toka Klabu ya Jet,  badala ya  kuvinunua katika hoteli ya Kilimanjaro.
Shirika hilo la ATC baadaye  likaanza kuyumba kiuchumi uliopelekea kupunguza baadhi ya  wafanyakazi wake mwaka 2002, miongoni mwao akiwa Juma Ubao.


Mwaka 2000 Six Manyara ilirekondi nyimbo za Somo somo, Leo leo zilizopigwa katika mahadhi ya mduwara. Wimbo wa ‘Zongolo jangu’  uliimbwa kwa lugha ya Kizaramo ikiwa na maana ya Jogoo langu. Wimbo wa Sakina ulipigwa katika mtindo wa rage na nyingine  ni Msichana, Tuluka chibite ulirekodiwa kwa lugha ya Kigogo ukiwa na maana ya Inuka tuondoke. Wimbo mwingine uliotia fora wakati huo ni Bide, alitunga na kuimba kwa lugha ya Kipogoro.
Demokrasia katika tasnia ya muziki ilifanya kazi yake  pale mwaka 2008, ilipomchagua Juma Ubao kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) Alichukuwa nafasi hiyo baada ya Kassim Mapili aliyekuwa mwenyekiti  wa kwanza wa  chama hicho, kumaliza muda wake.
Juma Ubao umekwisha pewa nafasi nyingi za uongozi katika tasnia ya muziki. Mwaka 2009, aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi  ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)
Juma Ubao ni baba wa familiya ya mke na watoto watano. Anamtaja mkewe Ashanti Mwinjuma kwamba katika kipindi chote katika muziki, ndiye aliyekuwa akimfariji na kumpa  moyo kila alipokuwa akikwama.
Watoto wake anawataja kwa majina ya Athumani, ambaye amefuata nyayo zake, yupo nchini Austria, akifanya mambo ya muziki.  Laizer, Ibrahimu, Aboubakar na Salma.

Nguli huyu hakuchelea kuiomba serikali kuwatambua  wanamuziki wa zamani ambao anasema walitoa mchango mkubwa kupitia tasnia ya muziki wakati wa kutafuta Uhuru, pia walishiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kuhamasisha maendeleo ya taifa letu.
“Kuthaminiwa kwa wanamuziki hawa si kwa kuwapa pesa pekee, la hasha, bali ni  kuwepo kwa utaratibu japo wa kuweka majina yao kwa baadhi ya mitaa, shule ama hospitali katika halmashauri za Manispaa zetu  ili yawe kama vielelezo kwa vizazi vijavyo….” anasisitiza Ubao.
Juma Ubao akatolea mifano ya maeneo ya Makumbusho ambako mitaa mingi imepewa majina ya nchi za Afrika.  Mzee Ubao hakuacha kamka mifano mingine akisema  “ ukienda Muhimbili Wodi zote zimepewa majina maarufu ya Mwaisela, Sewa Haji, pia kuna  shule za sekondari ya  Shaaban Robert, Benjamin Mkapa, mitaa ya Samora, Bibi Titi,  Fundikira, Makamba,  barabara ya Kawawa  barabara ya Ali Hassan Miwnyi na sasa hivi ipo ya Mwai Kibaki. Hizi ni kumbukumbu kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo…”

Aidha akaviomba  vyombo vya utangazaji hususani vya Redio, kutenga muda japo kidogo wa kupiga nyimbo zao za zamani.
Kama  gwiji huyo wa muziki hakusita kukemea vijana wa muziki wa kizazi kipya kufanya upuuzi wa kutotaka kujifunza kupiga ala za muziki. Kwa kufanya hivyo ni kama wanacheza ‘maigizo au makida makida’

Juma Ubao huku akikomelea msumari mwingine kwa wanamuziki wa kizazi kipya, akiwaasa  wasibweteke na sifa wanazopambwa na mashabiki wao kwani sifa na mafanikio waliyonayo, anasema si endelevu.
Juma Salim Laizer  ‘Ubao’ mwaka huu ametimiza miaka 63 ya kuzaliwa kwake. Huruma imemjaa kwa kuona jinsi vijana hao   walivyopoteza muelekeo katika muzuki. ‘ Wazee dawa’  Juma Ubao  ameamua kutumia ujuzi wake alionao  kuwafundisha muziki. “nipo tayari kutumia weledi wangu kuwafundisha kupiga ala za muziki na kuimba kwa wale vijana watakaopenda…” anamalizia nguli huyo.

JUMA UBAO AKIIMBA NA KULIUNGURUMISHA GITA LA SOLO.


No comments: